Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Trump adokeza mazungumzo huenda yakarejelewa, zuio la bandari za Iran likitekelezwa kikamilifu

Upande wa Iran bado haujatoa majibu kwa kauli za Trump, lakini Katibu Mkuu wa Umoja wa mataifa, António Guterres, amesema kuwa kuna haja mazungumzo yarejee tena.

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Makamu wa rais wa Marekani JD Vance aeleza nafasi ya Qalibaf Iran

    Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, ambaye ni makamu wa Rais Donald Trump, na ambaye siku chache zilizopita alifanya mazungumzo na Mohammad Bagher Qalibaf akiwa kiongozi wa ujumbe wa kidiplomasia wa Iran mjini Islamabad, amesema wazi katika mahojiano yake mapya ya televisheni kwamba kwa maoni yake, Bw. Qalibaf kimsingi ndiye “mtu anayeiendesha nchi (Iran).”

    Katika mahojiano hayo, Makamu wa Rais wa Marekani amesema kuwa uhasama na mivutano ya miaka 47 kati ya Iran na Marekani imefanya watu wengi wasiamini kuwa matokeo maalum yanaweza kupatikana kupitia mazungumzo ya moja kwa moja.

    “Hii ilikuwa ni mkutano wa ngazi ya juu zaidi kati ya maafisa wa nchi hizo mbili,” alisema katika mahojiano ya Jumanne.

    “Kwa kiongozi wa Iran ambaye kwa kweli ndiye anayeiongoza nchi kuketi na Makamu wa Rais wa Marekani… ni jambo la kawaida kuwa kumekuwa na hali ya mashaka makubwa kati ya nchi hizo kwa miaka mingi, na hakuna anayetegemea suala hili kutatuliwa katika mkutano mmoja.”

    Makamu huyo wa Rais wa Marekani alikuwa amesema jana kwamba aliamini mazungumzo ya Islamabad “yalipiga hatua fulani,” lakini akaongeza kuwa Iran haikupiga hatua ya kutosha.

    Soma zaidi:

  2. Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif kuzuru Saudi Arabia leo

    Taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu imesema kuwa Shehbaz Sharif ataondoka kuelekea Saudi Arabia leo kwa ziara rasmi.

    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ujumbe wa ngazi ya juu pia utaandamana na Waziri Mkuu kutoka Islamabad kuelekea Jeddah.

    Ikumbukwe kuwa Waziri wa Fedha wa Pakistan amethibitisha kuwa Saudi Arabia imeahidi kutoa amana nyingine ya dola bilioni tatu kwa Pakistan, ambazo zinatarajiwa kutolewa wiki ijayo.

    Waziri wa Fedha wa Shirikisho, Seneta Muhammad Aurangzeb, ameongeza kuwa amana zilizopo za Saudi Arabia za dola bilioni 5 hazitakuwa tena chini ya mfumo wa uongezaji wa mwaka hadi mwaka, bali zitaongezwa muda wake kwa kipindi kirefu cha miaka mitatu, yaani hadi mwaka 2028.

    Waziri wa Fedha wa Saudi Arabia, Mohammed bin Abdullah Al-Jadaan, alikutana na Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif Ijumaa usiku, kabla ya mazungumzo kati ya Iran na Marekani yaliyofanyika Islamabad Jumamosi iliyopita.

    Siku iliyofuata, Jumamosi, Wizara ya Ulinzi ya Saudi Arabia ilitangaza kuwa kikosi cha kijeshi kutoka Pakistan kiliwasili katika Kituo cha Anga cha King Abdulaziz katika eneo la mashariki, kikijumuisha ndege za kivita na za msaada kutoka Jeshi la Anga la Pakistan.

  3. CENTCOM: Zuio la bandari za Iran limetekelezwa kikamilifu

    Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) imesema kuwa zuio la bandari za Iran “limetekelezwa kikamilifu.”

    Shirika hilo limesema katika taarifa kwamba katika muda uliopita tangu hatua hiyo kuchukuliwa, vikosi vya Marekani vimesitisha kabisa mtiririko wa biashara ya kiuchumi kwenda na kutoka Iran kupitia njia ya baharini.

    Rais Donald Trump aliambia kituo cha Fox News kwamba vita na Iran “vinakaribia mwisho wake.”

    Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance amesema katika mahojiano ya televisheni kwamba uhasama na mivutano ya miaka 47 kati ya Iran na Marekani imefanya hakuna mtu kuamini kuwa matokeo maalum yanaweza kupatikana kupitia mkutano wa moja kwa moja wa mazungumzo.

    Kamanda wa Eneo la 10 wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ametangaza katika ujumbe kwamba “mlipuko mdogo” uliosababishwa na “viongozi wasaliti na wasio wazalendo” umetokea mjini Tehran.

    CENTCOM imesema pia kuwa zuio hilo limekuwa likiendelea kwa saa 36, ambapo vikosi vya Marekani vimesitisha kabisa biashara ya baharini kwenda na kutoka Iran.

    Aidha, CENTCOM imesema vikosi vya Marekani vinaendelea kudumisha ubabe wao wa kijeshi wa majini katika eneo la Mashariki ya Kati.

    Soma zaidi:

  4. Israel na Lebanon zakubaliana kuendelea kufanya mazungumzo ya ana kwa ana

    Israel na Lebanon zimekubaliana kufanya mazungumzo zaidi ya ana kwa ana baada ya hapo jana Jumanne kufanya mazungumzo yao ya kwanza ambayo hayajashuhudiwa kwa miongo mingi, yakifanyika wakati ambapo Jeshi la Israel linapambana vikali dhidi ya wanamgambo wa Hezbollah nchini Lebanon.

    Balozi wa Lebanon nchini Marekani Nada Hamadeh Moawad ameyataja mazungumzo hayo yaliyofanyika Washington kuwa yenye tija huku mwenzake wa Israel Yechiel Leiter akisema walikuwa na mashauriano mazuri na wamefikiana mambo ya msingi.

    Katika taarifa iliyotolewa baada ya mazungumzo hayo Jumanne, walisema walisisitiza "haja ya dharura ya utekelezaji kamili" wa makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa mnamo Novemba 2024.

    Ikumbukwe kuwa makubaliano hayo yalifikiwa baada ya mapigano ya miezi 13 kati ya Israel na Hezbollah, ambapo Hezbollah inayoungwa mkono na Iran ilipewa siku 60 kukomesha uwepo wake wa silaha kusini mwa Lebanon.

    Nida Hamada anasema pia ametoa wito wa kusitishwa kwa mapigano na watu waliokimbia makazi yao warudishwe makwao.

    Mkutano huo wa Washington uliosimamiwa na Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Marco Rubio, ndiyo wa kwanza wa kidiplomasia wa ana kwa kati ya Israel na Lebanon tangu mwaka 1993.

  5. Miaka mitatu ya vita Sudan, mamilioni wakabiliwa na janga la kibinadamu

    Ni miaka mitatu tangu vita vya wenyewe kwa wenyewe kuzuka nchini Sudan mnamo tarehe 15 Aprili 2023, vita ambavyo vimesababisha mzozo mbaya zaidi wa kibinadamu duniani.

    Maelfu ya watu wameuawa huku zaidi ya watu milioni 12 wakiachwa bila ya makazi na wengine wakikimbilia nchi jirani kama wakimbizi.

    Licha ya ukubwa wa mzozo huo, hakujakuwa na msaada wa kuridhisha kutoka kwa jumuiya ya kimataifa katika kuutatua mzozo huo na mashirika ya kutoa misaada ya kibinadamu yanasema ufadhili umekuwa mdogo mno.

    Wafadhili wanakutana leo Berlin kujadili namna ya kufufua juhudi za amani na upatikanaji wa misaada.

    Asilimia 65 ya Wasudan wanahitaji chakula,maji,makazi na dawa.

    Soma zaidi:

  6. Papa Leo aanza ziara Cameroon akitarajiwa kuhubiri amani

    Papa Leo anatembelea Cameroon leo katika hatua ya pili ya ziara yake barani Afrika.

    Alianza safari yake ya nchi nne nchini Algeria, ambako alihimiza mazungumzo ya kidini na msamaha.

    Ziara yake nchini Cameroon itaangaziwa na misa ya kiishara itakayofanyika Bamenda, mji ulio katikati ya mzozo wa silaha katika maeneo mawili ya nchi yanayotumia Kiingereza.

    Papa Leo atatumia siku tatu zijazo nchini Cameroon, akikutana na maafisa wa serikali na viongozi wa dini, kutembelea kituo cha watoto yatima na hospitali, pamoja na kuongoza misa kadhaa.

    Ziara yake inafanyika wakati ambapo nchi hiyo inakabiliwa na mzozo uliodumu kwa takribani muongo mmoja katika maeneo yake mawili yanayotumia Kiingereza.

    Katika mji wenye mvutano wa Bamenda, Papa anatarajiwa kutoa ujumbe mzito wa amani na maridhiano.

    Tangu mapigano yalipozuka mwaka 2017, Kanisa Katoliki limekuwa likitoa wito mara kwa mara wa mazungumzo na suluhisho la amani kwa mgogoro huo.

    Uamuzi wa Papa kuongoza misa Bamenda unaonekana kama ishara ya matumaini, na huenda ukawa hatua kuelekea kurejea kwa hali ya kawaida.

    Kabla ya ziara hiyo, wanamgambo wanaotaka kujitenga katika maeneo yanayotumia Kiingereza walitangaza kusitisha mapigano kwa muda wa siku tatu ili kuruhusu waumini kuhudhuria misa ya Papa.

    Soma zaidi:

  7. Mazungumzo yakusitisha mapigano DRC yaliyohamishiwa Uswisi kuanza leo

    Na Duru nyingine ya mazungumzo ya kujaribu kumaliza mapigano mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yanaanza leo nchini Uswisi.

    Wapatanishi kutoka Marekani na Qatar wanatarajiwa kujiunga na mazungumzo hayo kati ya serikali ya DRC na waasi wanaoungwa mkono na Rwanda wa kundi la M23.

    Mazungumzo ya kusitisha mapigano yalianza mwezi Aprili 2025 nchini Qatar.

    Hata hivyo, mapigano bado yanaendelea kushuhudiwa katika eneo hilo.

    Hatua muhimu zilizopatikana mjini Doha ni pamoja na kutiwa saini kwa azimio la Julai 19 kuhusu kanuni za mwongozo, makubaliano ya kufuatilia usitishaji wa mapigano ya Oktoba 14, pamoja na mifumo ya amani ya Novemba 15.

    ''Mazungumzo ya amani yamehamishiwa Uswisi kufuatia mgogoro unaoendelea katika Mashariki ya Kati, uamuzi uliotolewa na wapatanishi'', Oscar Balinda, msemaji wa M23, aliliambia gazeti la The New Times.

    Aidha, alieleza kuwa duru hii ya mazungumzo itajikita zaidi katika kuhakikisha msaada wa kibinadamu unawafikia wananchi walioko katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wao.

    Hii ni sehemu ya itifaki ya tatu kati ya nane zilizojadiliwa Doha.

    Kwa upande wake, alidai kuwa kikosi chake kimetekeleza itifaki ya kwanza ya kusitisha mapigano pamoja na kuachilia huru wafungwa wa vita, huku akiishutumu serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa kushindwa kutekeleza ahadi zake.

    “Tumekuwa tukitafuta mazungumzo ya amani, lakini serikali ya Congo bado inaendelea kutuchukulia hatua za kulipiza kisasi,” alisema Balinda.

  8. Vita Iran: Kenya yatangaza kupanda kwa bei ya petroli na dizeli

    Mamlaka ya udhibiti wa nishati na Petroli nchini Kenya EPRA imetangaza bei mpya za mafuta itakayotumika katika kipindi cha siku thelathini zijazo.

    Bei ya Petroli imeongezeka kwa shilingi 28.69, lita sasa itauzwa kwa shilingi 206.97, lita moja ya Dizeli imeongezeka kwa shilingi 40.30 na sasa itauzwa kwa shilingi 206.84 .

    Bei ya Mafuta ya taa itasalia kama ilivyokuwa mwezi uliopita ikiuzwa kwa shilingi152.78.

    Haya yanajiri, siku chache baada ya nchi jirani ya Tanzania kutangaza bei ya mafuta kupanda kutokana na uhaba wa mafuta yanayoingia nchini humo.

    Wanunuzi wa mafuta kwa bei ya rejareja yanayopitia bandari ya Dares salaam wanalazimika kuongeza shilingi 956 za Tanzania katika kila lita moja ya mafuta baada ya bei kufikia 3820 kutoka 2864.

    Lita moja ya petroli Dar es Salaam sasa inauzwa ghali zaidi kwa takriban KSh 13 (sawa na Tsh 260) ukilinganisha na Nairobi, ambako bei ya sasa ni KSh 178.28 (sawa na Tsh 3,565).

    Wamiliki wa magari wananunua dizeli ikiwa shilingi 3,806 huku raia wa kipato kidogo wakilazimika kununua mafuta ya taa shilingi 3,684 za Tanzania.

    Kwa wanunuzi wa mafuta ya petroli yanayopitia bandari ya tanga wanaingia mfukoni zaidi kwani sasa wanauziwa lita moja ya mafuta kwa shilingi 3881awali walikuwa wakiipata bidhaa hii kwa shilingi 2925.

    Tangu kuzuka kwa mzozo wa mashariki ya Kati, kumeshuhudiwa uhaba wa mafuta katika mataifa kadhaa.

    Kufungwa kwa Mlango Bahari wa Hormuz kumeathiri usafirishaji wa mafuta ambapo asilimia ishirini ya mafuta duniani hupitia hapo.

    Soma zaidi:

  9. Rais wa China atoa onyo kali kuhusu hali inayoendelea katika bandari ya Iran

    Kwa mujibu wa shirika la habari la serikali ya China, Xinhua, Rais wa China Xi Jinping ameonya kwamba dunia kwa mara nyingine inaelekea kurejea katika “sheria ya msituni (ubabe),” akimaanisha kuwa pasipo kuwepo kwa kanuni za kuongoza ulimwengu, kila jambo linaweza kufanyika bila mipaka.

    Kwa mujibu wa shirika hilo, Rais Xi alitoa kauli hiyo wakati wa mazungumzo na mwenzake wa Uhispania, Pedro Sánchez, ambaye yuko katika ziara nchini China.

    Akiashiria kinachoonekana kuwa ni vita vinavyoendelea katika Mashariki ya Kati, alisema dunia ipo katika hali ya “vurugu,” na kwamba kuna “mkanganyiko kati ya utekelezaji wa sheria na matumizi ya nguvu.”

    Katika mkutano huo, Rais Xi alisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya China na Uhispania ili kuzuia dunia isije ikaangukia katika “sheria ya msituni,” na kulinda “utaratibu wa kimataifa unaozingatia sheria za kimataifa.”

    Soma zaidi:

  10. Trump adokeza mazungumzo ya Iran yanaweza kurejelewa wiki hii

    Rais wa Marekani Donald Trump amedokeza kuwa mazungumzo kuhusu kuvimaliza vita vya Iran huenda yakarejea katika kipindi cha siku mbili zijazo.

    Mazungumzo kati ya maafisa wa Marekani na wa Iran yaliyofanyika nchini Pakistan mwishoni mwa Juma lililopita yalifeli na kuichochea Marekani kuanzisha operesheni ya Jeshi la majini ikilenga bandari za Iran kama sehemu ya shinikizo kwa Iran kuufungua Mlango Bahari wa Hormuz

    “Ningekushauri ubaki hapo [Islamabad], kwa kweli, kwa sababu kuna jambo linaweza kutokea ndani ya siku mbili zijazo, na tuna mwelekeo zaidi wa kwenda huko,” Trump alinukuliwa akisema katika mahojiano na New York Post.

    Kauli zake zilikuja wakati jeshi la Marekani liliposema kuwa hakuna meli yoyote iliyopita katika mzingiro uliowekwa na Marekani kwenye bandari na maeneo ya pwani ya Iran katika saa 24 za kwanza za operesheni hiyo.

    Mvutano huo umeibua mashaka kuhusu uwezekano wa kusitishwa kwa mapigano kwa muda wa wiki mbili ambako kunatarajiwa kumalizika wiki ijayo.

    Upande wa Iran bado haujatoa majibu kwa kauli za Trump, lakini Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, amesema kuwa kuna haja mazungumzo ya amani yarejee tena.

    Maafisa kutoka nchi za Ghuba, Pakistan na Iran pia wamesema kuwa timu za mazungumzo kutoka Washington na Tehran zinaweza kurejea Pakistan baadaye wiki hii, ingawa tarehe rasmi bado haijakubaliwa, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.

    Iran kwa kiasi kikubwa imefunga mlango bahari wa Hormuz, njia muhimu ya kimataifa ya usafirishaji wa mafuta na gesi, tangu iliposhambuliwa na mashambulizi ya anga ya Marekani na Israel tarehe 28 Februari.

    Zaidi ya meli za kivita kumi na mbili za Marekani pamoja na takribani wanajeshi 10,000 wa Marekani sasa wanatekeleza mzingiro dhidi ya meli za nchi yoyote zinazoingia au kutoka katika bandari za Iran, hali inayonyima Iran chanzo muhimu cha uhai wa kiuchumi.

    Pia unaweza kusoma:

  11. Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja ya Jumatano ya tarehe 15 Aprili 2026.