Christina Koch: Mwanamke wa kwanza kusafiri kwenda mwezini

Muda wa kusoma: Dakika 4

Mwaka wa 1968, Bill Anders, mmoja wa wanamisheni wa Apollo 8, alipiga picha ya dunia ambayo iliandikisha historia, na kuhamasisha kizazi kizima.

Christina Koch alizaliwa miaka 11 baadaye na alipokuwa mtoto aliona bango la "Earthrise", picha maarufu iliyopigwa kutoka obiti ya mwezi ambapo dunia inaonekana kwenye kivuli na mwezi ukiwa mbele yake.

Anasema wakati aliona picha hiyo kwa mara ya kwanza hapo ndipo aliamua kuwa mwanasayansi wa anga.

Jumatano, Aprili tarehe 1, alikua mwanamke wa kwanza kusafiri mwezini akiwa kwenye kikosi cha Artemis II ya NASA.

Alisafiri na wanasayansi wengine watatu, wakiwemo kamanda wa kikosi hicho Reid Wiseman, Jeremy Hansen wa Canada, na Victor J Glover, mwanaume mweusi wa kwanza kusafiri mwezini.

Kikosi hicho kiliandikisha historia ya kusafiri mbali zaidi na dunia kuliko binadamu yeyote katika historia, takriban kilomita 406,000 kutoka duniani.

Koch ameelezea kushiriki kwake katika Artemis II kama "jukumu kubwa," na alisema alihisi "shukrani kubwa kwa wale waliotengeneza njia ya wao kufika huko" na kuandikisha historia.

Kwa yeye, kuwa katika kikosi cha Artemis II ni ndoto iliyotimia.

Katika mahojiano na NASA, alieleza kuwa anatumai misheni yake itawawezesha kizazi kipya kupata uzoefu unaofanana na ule aliopata na kufanya dunia kuwa mahali pa matumaini zaidi, kama walivyofanya kikosi cha Apollo 8 mwaka 1968.

"Ukweli ni kwamba waliochukua picha za mwezi wakati ule walifanya tubadili jinsi tulivyofikiria kuhusu sayari yetu wenyewe."

Misheni ya Artemis II ya NASA ilikuwa ya kihistoria kwa kuwarudisha wanasayansi katika obiti ya mwezi, jambo ambalo halijatokea kwa zaidi ya miaka 50.

Kamanda wa kikosi hicho, Reid Wiseman, alisema katika mkutano na waandishi wa habari kuwa wanapanga kufika katika maeneo ya Mwezi ambayo hayajawahi kuonekana hapo awali na watafanya hivyo wakiwa kwenye chombo chao cha anga, cha Orion, ambacho timu yake ilichagua kukiita Integrity.

"Jina Integrity linaakisi misingi ya kuaminiana, heshima, uwazi, na unyenyekevu wa wanamisheni wote pamoja na wahandisi wengi, mafundi na wanasayansi waliokuwa muhimu kwa mafanikio ya misheni hii," walisema katika taarifa.

Kuvunja rekodi

Christina Koch alizaliwa Grand Rapids, Michigan, na kukulia Jacksonville, North Carolina.

Baada ya kupata shahada katika Fizikia na Uhandisi wa Umeme, Koch alifanya kazi kama mtafiti katika mradi wa Marekani wa Antarctic Program na kama mhandisi wa umeme katika kitengo cha anga katika chuo kikuu cha Johns Hopkins.

Kazi yake ya kuwa mwanasayansi wa anga ilianza mwaka 2013, katika darasa lililokuwa na idadi kubwa zaidi ya wagombea waliowahi kuchaguliwa katika programu ya NASA wanawake 3 na wanaume 4, ikijumuisha rubani wa Artemis II, Victor Glover.

Mwezi Oktoba 2019, pamoja na Jessica Meir, alishiriki katika nafasi ya kipekee ya kuenda angani kwa mara ya kwanza kwa kikosi cha wanawake pekee.

Akikumbuka tukio la kihistoria pamoja na Meir, Koch aliwaambia waandishi wa habari wa NBC "Tulipopewa idhini ya kuondoka ,macho yetu yakakutana."

"Tulijua jinsi wakati huo ulivyokuwa wa kipekee na sitawahi kusahau."

Aliporudi mwanzoni mwa mwaka 2020, aliandikisha historia kwa kukamilisha safari ndefu ya anga aliyowahi kufanya mwanamke, baada ya kutumia siku 328 mfululizo akiwa ISS.

Mbali na maarifa aliyopata kutokana na uchunguzi zaidi ya 200, Koch alileta data muhimu , kama ilivyobainishwa na mwanasayansi wa NASA, Bryan Dansberry.

"Wakati tunaposubiri kwenda mwezini na hatimaye sayari ya Mars, tunahitaji kweli kuelewa athari za muda mrefu wa kukaa angani kwa mwili wa binadamu," Dansberry alielezea.

Koch alikamilisha mizunguko 5,248 wa kuzunguka dunia na kusafiri kilomita milioni 223, sawa na safari ya mizunguko 291 kwenda mwezini kutoka duniani.

"Nina hisia nyingi na ninafuraha sana sasa hivi," aliwaambia waandishi wa habari baada ya kuandikisha rekodi hiyo, akiwa bado amekaa nje ya chombo cha anga, muda mfupi baada ya kutua katika theluji nchini Kazakhstan.

Baadaye alisema kuwa anataka kuhamasisha kizazi kijacho cha watafiti wa anga.

" Kuwa chanzo cha motisha kwa mtu mwingine itakuwa heshima ya kweli."

Tuko pekee yetu

Akijiandaa kwa misheni ya Artemis II, Koch alikusanya maandishi ya mikono kutoka kwa marafiki wa karibu na familia ili aende nayo na kuwa na "uhusiano wa kimwili" na wapendwa wake walioko duniani.

Alieleza kuwa safari hiyo ilikuwa mada ya mazungumzo ya mara kwa mara na mumewe, aliyetaka kujua safari hiyo inafanyika vipi, sehemu za hatari watakazofikia na iwapo ataweza kupumzika.

Lakini pia walizungumza kuhusu mambo mengine kama jinsi wangeweza kuwasiliana.

"Hataweza kunipigia simu kuniuliza kitu fulani kiko wapi kwa nyumba" alisema, akicheka. "Atalazimika kukipata mwenyewe," alisema Koch.

Kazi ya Koch kwenye Artemis II, ilikuwa kushughulikia masuala ya kiufundi na kisayansi kwenye chombo cha Orion, kama vile kuendesha mifumo ya chombo hicho cha anga, na kuhakikisha kwamba kila kitu kinafanya kazi ipasavyo.

Koch alieleza kuwa kikosi hicho kitakuwa na nafasi ya kusoma na kufahamu zaidi kuhusu mwezi kwa undani kwa muda wa saa tatu.

"Jicho la binadamu ni mojawapo ya vyombo bora vya kisayansi tulivyo navyo," alisisitiza.

Koch aliongeza kuwa wanasayansi wa NASA wanafurahia kwamba mwezi umeweza kutazamwa moja kwa moja na wanamisheni hao wanne.

"Tumekuwa tukijiandaa kufanya uchunguzi huo na kujibu ya baadhi ya maswali muhimu zaidi ya kama je tuko pekee yetu"

"Huenda tukaweza kujibu hilo baadaye kwa kusafiri hadi sayari ya Mars, lakini misheni hii inaweza kuwa hatua ya kwanza kwa binadamu kupata jibu hilo."