Kwa nini Urusi imekaa pembeni katika mgogoro wa Yemen?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 7

Maafisa wa Urusi, vyombo vya habari vya serikali na wanablogu nchini humo kwa kawaida hawazungumzi sana kuhusu yanayoendelea Yemen, hata wakati vita vya wenyewe kwa wenyewe na athari zake za kimataifa zilipozidi kuongezeka katika miezi ya hivi karibuni.

Hali hiyo inashangaza kwa kuwa Yemen ina umuhimu wa kimkakati kwa Urusi. Moscow ina uhusiano wa kihistoria na Yemen Kusini, iliyokuwa mshirika wa zamani wa Muungano wa Kisovieti, huku Iran, mshirika wake wa karibu kwa sasa, ikiwa na nafasi muhimu katika mgogoro huo.

Baadhi ya wachambuzi wanaona ukimya huo kama ishara kwamba Urusi inajaribu kudumisha nafasi yake ya mpatanishi huku ikiendelea kujenga uhusiano na pande mbalimbali zinazohusika katika mgogoro huo. Wengine wanaenda mbali zaidi na kudai kuwa Moscow imekuwa ikitoa aina fulani ya msaada kwa Ansar Allah (Wahouthi), kundi linaloungwa mkono na Iran na linalodhibiti sehemu kubwa ya kaskazini mwa Yemen.

Wachambuzi wa Urusi, wanaounga mkono Kremlin na wanaoikosoa, mara nyingi huangazia manufaa ambayo Moscow inaweza kuyapata kutokana na mzozo huo. Miongoni mwao ni uwezekano wa kupanda kwa bei ya mafuta duniani na kuongezeka kwa ushiriki wa Marekani nchini Yemen, jambo ambalo linaweza kuhamisha sehemu ya umakini na rasilimali zake kutoka vita vya Ukraine.

Wakati miungano na maslahi ya kisiasa yakiendelea kubadilika nchini Yemen, Urusi inaonekana kuendelea na mkakati wa kuweka milango wazi kwa pande zote. Hilo linaonekana katika matamko yake ya tahadhari na hatua zake za kutoegemea wazi upande wowote katika mgogoro huo.

Mkakati huo wa kujionyesha kama mpatanishi asiyeegemea upande wowote unaweza kuiruhusu Moscow kuendelea kuwa na mawasiliano na wadau wote wakuu wa mgogoro wa Yemen, huku ikihifadhi ushawishi wake wa kidiplomasia na kimkakati bila kujali mwelekeo wa vita hivyo.

Urusi katika mgogoro wa Yemen

Sera ya Urusi nchini Yemen inakwenda sambamba na mtandao tata wa maslahi yanayokinzana na ushindani kati ya wahusika mbalimbali.

Mwaka 2017, Urusi ilisimamisha shughuli za ubalozi wake mjini Sanaa na kuhamishia huduma za kibalozi nchini Saudi Arabia.

Miaka saba baadaye, Moscow ilitangaza mpango wa kurejesha shughuli zake za kibalozi nchini Yemen, safari hii katika mji wa Aden, ambao umekuwa makao makuu ya serikali inayotambuliwa kimataifa tangu mwaka 2015.

Serikali ya Yemen, iliyolazimika kuondoka Sanaa mwanzoni mwa vita vya wenyewe kwa wenyewe, iliupokea uamuzi huo kama ushindi wa kidiplomasia.

Balozi wa Yemen nchini Urusi alisema uamuzi huo unaonyesha uungaji mkono wa Moscow kwa Yemen na serikali yake halali.

Hata hivyo, Urusi imeendelea kuwa na uhusiano wa karibu na Ansar Allah (Wahouthi). Oktoba 12, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Georgy Borisenko, alisema Moscow imekuwa ikiwasiliana na kundi hilo kwa muda mrefu.

Aliongeza kuwa Ansar Allah ina mwakilishi maalumu nchini Oman, akionyesha kuwa nchi hiyo ni mojawapo ya njia za mawasiliano kati ya Urusi na Wahouthi.

Kwa mujibu wa gazeti la Novaya Gazeta Europa, mashirika ya habari ya serikali ya Urusi, RIA Novosti na TASS, pia yana uhusiano na Ansar Allah.

Mnamo Januari na Julai 2024, ujumbe wa Ansar Allah ulitembelea Moscow na kufanya mazungumzo na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Mikhail Bogdanov.

Wakati huo, maafisa wa Urusi walilaani mashambulizi ya Marekani na Uingereza dhidi ya maeneo ya kundi hilo, wakiyataja kuwa yasiyolingana na hali halisi.

Uhusiano kati ya Urusi na Ansar Allah una historia ya miaka kadhaa. Tangu angalau mwaka 2016, wawakilishi wa kundi hilo walikuwa tayari wameiomba Moscow msaada wa kibinadamu.

Wakati huohuo, Bogdanov aliifikishia serikali ya Yemen yenye makao yake Aden ujumbe wa "wasiwasi mkubwa" wa Urusi kuhusu mapigano yaliyoendelea nchini humo, huku wanadiplomasia wa Urusi wakikanusha madai kuwa Moscow ilikuwa ikiunga mkono rasmi Ansar Allah.

Ingawa mawasiliano ya kidiplomasia ya hadharani yamepungua katika miaka ya karibuni, Urusi imeendelea kudumisha mawasiliano na wahusika wakuu wote katika mgogoro wa Yemen.

Mbali na Ansar Allah na serikali inayotambuliwa kimataifa, maafisa wa Urusi pia walifanya mazungumzo mwaka 2024 na Baraza la Mpito la Kusini (STC), kundi la kujitenga linaloungwa mkono na Falme za Kiarabu na lenye ushawishi mkubwa kusini mwa Yemen.

Baraza hilo linapingana na serikali inayotambuliwa kimataifa pamoja na washirika wake, na linataka kuanzishwa kwa taifa huru kusini mwa Yemen, sawa na iliyokuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Yemen, mshirika wa zamani wa Muungano wa Kisovieti.

Baada ya mashambulizi ya Baraza la Mpito la Kusini kushindwa na wanachama wake kuondolewa serikalini Januari 2026, migogoro na mapigano kati ya makundi yanayopinga Ansar Allah yaliongezeka tena.

Msimamo wa Urusi kuhusu mgogoro wa Yemen ni upi?

Kadiri mapigano kati ya Ansar Allah na serikali inayotambuliwa kimataifa yenye makao yake mjini Aden yalivyozidi kushika kasi mwishoni mwa mwaka 2026, Urusi imeonyesha utayari wa kuchukua nafasi ya mpatanishi.

"Ikiwa pande husika zitavutiwa na mchango wetu katika juhudi za upatanishi, tuko tayari kutekeleza jukumu hilo kwa nia njema na bila upendeleo," Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Alexander Alimov, aliliambia shirika la habari la serikali la RIA Novosti.

Hata hivyo, alikiri kuwa hadi sasa hakuna upande uliowasilisha ombi rasmi kwa Moscow kuhusika katika upatanishi.

"Hatuwezi kujitokeza na kujilazimisha katika mchakato huo," alisema.

Awali, msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, alisema Urusi haikuwa imepokea ombi lolote la kupatanisha pande zinazohasimiana.

Tangu wakati huo, hata hivyo, kumekuwa na dalili kwamba Ansar Allah iko tayari kuunga mkono juhudi za upatanishi za Urusi.

Afisa mmoja mwandamizi wa kundi hilo aliliambia shirika la Associated Press tarehe 14 Oktoba kwamba wanakaribisha juhudi zozote za upatanishi zitakazoweza kumaliza vita na kuondoa mzingiro kati ya Sanaa na Riyadh.

Siku hiyo hiyo, Associated Press iliripoti kuwa afisa huyo alitaja Oman, Urusi na China kuwa miongoni mwa wahusika wanaojaribu kusaka makubaliano ya kusitisha mapigano kati ya Wahouthi na Saudi Arabia.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Georgy Borisenko, alitoa msimamo wa tahadhari katika mahojiano na kituo cha televisheni cha RTVI.

"Ni vigumu kubaini upande unaobeba lawama kubwa zaidi, na huenda pande zote hazijaonyesha kiwango cha tahadhari kinachohitajika. Hata hivyo, Urusi inalaani vikali mashambulizi dhidi ya miundombinu ya kiraia," alisema.

Borisenko alisisitiza kuwa Urusi inaitambua serikali yenye makao yake Aden kama serikali halali ya Yemen na inaunga mkono umoja wa taifa hilo. Wakati huohuo, alitetea kuendelea kwa mawasiliano kati ya Moscow na Ansar Allah, akisema mawasiliano hayo ni muhimu katika kutafuta suluhu ya mgogoro huo.

Urusi inanufaikaje na Ansar Allah?

Kwa mujibu wa Sergei Serebrov, mtafiti mwandamizi katika Taasisi ya Masomo ya Mashariki ya Chuo cha Sayansi cha Urusi, Ansar Allah ina mtazamo chanya kuhusu Urusi kutokana na msimamo wa Moscow wa kuunga mkono suluhu ya amani nchini Yemen kupitia mchakato unaoongozwa na Umoja wa Mataifa.

Aliongeza kuwa, ingawa Urusi inaunga mkono rasmi serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa, haijawahi kukatiza mawasiliano yake na Ansar Allah.

Mwaka 2024, Ansar Allah iliahidi kuhakikisha usalama wa meli za Urusi zinazopita katika Bahari ya Shamu (Red Sea), ahadi ambayo pia ilithibitishwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Mikhail Bogdanov.

Kumekuwa pia na ripoti zinazodai kuwa kundi hilo lilihusika katika kuwashawishi mamia ya raia wa Yemen kujiunga na vikosi vya Urusi vinavyopigana nchini Ukraine.

Hata hivyo, faida kubwa zaidi ambayo Ansar Allah imeiletea Moscow imekuwa ya moja kwa moja.

Mnamo Septemba 12, shirika la habari la RIA Novosti lilichapisha makala yenye kichwa: "Faida za mabilioni; Ansar Allah ya Yemen yampa Urusi zawadi kubwa."

Makala hiyo ilieleza jinsi bei ya mafuta ilivyopanda kufuatia operesheni za Ansar Allah dhidi ya usafirishaji wa meli katika Bahari ya Shamu. Mwandishi alibainisha kwamba bajeti ya Urusi ya mwaka 2026 ilikuwa imejengwa kwa makadirio ya bei ya dola 59 kwa pipa la mafuta ya Urals, ilhali bei ilikuwa tayari imevuka dola 90 kwa pipa.

Kwa mujibu wa ripoti ya Novaya Gazeta Europe, iliyonukuu chanzo kutoka sekta ya biashara ya mafuta, baada ya Ansar Allah kudhibiti Mlango-Bahari wa Bab al-Mandab, bei ya mafuta ya Urusi katika bandari za Bahari Nyeusi na Bahari ya Baltiki ilifikia karibu dola 100 kwa pipa.

Mchambuzi wa benki ya Urusi ya Promsvyazbank, Yekaterina Krylova, alisema kuwa ongezeko la hatari za kisiasa duniani lingeendelea kuunga mkono bei za juu za mafuta kwa kipindi fulani.

Alitabiri kuwa masoko ya mafuta yangerejea katika hali ya utulivu kadiri mwaka 2027 unavyokaribia.

Katika muktadha huohuo, mchambuzi wa masuala ya kijeshi Alexei Kargapoltsev alieleza kuwa kuongezeka kwa mvutano katika Bahari ya Shamu "si jambo baya kwa Urusi."

Aliandika kwenye blogu yake kwamba kadiri Marekani inavyolazimika kuelekeza nguvu na rasilimali zake katika migogoro mingine, ndivyo inavyopunguza uwezo wake wa kuisaidia Ukraine kijeshi.

Je, Urusi inaisaidia Ansar Allah?

Baadhi ya wachambuzi na wanablogu wa Urusi wamefikia hatua ya kudai kwamba Ansar Allah inapokea msaada wa moja kwa moja wa kijeshi kutoka Moscow.

Blogu ya Militarist ilidai kuwa kundi hilo hupokea "msaada wa kiintelijensia" kutoka Iran na Urusi.

Nayo tovuti ya Most Media, inayochapishwa kutoka uhamishoni, iliripoti kuwa Moscow ilianza kuvutiwa zaidi na Ansar Allah baada ya operesheni zake katika Bahari ya Shamu kuchangia kupanda kwa bei ya mafuta na kuvuruga biashara kati ya Magharibi na Asia Mashariki, licha ya uwezo mdogo wa kijeshi wa kundi hilo.

Tovuti hiyo ilidai pia kuwa mawasiliano kati ya Ansar Allah na Kremlin yamekuwa ya mara kwa mara, huku ikinukuu ripoti za vyombo vya habari vya Magharibi zilizodai kwamba Moscow imekuwa ikiipatia kundi hilo msaada unaojumuisha silaha, chakula na taarifa za kiintelijensia.

Hata hivyo, madai hayo hayakuambatana na ushahidi mahususi.

Mwaka 2024, baadhi ya waandishi wa habari katika vyombo vya habari vya serikali ya Urusi walitoa wito wa Ansar Allah kupewa silaha. Pamoja na hayo, hakuna ushahidi wa wazi unaoonyesha kuwa hatua kama hiyo iliwahi kutekelezwa.

Hata baadhi ya wakosoaji wa Kremlin wenye misimamo ya kupinga Magharibi wanaiona Ansar Allah kama mshirika anayeweza kuwa na manufaa kwa Urusi.

Igor Girkin, kamanda wa zamani wa kijeshi anayejulikana pia kama Strelkov na ambaye kwa sasa anatumikia kifungo jela, aliandika katika ujumbe uliochapishwa kupitia akaunti ya Telegram ya mke wake mnamo Septemba 11 kwamba haoni sababu ya msingi ambayo ingeweza kuleta mzozo kati ya Urusi na Ansar Allah.

Aliongeza kuwa, kwa mtazamo wake, kama Urusi ingekuwa na uongozi wenye ufanisi zaidi, ilipaswa kulisaidia kundi hilo.

Imetafsiriwa na Ambia Hirsi