Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Hospitali iliyoeneza virusi vya HIV kwa watoto kutokana na matumizi ya sindano zilizokwisha tumika
- Author, Ghazal Abbasi, Seamus Mirodan na Mohammad Zubair Khan
- Nafasi, BBC
- Muda wa kusoma: Dakika 8
Onyo: Makala haya yana maelezo ambayo wasomaji wanaweza kuyaona ya kusikitisha
Mohammed Amin alikuwa na umri wa miaka minane alipofariki muda mfupi baada ya kupimwa na kukutwa na virusi vya UKIMWI.
Alipata homa kali kiasi cha kusisitiza kuwa anataka kulala kwenye mvua, na alijikunja kwa maumivu "kama vile alikuwa ametupwa kwenye mafuta ya moto," anasema mama yake, Sughra.
"Alikuwa akipigana nami, lakini pia alinipenda," Asma mwenye umri wa miaka 10 anasema huku akipiga magoti kando ya kaburi la mdogo wake.
Muda mfupi baada ya kaka yake kuambukizwa virusi hivyo, Asma pia aligunduliwa na virusi vya UKIMWI. Familia yake inaamini watoto wote wawili waliambukizwa kutokana na sindano wakati wa matibabu katika hospitali ya serikali huko Taunsa, katika jimbo la Punjab, Pakistan.
Wao ni wawili kati ya watoto 331 ambao BBC Eye imewatambua kuwa walipimwa na kukutwa na virusi vya HIV jijini humo kati ya Novemba 2024 na Oktoba 2025.
Ni baada ya daktari katika kliniki binafsi kuhusisha mlipuko huo na hospitali inayoitwa THQ Taunsa, mwishoni mwa mwaka 2024, mamlaka za mitaa ziliahidi "msako mkali" na kumsimamisha kazi msimamizi wa matibabu wa hospitali hiyo Machi 2025.
Lakini uchunguzi wa BBC Eye unafichua kwamba vitendo hivyo hatari vya kutumia sindano zilizokwisha tumika bado vinaendelea.
Wakati wa saa 32 za upigaji picha wa siri katika hospitali ya THQ Taunsa mwishoni mwa mwaka 2025, tulishuhudia sindano zikitumika tena kwa dawa tofauti kwa zaidi ya mara 10 tofauti.
Hatujui kama kuna yeyote kati ya watoto hawa ana VVU, lakini utaratibu huu unaleta hatari ya maambukizi ya virusi.
"Hata kama wameunganisha sindano mpya lakini kwenye bomba lile lile la sindano – virusi bado vinaweza kuenea," anasema Dkt. Altaf Ahmed, mtaalamu mshauri wa vijidudu na mmoja wa wataalamu wa magonjwa ya kuambukiza nchini Pakistan, baada ya kutazama video zetu.
Licha ya picha kwenye kuta za hospitali zinazoonyesha udungaji salama wa sindano, tulirekodi wafanyakazi - akiwemo daktari - wakiwadunga wagonjwa bila glavu mara 66.
Mtaalamu mmoja alituambia video yetu inaonyesha udhaifu mkubwa katika mafunzo ya kudhibiti maambukizi nchini Pakistani.
Pia tulimtazama muuguzi akipekua-pekua kisanduku cha kutupa taka za matibabu bila glavu. "Anakiuka kila kanuni juu ya udungaji sindano," anasema Ahmed.
Lakini tulipomwonyesha mkuu mpya wa afya wa hospitali hiyo, Dkt. Qasim Buzdar, picha zetu zilirekodiwa, alikataa kukubali kwamba zilikuwa za kweli.
Alidai zinaweza kuwa zimerikodiwa kabla hajachukua hatamu au "picha hizi pia zinaweza kuwa zimepangwa," na akasisitiza hospitali ni salama kwa watoto.
Mlipuko wa VVU
Dkt. Gul Qaisrani, daktari katika kliniki binafsi ya eneo hilo, alikuwa wa kwanza kugundua mlipuko wa VVU mwishoni mwa mwaka 2024 baada ya kugundua ongezeko la watoto wanaokuja kliniki yake ambao walipimwa na kupatikana na virusi vya UKIMWI.
Karibu watoto wote kati ya 65 na 70 aliowagundua walikuwa wametibiwa katika hospitali ya THQ Taunsa, anasema.
Anakumbuka mama mmoja alimwambia binti yake alidungwa sindano sawa na binamu yake anayeishi na VVU, na sindano hiyo ilitumika kwa watoto wengine kadhaa.
Qaisrani anasema baba mmoja alimwambia alipinga matumizi ya sindano iliyokwisha tumika katika hospitali ya THQ Taunsa lakini alipuuzwa na wauguzi.
BBC Eye imekusanya data kutoka mpango wa uchunguzi wa UKIMWI wa mkoa wa Punjab, kliniki binafsi, na data zilizovujishwa na polisi ili kuwatabua watoto 331 waliopimwa na kupatikana na virusi vya UKIMWI katika jiji la Taunsa kati ya Novemba 2024 na Oktoba 2025.
Kati ya watoto 97 wenye VVU ambao familia zao pia zilipimwa, ni mama wanne pekee waliopimwa na kupatikana na virusi. Hii inaonyesha kuwa visa vichache sana kati ya hivi vilisababishwa na maambukizi kutoka kwa mama hadi mtoto.
Mama wa Mohammed Amin na Asma, Sughra, alipimwa na kupatikana hana VVU - mumewe alifariki miaka miwili iliyopita katika ajali ya barabarani.
Serikali ya Punjab iliingilia kati Machi 2025, iliposema idadi ya visa ilikuwa 106. Msimamizi wa matibabu wa Hospitali ya THQ Taunsa, Dkt. Tayyab Farooq Chandio, alisimamishwa kazi.
Lakini BBC Eye inaweza kufichua kwamba ndani ya miezi mitatu alikuwa akifanya kazi na watoto tena kama afisa mkuu wa matibabu katika kituo cha afya cha vijijini katika vitongoji vya Taunsa.
Madakari wazungumza
Aliiambia BBC Eye katika mahojiano kwamba alichukua hatua "haraka" baada ya kuarifiwa kuhusu kisa cha VVU katika hospitali ya THQ Taunsa, lakini anasema hospitali hiyo haikuwa chanzo cha mlipuko huo.
Nafasi ya Chandio ilichukuliwa na Buzdar, ambaye ameiambia BBC mapambano dhidi ya VVU ndio "lengo lake kuu" la kuchukua kazi hiyo Machi 2025 na ameweka sera ya "kutovumilia kabisa" uchomaji sindano usio salama.
"Tuliendesha programu za mafunzo kwa wahudumu wa afya na wauguzi kuhusu jinsi ya kuzuia na kushinda VVU. Wamefunzwa ipasavyo katika hili," anasema.
Hata hivyo, ushahidi wa BBC Eye unathibitisha kwamba vitendo visivyo salama vinaendelea miezi minane baadaye.
Picha zetu za Novemba na Desemba 2025, zilizorekodiwa kwa wiki kadhaa, zinaonyesha sindano na vichupa vinavyopaswa kuhifadhiwa vikiwa vimeachwa wazi kando ya sindano zilizokwisha tumika.
Pia tulimrekodi muuguzi mmoja akichukua bomba la sindano lililokwisha tumika kutoka kwenye droo yake ikiwa bado na dawa ambayo alimchoma mgonjwa mwingine. Badala ya kuitupa, alimkabidhi mwenzake, tayari kutumika tena kwa mtoto mwingine.
Tulipomwonyesha Buzdar video zetu za siri, alisisitiza kwamba zilirekodiwa kabla ya uongozi wake au ni zilipangwa.
Alipoulizwa anawaambia nini wazazi wa eneo hilo waliokuwa wakitazama video hii, amesema: "Naweza kuwaambia kwa uhakika, kwa kujiamini, mnapaswa kupata matibabu THQ Taunsa."
Taarifa ya Serikali
Katika taarifa, serikali ya mtaa ilisema "hakuna ushahidi uliothibitishwa kwamba THQ ndiyo chanzo" cha mlipuko huo.
BBC Eye imepata ripoti ya ukaguzi wa ujumbe wa pamoja wa shirika la kutoa misaada kwa watoto la Unicef, Shirika la Afya Duniani na idara ya afya ya kikanda ya mwezi Aprili 2025 kuhusu mlipuko katika jiji hilo, ambayo iligundua masuala mengi sawa na uchunguzi wetu kuhusu THQ Taunsa.
"Hali zilikuwa za kutisha hasa katika chumba cha dharura cha watoto," ripoti inasema - hii ni mojawapo ya idara zilizorekodiwa na BBC Eye.
"Dawa muhimu za watoto hazikuwepo, na mbinu zisizo salama za kuchoma sindano zilikuwa za kawaida. Vimiminika vya sindano vilikuwa vikitumika tena na tena, mabomba ya sindano hayana lebo, sindano zilizotumika ziliachwa zimezagaa. Usafi wa mikono unapuuzwa – sinki zimeziba, na hakukuwa na vitakasa mikono."
Dkt. Fatima Mir, profesa wa tiba ya watoto katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Aga Khan huko Karachi, anasema video yetu inaonyesha udhaifu katika mafunzo ya kudhibiti maambukizi nchini Pakistan. "Lazima tuwaonye wadungaji sindano: 'Mmekuwa wasambazaji wa magonjwa.”
Sababu nyingine
Uchunguzi wetu unaonyesha kwamba vitendo visivyo salama kwa kiasi fulani vinasababishwa na shinikizo la kimfumo ikiwa ni pamoja na watu kupendelea sindano kwa matibabu.
Pakistan ina moja ya viwango vya juu zaidi vya matumizi ya sindano duniani, nyingi zikiwa hazihitajiki kutumika kimatibabu. Umma kwa ujumla unaomba wadungwe sindano, ikiwa ni pamoja kwa ajili ya watoto wao, na madaktari wanakubali hilo.
Anasema Mir. "Wanapaswa kuweka sababu ya msingi ya kutumia sindano. Toa sindano kwa magonjwa yanayohatarisha maisha pekee. Kwa magonjwa madogo hadi ya wastani, tumia dawa za kumeza."
Uhaba wa dawa na vifaa pia huchochea vitendo visivyo salama. Mahitaji ya sindano ni mzigo kwenye rasilimali, ambazo hutengwa kwa ajili ya hospitali za serikali kupitia mifumo ya mgao.
Wakati wa upigaji picha wetu wa siri tuligundua kuwa vifaa mara nyingi vilikosekana katika wodi, na wagonjwa ambao wanamudu parasetamol waliambiwa wanunue wenyewe.
Matukio yaliyo rikodiwa THQ Taunsa yanafanana na milipuko mengine nchini Pakistani.
Mwaka 2019, mamia ya watoto katika mji wa Ratodero, katika jimbo la Sindh, walipimwa na kukutwa na VVU, wengi wao wakiwa na wazazi ambao walipimwa na kukutwa hawana.
Daktari wa watoto wa eneo hilo Dkt. Imran Arbani aliiambia BBC aligundua kuwa watoto hao walikwenda kliniki mara kwa mara na walichomwa sindano mara kwa mara katika historia yao ya matibabu. Ni lazima maambukizi haya yalitokea wakati wa matibabu yao, anasema.
Kufikia mwaka 2021 idadi ya watoto wenye VVU imeongezeka hadi 1,500 - na hata sasa, maambukizi mapya bado yanatokea.
Tulipokuwa tukirekodi huko Taunsa, maambukizi yametokea Karachi. Katika eneo la SITE Town, watoto waliotibiwa katika hospitali ya serikali ya mtaa, Hospitali ya Kulsoom Bai Valika, baadaye walipimwa na kukutwa na VVU.
Miongoni mwao alikuwa Mikasha mwenye umri wa miaka miwili.
Mwanafamilia mmoja alisema wafanyakazi wa hospitali walitumia sindano moja kwa watoto wengi: "Walijaza dawa katika bomba la sindano na kumchoma mtoto mmoja, kisha wakaijaza tena na kumchoma mwingine," waliambia BBC Eye.
Msimamizi wa matibabu wa hospitali hiyo Dkt. Mumtaz Shaikh alisema katika mahojiano "madaktari waliohitimu vyema hawatatumia tena" bomba la sindano iliyotumika, "kwa hivyo mambo kama hayo hayatokei katika hospitali za serikali".
Hata hivyo, waziri wa afya wa shirikisho amethibitisha hadharani kwamba mlipuko wa visa 84 ulisababishwa na matumizi ya kurudia mabomba ya sindano hospitalini.
Tulipowasilisha matokeo ya uchunguzi wetu kwa serikali ya kitaifa, msemaji alisema "ilichukua hatua haraka ya kuchunguza [na] kutekeleza hatua za kuzuia maambukizi," huku miongozo ikitumwa kwa vituo vya afya Machi 2025.
Huko Taunsa, familia ya Asma inasema anapunguza uzito, na sasa anakabiliwa na matibabu katika maisha yote dhidi ya virusi ambavyo hangepaswa kuwa ameambukizwa.
Unyanyapaa unaohusishwa na VVU unamaanisha kwamba majirani mara nyingi huwazuia watoto wao kucheza naye, na kumfanya awe peke yake, familia yake inasema. Anamuuliza mama yake: "Nina shida gani?"
Akiwa amesimama kwenye kaburi la kaka yake, Asma anasema, "nimemmisi, sasa yuko na Mungu."
Anaiambia BBC Eye kwamba anasema kwa bidii shuleni.
"Nitakapokuwa mkubwa," anasema, "nataka kuwa daktari."