'Natumai vita havitaanza tena': Wairan wana wasiwasi baada ya mazungumzo kutibuka

Motorists pass under a banner featuring a portrait of Mojtaba Khamenei, Iran's new Supreme Leader, on a busy street in Tehran

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Hakuna tarehe iliyowekwa kwa ajili ya duru mpya ya mazungumzo ya amani Wairan wakihofia mustakabali wao wa siku zijazo.
    • Author, Ghoncheh Habibiazad
    • Nafasi, Mwandishi Mwandamizi BBC News Persian
  • Muda wa kusoma: Dakika 3

Mazungumzo dhaifu ya kusitisha mapigano kati ya Marekani na Iran yamezidi kuwa magumu baada ya juhudi za kumaliza vita kati ya pande hizo mbili nchini Pakistan kumalizika bila makubaliano.

Jeshi la Marekani lilisema litaanza kuzuia meli zinazoondoka katika bandari za Iran, huku Tehran ikitishia kulipiza kisasi kwa shambulia bandari za mataifa majirani katika eneo la Ghuba.

Wairan wanafuatilia kwa makini matukio yanayoendelea, wakihofia kuzuka tena kwa uhasama.

"Kwa kweli nilifikiri wangefikia makubaliano," alisema mwanamume mwenye umri wa miaka 20 wa Karaj, jiji lililo karibu na Tehran.

"Nahisi vita [vitaanza tena] kesho au wiki ijayo au hivi karibuni," aliongeza.

Ndani ya Iran, mamlaka imekatiza kabisa huduma za intaneti kwa zaidi ya wiki sita, na kufanya kuwa vigumu kwa watu kuwasiliana ndani ya nchi.

Mamlaka za Iran mara nyingi hutoa sababi kama vile "kulinda nchi dhidi ya mashambulizi ya mtandao" ili kuhalalisha kuzuia ufikiaji wa mtandao.

BBC Idhaa ya KIajemi imezungumza Wairani kadhaa, ambao wote wanapinga utawala wa sasa. Maoni yao hayawakilishi jamii nzima ya Iran.

Ramani
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Natumai vita havitaanza tena lakini nahofia vitaanza," alisema mwanamume mmoja aliye na umri wa miaka 20 mjini Tehran. Alisema alikuwa akijaribu kujishughulisha ili "kutuliza akili"

Lakini mwanamke mmja mwenye umri wa makamo alikuwa bado anajaribu kujipatia matumaini.

"Sasa kwa kuwa hali imetulia, ninajihisi vizuri, lakini ninatumai [vita] vitamalizika hivi karibuni," alisema.

"Natumai mtandao utareshwa. Natumai watajadiliana na kufikia makubaliano kwa sababu vita vikiendelea si vyema kwa watu wa Iran hata kidogo."

Wairan wengi ambao wamewasiliana na BBC wakati wa mzozo huo wamekwazika na hali ya kutoweza kufikia mtandao wa inataneti.

Sio tu imewazuia kupata habari za kuaminika, lakini pia imeathiri biashara nyingi, wanasema.

"Hakuna anayeshinda," alisema mtu mmoja huko Tehran ambaye anafanya kazi kama mtayarishaji wa maudhui. "Akiba yangu inaweza kunisaidia kwa muda usiozidi miezi miwili, lakini basi tena sina jinsi ya kutafuta pesa."

"Ninajisikia vizuri ikilinganishwa na siku ambazo [Marekani na Israel] zilikuwa zikitushambulia kwa mabomu, lakini nina wasiwasi mkubwa," mwanamume mwingine mwenye umri wa miaka 20 alisema.

"Hata kama watafanya makubaliano, kwa uchumi huu uliodorora, maisha yatakuwa magumu sana. Nilitarajia kwamba wangefikia makubaliano lakini sasa kuna hali hiyo ya kutotulia."

Mwanamume aliye na umri wa miaka 30 huko Karaj alisema anaamini kuwa Rais wa Marekani Donald Trump hangeweza kuafikiana kufikia makubaliano kwa sababu ya uchaguzi ujao wa katikati ya muhula wa Marekani mwezi Novemba.

"Haya ni maoni yangu binafsi, lakini sidhani kama Marekani itarudi nyuma," alisema. "Kuunga mkono yoyote kunaweza kuwafanya kushindwa katika uchaguzi."

Mtu mwingine, aliyekasirishwa na mauaji ya waandamanaji wanaoipinga serikali nchini Iran mnamo Januari, alisema kujadiliana na Jamhuri ya Kiislamu - ambayo alielezea kama "wauaji wa watoto wa nchi hii" - haikuwa na maana.

"Sitawahi kusahau siku hizo walipokuwa wakipiga risasi barabarani mbele ya macho yangu," aliongeza.

Vikosi vya usalama vya Iran vilianzisha msako mkali dhidi ya waandamanaji wanaoipinga serikali mwezi Januari, na kuua waandamanaji 6,508 na kuwakamata wengine 53,000, kulingana na Shirika la Habari la Wanaharakati wa Haki za Kibinadamu (Hrana) lenye makao yake nchini Marekani.

Mkuu wa Shirika la Tiba ya Uchunguzi wa Iran amesema kuwa mamlaka imetambua miili ya watu 3,375 waliouawa wakati wa vita vya hivi majuzi.

Bado hakuna tarehe iliyowekwa kwa duru mpya ya mazungumzo ya amani kati ya Tehran na Washington, na Wairan wanakabiliwa na hali ya kutojua nini kitakachofuata.