Je, Trump atahatarisha wanajeshi wake kwa kufunga Mlango Bahari wa Hormuz?

Muda wa kusoma: Dakika 4

Siku ya Jumamosi, timu ya wana diplomasia ikiongozwa na Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance ilijaribu kusaka makubaliano ya kukomesha vita vya Marekani na Iran, lakini ilishindwa.

Rais Donald Trump akachukua hatu mpya. Aliandika kupitia Truth Social, kwamba Marekani itaweka "kizuizi cha majini" dhidi ya Iran. Aliongeza, "Mtu yeyote anayelipa ushuru haramu katika Mlango-Bahari wa Hormuz hatapita kwenye mlango huo."

Pia alisema Marekani itaendelea kuondoa mabomu ya chini ya maji kutoka Mlango-Bahari wa Hormuz ili kuhakikisha meli za washirika wake zinapita salama. Aliongeza kuwa jeshi la Marekani liko tayari kuanza tena mashambulizi dhidi ya Iran wakati unaofaa.

Trump alisema maendeleo fulani yalipatikana katika mazungumzo ya saa 20 huko Islamabad, lakini Iran haikukubali ombi la Marekani la kuachana na mpango wake wa nyuklia.

Hata hivyo, afisa wa Marekani aliyehusika katika mazungumzo hayo alisema mkwamo katika mazungumzo na Iran haukuwa tu kwenye suala hili, pia kulikuwa na orodha ndefu ya mambo ambayo pande hizo mbili hawakukubaliana.

Ikiwa ni pamoja na udhibiti wa Iran wa Mlango-Bahari wa Hormuz na uungaji mkono wake kwa makundi ya wawakilishi katika eneo hilo, kama vile waasi wa Houthi huko Yemen na Hezbollah huko Lebanon.

Jeshi la Marekani liko hatarini?

Je, shughuli za kuondoa mabomu baharini zitaongeza hatari ya mashambulizi ya Iran dhidi ya meli za Jeshi la Wanamaji la Marekani? Marekani itafanya nini kwa meli zinazotoa ushuru kwa Iran?

Je, Marekani itatumia nguvu dhidi ya meli za kigeni zinazopuuza kizuizi cha Jeshi la Wanamaji la Marekani? Nchi kama China zinazotegemea mafuta ya Iran zitafanya nini? Je, hatua hii, inayolenga kupunguza chanzo kikuu cha mapato ya Iran, itaongeza zaidi bei ya mafuta?

Majibu ya maswali haya hayako wazi.

Siku ya Jumapili, Kamandi Kuu ya jeshi la Marekani ilitangaza kwamba kizuizi cha jeshi la majini kitazuia meli zote kutoka na kwenda bandari za Iran, tofauti na pendekezo la awali la Trump.

"Sioni jinsi kizuizi katika mlango-bahari kitailazimisha Iran kufungua mlango huo," Seneta Mark Warner wa Virginia, mjumbe mwandamizi wa chama cha Democratic katika Kamati ya Ujasusi ya Seneti, aliiambia CNN.

Akizungumza katika kipindi cha CBS cha "Face the Nation," Mbunge wa Republican wa Ohio, Mike Turner, ambaye hadi mwaka jana alikuwa mwenyekiti wa Kamati ya Ujasusi ya Baraza la Wawakilishi, alisema njia hiyo ni mbinu ya kutatua hali ya sasa ya Hormuz.

Wiki iliyopita, kabla ya Iran na Marekani kukubaliana kusitisha mapigano kwa wiki mbili na mazungumzo ya ana kwa ana, Trump alijikuta katika hali ngumu.

Aliahidi kuzidisha mashambulizi ya Marekani, na kusababisha uharibifu wa muda mrefu kwa miundombinu ya kiraia ya Iran, kuzidisha mgogoro wa kibinadamu, na kuharibu zaidi uchumi wa dunia.

Wamarekani wengi hawaungi mkono vita hivi, na vimewakasirisha baadhi ya wafuasi wake ambao walimsikia akiahidi kuepuka vita vya muda mrefu katika nchi za kigeni hasa Mashariki ya Kati.

Kulingana na kura ya maoni ya CBS, Wamarekani wengi (59%) wanaamini vita hivi vinaenda vibaya kwa Marekani.

Wengi wanaamini malengo makuu ya Marekani, kama vile kuuweka Mlango-Bahari wa Hormuz wazi, kutoa uhuru zaidi kwa watu wa Iran, na kubomoa kabisa mpango wa nyuklia wa Iran, bado hayajafikiwa.

Karibu wiki moja imepita na licha ya madai ya Marekani ya ushindi, changamoto zinazomkabili Rais bado hazijabadilika.

Kamari ya Trump ina gharama

Akizungumza na Fox News Jumapili asubuhi, Trump alisema, mwishowe Iran itaipa Marekani "kila kitu" inachotaka. Pia alisema bei ya mafuta inaweza kubaki ilipo au kupanda katika miezi ijayo, lakini anaamini uchumi wa Marekani utaendelea kuwa imara.

Hii ni kamari.

Huku uchaguzi wa katikati ya muhula mwezi Novemba ukikaribia, ikiwa itabainika amefanya makosa, Chama chake cha Republican kinaweza kupata hasara kubwa katika uchaguzi huo.

Vita dhidi ya Iran vinaingia mwezi wake wa pili na usitishaji mapigano wa wiki mbili uko karibu kumalizika. Bado hakuna uhakika kipi kifuatacho ikiwa hakutakuwa na makubaliano ya kupata amani.

Mgogoro huu sasa umekuwa mtihani mkubwa kwa Trump na pengine kwa chama chake pia. Kwa upande mmoja. Iran imeonyesha ina uwezo nwa kuhimili mashambulizi yasiyokoma ya Marekani na Israeli.

Kwa upande mwingine, Trump ameonesha ana uwezo wa kuhimili shinikizo la kiuchumi na kisiasa ambalo vita hii vimesababisha.

Huu ni muhula wa mwisho kwa Trump, kwa maana nyingine hategemei kugombea tena kwa mujibu wa Katiba ya sasa, lakini Republican kama chama kitaendelea kuwepo na bila shaka maamuzi na sera za Trump zinaweza kuathiri chama hicho huko mbeleni na hasa katika uchaguzi ujao.