Jinsi Pakistan ilivyosaidia kusitisha vita kati ya Marekani na Iran

Muda wa kusoma: Dakika 2

Saa chache kabla makubaliano ya kusitisha mapigano kutangazwa kati ya Iran na Marekani, kulikuwa na matumaini ya hatua hiyo kuafikiwa kutoka Pakistan.

Chanzo kimoja kutoka Pakistan kiliambia BBC kuwa mazungumzo hayo yanafanyika kwa kasi sana, huku Pakistan ikijitahidi kuwapatanisha Iran na Marekani.

"Upande wa Pakistan ulijumuisha kundi dogo, hali ilikuwa tete na hatari, ingawa kulikuwa na matumaini ya makubaliano ya kusitisha mapigano kuafikiwa chini ya saa chache ambazo zilikuwa zimesalia"

Pakistan imekuwa mpatanishi kati ya Iran na Marekani katika siku za hivi karibuni, wakipitisha ujumbe kati ya pande zote mbili. Pakistan ina uhusiano wa kihistoria na Iran, huku wakiwa majirani na huchukulia uhusiano wao kuwa wa "kindugu."

Rais Trump alimwelezea mkuu wa jeshi la Pakistan Asim Munir kama mtu "anayempenda" na "anajua mengi kuhusu Iran kuliko mtu yeyote."

"Makubaliano hayatarajiwi." Akizungumza bungeni Jumatano usiku, waziri wa mambo ya nje wa Pakistan, Ishaq Dar, alisema, "hadi jana nilikuwa na matumaini makubwa kuwa mambo yangeendelea vizuri,kabla ya Israel kushambulia Iran siku ya Jumatatu, na Iran kushambulia Saudi Arabia siku ya Jumanne."

Pakistan ilisema kuwa bado inajaribu "kudhibiti mambo kadri inavyoweza."

Mkuu wa Jeshi la Pakistan akizungumza na viongozi wa kijeshi siku ya Jumatano, alisema shambulio dhidi ya Saudi Arabia "linadhoofisha juhudi za kutatua mgogoro huo kwa amani."

Hii ilikuwa lugha kali zaidi ambayo Pakistan imewahi kutumia dhidi ya Iran tangu vita vilipoanza ikionyesha wasiwasi na kukerwa na hatua za Tehran katika vita hivyo.

Pakistan ina mkataba wa ulinzi na Saudi Arabia, ambao unafaa kutekelezwa ikiwa kuna vitisho vya moja kwa moja dhidi ya usalama wa Saudi Arabia.

Usiku wa manane baada ya tishio la Trump, waziri mkuu wa Pakistan alichapisha kwenye mtandao wa X kuwa "juhudi za kidiplomasia zinaendelea, zimeonyesha kuwa na nguvu na uwezo wa kuleta matokeo mazuri katika siku za hivi karibuni."

Waziri huyo pia alimwomba Trump kuongeza muda wa wiki mbili kuruhusu mazungumzo hayo kuendelea na Iran kufungua mlango bahari wa Hormuz.

Balozi wa Iran nchini Pakistan, Reza Amiri Moghdam, pia usiku huo alichapisha kwenye X kuwa "Hatua imepigwa katika wakati huu wa hatari"

Mapema asubuhi, Waziri mkuu wa Pakistan alitangaza kuwa makubaliano ya kusitisha vita yameafikiwa, na kualika pande zote mbili mjini Islamabad siku ya Ijumaa tarehe 10 Aprili, "kuendeleza mazungumzo hayo na kuafikia makubaliano"

"Bado tunaheshimiwa" chanzo kimoja kiliambia BBC, "bado hakuna uaminifu kati ya pande zote mbili licha ya misimamo yao mikali."

Ila Pakistan ikiwa mwenyeji wa mazungumzo hayo, swali la kujiuliza ni iwapo matakwa muhimu za kila pande zitakubalika.

Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula na kuhaririwa na Ambia Hirsi