Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Waridi wa BBC: Mwanamke ambaye utunzaji maiti ndio ujasiri wake
- Author, Asha Juma
- Nafasi, BBC Swahili
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Katika jamii nyingi, kifo ni kitu ambacho huogopewa – watu hunong'onezana badala ya kukizungumzia wazi wazi.
Lakini nyuma ya pazia, mbali na mila, kuna watu ambao kazi yao inaanzia pale kifo kinapotokea. Katika Waridi wa BBC wiki hii, Asha Juma amezungumza na Linda Gacheri kutoka kaunti ya Meru, mhudumu wa makafani ili kuangazia ulimwengu huu ambao huwa umezungukwa na ukimya na mengi yasiofahamika.
Linda Gacheri anafanyakazi pale ambapo wengi wanachukulia kazi hiyo kama mwiko nikimaanisha katika makafani. Ndiye mwangalizi wakati jamii zimechanganyikiwa kipindi ambacho mpendwa wao ameaga dunia na mara nyingi familia huwa katika hali ya kujitayarisha kuanza safari ya mazishi. Naye huwa mstari wa mbele kufanikisha safari hiyo.
Katika taaluma hii ambayo inaghubikwa na desturi, uwoga na tamaduni. Wengi wanapoingia kwenye chumba cha makafani wanatazamia kumpata mtu mwenye umri mkubwa pengine hata jitu la miraba minne.
Dhana potofu
Uwepo wa Linda ambaye bado ni msichana katika tasnia hii huwa chanzo cha wengine kumuuliza maswali mengi. Alijipata vipi katika tasnia ambayo tunaweza kusema wengi wanaamini imetawaliwa na wanaume.
"Nilifiwa na bibi yangu, tulipokuwa tunaenda kumchukua katika chumba cha kuhifadhia maiti ambapo mwili wake ulikuwa unahifadhiwa, nilichokiona hakikunifurahisha. Hawakumhudumia vile ambavyo tulikuwa tunamtunza nyumbani. Tulikutana na wazee ambao walikuwa wanakaa kama wavutaji bangi, wanywaji pombe kwa sababu walitushughulikia kama watu ambao hawana elimu ya kile wanachokifanya," Linda anasema.
Kwa kuwa hawakuwa na lakufanya, walizazimika kutii kila kitu walichoambiwa.
Linda aliamua kufungua roho kwa jamaa wake na kuwajulisha kwamba anataka kusomea taaluma ya wahudumu wa afya wa makafani.
"Baba yangu alipinga wazo hilo, aliniambia wanaofanyakazi huko ni watu wanaovuta bangi," Linda anasema.
Baada ya Linda kujifanyia uchunguzi aligundua kuwa sifa anazosikia kutoka kwa wengine kuhusu wahudumu wa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti, sio kweli na kumuelezea baba yake kipya alichokuwa anakifahamu na kufanikiwa kumshawishi.
Uamuzi wa Linda kuanza kusomea kazi hiyo, ndio ulikuwa mwanzo wa mwelekeo mpya katika maisha yake. Lakini watu wanamchukuliaje kama mwanamke wanapokutana naye katika makafani?
"Nimepoteza marafiki wengi, kwa sababu wanaona huwezi kufanya kazi kwenye makafani bila kutumia mihadarati. Na huku nje, bado watu wanaamini kazi hii ni ya wanaume, na sio wanawake. Kuna wengine hata hukataa kunisalimia na kuniambia, hii ndio mikono ambayo umetumia kushika maiti. Sijui wanaona ndani ya makafani unaweza kuua mtu, kuna mambo sana," Linda anasema.
Hadi kufikia hapa ukweli ni kwamba kazi ya Linda sio rahisi. Pia, moja ya hisia inayomzungumka akiwa kazini ni huzuni. Hukutana na watu mbalimbali kila siku anapokuwa kwenye majukumu yake, ambao wanaingia kwenye mshutuko wa kumpoteza mpendwa wao au hata kama walilitarajia, msiba hupokelewa kwa njia tofauti. Pengine kuna wakati ambao hisia za huzuni zinakuzidia na unakabiliana vipi na hali hii?
"Ninaowahudumia kweli huwa wana huzuni, na si familia moja, mbili, wala tatu ambazo huja kwenye makafani wakiwa na huzuni. Nikisema nilie na kila mtu sitaweza. Lakini mimi huwa nazungumza nao kwa utu, na kuwafuatilia hadi siku watakayochukua mwili wa mpendwa wao," Linda anaendelea kusema.
Lakini kuna tukio ambalo mhudumu huyu wa chumba cha kuhifadhia maiti anasema hataweza kulisahau. Aliwahi kufiwa na rafiki yake wa karibu aliyeaga dunia ghafla. Hilo lilikuwa pigo kwake na licha kwamba yeye ni jasiri, alishindwa kushughulikia mwili huu kama ilivyo jambo la kawaida katika taaluma yake. Na hapo ndipo alipogundua kuwa kila nafsi itaonja mauti.
"Kifo huja kwa namna tatu. Ukakufa ukiwa wapi, nini kitakuua na itakuwa ni wakati gani. Hivi ndivyo kifo kilivyo. Ukiwa hapa dunia jaribu kufanya kila kinachokufarisha kwa sababu hujui kesho yako," Linda anasema.
Changamoto
Linda anasema licha ya kwamba wao wanakuwa na umuhimu mkubwa katika jamii kusaidia kulinda miili ya jamaa wakati hawapo tena duniani, watu huwaelewa vibaya.
"Huku nje watu wengi wanatuogopa, sijui wanafikiria unaweza kuua mtu. Watu wengi hawatupendi. Mimi kama mwanamke, wengi wananidharau. Unapata watu wakiwa wanaleta mwili. Kuna mwenye ataniona mimi ni msichana mdogo sifai kuwa hapo. Anaona ni kama sitaweza," Linda anasema.
Mila na desturi
Linda Gacheri anahifadhi na kutunza watu ambao hawana uhai tena. Jamii inamuamini na kumuachia miili ya wapendwa wao kwa ajili ya matunzo hadi kipindi watakapokuwa tayari kwa safari ya mwisho ya mwendazake. Unachukuliaje jukumu hili na lina uzito kiasi gani?
"Ninachoweza kusema, hii sio kazi rahisi. Sio ya kila mmoja. Ninachojitahidi kuwahakikishia jamaa ni kwamba nitatunza mwili wa mpendwa wao vizuri hadi siku watakarejea kuuchukua." Linda anasema.
Baadhi ya maeneo Afrika, inakuwa vugumu kuzungumzia simulizi hii bila kutaja mila na desturi. Linda anaangazia tukio ambalo aliwahi kushuhudia kwa maiti tunacho weza kusema ni miongoni mwa mambo ambayo ni nadra sana kushuhudiwa?
"Kulitokea tukio tukatayarisha mwili na kuukavalisha kama kawaida, tukauweka kwenye sanduku. Tukaupeleka kwa ajili ya jamaa waliofika kuutazama. Wakamaliza na tukauingiza kwenye gari tayari kwa safari. Gari halikusonga hata nchi moja na haikuwa imeharibika. Tukampigia mmiliki wa gari, akatuma gari nyingine, tukahamisha mwili kwenye gari la pili lakini nayo ikashindwa kusonga. Tukaita gari ya tatu lakini hali ilikuwa ile ile.''
Anaendelea kusema: ''Tulichofanya ni kumuita mzee aliyekuwa ametia saini yake wakati aliyekufa anatoka kwenye chumba cha makafani. Tukamuuliza kama pengine kuna chochote kilichotakiwa kufanywa kwa misingi ya mila na desturi, ila alisema kwa ufahamu wake anajua kila kitu kiko sawa.
..Tuliita familia na kuwashauri wakutane ili kupata ufumbuzi. Tukaambiwa turejeshe mwili ndani tena na tufunge milango. Hatujui walichokifanya jamaa wa karibu, maiti iliporejeshwa ndani. Lakini pia hatukutaka kujua chochote kinachoendelea kwa sababu hili lilikuwa suala lao la kibinafsi. Walipomaliza wakatuita na tukafunga tena sanduku. Na kulijeresha kwenye gari. Na moja kwa moja ilianza kusonga na wakaanza safari," Linda anasimulia.
Nyakati za mchana, Linda anakuwa katika ulimwengu wa kuhudumia waliokufa, na punde baada ya kutoka kwenye makafani, anakuwa katika ulimwengi wa walio hai. Linda anazungumzia vipi maisha?
"Uhai ni kitu ambacho hakipo. Maishani kitu ambacho hakina maana. Ukiwa hapa duniani jaribu kuishi na watu vizuri. Na hujui kesho yako itakuwaje. Pia jitahidi kufanya kitu cha kipekee ambacho ukiondoka duniani watu watakukumbuka nacho," Linda anasema.
Pia nilimuuliza Linda kama kumbukumbu anazozipata kazini huwa zinamuandamana kila aendapo?
"Hapana. Hazinifuati nyumbani. Kitu ambacho naweza kusema kinaweza kunisumbua ni kujiuliza, pale nilipouwacha mwili nilioupokea wakati natoka, je, utahudumiwa kama inavyotakikana. Kazi yangu ni kama ya kawaida na nikitoka kazini hakuna chochote cha kazini nitakachofikiria," Linda anasema.
Kazi hii imeathiri vipi mahusiano yake?
Kwa kuwa anachokifanya Linda na kumpa riziki, kazi ya kuhudumia watu katika makafani imekuwa ikichukuliwa jicho tofauti tofauti, nilitaka kujua kama kwa namna moja au nyingine imeathiri mahusiano yake.
"Ni kweli. Imeniathiri sana. Wengi wamekuja kwangu wakiwa na nia ya kuanzisha mahusiano ya mapenzi.
"Lakini kuna mmoja ambaye sijawahi kumsahau hadi leo. Tulipatana, tukazungumza kwa simu. Tukapanda tukutane siku fulani ili kujuana zaidi. Lakini katika mazungumzo yetu nilimuelezea kazi yangu na nilimpenda kwa sababu pia naye alikuwa muwazi upande wa kwake.
"Kijana huyo aliniambia, Linda, nimekupenda lakini kazi yako imenitia uwoga. Unaweza ukaniua usiku nikiwa nimelala, kwa sababu umezoea kukaa na watu waliokufa.
"Nilijaribu kumuelezea lakini hakunielewa. Niliishia kumwambia unataka mke lakini hutaki kazi yake. Mke ni wako, kazi ni ya mke wako. Kwa hivyo, ni jukumu lako uchague moja.
"Na, hakunionyesha ubaya wowote lakini baada ya kile mmoja kurejea kwake tulipomaliza mazungumzoa, mimi nilijiambia, ni kweli huyu kijana amenipenda, lakini hajapenda kazi yangu.
"Kun auwezekano akachukulia kazi yangu kivyengine. Pengine nikimpikia chakula atakuwa anaanza kusema nimetoka kushika maiti. Nikamwambia hata mimi simtaki, wacha aende. Kama hataki na kazi yangu, wacha tu aende," Linda anakumbuka.
Linda Gacheri bado ni msichana hajaanza hata familia. Lakini hilo sio kikwazo kwake. Ameamua kuvaa ujasiri ambao pengine wengi uliwashinda.
Kufanyakazi kila siku yenye kuhusisha kifo, taaluma ambayo imezungukwa na mila, unyanyapaa na matarajio vile vile. Huenda iwe vigumu kupima ujasiri wa Linda kwa maneno pengine uegemee ukakamavu.
Imehaririwa na Ambia Hirsi