Jinsi Iran Ilivyogeuza Mlango wa Hormuz kuwa silaha yenye nguvu zaidi duniani

.

Chanzo cha picha, NurPhoto/Getty images

Muda wa kusoma: Dakika 4

Vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran, vimedumu kwa takriban siku 40, na sasa vita hivyo vimegeuka kutoka kuizuia Iran kutengeneza silaha za nyuklia hadi kuitaka ifungue mlango bahari wa Hormuz.

Vita hivyo vilipoanza, vilikuwa vya kutaka kubadilisha utawala wa Iran, na mashambulizi mengi ya Israel na Marekani yalikuwa yakiwalenga viongozi wakuu wa taifa hilo.

Iran ilijibu kwa kuzishambulia kambi za kijeshi za Marekani katika mataifa ya Ghuba kwa makombora na ndege zisizo na rubani, na vita vilipozidi kutanuka, Tehran iliamua kuvuruga usafiri wa baharini kwa kuzuia meli kupita katika Mlango wa Bahari wa Hormuz.

Hatua hiyo imeipa Marekani shinikizo kubwa pamoja na washirika wake wanaotegemea mafuta na gesi ambazo husafirishwa kupitia mlango huo wa bahari.

Jeshi la Iran la Revolutionary Guard, liliona kuwa kudhibiti mlango huo wa bahari, kutaipa Iran nguvu ya kimkakati, kuliko kutumia njia ya zamani ya kujibu mashambulizi.

Iran imetishia uchumi wa dunia, na kuilazimu Marekani kubadili mtazamo wake, na sasa kutaka kufunguliwa kwa mlango wa bahari wa Hormuz umegeuka kuwa lengo kuu la vita hivyo.

Ingawa Iran imetishia awali kuwa ikishambuliwa itafunga mlango huo wa habari, tishio hilo halijawahi kutekelezwa kikamilifu kama ilivyofanyika sasa. Katika vita vya Iraq na Iran, meli za mafuta zilishambuliwa ila mlango huo wa bahari haukufungwa.

Sasa maafisa wakuu wa Iran na viongozi wa vikosi vya usalama wanajadili jinsi wanafaa kudhibiti mlango huo wa bahari katika siku za usoni. Bunge la Iran kupitia tume ya usalama wa taifa, wameandaa mswada wa kulazimisha meli zote kupitia mlango huo wa bahari.

Mbunge mmoja alisema, Iran inaweza kutoza ada ya dola moja kwa kila pipa tatu ya mafuta inayosafirishwa kupitia mlango huo wa bahari.

Picha ya ushindi

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Shirika la habari la kitaifa la Iran, ilitoa taswira kuwa wameshinda vita hivyo baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano kutangazwa.

Ubalozi wa Iran nchini Kuwait ulichapisha video yenye mada "Wakati ushindi wa mwenyezi mungu unapokuja" kwa heshima ya kiongozi mkuu wa awali Ayatollah Ali Khamenei.

Hii ni nadharia ambayo imesambaa nchini Iran kuwa wameshinda vita hivyo kwa kukataa ushawishi wa mataifa ya kigeni.

Naibu rais wa taifa hilo pia aliunga mkono nadharia hiyo kwa kusema hii ni ushindi wa Khamenei ambaye aliuawa siku ya kwanza ya vita hivyo.

Jeshi la Iran pia limerekodi hasara kubwa , huku uchumi wa taifa hilo ukiwa umeathirika baada ya miaka mingi ya kuwekewa vikwazo na Marekani.

Kufunguliwa kwa mlango bahari wa Hormuz, bado ndio lengo kuu katika mazungumzo ya kusitisha vita kati ya Marekani na Iran.

Iran siku ya Jumatano ilionya kuwa meli itakayopita katika mlango huo wa bahari bila idhini ya jeshi la Revolutionary Guard, watashambuliwa.

Naibu Waziri wa mambo ya kigeni wa Iran Saeed Khatibzadeh aliambia BBC kuwa taifa lake litakuwa linatoa "ulinzi" wa meli zinazopita eneo hilo na kusisitiza kuwa mlango huo wa bahari umekuwa wazi kwa maelfu ya miaka hadi Marekani ilipoamua kuishambulia Iran.

Ila alisema kuwa mlango huo utakuwa wazi kabisa "iwapo marekani itasitisha mashambulizi yake"

Hatibzadeh alisema Iran itazingatia "kanuni za kimataifa na sheria za kimataifa." Hata hivyo, alibainisha kuwa mlango huo wa Hormuz haupo kwenye maji ya kimataifa, na kwamba usalama wa meli zinazopitia eneo hilo kunategemea "nia njema ya Iran na Oman."

Mlango bado unajadiliwa chini ya sheria za kimataifa za baharini na Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Sheria ya Bahari (UNCLOS), ambao unalenga kuhakikisha usafiri salama wa meli za kiraia baharini.

Mfano mbaya

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Hatua inayofuata kwa Iran ni gani?

Mswada uliowasilishwa katika bunge la Iran wa kudhibiti mlango huo una vipengele tisa.

Moja ya vifungu inasema kwamba "meli za adui hazitaruhusiwa kupita." Iran itatoa huduma za usafiri na itahitaji kampuni za meli kuilipa Iran na kufungua akaunti katika benki za Iran. Pia meli zitahitajika kutangaza mzigo zinazobeba

Huu ni mswada tata sana na bado haujapigiwa kura.

Ikiwa Iran itajaribu kutoza ada kwa meli zinazopita katika Mlango wa Hormuz, swali kuu ni kama Marekani, nchi za Magharibi, na washirika wa kikanda watakubali hatua hiyo.

Ikiwa Iran itafaulu, hii itakuwa ushindi mkubwa wa kimkakati unaoonyesha uwezo wake wa kudhibiti mojawapo ya njia muhimu zaidi za baharini duniani.

Hata hivyo, hatua kama hiyo ina hatari ya kuleta matokeo mabaya na kusababisha Marekani, washirika wake, wanachama wa NATO, na mamlaka za kikanda kuungana dhidi ya Iran, na hivyo kuchochea majibu ya pamoja ya kidiplomasia, kiuchumi, na hata kijeshi.