Tunachokijua kuhusu kusitishwa kwa mapigano kati ya Israel na Lebanon

Baadhi ya watu nchini Lebanon wamefurahia tangazo hilo, huku maeneo yaliyoathiriwa na mashambulizi ya hivi karibuni ya Israel yakionyesha wazi uharibifu mkubwa kote nchini.

Chanzo cha picha, Adnan Abidi / Reuters

Maelezo ya picha, Baadhi ya watu nchini Lebanon wamefurahia tangazo hilo, huku maeneo yaliyoathiriwa na mashambulizi ya hivi karibuni ya Israel yakionyesha wazi uharibifu mkubwa kote nchini.
    • Author, Yang Tian
    • Author, Helen Sullivan
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza kuwa viongozi wa Israel na Lebanon wamekubaliana kusitisha mapigano kwa muda wa siku 10, ambayo ilianza kutekelezwa saa 17:00 EST (21:00 GMT; usiku wa manane kwa saa za eneo la huko) tarehe 16 Aprili.

Katika taarifa yake, Trump hakutaja kundi la wapiganaji linaloungwa mkono na Iran, Hezbollah, ambalo limekuwa likishambuliana na Israel kwa wiki sita zilizopita.

Hata hivyo, katika chapisho la baadaye kwenye mtandao wake wa Truth Social, aliitaka Hezbollah kuheshimu makubaliano hayo, akisema: "Natumaini Hezbollah watafanya vizuri na kwa njia nzuri katika kipindi hiki muhimu."

Baada ya tangazo hilo, rais huyo wa Marekani pia aliwaalika Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Rais wa Lebanon Joseph Aoun kwenda Ikulu ya White House kwa mazungumzo zaidi.

Haya ndiyo tunayojua kuhusu makubaliano hayo ya kusitisha mapigano.

Makubaliano ya kusitisha mapigano yanaeleza nini?

Masharti ya makubaliano yanaeleza kuwa kusitishwa kwa mapigano kutadumu kwa siku 10, na kuna uwezekano wa kuongezwa kwa makubaliano ya pande zote mbili ikiwa mazungumzo yataonesha dalili za mafanikio.

Kulingana na maelezo zaidi yaliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani :

  • Israel inaendelea kuwa na "haki ya kuchukua hatua zote muhimu za kujilinda, wakati wowote, dhidi ya mashambulizi yaliyopangwa, yanayokaribia au yanayoendelea."
  • Lebanon inapaswa kuchukua "hatua za maana" kuzuia Hezbollah na makundi mengine yote "yasiyo ya serikali na yenye silaha" kufanya mashambulizi dhidi ya Israel.
  • Wahusika wanakubali kwamba vikosi vya usalama vya Lebanon vina jukumu la kipekee la kulinda usalama wa nchi hiyo.
  • Israel na Lebanon wameomba Marekani iendelee kuwezesha mazungumzo ya moja kwa moja yenye lengo la "kutatua masuala yote yaliyobaki."

Taarifa hiyo iliongeza kuwa kusitishwa kwa mapigano ni "ishara ya nia njema" kutoka Israel ili kuruhusu "mazungumzo ya kweli kuelekea makubaliano ya kudumu ya usalama na amani" kati ya pande hizo mbili.

Pande mbalimbali zimesemaje kuhusu makubaliano hayo?

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Viongozi wa Israel na Lebanon wameunga mkono kusitishwa kwa mapigano, huku Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu akikiita kuwa "fursa ya kufikia makubaliano ya kihistoria ya amani."

Waziri Mkuu wa Lebanon Nawaf Salam amesema anatumai makubaliano hayo yatawaruhusu watu waliokimbia makazi yao kurejea nyumbani.

Hezbollah pia wameonesha utayari wa kushiriki katika makubaliano ya kusitisha mapigano, lakini wakisisitiza kuwa lazima kuwe na "kusitishwa kikamilifu kwa mashambulizi" kote Lebanon na "kutokuwepo kwa uhuru wa majeshi ya Israel kufanya operesheni."

Kundi hilo linaloungwa mkono na Iran, ingawa limejikita sana ndani ya Lebanon, si sehemu ya mfumo wa usalama wa serikali ya Lebanon.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran iliunga mkono kusitishwa kwa mapigano, ambapo msemaji Esmail Baghaei alionesha "mshikamano" wake na Lebanon.

Tehran ilikuwa imesisitiza kuwa usitishaji wake wa mapigano wa wiki mbili na Marekani unapaswa kujumuisha Lebanon, jambo ambalo Marekani na Israel walisema halikuhusishwa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres alisifu jukumu la Marekani katika kuwezesha makubaliano hayo na akazitaka pande zote kuheshimu kikamilifu na kufuata sheria za kimataifa wakati wote.

Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen alielezea makubaliano hayo kama "nafuu," akisema Ulaya itaendelea kusisitiza kuheshimiwa kwa uhuru na mipaka ya Lebanon.

Kiongozi wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas aliongeza kuwa usitishaji wa mapigano unapaswa kutumika "kuondoka katika ghasia" na kufungua nafasi ya mazungumzo kuelekea "amani ya kudumu zaidi."

Kwanini Israel inabaki kusini mwa Lebanon?

Licha ya makubaliano hayo, Benjamin Netanyahu amesema wanajeshi wa Israel wataendelea kuwekwa umbali wa kilomita 10 (maili 6.2) ndani ya kusini mwa Lebanon.

Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonesha kuwa nchini Lebanon, zaidi ya watu milioni 1.2 wameyahama makazi yao, wengi wao wakitoka kusini mwa nchi hiyo.

Israel ilirejea kusini mwa Lebanon baada ya mashambulizi ya Hezbollah mapema Machi, na imeeleza eneo hilo lililochukuliwa kama "eneo la usalama," huku Netanyahu akisema wiki hii: "Tupo hapo, na hatutoki."

Waziri wa Ulinzi wa Israel, Israel Katz hapo awali alisema eneo linalokaliwa linaweza kufikia Mto Litani kusini mwa Lebanon, takribani kilomita 30 (maili 18.6) kutoka mpaka wa Israel.

Pia alisema nyumba zote katika vijiji vya Lebanon vilivyo karibu na mpaka wa Israel zitabomolewa.

Katika wiki za tangu vita kuanza, utafiti wa BBC Verify umebaini kuwa zaidi ya majengo 1,400 yameharibiwa na Israel kusini mwa Lebanon.

Waziri wa Ulinzi wa Lebanon Meja Jenerali Michel Menassa alisema kauli za Katz zinaonesha "nia ya wazi ya kulazimisha uvamizi mpya wa ardhi ya Lebanon."

Nchi za Ulaya, Canada na Umoja wa Mataifa pia zimekosoa tangazo hilo la Israel.

Makubaliano ya awali ya kusitisha mapigano kati ya Israel na Hezbollah, ambayo yalimaliza mgogoro wa miezi 13, bado yalishuhudia mashambulizi ya mara kwa mara karibu na mipaka kila siku.

Makubaliano hayo yalifikiwa vipi?

Israel na Lebanon zilifanya mazungumzo ya moja kwa moja nadra mjini Washington mapema wiki hii, yakilenga kupunguza vita vilivyosababisha mashambulizi ya anga yenye maafa katika sehemu ya mji mkuu wa Lebanon, Beirut, pamoja na mapigano kusini mwa nchi hiyo.

Tangazo la Rais Donald Trump lilisema makubaliano hayo yalitokana na "mazungumzo mazuri sana" na Joseph Aoun na Benjamin Netanyahu, lakini halikufafanua kama Hezbollah ilihusika moja kwa moja kwenye mazungumzo hayo.

Baadaye, Trump aliitaka Hezbollah "kutenda vizuri na kwa utulivu katika kipindi hiki muhimu" kupitia mitandao ya kijamii.

Netanyahu, licha ya kuunga mkono kusitishwa kwa mapigano, pia alionesha kuwa hakutoa makubaliano mengi katika eneo la vita ardhini.

Alisema Hezbollah ilikuwa imeweka masharti mawili: kuondoka kwa majeshi ya Israel nchini Lebanon na kanuni ya "utulivu."

Hata hivyo, inaonekana tangazo la kusitishwa kwa mapigano lilikuja kwa mshangao kwa Israel, hata ndani ya baraza lake la usalama.

Chombo kimoja cha habari cha Israel kilichoheshimika kiliripoti kwamba Netanyahu aliitisha mkutano wa baraza la usalama kwa taarifa ya dakika tano kabla ya tangazo hilo.

Taarifa zilizovuja kutoka kwenye mkutano huo zinasema mawaziri hawakupata nafasi ya kupiga kura kuhusu makubaliano hayo.

Inahusikaje na vita vinavyoendelea nchini Iran?

Wakati makubaliano ya kusitisha mapigano na Iran yalipotangazwa, kulikuwa na taarifa zinazokinzana kuhusu kama Lebanon ilihusika au la. Maafisa wa Pakistan, waliosaidia katika mazungumzo ya makubaliano hayo, pamoja na maafisa wa Iran, walisema Lebanon ilikuwa sehemu ya makubaliano, lakini Israel ilisema haikuhusika.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani Karoline Leavitt baadaye pia alisema Lebanon haikuwa sehemu ya makubaliano hayo.

Israel ilianzisha mashambulizi nchini Lebanon tarehe 2 Machi, kujibu mashambulizi yaliyofanywa na Hezbollah. Hii ilitokea baada ya Marekani na Israel kufanya mashambulizi dhidi ya Iran, jambo lililosababisha Iran kulipiza kisasi dhidi ya washirika wa Marekani katika Ghuba, pamoja na vikundi vinavyoiunga mkono Iran, ikiwa ni pamoja na kundi hilo la Lebanon.

Israel na Hezbollah wameendelea kushambuliana tangu wakati huo, licha ya wito wa Waziri Mkuu wa Lebanon wa pande zote mbili kusitisha mapigano.

Zaidi ya watu 2,100 wameuawa na wengine 7,000 kujeruhiwa katika mashambulizi ya Israel nchini Lebanon tangu 2 Machi, kulingana na Wizara ya Afya ya nchi hiyo, ambayo haitofautishi wapiganaji na raia. Takwimu hizo zinajumuisha wanawake wasiopungua 260 na watoto 172. Wizara hiyo inasema wahudumu 91 wa afya wameuawa na wengine 208 kujeruhiwa, huku zaidi ya mashambulizi 120 yakilenga ambulansi na vituo vya huduma za afya.

Uchambuzi wa BBC Verify umebaini kuwa zaidi ya majengo 1,400 nchini Lebanon yameharibiwa.

Kwa upande wa Israel, mashambulizi ya Hezbollah yameua raia wawili katika kipindi hicho, huku askari 13 wa Israel wakiuawa katika mapigano ndani ya Lebanon, kulingana na mamlaka za Israel.

Siku ya Alhamisi, jeshi la Israel liliharibu daraja la mwisho lililounganisha kusini mwa Lebanon na maeneo mengine ya nchi, hatua iliyozidisha kutengwa kwa eneo hilo na kuongeza hofu kwamba huenda ikasababisha uongozi wa muda mrefu wa kijeshi katika baadhi ya maeneo.