Wanaanga wa Artemis II : 'Tuliondoka kama marafiki,tukarudi tukiwa marafiki zaidi'

Muda wa kusoma: Dakika 3

Wanaanga wa kikosi cha Artemis II walisema safari yao ya angani iliipa dunia matumaini na umoja, wakati ambapo dunia ilikuwa na upungufu wa vitu hivyo.

Katika kikao chao cha kwanza na wanahabari baada ya kurejea Ijumaa iliyopita, Reid Wiseman, Victor Glover, Christina Koch na Jeremy Hansen walisema walienda angani kama marafiki na wakarudi wakiwa na uhusiano wa karibu sana.

Wanne hao walisema safari hiyo iliwakumbusha umuhimu wa kuwa binadamu ambayo ni kucheka,kufurahi, kulia na kuwa na hisia na watu wengine.

Ujumbe wao ulikuwa mmoja: kutua kwenye mwezi kwa sasa sio ndoto ambayo haiwezi kutimia.

"Tulitaka kujaribu kufanya kitu ambacho kingeileta dunia pamoja, na tulishangaa kuona tunaungwa mkono kote duniani, na tunataka kushukuru dunia kwa kutufuatilia"

Walizungumzia chombo kilichowapeleka angani cha Orion walichokiita Integrity, na chombo kilichowasukuma angani, na kusema kuwa ni matokeo ya ushirikiano wa kimataifa.

"Asante kwa kila mmoja aliyehusika kujenga chombo hicho, kwasababu kilikuwa chombo kizuri"

Wanaanga hao wa Artemis II walifika umbali mrefu kutoka duniani umbali ambao hakuna binadamu amewahi kufika.

Victor Glover alikuwa mwanaume wa kwanza mweusi kufika angani, Christina Koch alikuwa mwanamke wa kwanza kufika umbali huo na Jeremy Hansen alikuwa raia wa kwanza wa Canada kufika angani.

Kwa Koch, ukubwa wa kile walichokuwa wamekifanya ulianza tu kueleweka, pale mume wake alipomwambia kwa njia ya simu kuwa misheni hiyo ilikuwa imevuka mipaka na kuwaunganisha watu. Alishindwa kujizuia.

"Mume wangu aliponiangalia machoni kwa njia ya video na kusema, 'mmeleta mabadiliko,' ilifanya nilie, na nikasema, hicho ndicho tulichokitaka."

Glover alisema walifurahia kuishirikisha dunia nzima katika misheni hiyo.

Hansen alisema kwamba kurejea duniani kulikuwa kumeimarisha imani yake kwa watu.

"Huwa hatufanyi mambo makubwa kila wakati, sisi si waadilifu kila wakati, ila tunajaribu kuwa wazuri na kutendeana mema. Nilichokiona kilinipa furaha, na matumaini ya siku za usoni."

"Kile tulichokiona hakiwezi kufafanuliwa kwa fikra za kawaida."

Wiseman alielezea tukio la jua kupita nyuma ya mwezi na kupatwa kwa jua kulikoshuhudiwa kwa umbali wa maili 250,000 , kama jambo lililozidi uwezo wa akili ya binadamu kulielewa.

Aliporejea kwenye meli ya uokoaji baada ya kutua, alimtafuta kasisi, akitaka kumuelezea kile alichokiona ambacho sayansi haikuweza kumpa majibu.

"Mimi si mtu wa dini sana," alisema, "lakini hakukuwa na njia nyingine ya kuelezea chochote tulichokishuhudia. Hivyo nikaomba kumwona kasisi kwenye meli ya wanamaji na nikaanza kulia.

"Sidhani kama ubinadamu umefikia hatua ya kuweza kuelewa tulichkiona sasa hivi, kwa sababu kilikuwa cha ajabu kupita maelezo ya kawaida."

Mbali na hisia walizokuwa nazo, pia walipata mshangao mkubwa wa kuona kila kitu kwa macho. Hansen alijikuta amevutiwa sana na kina cha anga za mbali. "Tuliona mambo mengi ya kushangaza sana," alisema. "Niliona kina cha galaksi ambacho sijawahi kushuhudia"

Koch alielezea jinsi alivyozoea hali ya kutokuwa na uzito na aliporudi duniani aliacha shati akitarajia litaelea na akashangaa lilipoanguka chini.

Ila sio kila kitu kilikwenda sawa. Wanaanga hao walikuwa wazi kuhusu tatizo la mara kwa mara la kuziba kwa vyoo.

Kifaa cha anga cha Orion, hata hivyo, kiliwavutia sana wahudumu wake. Na Wiseman, alipokuwa akitafakari jinsi walivyokuwa wamekaribia uso wa mwezi, alitoa kauli ambayo bila ilisikika katika chumba cha mipango cha NASA.

"Kama tungekuwa na kifaa cha kutua kwenye mwezi katika safari hiyo ya kwanza ndani ya chombo hicho najua angalau wenzangu wangeingia humo, na kujaribu kutua kwenye mwezi."

Mara kwa mara, misheni zenye umuhimu mkubwa zaidi huipa anga sura ya kibinadamu, na kuwawezesha wale wanaotazama kutoka duniani kuhisi kana kwamba nao walikuwa sehemu ya safari hiyo, na Artemis II ilifanya hivyo.

Rais wa zamani wa Marekani, John F. Kennedy aliwahi kusema kuwa, Marekani ilichagua kwenda mwezini "si kwa sababu ilikuwa rahisi bali kwa sababu ilikuwa vigumu."