Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Arsenal na mbio za ubingwa EPL, historia inajirudia?
Kwa misimu ya karibuni, Arsenal wamekuwa wakionekana kuwa karibu sana na kutwaa ubingwa wa Ligi kuu England (EPL), lakini kila mara wanapofika hatua za mwisho, mambo hubadilika. Msimu huu ulionekana kuwa tofauti, hasa baada ya kukaa kileleni kwa muda mrefu na kutengeneza pengo kubwa la alama dhidi ya wapinzani wao wakuu, Manchester City na Liverpool.
Hata hivyo, matokeo ya hivi karibuni, yakiwemo kuchapwa 2-1 nyumbani na AFC Bournemouth na jana 2-1 tena ugenini dhidi ya Manchester City, yameanza kuibua hofu ile ile ya zamani. Tofauti ya alama imepungua mpaka kufikia 3, na presha ya mbio za ubingwa sasa imekuwa kubwa.
City, ambao wana uzoefu mkubwa wa kushinda ubingwa katika miaka ya karibuni, wanaonekana kuingia katika kasi yao ya kawaida ya mwisho wa msimu. Hili limekuwa jambo la kawaida chini ya Pep Guardiola kuanza polepole, kisha kumaliza kwa nguvu kubwa.
Sasa, huku msimu ukielekea ukingoni, swali linabaki wazi: je, Arsenal wataweza kuvunja mwiko wao wa kushindwa dakika za mwisho, au historia itajirudia tena?
Aprili - mwezi mgumu kwa Arteta
Kwa Mikel Arteta, mwezi Aprili umeendelea kuwa changamoto kubwa. Takwimu zinaonyesha wazi kuwa huu ndio mwezi ambao timu yake hupoteza uthabiti, jambo ambalo linaonekana tena msimu huu.
Mwaka 2021, Arsenal chini ya Arteta ilicheza mechi 4 mwezi Aprili, ikishinda 1 tu, sare 1 na kupoteza 2. Mwaka 2022, ilicheza mechi 5, ikishinda 2 lakini ikipoteza 3, bila sare.
Mwaka 2023, ilicheza mechi 5, ikishinda 1, sare 3 na kupoteza 1. Mwaka 2024 ulikuwa bora zaidi, ilicheza mechi 6, ikishinda 5 na kupoteza 1 pekee. Mwaka 2025, ilicheza mechi 5, ikishinda 2, sare 3 bila kupoteza.
Na Mwaka 2026, hadi sasa imecheza mechi 2 na zote imepoteza. Licha ya hali hiyo, Arteta anaendelea kusisitiza kuwa matumaini bado yapo. Aliwaambia waandishi wa habari:
"Tuna imani kamili kwamba tunaweza kufanya hili. Leo tumeonyesha tena sisi ni timu gani. Iko mikononi mwetu."
Aliongeza pia:
"Tumepoteza nafasi kwa matokeo. Wao wana mchezo mkononi, sisi tuna alama tatu. mbio za ubingwa bado zinaendelea."
City na ubora katika dakika za lala salama
Manchester City wanaonyesha ubora mkubwa sana katika misimu minne ya mwisho ya EPL, ambapo katika mechi 10 za mwisho za kila msimu wamekuwa wakitawala kwa kiwango cha juu. Msimu wa 2021-22 walishinda mechi 7 bila kupoteza, wakitoa sare 3. Msimu wa 2022-23 walizidi kuwa bora zaidi wakishinda mechi 9 na kutoa sare 1 bila kupoteza kabisa.
Msimu wa 2023-24 walishinda 8, sare 1 na kupoteza 1 pekee, huku 2024-25 wakirudia ubora kwa kushinda 7 na kutoa sare 3 bila kichapo.
Kwa ujumla, katika miaka hiyo minne katika za mwisho jumla 40 walizocheza, wameshinda mechi 31, sare 8 na kupoteza mechi 1 tu, jambo linaloonyesha uthabiti na ubabe wao mkubwa.
Nahodha wa timu Bernardo Silva alisisitiza umuhimu wa ushindi dhidi ya Arsenal jana kwamba:
"Ni ushindi mkubwa sana. Unatuweka kwenye nafasi ambapo tukishinda mchezo wetu mkononi tunakuwa sawa kwa alama."
Kwa wachambuzi, hali hii inaipa City faida kubwa. Danny Murphy alisema:
"nafikiri watatwaa ubingwa kwa tofauti ya mabao."
Ubora huu wa kumaliza msimu kwa nguvu ndio unaowafanya City kuwa tishio kubwa zaidi katika mbio hizi.
Historia inajirudia?
Swali kubwa linalobaki ni kama Arsenal wataweza kubadilisha simulizi yao ya miaka ya karibuni. Mara nyingi wamekuwa wakianza vizuri, lakini kushindwa kumaliza kazi.
Kwa upande mwingine, City wamejijengea sifa ya kushinda katika mazingira ya presha kubwa. Wachambuzi wengi wanaamini hilo linaweza kujirudia tena.
Wayne Rooney ana mtazamo tofauti kidogo:
"Mbio hizi za ubingwa bado haijaisha… bado kutakuwa na mabadiliko. Arsenal bado wana nafasi kubwa kidogo."
Lakini wengine wanaona tofauti. Mchambuzi Gary Neville alisema City:
"Wako kwenye mstari sahihi na ni treni ambayo ni ngumu kuizuia."
Hata hivyo, matokeo ya mwisho yataamuliwa na nani ataweza kudhibiti presha katika mechi zilizobaki, City akibakiza mechi 6, na Arsenal 5. Kama ilivyokuwa misimu iliyopita, hatua hizi za mwisho ndizo zitaamua kila kitu.