Jinsi mazingira ya ajira za Uarabuni yalivyo magumu hivi sasa

    • Author, Azadeh Misheri, Joel Gunto
    • Nafasi, BBC Dubai
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Wakati milio ya ving'ora ikisikika angani, Norma huanza kusali kimya kimya.

Norma, mwenye umri wa miaka 49, anafanya kazi kama mfanyakazi wa ndani katika nchi ya Mashariki ya Kati ya Qatar. Anatoka Ufilipino, huku mumewe na watoto wake watatu wakiishi maelfu ya kilomita mbali.

Qatar ni miongoni mwa nchi za Ghuba zinazohusishwa katika vita kati ya Marekani, Israel na Iran. Norma anaomba arejee nyumbani salama.

"Kila ninapoona picha na video za makombora angani, nahisi hofu na wasiwasi," aliiambia BBC.

"Lazima niishi kwa ajili ya familia yangu. Mimi ndiye tegemeo lao pekee."

Kadiri nchi tajiri za Ghuba zilivyoanza kulengwa na mashambulizi ya Iran kwa sababu ya kuhifadhi vituo vya kijeshi vya Marekani, idadi kubwa ya wageni iliondoka, na watalii wakasitisha safari zao.

Hata hivyo, hali imekuwa ngumu zaidi kwa mamilioni ya wafanyakazi wahamiaji ambao mustakabali wao sasa haujulikani.

Kuanzia wafanyakazi wa ndani hadi wafanyakazi wa ujenzi, kwa muda mrefu wamekuwa wakitegemeza uchumi wa nchi hizi huku wakisaidia familia zao kujikwamua kutoka umaskini nyumbani.

Norma alitarajia kutumia kipato chake kugharamia sherehe ya mahafali ya mwanawe wa miaka 23 na kusaidia binti zake wawili kupata elimu ya uuguzi ili wapate ajira nzuri nje ya nchi.

Ndiyo maana ametumia zaidi ya miongo miwili kufanya kazi Qatar, Saudi Arabia na Falme za kiarabu UAE.

Kile kilichowafanya waendelee kubaki ni mshahara.

Wafanyakazi wa ndani kutoka Ufilipino hupata angalau dola 500 kwa mwezi mara nne hadi tano zaidi ya wanachopata nyumbani.

"Nina matumaini dunia itakuwa na amani tena," anasema Norma. "Ninaomba vita viishe."

Lakini vita hivi vinamlazimisha kufikiria upya maisha yake. Anapanga kurejea nyumbani na kuanzisha biashara ndogo na mumewe.

Miongoni mwa wahanga wa mwanzo wa vita hii alikuwa Mary Ann Violaskis, mwenye miaka 32, aliyekuwa akifanya kazi kama mlezi nchini Israel.

Alijeruhiwa alipokuwa akimsaidia mgonjwa wake kujinusuru baada ya kombora kupiga makazi yao huko Tel Aviv.

Kwa mujibu wa Shirika la Kazi Duniani, takriban wafanyakazi wahamiaji milioni 2.4 wanafanya kazi katika eneo la Ghuba ikiwa ni kituo kikubwa zaidi cha ajira kwa wafanyakazi wa nje duniani.

Wengi wao wanatoka India, Pakistan, Bangladesh, Sri Lanka, Ufilipino, Indonesia na Kenya.

Wengi hufanya kazi za kipato kidogo na zisizo na uhakika, huku wakikosa huduma muhimu kama afya.

Angalau wafanyakazi 12 wa Asia Kusini wameripotiwa kufariki hadi sasa kutokana na vita hivyo.

Miongoni mwa waliouawa katika vita hivyo ni Dibas Shrestha, raia wa Nepal mwenye umri wa miaka 29 ambaye alifanya kazi kama mlinzi huko Abu Dhabi. Aliuawa katika shambulio la Iran mnamo Machi 1.

"Nilijaribu kumshawishi arudi Nepal, lakini alisema alipenda kazi yake huko Abu Dhabi na alikuwa na maisha mazuri huko," mjombake Ramesh aliambia BBC.

"Ndugu zetu wengi wamekwenda nchi za Ghuba kufanya kazi, kwa hivyo tulikuwa na wasiwasi sana juu yao."

Vita vilipoanza, Shrestha aliihakikishia familia yake kwamba kila kitu kilikuwa salama huko. Katika chapisho la Facebook, aliandika kwamba "alikuwa na wasiwasi" na habari, lakini pia alihisi kwamba "habari wakati mwingine hutia chumvi au kupotosha habari."

Kulingana na mjomba wake, Shrestha alikuwa akiweka akiba pesa za kujenga upya nyumba ya wazazi wake, ambayo iliharibiwa na tetemeko la ardhi mnamo 2015 ambalo liliua mamia ya watu.

Ramesh anasema, "Alikuwa mtoto wa pekee wa wazazi wake, mkarimu sana na mwenye akili."

Mfanyakazi mwingine, Ahmed Ali, mwenye miaka 55 kutoka Bangladesh, alifariki baada ya mabaki ya kombora kuanguka Dubai.

Mwanawe Abdul Haq alisema pia alikwenda kufanya kazi katika Umoja wa Falme za Kiarabu na baba yake, lakini alirejea Bangladesh kabla ya vita kuanza.

Baba yake mara kwa mara alimtumia pesa nyumbani, dola 500 hadi 600 kwa mwezi, ambazo zinachukuliwa kuwa kiasi kikubwa katika nchi hii maskini ya Asia Kusini.

Kifo cha Ahmed kilitokea wakati wa mwezi wa Ramadhani, na mtoto wake aliambiwa kuwa tukio hilo lilitokea jioni, wakati ambao watu walikuwa wakifuturu.

"Alipenda sana watu wa Dubai," anasema mwanawe Abdul Haq. "Alikuwa akisema kwamba watu walimkaribisha hapa na ilikuwa mahali pazuri pa kuishi."

"Sidhani hata walijua vita vinaendelea. Hawakusoma habari na hawakuwa na simu janja."

Kulingana na Abdul Haq, maoni yake kuhusu Dubai na eneo zima sasa yamebadilika: 'Si salama tena, hakuna anayetaka kumpoteza baba yake.'

Serikali barani Asia zinafanya juhudi za dharura kuwarudisha nyumbani wafanyikazi wahamiaji.

Lakini tishio la mashambulizi ya makombora limetatiza safari za kwenda na kutoka Dubai, Abu Dhabi na Qatar, na kuwalazimu wanaotaka kuondoka kuchukua njia ndefu kurejea nyumbani.

Kwa mfano, wafanyakazi 234 kutoka Kuwait, Qatar na Bahrain walilazimika kusafiri kwa saa nane kwa barabara hadi Saudi Arabia ili kupata ndege ya kurudi nyumbani.

Hadi Machi 23, karibu wafanyakazi 2,000 kutoka Ufilipino walikuwa wamesharejeshwa nyumbani.

Mashariki ya Kati ni nyumbani kwa karibu nusu ya Wafilipino zaidi ya milioni mbili wanaofanya kazi nje ya nchi, na fedha zao zinazotumwa huchangia takriban asilimia 10 ya uchumi wa nchi hiyo.

Uhamisho ni muhimu vile vile kwa Bangladesh, kwani wengi wa wafanyikazi wake wahamiaji karibu milioni 14 wanafanya kazi katika Mashariki ya Kati.

Takriban wafanyakazi 500 wa Bangladesh wamerejeshwa makwao tangu mzozo huo uanze, na serikali ya Dhaka imepanga angalau safari mbili za ndege kutoka Bahrain.

Hata hivyo, kwa baadhi ya watu, si rahisi kuondoka.

Su Su, raia wa Myanmar, anaiona Dubai kuwa kimbilio salama baada ya kukimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Amekuwa akifanya kazi katika kampuni ya mali isiyohamishika huko Dubai kwa miaka miwili iliyopita.

Anasema mfumo wa sasa wa kufanya kazi unamkumbusha vikwazo vya kutotoka nje vilivyowekwa wakati wa Covid, tofauti pekee ni kwamba sasa lazima akae mbali na dirisha wakati ving'ora vinapolia.

"Nina begi la dharura tayari endapo nitalazimika kuhamia mahali pengine... Nilichukua tabia hii nilipokuwa nyumbani Myanmar."

Bado, anasema, "Kuna hali ya amani hapa. naamini mwishowe mambo yatakuwa sawa."

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid