Picha za satelaiti zilivyofichua ukubwa wa mashambulizi ya Israel huko Lebanon

Miji na vijiji vya kusini mwa Lebanon vinaripotiwa kubomolewa kupitia uharibifu unaofanywa na Israel, kulingana na picha za setilaiti na video zilizochunguzwa na BBC Verify.
Uchambuzi wa BBC Verify umegundua kuwa zaidi ya majengo 1,400 yameharibiwa tangu tarehe 2 Machi, kwa kuzingatia ushahidi wa picha uliohakikiwa.
Hii ni sehemu ndogo tu ya picha ya jumla ya uharibifu unaosababishwa na mashambulizi ya anga na ubomoaji, kwa sababu kuna upatikanaji mdogo wa taarifa za moja kwa moja kutoka maeneo ya vita pamoja na upungufu wa picha za setilaiti. Hivyo, kiwango halisi cha uharibifu huenda ni kikubwa zaidi.
Ushambuliaji wa majengo haya unafuatia agizo la Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz, la tarehe 22 Machi la "kuharakisha uharibifu wa nyumba za Lebanon" zilizo karibu na mpaka wa Israel, likitumia "mfano wa Gaza" kama sehemu ya kampeni dhidi ya Hezbollah.
Uharibifu wa kimfumo wa miji na vijiji hivi huenda ukachukuliwa kama uhalifu wa kivita, wataalamu wa sheria za kimataifa waliiambia BBC Verify.
Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limesema kuwa linafanya kazi kwa kufuata Sheria za Vita na haliruhusu uharibifu wa mali isipokuwa pale ambapo kuna ulazima wa kijeshi usioepukika.
Pia lilibainisha, bila kutoa ushahidi, kwamba Hezbollah imeweka miundombinu ya kijeshi ndani ya maeneo ya raia katika eneo hilo.
Tarehe 2 Machi, kundi la kijeshi linaloungwa mkono na Iran, Hezbollah, lilirusha makombora na ndege zisizo na rubani kuelekea Israel kama kulipiza kisasi kwa kuuawa kwa kiongozi mkuu wa Iran mwanzoni mwa vita kati ya Israel na Marekani.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Jeshi la Ulinzi la Israel lilijibu kwa mashambulizi ya anga kote Lebanon, likilenga kile lilichosema kuwa ni miundombinu ya Hezbollah, na baadaye likaanzisha uvamizi wa ardhini kusini mwa Lebanon.
Msemaji wa IDF awali alitoa agizo kwa raia wa Lebanon wanaoishi karibu na mpaka kuondoka tarehe 2 Machi. Siku chache baadaye, agizo hilo la kuondoka lilipanuliwa hadi kwa wanaoishi kusini mwa Mto Litani, takribani kilomita 30 (maili 20) kutoka mpaka, na baadaye likapanuliwa zaidi hadi wale wanaoishi kusini mwa Mto Zahrani, umbali wa takribani kilomita 40 kutoka eneo la mpaka.
Tarehe 16 Machi, IDF ilisema wanajeshi wake wameanza operesheni ya ardhini dhidi ya Hezbollah, kundi la kisiasa na kijeshi la Waislamu wa Shia, kusini mwa Lebanon.
Zaidi ya watu milioni 1.2 wanakadiriwa kuwa wamehama makazi yao nchini Lebanon, ikiwa ni pamoja na 820,000 kutoka kusini, kulingana na takwimu za Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Uratibu wa Masuala ya Kibinadamu (OCHA).
Ilisema kuwa vita nchini Lebanon vimewalazimisha watu wengi kukimbilia maeneo ya kaskazini zaidi au kuvuka kwenda Syria.
Wizara ya afya ya Lebanon inasema zaidi ya watu 2,000 wameuawa tangu vita kuanza.
Mamlaka za Israel zilisema kuwa wanajeshi 13 na raia wawili wameuawa na Hezbollah katika kipindi cha wiki sita zilizopita.
Miji na vijiji vya milimani mpakani mwa Lebanon sasa ni vigumu kutambulika. Zamani vilijulikana kwa mitaa yake inayopinda iliyopambwa na majengo ya mawe yakitazama mabonde mapana, lakini video zilizothibitishwa sasa zinaonesha jinsi maeneo hayo yamegeuka kuwa ya kijivu kutokana na vumbi na mabaki ya milipuko.
Mpango wa Katz wa eneo la "usalama" linalodhibitiwa na Israel, linaloanzia mpakani hadi Mto Litani, ungeshika takribani asilimia 10 ya eneo la Lebanon.
Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu alisema kuwa lengo lake ni "kuzuia tishio la uvamizi".
Kwa kutumia picha za video zilizothibitishwa na uchambuzi wa picha za satelaiti zinazopatikana, BBC Verify imegundua ushahidi wa ubomoaji unaodhibitiwa na Israel katika takribani miji na vijiji saba vya mpakani.
Mji wa Taybeh, ulioko takribani kilomita 4 (maili 2.4) kutoka mpakani, umekumbwa na uharibifu mkubwa zaidi kutokana na mashambulizi. Video 11 zilizothibitishwa zinaonesha sehemu nzima za mji huo zikilipuliwa kwa wakati mmoja.
Ulinganisho wa picha za satelaiti zilizopigwa tarehe 28 Februari na 11 Aprili unaonesha kuwa zaidi ya majengo 400, yakiwemo msikiti, yamesambaratishwa na kuwa vifusi.
Wakati huohuo, katika mji wa Khiam na vijiji vya Qouzah, Deir Seryan, Markaba na Aita al-Shaab, video nyingine zilizothibitishwa zinaonesha milipuko iliyopangwa ikipiga majengo kadhaa kwa wakati mmoja.
Tumegundua kuwa zaidi ya majengo 460 yalipigwa Aita al-Shaab pekee. Pia, mashine za kuchimba na magari ya kivita yanaonekana kwenye picha za satelaiti za kijiji hicho, kulingana na Tony Reeves, mwanzilishi wa kampuni ya uchambuzi wa kijasusi MAIAR.
Katika mji wa pwani wa Naqoura, mashambulizi yanayofanywa na Israel pia yameharibu makao makuu ya kikosi cha kulinda amani cha Umoja wa Mataifa kusini mwa Lebanon.
Kandice Ardiel, msemaji wa Kikosi cha Muda cha Umoja wa Mataifa nchini Lebanon (UNIFIL) kilichoko katika makao hayo makuu, alisema ameona uharibifu wa mara kwa mara wa majengo kadhaa kwa wakati mmoja tangu mwanzoni mwa Aprili.
Uchambuzi wetu wa picha za satelaiti unaonesha kuwa takribani majengo 100 yamesambaratishwa na kuwa vifusi huko Naqoura katika wiki za hivi karibuni.
Ardiel alisema kuwa sehemu kubwa ya majengo yaliyo mkabala na makao makuu ya UNIFIL sasa yameharibiwa, akielezea "kiwango cha uharibifu" katika Naqoura kama "cha kuhuzunisha sana". Aliongeza: "Haya si majengo tu, yanawakilisha jamii."
Uharibifu wa makusudi wa majengo si mbinu mpya ya kijeshi ya Israel. Umetumika katika maeneo makubwa ya Gaza wakati wa vita vilivyochochewa na shambulio lililoongozwa na Hamas dhidi ya Israel tarehe 7 Oktoba 2023.
"Ilikuwa wazi tangu Oktoba 7 na tangu Israel na Hezbollah walipoanza vita kwamba kumekuwa na mkakati wa Israel kubadilisha mizania ya nguvu katika eneo hili," alisema Renad Mansour, Naibu Mkurugenzi wa Mpango wa Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini katika Chatham House, taasisi ya utafiti yenye makao yake Uingereza.
Wataalamu kadhaa wa sheria waliiambia BBC Verify kuwa uharibifu wa mali umepigwa marufuku vikali na sheria za kimataifa za kibinadamu, isipokuwa tu pale unapohitajika na ulazima wa kijeshi.
Kiwango cha kuthibitisha ulazima huo ni cha juu zaidi kuliko urahisi au faida ya kijeshi, kulingana na Profesa Janina Dill, mtaalamu wa usalama wa kimataifa na sheria za kimataifa katika Chuo Kikuu cha Oxford: "Hakika haujumuishi kubomoa vijiji vizima kama njia ya kujenga usalama wa muda mrefu wa taifa."
Pia inahitaji uchambuzi wa kila kesi wakati wa kuamua ni majengo gani yana umuhimu wa kijeshi, alisema Yuval Shany, mtaalamu wa sheria kutoka taasisi ya Israel Democracy.
Uwezo wa baadhi ya majengo ya kiraia kutumika kwa shughuli za kijeshi "hauhalalishi sera ya jumla ya kuunda maeneo ya kinga karibu na mpaka ambapo ndani yake majengo yote yanapaswa kubomolewa," aliongeza.
Profesa Ben Saul, Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu kupambana na ugaidi na haki za binadamu, alisema kuwa "uharibifu mkubwa wa maeneo ya makazi wa Israel, hasa Kusini mwa Lebanon lakini pia katika baadhi ya sehemu za Beirut," unaonekana kukiuka sheria za kimataifa za kibinadamu.
Jamii za Waislamu wa Kishia zinaunda idadi kubwa ya wakazi wa kusini mwa Lebanon, lakini pia kuna makundi mengine yanayoishi huko, ikiwa ni pamoja na Wakristo.
"Katika baadhi ya maeneo, muundo wa mashambulizi unaonekana kulenga 'kusafisha' vijiji na watu walio wengi wa Kishia kutoka kusini, kwa kuwaadhibu kwa pamoja raia ambao ndani yao wapiganaji wa Hezbollah wanaweza kuchanganyika," alisema Saul.
Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilijibu kwa kusema kuwa "madai yoyote kwamba IDF inachukua hatua za 'kusafisha' raia, kuadhibu jamii, au kulenga raia kwa misingi ya dini au madhehebu si ya kweli kabisa."
"Onyo kama hayo hayakusudiwi kuwahamisha raia kabisa au kuwazuia kurejea kisheria makwao," liliongeza.
Dkt. Lawrence Hill-Cawthorne, mkurugenzi mwenza wa Kituo cha Sheria za Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Bristol, alisisitiza tena kwamba "kanuni ya msingi ya sheria" ni kwamba mali za kiraia hazipaswi kulengwa.
"Si utetezi unaokubalika kudai kwamba uharibifu kamili wa miji na vijiji kusini mwa Lebanon ni muhimu ili kuunda eneo la kinga dhidi ya Hezbollah," alisema. "Hata kama vita vya Israel nchini Lebanon vinaweza kuchukuliwa kama kujilinda dhidi ya mashambulizi ya Hezbollah, namna vinavyoendeshwa inaonekana kwenda mbali zaidi ya vita vya kujilinda vilivyo na mipaka dhidi ya mashambulizi maalum."















