Wanyama wanaofugwa nyumbani wanavyozikwa kifahari nchini Kenya

- Author, Mariam Mjahid
- Nafasi, Mwandishi BBC Swahili
- Muda wa kusoma: Dakika 8
Mapema asubuhi moja nilipotembelea mtaa wa Karen, jijini Nairobi Kenya, nilijipata katika mazingira ambayo sio ya kawaida.
Kisa? Ni eneo ambalo liko kando lililo na utulivu wa kipekee - utulivu unaobeba simulizi zisizosikika kwa masikio ya haraka: makaburi ya wanyama wanaofugwa nyumbani.
Nilipoingia ndani ya makao ya Shirika la Kulinda na Kutunza Wanyama cha Kenya (KSPCA), nilikutana na paka waliokuwa wakifanya tantarira zao, huku mbwa wakibweka, ishara ya kuwaambia wenyeji kuna mgeni. Nilielekezwa hadi katika lango kuu la rangi ya buluu lililokuwa limeandikwa 'Crematorium' ikimaanisha ni eneo la kuchoma maiti.
Sikulitia maanani hadi pale nilipoona makaburi madogo yaliyopangwa kwa ustadi, upepo ukivuma huku ukipeperusha maua yaliyokauka na kugusa mawe yenye majina yaliyoandikwa kwa uangalifu, ''Snow, spooky, Mkombozi,'' kila jina likiwa ushuhuda wa uhusiano.
Salaaala! Nilimaka! Sio makaburi tulioyazoea ya binadamu ni ya wanyama wanaofugwa nyumbani.
Maandishi kwa kila jiwe yanaashiria mengi, baadhi yao ni ya familia moja yamezikwa kwando ya mwengine kama vile Sweet Daisy na Mzee wake Spike, Goofy na Chubby Patel pia walikuwa ni wa damu moja.
Sio rahisi kutofautisha kaburi hili limezikwa paka, mbwa au Kasuku.
Ni kawaida kwa binadamu kuwazika wapendwa wao lakini kwanini tuwazike paka na mbwa,? niliuliza Wangari Kariuki ambaye ni msimamizi katika kituo cha KSPCA.
''Maisha ni uhalisia, haijalishi ni paka ama mbwa ana uhai, ni vile tu sisi binadamu huwa tunajipa umuhimu. Lakini wamiliki wa wanyama wanaofugwa nyumbani huamini kama vile binadamu wanahaki ya kuzikwa vizuri basi pia wanyama wanapaswa kufanyiwa vivyo hivyo pindi wanapofariki'', ananiambia Wangari Kariuki, msimamizi wa kituo kinacholinda wanyama wanaofugwa nyumbani nchini Kenya.
Awali waliotaka kuwalaza wanyama wao wapendwa katika eneo hili walilazimika kukabiliana na gharama dola 5000.

Na japo bei sio ya mwananchi wa kawaida, kutokana na idadi ya watu wanaotaka kuaga wanyama wao kwa ustaarabu bei haijawazuia kutimiza hilo kwa idadi ya wateja imezidi kuongezeka tangu kituo hiki kuanzishwa mwaka 1985 na kwa sasa eneo hili limejaaa.
Wamiliki wa wanyama wanaofugwa nyumbani wameongezeka tangu Kutokana na idadi ya watu wengi kufuga wanyama hawa, pia hitaji la mahali pa kuwazika limeongezeka maradufu.
Kulingana na mkurugenzi wa makao ya Shirika la Kulinda na Kutunza Wanyama nchini Kenya (KSPCA), Wangari Kariuki ameanzisha njia mbadala ya kukhitari viumbe hao rafiki wa binadamu kwa ustaarabu.
''Lazima uwe mwanachama wa kspca ili mnyama wako afanyiwe ibada ya mwisho'' ananielezea Wangari.

Shughuli ya kuchoma mizoga inafanywaje?

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kama vile tu binadamu hutayarishwa kuchomwa anapofariki dunia, pia kwa wanyama kama paka na mbwa ni vivyo hivyo.
uchomaji wa miili yao (cremation) umeanza kuwa sehemu ya utamaduni unaochipuka nchini Kenya.
Kwa bahati, nilipata paka kwa jina Max akitayarishwa kuchomwa baada ya wamiliki wake kumleta afanyiwe shughuli hiyo ya kuanza safari ya kwenda jongomeo.
Hapa, mambo yalianza kwa paka huyo aliyekuwa amegandishwa baada ya kuwekwa kwenye jokovu akiletwa na kuwekwa juu ya meza iliyokuwa imetandikwa shuka jekundu.
Mara yangu ya kwanza nilipoona paka huyo akiwa amekafiniwa na shuka lililopendekezwa na mmiliki wake niliingiwa na hofu pamoja na shauku.
Moses Wambua, mtayarishaji wa mzoga huo ananiambia huku akionekana ni jambo ambalo ana uzoefu nalo kuwa wamiliki wa 'Max' walimuagiza awafanyie ibada ya mwisho kisha akamuekea maua ya waridi kando yake, ''Wamiliki wa Max kutokana na majonzi waliyokuwa nayo walishindwa kuvumilia kushuhudia dakika za mwisho za mwanafamilia wao duniani na kuniagiza nimfanyie ibada na kumuwekea maua ya waridi kabla ya kumchoma ''kwa hadhi ya juu'' anasema Moses.
Haikuwa rahisi kwangu kushuhudia yote haya. Kadri muda ulivyosonga akimfanyia paka huyo ibada ya mfu niliona tofauti kidogo.
Hakika, niliposhuhudia shughuli hii, dhana ya "kufuga mnyama" inapoteza maana yake ya zamani. Kinachoonekana hapa si umiliki, bali uhusiano wa kifamilia.
Haikuchukua muda tayari alikuwa amewekwa kwenye chemba cha kuchoma na kuelezwa kuwa itachukua muda wa saa mbili kabla ya mmiliki kupata majivu ya paka wao. Alinihakikishia kuwa utaratibu huo ni wenye ustaarabu mno na hauna tofauti kubwa na binadamu wanapochomwa.
''Mmiliki wa mnyama atapatiwa jivu baada ya kuchomwa kwa kiumbe hicho na pia cheti ambacho kitamhalalishia kusafiri kwa ndege na jivu hilo'', anasema Moses.

''Sikuamini binadamu anaweza kugharamika kwa sababu ya mnyama''

Kwa wengi bado wanadhani hii ni ndoto, la hasha ni mambo kwa ushahidi. Nikamuuliza Moses, watu wanaomiliki viumbe hawa hugharamika kiasi gani ili wafanyiwe haya ya maajabu?
Kwa msisimko aliniambia ''gharama hulingana na uzani wa mnyama. Paka hana uzani mkubwa ukilinganisha na mbwa lakini mmiliki wa mnyama atalipa kuanzia shilingi dola $100 hadi $270 ili mnyama wake azikwe kwa ustaarabu''.
''Nikafikiria..pesa zote hizo kwa mnyama?, nilijiuliza maswali balagha''.
Nadhani aliniona nikitafakari akaniambia ''usifikirie kwa misingi ya pesa, wanawachukulia kama rafiki, mtiifu na jamaa wao kama vile binadamu uhangaikia damu yao'', aliniambia kunihakikishia kuwa idadi ya watu wanaogharamika imeongezeka mara dufu tangu mwaka 2025.
Majonzi ya kuondokewa na mnyama

Lakini nyuma ya takwimu na mabadiliko haya, kuna simulizi za watu binafsi, zinazogusa moyo na kubeba ukweli usiofichika.
Nilikutana na Victoria Soo, mwanamke ambaye anapenda kufuga paka lakini kwa sasa hamu hiyo imepungua.
Ananisimulia jinsi yeye na familia yake walivyokuwa na paka kwa jina Ella', alimchukulia kama mmoja wa watoto wake na hata rafiki wa watoto wake.
"Alikuwa rafiki yangu wa kila siku. Niliporudi nyumbani, alikuwa wa kwanza kunipokea. Nilimchukulia kama mtoto wangu na hata watoto wangu walimpenda sana. Ella alikuwa paka mrembo na kila mtu alimpenda'', anasema Victoria.
Anakumbuka siku ya tukio kwa uzito usiofichika. Sauti yake ilitetemeka, si kwa udhaifu, bali kwa uzito wa kumbukumbu.
"Ella hakuwa paka wa kawaida," alianza, macho yake yakitazama mbali kana kwamba yanafuatilia kivuli cha rafiki aliyepotea. "Alikuwa rafiki yangu wa kila siku. Niliporudi nyumbani, alikuwa wa kwanza kunipokea. Ukimya wa nyumbani sasa… haujawahi kuwa ule ule tena."
Kifo cha Ella hakikuja kwa utaratibu wa kawaida. Kilikuwa cha ghafla, chenye maswali mengi kuliko majibu.
"Ninahisi alipewa sumu na jirani yangu ambaye hakupenda paka," alisema kwa msisitizo wa uchungu. "Huwezi kuelezea tu namna alivyobadilika ghafla. Kuna mambo hayako sawa."
Kuhusu mgogoro wa jirani na paka huyo ni dai ambalo BBC hatujalithibitisha.
Ananieleza hakuwa na mtu wa kumkimbilia paka huyo alipogaagaa akikata roho asijue la kufanya.
''Mimi na watoto wangu tulilia hadi tukatoa machozi'', anaendelea kunieleza.
"Watu wengi hawataelewa. Watasema 'ni paka tu'. Lakini kwangu, ilikuwa ni hasara halisi. Nilihuzunika kama mtu aliyepoteza ndugu. Maumivu niliyoyapata hadi sasa sina nguvu ya kufuga paka mwingine", anasema Victoria.
Katika maumivu hayo, alilazimika kufanya uamuzi, jinsi ya kumuaga Ella. Kama wamiliki wengine wengi wa kisasa, alitafuta njia yenye heshima.
"Sikutaka tu kumtupa au kumzika kiholela. Niliamua kufanya kitu cha mwisho kwa heshima yake. Nilichimba kaburi nikiwa na watoto wangu, tukamzika karibu na nyumba yetu na tukaweka maua juu ya kaburi lake", anafungua simu huku akinionyesha uhusiano wa karibu aliokuwa na paka wake kupitia picha.
''Sio paka wakula panya, ni rafiki anayekutoa msongo wa mawazo''

Mtaalamu wa afya ya wanyama katika kliniki ya City Paws, Muthoni Nyokabi aliiambia BBC swahili kuwa mabadiliko haya yanatokana na uelewa mpana zaidi wa nafasi ya wanyama katika maisha ya binadamu.
"Zamani paka walifugwa kwa kazi za kuwinda panya," alieleza. "Lakini leo, wanachukua nafasi ya kuwa wenza wa kihisia. Hii inamaanisha wanahitaji matunzo bora, lishe kamili, si mabaki ya chakula kama ilivyozoeleka katika baadhi ya jamii."
Vile vile, mtaalam amependekeza kuwa wanaoamua kufuga wanyama wanapaswa kuhakikisha wanyama hao wanapata chanjo kila mwaka na kuwatafutia matibabu wanapoona hali ya afya ya wanyama wao inadhoofika.
Aliongeza kwa msisitizo:
"Kumtunza mnyama si anasa tena, ni wajibu. Na jinsi unavyomtunza akiwa hai, ndivyo pia unavyopaswa kumheshimu anapofariki."
Mtaalamu huyo ambaye ni msichana wa umri kati ya miaka 26 anatueleza kuwa kizazi cha Gen z kinabadilisha mtazamo kuhusu ufugaji wanyama akiwataja kuwa wanawachukulia kama '' rafiki asiye bagua na kuhukumu ukilinganisha na marafiki wa kibinadamu''.
''Paka anafaa kupata chanjo ya kila mwaka, kuoshwa, kukatwa kucha na pia siku hizi anachukuliwa kama rafiki asiyebagua miongoni mwa vijana'', Muthoni aliiamba BBC.
Kadiri jua linavyochomoza juu ya makaburi yale, likiangazia majina yaliyoandikwa kwa hisia, simulizi hizi zinaendelea kuishi- si tu kama kumbukumbu za wanyama waliofariki dunia, bali kama ushahidi wa mabadiliko ya moyo wa binadamu.















