Iran na Marekani kukutana Pakistan usiku; nani wanahudhuria na nini kiko mezani?

Muda wa kusoma: Dakika 3

Mazungumzo ya ngazi ya juu kati ya Marekani na Iran yanatarajiwa kufanyika Islamabad, Pakistan, ( saa 9 usiku) kuamkia kesho kwa saa za Afrika Mashariki, katika juhudi za kusaka amani baada ya kusitisha mapigano kwa wiki mbili huko Mashariki ya Kati.

Mazungumzo hayo, ambayo Pakistan inasimamia kama mpatanishi, yanakuja katika mazingira ya sintofahamu kubwa, huku mapigano na mvutano vikiendelea, na mustakabali wa usitishaji mapigano ukiwa bado dhaifu.

Ikulu ya White House imesema mazungumzo yataendelea na hakuna makubaliano ya mwisho yaliyofikiwa.

Msemaji wa White House Anna Kelly amesema Marekani haitafanya majadiliano kupitia vyombo vya habari, lakini Rais Donald Trump anaamini mpango uliopo unaweza kuwa msingi wa amani ya kudumu Mashariki ya Kati.

Watakaohudhuria Islamabad

Ripoti zinaonyesha mkutano huu utahusisha watu wazito na viongozi wakubwa, ili kurahisha maamuzi ya haraka na kufikia makubaliano.

Kwa upande wa Marekani ripoti zinasema itawakilishwa na ujembue utakaoongozwa na Makamu wa Rais, JD Vance, mshauri wa karibu wa Rais Jared Kushner, na mjumbe maalum Steve Witkoff. Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Makamu wa Rais kushiriki moja kwa moja katika mazungumzo ya aina hii kuhusu Iran na mashariki ya kati.

Kw aupande wa Iran yenyewe inatarajiwa kuwakilishwa na viongozi wa ngazi ya juu akiwemo Spika wa Bunge, Mohammad Bagher Qalibaf na Waziri wa Mambo ya Nje Abbas Araghchi.

Pakistan, kupitia Waziri Mkuu Shehbaz Sharif, imekuwa ikicheza nafasi ya upatanishi, ikialika pande zote mbili kukutana Islamabad kwa lengo la kufikia makubaliano ya muda mrefu zaidi. Sharif anatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya kuongoza mkutano huo.

Mgogoro bado ni tete

Mazungumzo haya yanakuja wakati ambapo bado kuna tofauti za tafsiri kuhusu makubaliano ya kusitisha mapigano, hususan kama yanahusisha operesheni za kijeshi katika Lebanon. Marekani na Israel wamesema Lebanon haikuwa sehemu ya makubaliano hayo, wakati Pakistan awali ilieleza vingine.

Rais Trump pia ameripotiwa kushinikiza Israel kupunguza mashambulizi nchini Lebanon, akisema ni muhimu kuepuka kuvuruga mazungumzo ya amani.

Mlango wa Hormuz, unaopitisha takriban asilimia 20 ya mafuta ya dunia, unatarajiwa kuwa mojawapo ya hoja kuu katika mazungumzo hayo.

Ripoti zinaonyesha mvutano umeongezeka kuhusu iwapo Iran inaweza kudhibiti au kutoza ada kwa meli zinazopita, jambo ambalo Marekani inaliona kama tishio kwa usalama wa usafirishaji wa mafuta duniani.

Trump amesisitiza kuwa mlango huo lazima ubaki wazi ili makubaliano ya kusitisha mapigano yaweze kudumu, huku akionya dhidi ya hatua yoyote ya kuufunga

Matarajio ya mkutano na masharti 10 ya Iran

Ingawa pande zote zinaonyesha nia ya mazungumzo, matarajio sio makubwa sana kutokana tofauti kubwa za kisera zinazoendelea kuonyeshwa, hasa kuhusu vikwazo, urani, na usalama wa kikanda.

Hata hivyo, Rais Trump ameeleza matumaini ya kufikiwa kwa makubaliano, akisema kuna uwezekano wa "mkataba wa amani" kupatikana iwapo pande zote zitajadiliana kwa nia njema.

Kulingana na televisheni ya kitaifa ya Iran, Iran imetoa masharti 10 kuelekea mkutano huo, masharti yanayojumuisha:

  • Kusitishwa kwa vita nchini Iraq, Lebanon na Yemen.
  • Vita dhidi ya Iran visitishwe kikamilifu bila vikwazo vya muda.
  • Kusitishwa kwa vita vyote ukanda huo.
  • Usalama na uhuru wa mlango bahari wa Hormuz.
  • Kufunguliwa kwa Mlango bahari wa Hormuz.
  • Iran kufidiwa ili kujenga miundo mbinu iliyoharibiwa.
  • Kuondolewa vikwazo vya kiuchumi.
  • Kuachiliwa kwa fedha na mali za Iran zinazozuiliwa na Marekani.
  • Iran kutomiliki silaha za nyuklia.

Ingawa upande wa Marekani umeonyesha dalilia za kukubali baadhi ya masharti, bado si rahisi kukubalika yote. Iwapo yote yatakubaliwa, makubaliano ya kudumu ya kusitisha mapigano yanaweza kufikiwa kirahisi.

Imetafsiriwa na Beldeen Waliaula na kuhaririwa na Y.Mazimu