Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Ni kipi kitafuata baada ya mazungumzo ya amani ya Iran na Marekani kuvunjika?
- Author, Lyse Doucet
- Nafasi, Mwandishi mkuu wa kimataifa, mjini Islamabad
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Saa ishirini na moja hazitoshi kumaliza miaka 47 ya uhasama kati ya Iran na Marekani.
Mazungumzo haya ya kihistoria ya ngazi ya juu yaliyofanyika Islamabad, wakati wa kipindi cha utulivu kilichotokana na wiki kadhaa za mapigano makali, hayakuweza kwa urahisi kuzaa matokeo tofauti.
Kuyaita mazungumzo haya ya muda mrefu kuwa yameshindwa kungepunguza ukubwa wa changamoto zilizopo katika kuziba pengo kubwa la masuala tata, kuanzia mashaka ya muda mrefu kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran hadi changamoto mpya zilizoletwa na vita hii, hususan udhibiti wa Iran juu ya Mlango wa bahari wa Hormuz, kufungwa kwake kukisababisha msukosuko wa kiuchumi duniani.
Ili kufikia makubaliano, pande zote zilihitaji pia kushinda hali ya kutoaminiana iliyojikita kwa kina kati yao.
Siku moja kabla ya mazungumzo hayo, hakukuwa hata na uhakika kuwa pande hizo mbili zingekutana, achilia mbali kukaa pamoja katika chumba kimoja.
Utamaduni wa kisiasa uliodumu kwa muda mrefu umevunjwa.
Swali la dharura sasa ni: nini kinafuata?
Ni kipi kitakachofuata? 40275601
Ni nini kitakachotokea kwa usitishaji mapigano wa wiki mbili wenye utata, ambao umezuia dunia kukumbwa na tishio hatari la Rais wa Marekani Donald Trump la "kuangamiza kizazi kizima" nchini Iran? Je, rais atakuwa tayari kuwarejesha wawakilishi wake mezani kwa mazungumzo?
Tunasikia ripoti kutoka vyanzo vya Islamabad kwamba baadhi ya mazungumzo yaliendelea baada ya Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, kuwasili asubuhi hii, akitangaza kuwa ujumbe wa Marekani uliwasilisha "pendekezo lao la hivi karibuni na bora zaidi."
Hivyo basi, je, Marekani itaongeza mvutano au itaendeleza mazungumzo? Bado haijafahamika kikamilifu kilichotokea nyuma ya milango iliyofungwa kwa ukali katika hoteli ya kifahari huko Islamabad, wakati wa mazungumzo ya usiku kucha.
Maelezo ni machache kuhusu tofauti na mijadala kati ya pande hizo mbili, ambayo iliwezeshwa na wapatanishi wa Pakistan, mawasiliano na wataalamu na washauri, na pia, kulingana na Vance, "makumi" ya simu kwa Trump mwenyewe.
Makamu wa rais alizungumzia "lengo kuu" la Marekani wakati wa mkutano mfupi na waandishi wa habari mapema leo asubuhi.
"Tunahitaji kuona dhamira ya wazi kwamba [Iran] haitafuti silaha za nyuklia, na kwamba haitafuti vifaa vitakavyoiwezesha kupata silaha hizo kwa haraka," alisema.
Katika duru ya mwisho ya mazungumzo mwezi Februari, kabla ya mashambulizi ya kijeshi kuanza tena, Iran ilitoa mapendekezo mapya, ikiwa ni pamoja na kupunguza akiba yake ya kilo 440 za urani iliyoboreshwa hadi asilimia 60 kiwango kilicho karibu hatarishi na daraja la silaha.
Hata hivyo, bado inasisitiza "haki" yake ya kuendelea na urutubishaji huo, na haiko tayari kuachana na akiba hiyo, ambayo sasa inasemekana imefichwa kwa kina chini ya vifusi vya mashambulizi ya mabomu ya Marekani na Israel mwaka uliopita.
Pia imekataa mara kwa mara wito wa kufungua Mlango wa Hormuz ili kuruhusu mtiririko huru wa mafuta, gesi, na bidhaa nyingine muhimu bila kufikiwa kwa makubaliano mapya.
Marekani na Iran zote ziliwasili Islamabad zikiwa na kujiamini kuwa ndizo zenye uwezekano mkubwa wa kushinda vita hivi.
Na ziliingia katika mazungumzo zikijua kuwa, zikishindwa, kulikuwa na chaguo la kuendelea na vita bila kujali mateso yanayoongezeka kwa raia wao na dunia iliyoshtushwa na gharama za vita hii pana.
Kulikuwepo pia kile ambacho Dk. Sanam Vakil wa Chatham House alikieleza kama "uelewa mdogo wa kisaikolojia kuhusu adui na kile ambacho maridhiano halisi yanahitaji."
Vance alizungumzia habari njema "tumekuwa na mazungumzo mengi yenye uzito" na habari mbaya: "hatujafikia makubaliano."
Alitangaza kuwa hii ni "habari mbaya zaidi kwa Iran kuliko kwa Marekani."
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei, alikosoa "madai yaliyopitiliza na yasiyo halali" ya Marekani kupitia ujumbe kwenye mtandao wa X.
Vivyo hivyo, Spika wa Bunge la Iran, Mohammad Bagher Ghalibaf, aliyeongoza ujumbe wa Iran, aliandika kuwa "upande wa pili hatimaye umeshindwa kupata imani ya ujumbe wa Iran katika duru hii ya mazungumzo."
Iran inaonyesha utayari wa kuendelea na mazungumzo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Pakistan, Ishaq Dar, amezihimiza pande zote kudumisha usitishaji mapigano ulio dhaifu na amesema wataendelea na juhudi za kuhimiza mazungumzo, mtazamo unaoshirikiwa na miji mingine mikuu yenye wasiwasi kuhusu hali hiyo.
Mustakabali wa vita Iran ni upi?
Ikiwa historia ni mwongozo, mara ya mwisho Iran ilipofikia makubaliano ya nyuklia na Marekani na mataifa mengine yenye nguvu mwaka 2015, ilichukua miezi 18 ya maendeleo ya vipindi na kuvunjika mara kwa mara.
Trump ameweka wazi kuwa hataki kushiriki katika mazungumzo ya muda mrefu. Vance hapo awali ameonya kuwa Marekani haitakubali iwapo Tehran itajaribu "kutudanganya."
Donald Trump amependekeza kuweka kiziuzi cha kijeshi katika mlango wa bahari wa Hormuz nchini wa Iran kufuatia mazungumzo kufurukuta, sawa na hatua zilizoshuhudiwa kabla ya kuondolewa madarakani kwa Rais wa zamani wa Venezuela, Nicolas Maduro, mwezi Januari.
Huenda akidokeza suala hilo hilo, mwishoni mwa wiki, wakati mazungumzo yakiendelea, afisa mwandamizi wa jeshi la Marekani alitoa taarifa akitangaza kuanzishwa kwa njia salama ya baharini kupitia usafishaji hai wa njia ili kufungua tena Mlango wa Hormuz.
Haijulikani iwapo hatua hii inaweza au itachukuliwa sambamba na kurejelewa kwa mashambulizi ya mabomu ya Marekani dhidi ya Iran.
Je, ni vita vya subira?
Je, kuongezeka kwa mvutano kutoka Washington kumeondolewa kwenye ajenda- angalau kwa sasa? Na je, Donald Trump ameanza kuchukua mkakati wa subira na wa kimkakati zaidi?
Baadhi ya wataalamu wanasema ndiyo, na wanaamini kuwa Iran bado ina nguvu ya kujadiliana dhidi ya Marekani, hasa kutokana na kuendelea kuvurugika kwa biashara ya kimataifa, kuendelea kuwepo kwa uongozi wa Iran pamoja na washirika wake, na uwepo wa akiba ya urani iliyoboreshwa.
Shirika la habari la Tasnim lilinukuu chanzo kikisema: "Iran haina haraka ya kufanya mazungumzo." Chanzo hicho kiliongeza kuwa "mpira uko upande wa Marekani."
"Funzo kubwa hapa ni kwamba matumizi ya nguvu ya moja kwa moja hayajawasukuma Wairani kufikia hatua ya kuhisi wanalazimika kutoa masharti," anasema Azadeh Moshiri, mwandishi wa BBC wa Asia Kusini.
Athari za vita kuendelea
Hatimaye, mwandishi mkuu wa masuala ya kimataifa wa BBC, Liz Doost, anasema rais wa Marekani anapaswa kufahamu mambo mawili. "Kwanza, [kurudi vitani] hakutakuwa maarufu ndani ya nchi," anasema.
Donald Trump atafahamu athari za ndani za mzozo wowote wa kimataifa wa muda mrefu, hasa iwapo gharama ya maisha itaendelea kupanda, huku uchaguzi wa katikati ya muhula wa mwezi Novemba ukikaribia.
Kiwango cha hivi karibuni cha bei za wanunuzi, kinachopima gharama ya kikapu cha bidhaa na huduma, kimefikia kiwango chake cha juu zaidi katika karibu miaka miwili nchini Marekani ishara ya tahadhari kuhusu kinachoweza kutokea.
"Pili, haitafanya kazi," anaongeza Liz Doost. "Iran itajibu kwa mapambano."
Mwandishi wa habari wa Pakistan, Kamran Yousaf mmoja wa mamia ya waandishi wa habari waliokesha usiku kucha kufuatilia hali hiyo huku taarifa zikiwa chache, alisema duru hiyo "haikuwa ushindi wa wazi, lakini pia haikuwa anguko kamili."
Dunia inasubiri uamuzi wa mwisho, hasa wa Trump.