Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Sababu tano zinazotajwa kukwamisha mazungumzo ya Marekani na Iran
Mazungumzo ya ngazi ya juu kati ya Marekani na Iran yaliyofanyika Islamabad, Pakistan, yamefikia ukomo bila makubaliano, baada ya saa 21 za majadiliano makali yaliyoonekana kuwa na matumaini mwanzoni.
Haya yalikuwa miongoni mwa mazungumzo muhimu zaidi katika miongo ya hivi karibuni, yakilenga kumaliza mgogoro unaoendelea katika Mashariki ya Kati. Ingawa pande zote zimeashiria kuwa mazungumzo yanaweza kuendelea, tofauti kubwa bado zinaonekana kuwepo.
Kabla ya mazungumzo hayo, kulikuwa na matarajio makubwa kutoka kwa Pakistan na wadau wa kimataifa kwamba huenda yakaleta mwanga wa suluhisho la kudumu. Hata hivyo, changamoto zilizokuwa zikitajwa mapema zilijitokeza wakati wa majadiliano.
Kwa mujibu wa vyombo kadhaa vya habari na wachambuzi, ikiwemo Times of India, masuala yafuatayo yalikuwa miongoni mwa maeneo yenye tofauti kubwa, na huenda yalichangia kukwamisha mazungumzo hayo.
Lebanon, masuala ya kikanda na fidia ya vita
Iran imejaribu kupanua wigo wa mazungumzo kwa kuingiza masuala ya migogoro ya kikanda, ikiwemo Lebanon na makundi kadhaa ya waanamgambo katika eneo la Mashariki ya kati kama Hezbollah (Lebanon), Houthi (Yemen), Hamas (Gaza) na mengine nchini Iraq.
Pia imeibua madai ya fidia ya uharibifu uliotokana na migogoro ya muda mrefu, hatua iliyoonekana kuongeza ugumu wa mazungumzo.
Kwa upande wa Marekani, msisitizo umebaki katika masuala ya nyuklia na usalama wa bahari badala ya ajenda pana ya kikanda.
Mlango wa Hormuz
Mlango wa Hormuz, unaopitisha takribani asilimia 20% ya mafuta duniani, umeendelea kuwa eneo nyeti la mgogoro.
Iran imekuwa ikitafuta nafasi ya kuongeza udhibiti wake juu ya njia hiyo, ikiwemo uwezekano wa kutoza ada kwa meli zinazopita.
Marekani na washirika wake wameendelea kusisitiza umuhimu wa kuhakikisha uhuru wa usafirishaji wa kimataifa katika eneo hilo nyeti.
Ilikuwa sehemu kubwa ya ajenda. Mvutano kuhusu suala la Hormuz ulikuwa umejitokeza hata kabla ya mazungumzo, huku kukiwa na hofu miongoni mwa wadau wa usafirishaji wa kimataifa.
Mpango wa nyuklia wa Iran
Suala la nyuklia linaonekana kubaki kuwa kiini cha mgogoro kati ya pande hizi mbili. Marekani imekuwa ikisisitiza umuhimu wa Iran kutoa dhamira ya wazi ya kutoendeleza silaha za nyuklia.
Ripoti zinaonyesha kuwa Washington ilitaka kuwepo kwa vikwazo vikali zaidi juu ya urutubishaji wa urani pamoja na udhibiti wa teknolojia zinazoweza kutumika katika kutengeneza silaha hizo.
Kwa upande wake, Iran imeendelea kusisitiza kuwa ina haki ya kuendeleza mpango wake wa nyuklia kwa matumizi ya kiraia kama kwa sababau ilitia saini mkataba wa kuzuia na kuenea kwa silaha za nyuklia.
Suala hili limekuwa chanzo cha mvutano kwa muda mrefu na lilikuwa tayari ni kikwazo hata kabla hata ya mazungumzo kuanza.
Vikwazo na mali zilizoshikiliwa
Moja ya maeneo yaliyotajwa kuwa na tofauti kubwa ni suala la vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Iran. Tehran imekuwa ikisisitiza kuondolewa kwa vikwazo hivyo kama sehemu ya makubaliano yoyote.
Pia kulikuwa na madai ya kurejeshwa kwa mali za Iran zilizoshikiliwa nje ya nchi, ikiwa ni pamoja na fedha zilizopo katika mataifa mbalimbali.
Hata hivyo, ripoti zinaonyesha kuwa Marekani haikuonyesha kukubaliana moja kwa moja na masharti hayo, jambo linaloonyesha kuwepo kwa pengo kati ya matarajio ya pande hizi mbili.
Kwa mujibu wa wachambuzi, tofauti hizi zilikuwa tayari zinajulikana kabla ya mazungumzo na ziliendelea kujitokeza wakati wa majadiliano.
Mazingira ya kutoaminiana
Mazungumzo hayo yanatajwa kufanyika katika mazingira yenye mvutano na historia ndefu ya kutokuaminiana kati ya pande hizi mbili.
Ripoti zinaonyesha kuwa kulikuwa na hali ya kupanda na kushuka kwa mvutano wakati wa majadiliano, huku kila upande ukionekana kushikilia msimamo wake.
Wizara ya mambo ya nje ya Iran ilisema 'mazungumzo yalifanyika katika mazingira ya kutoaminiana, kutiliwa shaka na mashaka'.
Kwa mujibu wa wachambuzi, ukosefu huu wa uaminifu ni changamoto ya muda mrefu inayofanya mazungumzo ya aina hii kuwa magumu.
Hali hiyo pia ilionekana hata kabla ya mazungumzo kuanza.
Taarifa hii iemerejea pia mchango wa mwandishi wa masuala ya Diplomasia, Paul Adams.