Kwa nini Bernardo Silva atakumbukwa kama gwiji wa Manchester City

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Keifer MacDonald
- Nafasi, BBC Sport journalist
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Baada ya miaka tisa na zaidi ya mechi 450, Bernardo Silva anajiandaa kufunga rasmi safari yake yenye mafanikio makubwa katika klabu ya Manchester City mwishoni mwa msimu huu.
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 31, aliyejiunga na City kutoka AS Monaco mwaka 2017 kwa ada £43m iliyokuwa ndogo ukilinganisha na thamani yake ya sasa, amethibitisha kuwa ataondoka klabuni mara tu mkataba wake utakapomalizika majira ya kiangazi.
Katika kipindi chake ndani ya uwanja wa Etihad, Silva ameshinda mataji 19 makubwa, yakiwemo sita ya Ligi ya Uingereza pamoja na taji la kwanza la klabu hiyo la Ligi ya UEFA.
Anaweza bado kuongeza mafanikio hayo kabla ya kuondoka, huku kikosi kinachonolewa na Pep Guardiola kikiwania ubingwa wa ligi na pia kombe la FA.
Hata hivyo, bila kujali matokeo ya mwisho wa msimu, nafasi ya Silva katika historia ya klabu hiyo tayari imeimarika.
Atakumbukwa sambamba na mastaa wa kisasa kama Sergio Aguero, Vincent Kompany na Kevin De Bruyne kama mmoja wa nyota waliobadilisha historia ya mafanikio ya Manchester City.
Katika makala haya, BBC Sport inaangazia kwa nini Silva atakumbukwa kama mmoja wa wachezaji bora kuvaa jezi ya Manchester City.
End of Pia unaweza kusoma:
'Hakuna mtu anayeweza kufanya anachofanya'
Tangu ajiunge na City 2017, Silva amekuwa kiungo muhimu katika mafanikio ya timu hiyo. Ameisaidia kushinda ubingwa wa ligi mara sita katika misimu minane iliyopita.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hata hivyo, miaka tisa baadaye, Silva - ambaye sasa ndiye mchezaji wa pili kwa muda mrefu zaidi katika klabu hiyo - amesaidia kubadilisha City na kuwa na nguvu kubwa katika mchezo wa Uingereza na alicheza kiungo muhimu katika kikosi chake kushinda taji la Ligi ya Uingereza katika misimu sita kati ya minane iliyopita.
Msimu wake wa kwanza ulikuwa wa kihistoria, ambapo City ilifikisha alama 100 katika msimu mmoja wa ligi.
Mwaka 2019 walitwaa ubingwa kwa tofauti ya pointi moja dhidi ya Liverpool FC, ikiwa ni mechi iliyokuw ana ushindani mkali.
Kati ya mwaka 2021 hadi 2024, Silva aliisaidia City kuweka rekodi kwa kushinda mataji manne mfululizo ya ligi.
Silva bado anaweza kushinda taji la saba la Ligi ya Uingereza mwishoni mwa msimu huu, huku City wakiwa bado wanawinda Arsenal katika wiki za mwisho za msimu huu.
Kwa jumla, ameichezea City mechi 451, akifunga mabao 76 na kutoa pasi za mabao 77.
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ureno, Bernardo Silva, pia amekuwa mhimili muhimu katika kuibadilisha Manchester City kuwa nguvu kubwa barani Ulaya na katika jukwaa la kimataifa.
Hadi sasa, Silva ameichezea City jumla ya mechi 451, ikiwa ni ya saba kwa wingi katika historia ya klabu, akifunga mabao 76 na kutoa pasi za mabao 77.
Kimataifa, alikuwa muhimu pia. Mwaka 2023 alitoa kiwango cha juu sana dhidi ya Real Madrid katika nusu fainali ya Ligi ya mabingwa Ulaya, kabla ya City kuifunga Inter Milan na kutwaa taji hilo pamoja na kukamilisha ushindi wa makombe matatu katika msimu mmoja na kuweka historia.
Kwa namna nyingi, yeye ni taswira kamili ya falsafa ya Pep Guardiola: mchezaji mwenye kipaji cha asili, anayechanganya ubunifu na juhudi zisizo na kikomo pamoja na ari ya ushindani wa hali ya juu.
Hata hivyo, mchango wake hauishii uwanjani pekee. Katika miaka ya karibuni, ameibuka kama mmoja wa viongozi wakuu wa kikosi kufuatia kuondoka kwa wachezaji muhimu kama Vincent Kompany, Sergio Aguero, Kevin De Bruyne na Kyle Walker, hatua iliyompelekea kuteuliwa kuwa nahodha wa klabu mwaka 2025.
Baada ya tangazo lake la kuondoka, beki wa zamani wa City na England, Steph Houghton, alimpongeza Silva kwa uongozi wake wa vitendo ndani ya miaka tisa aliyotumikia klabu.
Alisema hakuna mchezaji mwingine anayeweza kufanya kile anachokifanya Silva, akisisitiza kuwa aina yake ya uongozi ni tofauti na ile ya Kompany au Fernandinho.
Kwa mujibu wake, Silva huongoza zaidi kwa vitendo uwanjani, na juhudi zake hazina dosari kila anapovaa jezi ya Manchester City, bila kujali anacheza nafasi ipi, huwa anajitoa kwa asilimia mia moja.
"Hakuna mtu anayeweza kufanya kile anachofanya. Akiwa na Bernardo, yeye ni kiongozi wa aina tofauti na Kompany au Fernandinho," aliiambia 5 Live.
"Mengi ni kupitia uchezaji na kuhusu yeye kuwaongoza wavulana katika kufanya mambo fulani. Huwezi kulaumu juhudi zake kila mara anapovaa jezi ya Manchester City.
"Haijalishi anacheza wapi, anajitolea kwa kila hali."
Uchambuzi: 'Amekuwa mapigo ya moyo ya mafanikio ya Manchester City'
Mwandishi wa soka Phil McNulty anaeleza kuwa uwiano wa Silva wa mataji 19 katika mechi 451 unaonyesha ukubwa wake.
Alijiunga na Manchester City akitokea AS Monaco mwezi Mei 2017, baada ya kuwa mhimili muhimu katika kikosi kilichoiondoa timu ya Pep Guardiola kwenye Ligi ya bara Ulaya UEFA msimu uliotangulia.
Kikosi hicho cha Monaco kilikuwa na vipaji vikubwa, akiwemo Kylian Mbappe.
Tangu wakati huo, Bernardo Silva amekuwa kiini cha mafanikio ya kikosi cha City kilichotawala soka, hasa kilipofikia kilele chake mwaka 2023.
Mwaka huo walitwaa taji lao la kwanza la Ligi ya mabingwa Ulaya kwa kuifunga Inter Milan mabao 1-0 mjini Istanbul, na kukamilisha ushindi wa vikombe vitatu ndani ya msimu mmoja baada ya kuwa tayari wameshinda Ligi kuu ya Uingereza pamoja na FA Cup.
Katika msimu huu, akiwa nahodha, ameendelea kuwa na mchango mkubwa licha ya kuwa na umri wa miaka 31, huku City ikiikaribia kwa kasi timu inayoongoza ligi, Arsenal FC. Tayari wamefanikiwa kutwaa Carabao Cup, na wanajiandaa kwa nusu fainali ya FA Cup dhidi ya Southampton FC.
Bado ana nafasi ya kuhitimisha safari yake kwa kishindo, endapo ataiongoza City kutwaa tena mataji matatu ndani ya England.
Mchezaji huyo wa Ureno, Bernardo Silva, amekuwa na bado ni kiungo kamili anayemudu majukumu yote ya eneo la kati, huku kiwango chake kikiendelea kuwa cha juu kiasi cha kuvutia vilabu vikubwa barani Ulaya kama FC Barcelona na Juventus FC, na huenda hata nje ya Ulaya, hususan Saudi Arabia.
Silva ni mbunifu wa hali ya juu na mpambanaji asiyechoka, mchezaji mwenye ubunifu wa kisanii lakini pia mwenye ushindani mkali, anayechukia kushindwa na ambaye daima amekuwa akidai viwango vya juu kutoka kwake na wenzake, huku akiendelea kuwapa msaada ndani na nje ya uwanja.
Alisherehekea mafanikio kwa shauku kubwa, lakini pia anakumbukwa kwa tukio la mwaka 2020 alipokataa kupiga makofi kuwapongeza Liverpool FC waliokuwa wametawazwa mabingwa wapya wa Ligi kuu ya Uingereza walipokutana katika Uwanja wa Etihad. Aliuelezea utaratibu huo kama aina 'fulani ya unafiki'.
Hatua hiyo ilikosolewa na baadhi ya wadau, lakini kwa mashabiki wa Manchester City ilizidi kuimarisha hadhi yake kama mmoja wa alama muhimu za enzi ya mafanikio makubwa ya klabu hiyo.
Kwa mtazamo wa Pep Guardiola na uongozi mzima wa Manchester City, hakuna shaka kuwa kumziba pengo la Bernardo Silva kutakuwa kazi ngumu sana.
End of Soma Zaidi:
Je, mashabiki wamesema nini kumhusu?
Ian kutoka Mkoa wa Lake: "Neno hili hutumika sana siku hizi, lakini yeye ni gwiji wa kweli."
Alex kutoka Manchester: "Ni miongoni mwa wachezaji bora kabisa kuwahi kuivaa jezi ya Manchester City, lakini wengi hawakumthamini ipasavyo. Tusingefanikisha tuliyofanikisha bila yeye. Dhidi ya Real Madrid nyumbani katika msimu wa kubeba vikombe vitatu ndani ya msimu mmoja, hakuwa na mpinzani. Ataacha pengo kubwa sana lisiloweza kuzibika."
Martin kutoka Northampton: "Amekuwa nguzo imara katika kipindi chake chote City. Anafafanua kikamilifu maana ya gwiji wa klabu. Asante, Bernardo Silva."
Ollie kutoka Richmond: "Ndiyo mchezaji aliyekaribia zaidi kiwango cha Lionel Messi kuwahi kuonekana katika ligi hii. Ni mchezaji wa kuvutia sana kumtazama, na City ina kazi kubwa sana kumpata mbadala wake."
Duncan kutoka High Peak: "Kucheza zaidi ya mechi 450 katika enzi ya kisasa yenye ratiba ngumu na isiyopumzika ni ushahidi wa tabia na uimara wa mwili wa Bernardo. Kama ilivyotajwa, usiku wake bora ulikuwa dhidi ya Real Madrid katika nusu fainali ya Ligi ya mabingwa Ulaya UEFA msimu wa 2022 hadi 2023. Hakuwa anazuilika kabisa."
Salal kutoka Uingereza: "Bernardo anaondoka akiwa gwiji wa kweli wa City na soka la England. Kwa miaka mingi alikuwa kiungo kilichounganisha timu, hasa baada ya kuondoka kwa Yaya Toure na Sergio Aguero. City isingeshinda hata nusu ya mataji iliyonayo bila yeye."
Dermot, shabiki wa Manchester United kutoka Belfast: "Kama shabiki wa Manchester United, nitafurahi kumuona akiondoka kwa sababu alinipa wakati mgumu mara kadhaa. Lakini ilikuwa furaha kubwa kumtazama akicheza katika Premier League. Ni mchezaji wa kiwango cha juu. Kila la heri huko mbele, Bernardo."












