Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Marekani na Iran zashindwa kufikia makubaliano

Nchi hizo, zilfanya mazungumzo marefu ya saa 21 huko Islamabad, Pakistan, lakini kwa mujibu wa Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, pande hizo mbili hazikuweza kukubaliana juu ya masharti ya mwisho.

Moja kwa moja

Na Yusuph Mazimu

  1. Pakistan yataka Marekani na Iran kuheshimu usitishaji mapigano baada ya kushindwa kukubaliana

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Pakistan imetoa wito kwa Marekani na Iran kuendelea kuheshimu makubaliano ya muda ya kusitisha mapigano kufuatia mazungumzo ya amani yaliyofanyika Islamabad.

    Katika taarifa iliyotolewa, Pakistan imesisitiza kuwa ni “muhimu sana” kwa pande zote mbili kuendelea kusimamia ahadi yao ya kusitisha mapigano, licha ya kushindwa kufikia makubaliano ya mazungumzo kuhusu mzozo wao.

    Taarifa hiyo imeeleza matumaini kuwa Marekani na Iran wataendeleza mazungumzo kwa nia njema ili kufikia amani ya kudumu na ustawi si tu katika eneo la Mashariki ya Kati bali pia kimataifa.

    Pakistan, ambayo imekuwa mpatanishi mkuu wa mazungumzo hayo, imesema itaendelea kuwezesha mazungumzo kati ya pande hizo mbili katika siku zijazo, ikilenga kusaidia kupunguza mvutano na kusaka suluhisho la kudumu.

    Nchi hizo zilikaa kwa saa 21 usiku wa kuamkia leo kwa saa za Afrika Mashariki, lakini zilishindwa kufikia makubaliano ya kusitisha vita kutokana na kila upande kusema masharti ya mwezie hayakuwa yanakubalika.

  2. Marekani na Iran zashindwa kufikia makubaliano baada ya mazungumzo ya kihistoria Pakistan

    Marekani na Iran zimeshindwa kufikia makubaliano ya kumaliza vita baada ya mazungumzo ya ngazi ya juu yaliyofanyika Islamabad, Pakistan.

    Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, amesema licha ya mazungumzo marefu yaliyodumu kwa saa 21, pande hizo mbili hazikuweza kukubaliana juu ya masharti ya mwisho.

    Amesema Iran “haikukubali masharti ya Marekani”, huku akisisitiza kuwa Washington inahitaji kuona dhamira ya wazi kutoka Tehran ya kuacha kabisa mpango wa kutengeneza silaha za nyuklia.

    Kwa upande wake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran imesema mazungumzo hayo yalikuwa “ya kina”, lakini ikaishutumu Marekani kwa kutoa “matakwa makubwa na yasiyo halali”.

    Mazungumzo hayo yalikuwa yakisimamiwa na Pakistan, huku Waziri Mkuu wake, Shehbaz Sharif akitajwa kupongezwa kwa juhudi za upatanishi.

    Licha ya kushindwa kufikia makubaliano, Donald Trump amesema matokeo hayo “hayajaleta tofauti” kwa Marekani, akisisitiza kuwa nchi yake bado ipo katika nafasi ya ushindi.

    Mazungumzo hayo yalikuwa yakilenga kufikia makubaliano ya kusitisha vita vinavyoendelea huko Mashariki ya Kati, lakini hadi sasa hatma ya mgogoro huo bado haijulikani.

  3. Hujambo na karibu katika habari zetu za moja kwa moja leo April 12, 2026