Mitazamo sita ya lishe ambayo hufai kuamini

    • Author, Tai Ibitoye
    • Nafasi, BBC Food
  • Muda wa kusoma: Dakika 3

Kama mtaalam wa lishe mimi hukumbana na habari potovu kuhusu lishe, haswa kutoka kwa watengeneza maudhui kwenye mitandao ya kijamii.

Wacha nikufafanulie baadhi ya misemo na mitazamo potovu zinazoenea kwenye mitandao ya kijamii.

Je, nafaa kuacha kula vyakula vya wanga (Carbohydrates)?

Kuacha vyakula vya wanga kunaweza kuchangia kupunguza uzito wa mwili, ila kwa mara nyingi huchangia kupoteza kiwango cha maji mwilini kuliko mafuta.

Ila kuacha kula vyakula vya wanga kabisa huwa suala gumu kuzingatia au kumudu.

Vyakula vya wanga ni lishe muhimu na chanzo kikuu cha kuipa mwili nguvu na huchangia kwa 50% kuipa mwili nguvu.

Kwa hivyo badala ya kuondoa vyakula vya wanga kabisa kwenye lishe yako, ni bora kuchagua nafaka inayofaa kama mchele wa kahawia, tambi, mboga, matunda pamoja na viazi.

Vyakula hivi vitakuzuia usihisi njaa kwa haraka na pia huongeza nyuzinyuzi kwenye lishe yako.

Je, sukari kutoka kwa matunda ni hatari?

Fructose ni sukari inayopatikana asili ndani ya matunda yote na haizingatiwi kama "sukari huru".

Matunda ni vyanzo bora vya vitamini, madini, phytochemicals, na nyuzi zote ambazo ni muhimu kwa afya yako. Zaidi ya hayo, kula matunda pamoja na mboga inasaidia katika kupunguza hatari ya kupata shinikizo la damu na magonjwa ya moyo.

Je, lishe za kuondoa sumu mwilini husaidia kusafisha mwili?

Lishe nyingi za kuondoa sumu mwilini, zinaweza kuwa hatari na hazina ushahidi thabiti wa kisayansi.Faida za lishe hizo zinazotolewa zinaweza kudumu kwa muda mfupi tu.

Mwili tayari una mifumo yake ya asili ya kusafisha mwili, utumbo, ini, na figo hufanya kazi hii.

Kwa hivyo, vyakula, vinywaji, au virutubisho maalumu vya kuondoa sumu mwilini si lazima.

Baadhi ya lishe za kuondoa sumu mwilini zinahimiza ulaji wa matunda na mboga na kupunguza vyakula vyenye mafuta mengi , chumvi, na sukari, lakini pia zinashauri kuondoa makundi yote ya vyakula,hii inaweza kusababisha upungufu wa lishe unaohitajika mwilini.

Badala yake, kula lishe yenye vyakula mbalimbali, kupata usingizi wa kutosha, kuwa makini na unywaji wa pombe, usivute sigara, kupumua hewa safi, huimarisha afya ya mwili.

Je, bidhaa za mboga zina afya zaidi?

Lishe ya mboga inaweza kuwa na virutubisho na kusaidia kuchangia mtu kuwa na maisha yenye afya.

Baadhi ya vyakula vya mboga huwa zimesindikwa na zinaweza kuwa na kiasi kikubwa cha mafuta, chumvi, na sukari.

Kwa hivyo ni bora kusoma maelekezo ya virutubisho na kuangalia viambato vilivyoongezwa kabla ya kununua chakula.

Je, bidhaa za maziwa ni muhimu katika lishe?

Bidhaa za maziwa zina protini nyingi sana, kalsiamu, aidini, fosforasi, potasiamu, na vitamini B.

Baadhi ya bidhaa za maziwa zilizochachushwa, kama maziwa ya mtindi zina probiotic, kwa hivyo pia zinaweza kusaidia afya ya utumbo.

Bidhaa za maziwa zina sukari asili inayoitwa lactose. Hata hivyo, haizingatiwi kama "sukari huru" kwa sababu ipo pamoja na virutubisho vingine muhimu.

Isipokuwa ikiwa una mzio au kushindwa kustahimili maziwa, hakuna haja ya kuacha kutumia bidhaa za maziwa.

Iwapo unachagua kuepuka kutumia bidhaa za maziwa hakikisha bidhaa unazotumia zimeimarishwa na aidini, kalsiamu, na vitamini B.

Je, virutubisho vya mtu binafsi na virutubisho vya ziada huimarisha kinga ya mwili?.....

Kuna virutubisho vingi muhimu vinavyosaidia mfumo wetu wa kinga kufanya kazi vizuri, lakini vinahitaji kufanya kazi pamoja. Usizingatie virutubisho vya aina moja kama zinki au vitamini C tu, virutubisho vingine pia vina nafasi muhimu.

Lishe yenye usawa inayojumuisha matunda, mboga, nafaka kamili, bidhaa za maziwa , karanga, mbegu, nyama, samaki, na protini za mimea kama maharagwe na kunde ni vya kutosha kusaidia mfumo wa kinga.

Baadhi ya watu wanaweza kuhitaji virutubisho vya ziada, kama kina mama wajawazito na wale wanatumia lishe ya mboga pekee .

Kupata usingizi wa kutosha, kufanya mazoezi ya mwili mara kwa mara, na kudhibiti msongo wa mawazo pia ni muhimu sana.

Wakati mwingine ukiona "taarifa ya kiafya" kwenye mitandao ya kijamii, zingatia ni nani anayesema na ikiwa sayansi kweli inaiunga mkono taarifa hiyo.

Taarifa hii haikusudiwi kuchukua nafasi ya uchunguzi wa matibabu au ushauri wa lishe unaotolewa na mtaalamu wa lishe.