Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jinsi utamaduni unavyoendelea kuathiri wanawake Afrika
''Muacha mila ni mtumwa'', ni kauli ambayo umekuwa ukiisikia hasa kama ni mzaliwa au ni jirani ya familia za pwani.
Neno hilo mara nyingi hutumiwa kuelekeza mtu afuate mila zake na huhusishwa na fahari, utambulisho, na urithi wa jamii.
Lakini mwaka 2026, swali linalozidi kuwa muhimu ni: je, baadhi ya mila hizi zinawalinda wanawake au zinawadhuru kwa njia moja au nyingine?
Kwenye maeneo mbalimbali duniani, si tu vijijini au maeneo yaliyosahaulika, bado kuna desturi zinazodhibiti miili ya wanawake, zinawanyima uhuru wao wa maamuzi, na wakati mwingine kuacha majeraha yasiyofutika katika nafsi na mwili.
Na katika makala haya tunaeleza mambo ambayo kimila yanaonekana kuwa muhimu lakini katika jicho lingine linaondoa fahari ya mwanamke kama binadamu.
1. Ukeketaji
Kuna mila na desturi tano zenye ukatili zinazoumiza wanawake na wasichana.
Ya kwanza kabisa ni ukeketaji.
Ukeketaji ni kitendo cha kuondoa kwa sehemu au kwa jumla sehemu za siri za mwanamke bila sababu za kitabibu.
Ukeketaji wa wanawake (FGM) unafanywa zaidi kwa wasichana wachanga kuanzia utotoni hadi umri wa miaka 15.
FGM ni ukiukaji wa haki za binadamu za wasichana na wanawake.
Matibabu ya matatizo ya kiafya yanayotokana na FGM yanakadiriwa kugharimu mifumo ya afya dola za Marekani bilioni 1.4 kwa mwaka, idadi inayotarajiwa kuongezeka ikiwa hatua za dharura hazitachukuliwa kuelekea kukomeshwa kwake.
Zaidi ya wanawake na wasichana milioni 230 duniani wamepitia ukatili huu. Unasambaa zaidi katika nchi kama Kenya, Sudan, Misri, na Ethiopia.
Ukeketaji mara nyingi huchukuliwa kuwa sehemu muhimu ya kulea msichana, na njia ya kumtayarisha kwa utu uzima na ndoa. Hii inaweza kujumuisha kudhibiti jinsia yake ili kukuza ubikira kabla ya ndoa na uaminifu katika ndoa.
Hata hivyo una madhara mengi kwa mwili wa mwanamke anapokeketwa. Ni pamoja na kufariki dunia, usumbufu wakati wa kujifungua, uchungu wakati wa kujamiiana na pia kukumbwa na unyanyapaa.
Nchini Kenya, ukeketaji ni kosa la jinai.
Adhabu yake ni kifungo cha angalau miaka mitatu au faini kubwa.
Takwimu zinaonyesha kupungua kwa viwango vya kitaifa katika miongo ya hivi karibuni, lakini katika baadhi ya jamii bado unaendelea.
Hata hivyo, mwenendo mpya wa "kutabibishwa" kwa ukeketaji unatia hofu.
Wahudumu wa afya wanafanya kitendo hicho kwa siri katika nyumba au kliniki binafsi ili kukwepa mkono wa sheria.
Hili linatoa taswira ya uhalali wa kitabibu kwa tendo ambalo ni ukiukwaji wa haki za binadamu na lina madhara ya kudumu kimwili na kisaikolojia.
2. Kunyoosha au Kupiga Matiti
Kuchoma matiti, au "kupunguza ukubwa wa matiti kwa kupiga au kuchoma", ni desturi ya kitamaduni ambapo matiti ya wasichana wachanga hupigwa au kuchomwa kwa kutumia vitu vyenye moto au vyenye nguvu, kwa lengo la kuchelewesha ukuaji wao au kuficha dalili za mwanzo wa ujana, kulingana na Shirika la Afya la Afrika (Africa Health Organization – AHO).
Shirika hilo linaeleza kuwa jamii zinazotekeleza desturi hii zinaamini itapunguza mvuto wa wasichana kwa wanaume, hivyo kuwalinda dhidi ya unyanyasaji, ubakaji, utekaji nyara, ndoa za utotoni zenye kulazimishwa, na pia kuhakikisha wanabaki shuleni.
Hata hivyo, mashirika ya afya na makundi ya haki za binadamu yanasisitiza kuwa desturi hii ni aina ya ukeketaji wa kimwili unaoharibu ustawi wa kijamii na kisaikolojia wa mtoto, na unaochangia ongezeko la idadi ya wasichana wanaoacha shule.
Umoja wa Mataifa (UN) unasema kuwa kuchoma matiti kunawaathiri wanawake takriban milioni 3.8 barani Afrika, na kuorodheshwa kama mojawapo ya uhalifu wenye taarifa chache zaidi unaohusiana na ukatili wa kijinsia.
Takriban asilimia 25 hadi 50 ya wasichana katika nchi kama Cameroon na baadhi ya sehemu za Nigeria wanakabiliwa na desturi hii, kulingana na data iliyochapishwa katika jarida la Annals of Medical Research and Practice.
Wasichana wengi hupitia changamoto za kunyonyesha mtoto wanapojifungua, maumivu makali, kuungua, maambukizi, na makovu ya kudumu.
Miili yao hugeuzwa kuwa uwanja wa mapambano dhidi ya hofu ya kijamii.
3. Utumwa wa kijinsia wa kingono
Katika baadhi ya maeneo ya Ghana, Togo, na Benin, bado kuna desturi inayojulikana kama trokosi.
Wasichana hutolewa kwenda katika madhabahu ya kidini kama kafara ya makosa yanayodaiwa kufanywa na wanafamilia wao.
Huko, hulazimishwa kufanya kazi ngumu na mara nyingi kukumbana na unyanyasaji wa kijinsia kwa miaka mingi. Desturi hii huwanyima wanawake fursa za kuendelea na elimu, saikolojia yao na hata ustawi wa kimwili.
Ingawa baadhi ya nchi zimepiga marufuku desturi hii, utekelezaji wake ni dhaifu.
4. Vipimo vya ubikira
Vipimo vya ubikira ni uchunguzi wa kimwili unaodai kuthibitisha kama mwanamke au msichana amewahi kufanya ngono. Hakuna msingi wa kisayansi wa kipimo hiki.
Mchakato huo unaojulikana kama ''two finger'', mwanamke huingiza vidole kwa sehemu zake za siri ili kubaini kama bado kuna kizinda na jamii nyingi huamini hukosekana pale msichana anaposhiriki ngono. Hata hivyo, kuna baadhi ya wanawake ambao huzaliwa bila kizinda au kizinda chao huzibuliwa wanaposhiriki baadhi ya michezo.
Mashirika ya Umoja wa matifa yameeleza kuwa iankiuka utu wa mwanamke na kisayansi haina maana yeyote mwanamke anapokosa kizinda.
Wanawake wengi wanakabiliwa na athari hasi kuanzia za kimwili hadi za kiakili.
Hii ni pamoja na mfadhaiko, msongo wa mawazo na pia wengine huwa na wasiwasi maisha yao tote baada ya kukaguliwa iwapo ni bikra.
''Baadhi ya wasichana hufikiria kujitoa uhai wanapofanyiwa uchunguzi, na sio sawa kwani hizo jamii zinaamini mwanamke kujihusisha na ngono ni hadi aingie kwa ndoa na inamnyima mwanamke uhuru kama binadamu'', anasema daktari Simelela alipokuwa akizungumza na gazeti la Nation nchini Kenya.
Desturi hii bado inafanyika katika baadhi ya maeneo ya Kenya haswa Mombasa, Afrika Kusini na Misri.
5. Mila za unyanyasaji kwa wajane
Katika baadhi ya jamii za Kenya, Nigeria, Uganda, Zambia, Ghana, na Tanzania, mjane hulazimishwa kupitia taratibu za udhalilishaji baada ya kifo cha mume wake.
Baadhi ya kuondokewa na mwenza wako, mwanamke hujipata na changamoto nyingi na kujiuliza maswali jinsi ya kuishi bila mumewe. Lakini maumivu huzidishwa zaidi na baaadhi ya mila zinazotaka wajane wafanye tambiko ishara ya kuonyesha alimuenzi mume wake.
Katika eneo la Ukerewe nchini Tanzania kama ilivyo katika maeneo mengi ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, hali ya kuwa mjane huonekana kama uchafu wa kiroho. Inaaminika kwamba ikiwa mjane hatapitia taratibu za kutakaswa, roho ya mume wake aliyefariki itaisumbua familia yote iliyofiwa, na kuleta mikosi au hata vifo.
Ili kuzuia hali hiyo, desturi inaelekeza kwamba mjane lazima alale kimwili na mwanaume mjane kutoka ukoo wa marehemu mume wake, na baadaye alale na mwanaume mwingine kutoka nje ya kijiji, mtu ambaye hana uhusiano wowote naye wala na familia yake.
Sio Tanzania tu, hata Kenya wajane hukabiliwa na madhila chungu nzima.
Kwa mfano kaunti ya Nyamira nchini Kenya, kuna mwanamke ambaye alifiliwa na mumewe na wakati wa mazishi alipokataa kurusha mchanga ishara ya kumuaga kama alivyoshurutishwa na mila za familia hiyo alipigwa na kukejeliwa na matusi ya nguoni.
Vile vile nchini Kenya, Jamii ya Waluo humtaka mjane anyoe nywele zake na wengine kuamrishwa wakubali kuolewa na kaka yake mume wake.
Kenya haiko peke yake katika vita hivi. India imeharamisha mila ya wajane ya kibaguzi katika majimbo kadhaa na inatoa pensheni ya serikali na usaidizi wa makazi kwa wajane. Nepal
Rwanda ilifanya mageuzi ya urithi wake na sheria za ardhi ili kulinda haki za wajane kwa mali na urithi baada ya mauaji ya kimbari. Togo ilitunga sheria zinazoadhibu mila ya kitamaduni ya utakaso na kutekeleza ulinzi wa wajane chini ya kanuni zake za adhabu.
Nchi hizi zinaonyesha kuwa madhara yanayohusiana na wajane si suala la kitamaduni la kuvumiliwa, bali ni ukiukwaji wa haki za binadamu unaopaswa kukomeshwa.
Taswira pana
Duniani kote, mwanamke mmoja kati ya watatu atakumbana na ukatili wa kimwili au kijinsia katika maisha yake.
Vilevile, nchi nyingi bado zinaruhusu ndoa za utotoni, jambo linalokatisha ndoto za elimu, fursa za kiuchumi na maisha bora ya wasichana. Kwa wanawake milioni 676 wanaoishi karibu na maeneo yenye migogoro, mifumo ya kisheria mara mingi haipo, na wahalifu wanaendelea kuendesha matendo bila kuadhibiwa.
Kuhakikisha haki halisi kunahitaji hatua thabiti na mshikamano wa kimataifa. Sheria zinazolinda wanawake na wasichana dhidi ya ukatili, ubaguzi na unyonyaji lazima zitekelezwe kikamilifu, huku mahakama zikihakikisha kuwa kila mwanamke ana imani na ulinzi.
Utamaduni unaweza kuwa nguzo ya utambulisho. Lakini pale unapogeuka kuwa chombo cha maumivu, unahitaji kuthubutu kubadilishwa.
Mapambano si tena ya kuthibitisha kuwa mila hizi zipo. Ni ya kuhakikisha kwamba hazipo tena.