Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mwaka mmoja wa Tundu Lissu gerezani; nini kinaendelea?
Leo Aprili 9, 2026, imetimia mwaka mmoja tangu Tundu Lissu, Mwenyekiti wa Chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania (CHADEMA), kukamatwa na kuwekwa gerezani kwa mashtaka ya uhaini na uchochezi.
Kesi yake imekuwa ya kivutio kimataifa, ikichochea mjadala kuhusu haki za kikatiba, uwazi wa mahakama, na uhuru wa kisiasa nchini Tanzania. Wafuasi wake wanadai kesi hiyo ni ya kisiasa, huku serikali ikisisitiza ni hatua ya kisheria inayolenga kulinda usalama wa taifa.
Hii kesi ni mojawapo ya kesi kubwa zaidi za kisiasa nchini Tanzania tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992. Katika kipindi cha hivi karibuni, Freeman Mbowe, aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA kabla ya Lissu, alikamatwa na kushikiliwa kwa zaidi ya nusu mwaka kutokana na mashtaka ya ugaidi, kabla ya kesi yake kufutwa.
Ni muhimu kufahamu muendelezo wa matukio muhimu ya mwaka huu mmoja wa Lissu tangu akamatwe na mwenendo wa kesi zake zinazomkabili.
April 9-10, 2025 – Kukamatwa na kufikishwa Mahakama ya Kisutu
Tarehe 9 Aprili 2025, Tundu Lissu alikamatwa mjini Mbinga, mkoani Ruvuma, akiwa katika kampeni ya kuhamasisha msimamo wa chama chake wa "No Reforms, No Election."
Polisi walisema kukamatwa kwake kulihusiana na hotuba zake zilizodaiwa kuhamasisha umma kupinga kufanyika kwa uchaguzi, jambo ambalo serikali ilisema linakiuka sheria za uhaini na usalama wa taifa.
Mara baada ya kukamatwa, Lissu alisafirishwa usiku hadi Dar es Salaam. Siku iliyofuata, 10 Aprili 2025, alifikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, ambapo alisomewa mashtaka ya uhaini na uchochezi.
Hata hivyo, shitaka kubwa la uhaini halikusikilizwa katika Mahakama hiyo, kwani mahakama hiyo haina mamlaka ya kuamua mashtaka hayo. Badala yake, ilikuwa Mahakama ya ukabidhi, katika hatua ya uwasilishwaji (committal proceedings) ili kuamua kama kuna ushahidi wa kutosha kumpeleka Mahakama Kuu.
Mbali na mashtaka ya uhaini, Lissu anatuhumiwa pia kwa uchapishaji wa taarifa za uongo kuhusu uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024, ikiwa ni pamoja na madai ya kuiba kura na majaji kutotenda haki.
April 24, 2025 – Kesi kusikilizwa kwa njia ya mtandao na ulinzi mkali
Tarehe 24 Aprili 2025, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilianza kusikiliza baadhi ya mashtaka madogo ya uchochezi kwa njia ya mtandao (video conferencing).
Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Franco Kiswaga alikuwa akisikiliza kesi ya uhaini na Geofrey Mhini alisikiliza mashtaka matatu ya uchochezi.
Lissu alipinga hatua hii ya kesi kusikilizwa kwa njia ya mtandao.
Ulinzi mkali ulitumika kutokana na tahadhari ya usalama, ambapo Jeshi la Polisi lilisimamia maeneo ya nje ya mahakama na maeneo ya ndani.
Ulinzi wa Polisi katika kesi hii hasa katika hatua za awali ulisababisha baadhi ya viongozi na wafuasi wa CHADEMA wakijeruhiwa, wakiwatupia lawama Polisi.
Kesi kurushwa mubashara na Mahakama wazi
Kesi ilipangwa kusikilizwa mtandaoni ili kupunguza msongamano na kuhakikisha usalama. Hata hivyo, Lissu alikataa hali hiyo na kuhitaji kuwepo kizimbani Mahakama ya Kisutu.
Mahakama ilikubali ombi lake, ikihakikisha kesi inafanyika mahakamani kwa uwazi kupitia Mahakama ya wazi. Uamuzi ulipokelewa na vyombo vya haki za binadamu na mashirika ya kimataifa kama hatua muhimu ya uwazi wa kisheria, ingawa ilibaki na changamoto za kiusalama kwa wafuasi wa CHADEMA waliokuwa mahala hapo.
Hata hivyo upande wa kuonyeshwa mubabashara Mahakama ilikataa kupitia uamuzi wa 18 Agosti 2025.
June 2025 – Kujitetea mwenyewe
Kwa kuendelea kwa kesi, Lissu aliamua kujitetea mwenyewe kortini, baada ya kudai kuwa mawakili wake wamekuwa wakizuiwa kuwasiliana nae kwa faragha wanapomfuata gerezani.
Awali, alikuwa akitetewa na mawakili zaidi ya 10, ikiwemo Rugemeleza Nshala, Wakili Peter Kibatala na kaka yake Lissu, anayeitwa Alute Mughwai na baadhi ya wakili wengine mashuhuri nchini Tanzania.
Mahakama ilikubali ombi lake. Lissu aliendelea kujitetea katika kila hatua.
August 2025 - Kuhamishiwa Mahakama Kuu
Baada ya Mahakama ya uwasilishaji, Kisutu kumalizika, ilionakana kesi yake inaweza kupelekwa Mahakama kuu kwa hatua ya usikilizwaji kwa kesi ya uhaini.
Katika Mahakama hii, sasa inasikiliza ushahidi kamili kutoka kwa Jamhuri, ikiwemo video ya hotuba yake na nyaraka zinazothibitisha mashtaka.
Mahakama Kuu ndiyo yenye uhalali kisheria wa kusikiliza mashtaka makuu ya uhaini, na Mahakama ya Kisutu haikuhusika moja kwa moja kusikiliza uhaini zaidi ya kuandaa mwenendo.
Mapingamizi na hatua za kisheria
Katika kipindi hiki, Lissu aliwasilisha pingamizi mengi na hata upande wa mashtaka. Lakini mapingamizi makubwa mawili yaliyoteka mjadala ni ushahidi wa video, mashaihid wa siri na ongezeko la ushahidi.
Oktoba 17, 2025 Jamhuri kupitia shahidi wake wa tatu katika kesi ya uhaini inayomkabili Lissu iliiomba mahakama ipokee video inayomuonesha Lissu akitamka maneno yanayodaiwa kuwa ya uhaini. Lakini Lissu aliweka pingamizi na akatoa sababu nne ambazo Jamhuri nao walijibu. Ombi hili lilikataliwa na vido hiyo kuondolewa kama sehemu ya ushahidi.
Akiwa Kisutu Lissu pia alipinga uwepo wa Mashahidi fiche ama wa siri ambao hawataonekana wala kujulikana, Mahakama ilikataa ombi lake. Na Mahakama kuu pia Jaji Elizabeth Mkwizu katika ombi hilo hilo la Lissu alisema kuwa, maombi hayo hayakuwa na mashiko akibainisha kuwa uamuzi wa Mahakama ya Kisutu ulizingatia haki ya pande zote ikiwemo mshtakiwa kusikilizwa kwa usawa na usalama wa mashahidi.
Kuhusu ombi la kuongeza ushahidi lililiowasilishwa na upande wa Mashtaka, Februari 23, 2026, Lissu alipinga na Mahakama kukubaliana naye.
Nini kinaendelea?
Kwa sasa kesi ya uhaini inayomkabili kiongozi huyu wa Chadema, Tundu Lissu sasa imehamia Mahakama ya Rufani.
Baada ya uamuzi ule wa Mahakama kuu kuhusu kuongezwa kwa ushahisi, Jamhuri ikafungua shauri la mapitio Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu Masijala Ndogo Dar es Salaam, kutupilia mbali notisi yake ya kuwasilisha ushahidi mpya katika kesi hiyo.
Kutokana na hatua hiyo, Mahakama Kuu ikatangaza kusimamisha usikilizwaji wa kesi hiyo mpaka Mahakama ya Rufani itakapotoa uamuzi kuhusu shauri hilo.
Akiwa Mahakamani hapo Lissu alieleza kwa mujibu wa kifungu cha 8(2D) cha sheria ya Mamlaka ya Rufaa kwamba hakiruhusu rufaa wala mapitio wala marejeo ya maamuzi ya mahakama ambayo hayamalizi shauri la msingi.
Aksema anafahamu rufaa hiyo imewasilishwa ili aendelee kukaa gerezani. Ingawa upande wa Serikali unasema, ni haki ya kisheria kukata rufaa.
Sasa kinachosubiriwa ni jopo la majaji wa Mahakama ya rufaa kukaa, kufanya mapitio ya uamuzi huo wa Mahakama kuu na kutoa uamuzi. Bado tarehe rasmi haijafahamika.
Awali kati ya mwezi Mei hadi Disemba 2025, kumekuwa na mfululizo wa matamko, maazimio na miito kutoka kwa jumuiya za kimataifa zikieleza wasiwasi kuhusu mwenendo wa kesi ya kiongozi huyo, huku zikisisitiza haja ya kuheshimiwa kwa haki za msingi za kisheria licha ya kesi kuendelea mahakamani.
Katika kipindi hicho, Bunge la Ulaya lilipitisha maazimio mawili kwa wakati tofauti kuhusu Lissu, mwezi Mei na Novemba, likitaka kuachiwa kwake au kuhakikisha anapata haki kamili ya kusikilizwa kwa mujibu wa viwango vya kimataifa.