Nani kipa bora zaidi duniani? Je ni Raya, Neuer au Maignan?

    • Author, Marissa Thomas
    • Nafasi, BBC Sport journalist
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Ilikuwa kama simulizi ya makipa wawili katika Ligi ya Mabingwa Ulaya.

David Raya alisifiwa kuwa "kipa bora duniani" na baadhi ya wachezaji wenzake baada ya kiwango chake bora katika ushindi wa 1-0 wa Arsenal dhidi ya Sporting CP.

Wakati huo huo, Manuel Neuer alionyesha kiwango cha hali ya juu akiwa na Bayern Munich dhidi ya Real Madrid, na hata kuibua mjadala wa kurejea kwake katika timu ya taifa ya Ujerumani licha ya umri wa miaka 40.

Hali hii imeanzisha mjadala mpya: nani ndiye kipa namba moja duniani, hasa wakati Kombe la Dunia linakaribia?

BBC Sport inatathmini madai ya baadhi ya wagombea.

David Raya - Arsenal

Tangu kuanza kwa msimu uliopita, Raya amecheza mechi 23 katika mashindano hayo, akiruhusu mabao 12 pekee na kuokoa takribani mabao 9 yaliyokuwa hatarini kufungwa.

Ameongoza kwa kuwa ana mechi zaidi ya 22 ambazo hakuruhusu goli miongoni mwa makipa wote katika ligi tano kubwa barani Ulaya, katika mashindano yote.

Aliteuliwa kuwania Tuzo ya Yashin ya mwaka 2025, tuzo inayotolewa kila mwaka kwa kipa bora duniani katika hafla ya Ballon d'Or lakini hakufanikiwa kumaliza katika nafasi tatu za juu.

Hata hivyo, bado ni mmoja wa makipa wachache kwenye orodha hii ambaye si chaguo la kwanza katika timu yake ya taifa.

Unai Simon, ambaye ameichezea maisha yake yote ya klabu Athletic Bilbao, ametajwa hivi karibuni na kocha wa timu ya taifa ya Hispania Luis de la Fuente kuwa chaguo lisilopingika langoni.

Kwa upande mwingine, beki wa zamani wa Arsenal na timu ya taifa ya England, Lee Dixon, alimuelezea Raya kama kipa wa kiwango cha dunia akizungumza na BBC Radio 5 Live. Aliongeza kuwa bado ana safari ya kufikia hadhi ya David Seaman, lakini ana uwezo mkubwa wa kuongoza safu ya ulinzi na kuaminiwa na wachezaji wenzake.

Manuel Neuer - Bayern Munich

Licha ya kustaafu soka la kimataifa Agosti 2024, Manuel Neuer bado anaonyesha ushindani mkubwa akiwa na umri wa miaka 40.

Katika mechi ya Ligi ya Mabingwa dhidi ya Real Madrid, aliandika rekodi ya kucheza mechi yake ya 136 akiwa na Bayern Munich na akaonyesha kiwango cha hali ya juu kana kwamba amerudi enzi zake bora.

Nguli wa makipa Peter Schmeichel, akichambua mchezo huo kwa CBS Sports, alisema Neuer "alicheza moja ya mechi bora zaidi kuwahi kuona," na kwamba kuokoa kwake dhidi ya Kylian Mbappe ni "huenda ndiyo ukipa bora zaidi msimu huu."

Ingawa hajawahi kuteuliwa kuwania Tuzo ya Yashin, Neuer ana mafanikio makubwa, akiwa ametwaa mataji 12 ya Bundesliga, mataji mawili ya Ligi ya Mabingwa, pamoja na Kombe la Dunia akiwa na Ujerumani.

Ni Iker Casillas pekee aliyewahi kucheza mechi nyingi zaidi za Ligi ya Mabingwa akiwa na klabu moja (149 na Real Madrid), huku Neuer akilingana na Lionel Messi kwa mechi 136 akiwa na Barcelona.

Baada ya kiwango chake bora mjini Madrid, kumekuwa na wito wa arejee katika timu ya taifa ya Ujerumani, ambako kwa sasa Oliver Baumann ndiye chaguo la kwanza langoni.

Thibaut Courtois - Real Madrid

Thibaut Courtois kwa sasa hayupo uwanjani kutokana na jeraha la paja, na kukosekana kwake kunaathiri kwa kiasi kikubwa kikosi cha Real Madrid.

Tangu msimu uliopita, amecheza mechi 23 za Ligi ya Mabingwa na kufanikisha kuokoa mashuti 105, akiwa na wastani wa asilimia 78.2 ya kuokoa mashuti.

Hata hivyo, ameruhusu mabao 29 katika kipindi hicho, mabao 17 zaidi kuliko David Raya.

Kocha wake Alvaro Arbeloa amewahi kumtaja kama "kipa bora zaidi katika historia," na Courtois ameonyesha ubora wake kwa kushinda mataji mawili ya Ligi ya Mabingwa na matatu ya La Liga akiwa Real Madrid pamoja na taji moja la La Liga akiwa Atletico Madrid.

Kipa huyo wa Ubelgiji, aliyewahi kung'ara akiwa Chelsea kabla ya kuhamia Real Madrid, pia alitwaa Tuzo ya Yashin mwaka 2022.

Emiliano Martinez - Aston Villa

Bingwa wa Kombe la Dunia 2022 akiwa na Argentina, Emiliano Martinez ameendelea kung'ara kwa kushinda tuzo nyingi za ukipa tangu ushindi huo.

Alitwaa Tuzo ya Yashin mwaka 2023 na 2024, na pia alichaguliwa kuwa Kipa Bora wa FIFA mwaka 2022 na 2024.

Kocha wake Unai Emery amewahi kumtaja kama "kipa bora zaidi duniani."

Katika msimu uliopita wa Ligi ya Mabingwa, Martinez alicheza mechi 12, akifanya saves 49 na kuwa na wastani wa asilimia 80 ya kuokoa mashuti.

Alisson - Liverpool

Wakati Liverpool ilipopata ushindi wa 1-0 dhidi ya Paris Saint-Germain katika mchezo wa kwanza wa hatua ya 16 bora ya Ligi ya Mabingwa msimu uliopita, kulikuwa na sababu moja iliyo wazi kabisa:

Alisson Becker.

Kipa huyo wa Brazil alikuwa katika kiwango cha juu sana jijini Paris, na kocha wake Arne Slot aliambia TNT Sports baada ya mechi kuwa, "Sidhani kama kuna kipa aliyewahi kucheza katika kiwango hiki ambacho ni cha kawaida kwa sababu yeye ndiye bora duniani."

Tangu kuanza kwa msimu uliopita wa Ligi ya Mabingwa, Alisson ana wastani wa kuokoa mashuti wa asilimia 86.1 katika mechi 12, akiwa alizuia magoli 37.

Alitwaa Tuzo ya kwanza kabisa ya Yashin mwaka 2019, na kumaliza wa pili mwaka 2022 na 2025. Pia alikuwa imara sana langoni wakati Liverpool ilipotwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa mwaka 2019.

Gianluigi Donnarumma - Manchester City

Tangu ajiunge na Manchester City mwezi Septemba, Gianluigi Donnarumma amekuwa kipa namba moja asiye na mpinzani chini ya kocha Pep Guardiola.

Guardiola alisema kuhusu Donnarumma: "Ana urefu mkubwa na mwili imara. Makipa wote wanapaswa kuipa timu kujiamini na uongozi, na yeye ana uwepo mkubwa hasa kwenye mechi kubwa."

Hata hivyo, wakati mwingine Donnarumma hupata changamoto kutokana na nguvu na ushindani wa Ligi Kuu England, hasa kwenye mipira ya kona.

Tangu kuanza kwa Ligi ya Mabingwa msimu uliopita ambapo alitwaa ubingwa akiwa na Paris Saint-Germain ameruhusu mabao 25 katika mechi 24, na amepangua magoli tisa.

Alitwaa Tuzo ya Yashin mwaka 2021 na 2025, lakini bado hajawahi kushiriki Kombe la Dunia akiwa na Italia baada ya taifa hilo kushindwa kufuzu kwa mashindano hayo mara tatu mfululizo.

Mike Maignan - AC Milan

Mchezaji aliyerithi nafasi ya Gianluigi Donnarumma katika AC Milan baada ya kuhamia Paris Saint-Germain ni Mike Maignan na tangu hapo amejijengea hadhi ya kuwa miongoni mwa makipa bora duniani akiwa Italia.

Alianza safari yake kupitia akademi ya PSG, lakini alipokuwa Lille ndipo alipojitambulisha zaidi kimataifa.

Katika msimu wake wa kwanza akiwa Milan, aliisaidia klabu hiyo kutwaa ubingwa wa Serie A (Scudetto) kwa mara ya kwanza baada ya miaka 11, huku akiwa kinara wa kupangua mabao na asilimia ya kuokoa mashuti.

"Kwa sababu ya uthabiti wake, yeye ndiye bora zaidi duniani," alisema kipa wa zamani wa Brazil Dida akizungumza na La Repubblica. "Kisha ningemfuatisha Donnarumma, na mwingine ninayemkubali ni Raya wa Arsenal."

Kutajwa kwa heshima - Yassine Bounou

Yassine Bounou alicheza Uropa kwa mara ya mwisho miaka mitatu iliyopita akiwa na Sevilla na tangu wakati huo amehamia ligi ya Saudi ya Al-Hilal.

Alishika nafasi ya tatu kwa Kombe la Yashin mwaka wa 2023 baada ya kuisaidia Morocco kuwa taifa la kwanza la Kiafrika na Kiarabu kufika nusu fainali katika Kombe la Dunia.

Bounou alikuwa na ushawishi mkubwa wakati Morocco ilipoandaa Kombe la Mataifa ya Afrika 2025, akiokoa mikwaju miwili ya penalti kwenye nusu fainali dhidi ya Nigeria.

Taifa lake limekabidhiwa taji la Afcon baada ya Shirikisho la Soka Afrika kutengua matokeo ya fainali hiyo, ingawa Senegal imekata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Ambia Hirsi