Mwaka mmoja baada ya Raila: Nini kimebadilika?

    • Author, Ambia Hirsi
    • Nafasi, BBC Swahili
    • Akiripoti kutoka, Nairobi
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga kimeacha alama kubwa katika siasa za Kenya, huku mjadala ukiendelea kuhusu urithi wake na mwelekeo wa kisiasa alioujenga kwa zaidi ya miongo minne.

Ushawishi wake ulivuka mipaka ya chama cha Orange Democratic movement (ODM) na ngome zake za kisiasa, ukigusa siasa za kitaifa, harakati za upinzani, na ajenda za maendeleo katika maeneo mbalimbali ya nchi. Mwaka mmja baadaye, maswali kuhusu nani atakayejaza pengo hilo na jinsi mazingira ya kisiasa yalivyobadilika tangu kuondoka kwake yanaendelea kujitokeza. Tunaangazia mambo matano makuu yaliyobadilika.

1. Migawanyiko ndani ya ODM

Kifo cha Raila Odinga, muasisi na kiongozi wa muda mrefu wachama cha Orange Democratic Movement (ODM), kimeacha pengo kubwa la uongozi ndani ya chama hicho na kukiweka katika kipindi muhimu cha mpito. Huku viongozi wakisaka mwelekeo mpya baada ya kuondoka kwa kiongozi aliyekiunganisha kwa miongo kadhaa, nafasi ya Katibu Mkuu ikiibuka kuwa mojawapo wa chanzo kikuu cha mvutano na mapambano ya ushawishi ndani ya chama.

''Mambo yamekua magumu.'' Gavana wa Siaya James aliiambia BBC alipoulizwa hali ilivyokua chamani humo mwaka mmoja baadaye: ''Unajua Baba alijua namna ya kuendesha siasa zake na kile chama cha alichokua akikiongoza.''

Kauli yake inaashiria matukio kadhaa makuu yaliyoikumba chama hicho ingawa uongozi wake ulisema mambo yatatulia. Wiki chache baada ya Raila Odinga kufariki ODM iliadhimisha miaka 20 tangu kuanzishwa kwake.

Maadhimisho hayo yalikumbwa na migawanyiko na mizozo ya ndani ya mamlaka huku viongozi wakitofautiana kuhusu nani anayefaa kushika usukani na kuelekeza mwelekeo wa chama kuelekea uchaguzi mkuu ujao wa 2027.

Kilele cha mivutano hiyo iliishia kutimuliwa kwa Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna. Kamati ya Kitaifa ya Uongozi (NEC) ilimvua Sifuna wadhifa wa Katibu Mkuu na kumteua Catherine Omanyo kukaimu nafasi hiyo Mnamo Februari 2026. Hata hivyo, Mahakama Kuu na Jopo la Kutatua Mizozo ya Vyama vya Kisiasa (PPDT) zilisitisha kwa muda utekelezaji wa uamuzi huo zikieleza kuwa kulikuwa na maswali kuhusu taratibu zilizofuatwa.

Mnamo Juni, ODM ilimwondoa rasmi Sifuna kwa madai ya kukiuka katiba ya chama na kukaidi misimamo yake, kabla ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa kuthibitisha mabadiliko hayo mwezi Julai.

Zaidi ya mzozo wa uongozi, sakata hilo lilionekana kama mtihani mkubwa wa kwanza kwa ODM katika enzi ya baada ya Raila. Kwa miaka mingi, Raila alikuwa nguzo ya umoja ndani ya chama na msuluhishi wa migogoro ya ndani.

Kuondolewa kwa Sifuna kulifichua makundi tofauti yanayoshindania ushawishi na mwelekeo wa chama. Wakati baadhi ya viongozi walitetea hatua hiyo kama njia ya kuimarisha nidhamu ya chama, wengine waliiona kama dalili ya mapambano ya urithi wa kisiasa ndani ya ODM.

2. UDA yaongeza ushawishi Magharibi mwa Kenya

Mwelekeo wa siasa za Kenya umebadilika kwa kiasi kikubwa mwaka mmoja baada ya kifo cha kiongozi wa upinzani Raila Odinga, hasa katika maeneo ya Nyanza na Magharibi mwa Kenya ambayo kwa muda mrefu yalikuwa ngome zake za kisiasa. Katika mazingira hayo, chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) kimeongeza juhudi za kupanua ushawishi wake katika maeneo ambayo hapo awali yalikuwa na uungwaji mkono mkubwa wa ODM.

Miongoni mwa sababu zinazotajwa kuchangia hali hiyo ni kudhoofika kwa ODM na mjadala unaoendelea kuhusu urithi wa kisiasa wa Raila. Kifo chake kiliacha pengo kubwa la uongozi ndani ya chama hicho, ambacho kwa miaka mingi kilitegemea ushawishi wake katika kuunganisha wafuasi wake. Kutokuwepo kwa mrithi mwenye uzito sawa wa kisiasa kumezua mijadala kuhusu mustakabali wa chama na mwelekeo wa ngome zake za jadi za kisiasa.

Hali hiyo imeipa UDA fursa ya kujijengea nafasi katika Magharibi mwa Kenya na Nyanza kupitia ushirikiano na viongozi wa eneo hilo, ziara za kisiasa na juhudi za kuimarisha uwepo wake miongoni mwa wapigakura. Aidha, Rais William Ruto amekuwa akiendesha mikutano ya mara kwa mara inayowashirikisha viongozi wa ODM, jambo ambalo baadhi ya wachambuzi wanalitazama kama mkakati wa kuimarisha ushawishi wa UDA katika maeneo yaliyokuwa ngome za chama hicho cha upinzani.

Akizungumza na BBC, Gavana wa Siaya James Orengo alieleza wasiwasi wake kuhusu mwelekeo wa ODM, akisema chama hicho kimezidi kupoteza sura yake ya upinzani kutokana na ukaribu wake na UDA. "Sijaona chama rasmi cha upinzani kikiitwa kwenye vikao Ikulu. Sasa ODM na UDA zimekuwa kama sura moja. Unamuona Rais Ruto kwenye vikao vya ODM kuliko hata vikao vya UDA. Sura ya ODM imegeuka sana," alisema Orengo.

Mvutano kati ya familia ya Raila na ODM

Baada ya kifo cha Raila Odinga, tofauti za maoni zimeanza kujitokeza kati ya baadhi ya wanafamilia wake na viongozi wa ODM kuhusu mwelekeo wa chama hicho na namna ya kusimamia urithi wake wa kisiasa.

Mvutano huo uliibuka baada ya Winnie Odinga kumkosoa hadharani mjomba wake, Dkt Oburu Oginga, akieleza mashaka kuhusu uwezo wake wa kuliongoza ODM na kusimamia uhusiano wa chama hicho na serikali ya Rais William Ruto.

Kauli hizo zimezua mjadala ndani ya ODM wakati chama hicho kikijaribu kujipanga upya baada ya kuondokewa na kiongozi wake wa muda mrefu.

Akijibu, Dkt Oburu alitetea msimamo wa chama wa kuendelea kushirikiana na serikali na kusisitiza umuhimu wa kudumisha umoja ndani ya ODM huku kikijiandaa kwa uchaguzi mkuu wa 2027.

Tofauti hizo zimeonekana pia katika maandalizi ya maadhimisho ya kumbukumbu ya Raila. Familia yake imesisitiza kuwa shughuli za kumbukumbu ziandaliwe chini ya uongozi wake, huku ODM ikizindua ratiba yake ya maadhimisho ya mwezi mzima chini ya kaulimbiu ya "Mwezi wa Baba".

Matukio haya yameibua maswali kuhusu nani atakayekuwa msimamizi mkuu wa urithi wa kisiasa wa Raila Odinga na mwelekeo wa ODM katika kipindi cha baada yake.

Hofu kuhusu usalama wa shughuli za kisiasa

Mwaka mmoja baada ya Raila Odinga kuaga dunia mazingira ya kisiasa nchini Kenya yamebadilika kwa kiasi kikubwa, huku maswali kuhusu usalama na mustakabali wa ushindani wa kisiasa yakizidi kujitokeza kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027

Kwa zaidi ya miongo miwili, Raila alikuwa mmoja wa nguzo kuu za upinzani nchini, na kuondoka kwake kumeacha pengo kubwa ambalo limeathiri mizani ya kisiasa, mienendo ya vyama na ushindani wa uongozi katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Miongoni mwa masuala yanayozua hofu ni ongezeko la makundi ya wahuni wanaodaiwa kufadhiliwa na wanasiasa kwa malengo ya kisiasa. Waziri wa Mambo ya Ndani, Kipchumba Murkomen, amewahi kueleza wasiwasi kuhusu uwepo wa makundi ya kihalifu yanayotumiwa kuvuruga mikutano ya kisiasa na kuhatarisha usalama wa umma, hali inayoongeza wasiwasi wa uwezekano wa machafuko kadri uchaguzi unavyokaribia.

Wakati huohuo, kumekuwa na malalamiko kuhusu matumizi ya nguvu kupita kiasi na vyombo vya usalama wakati wa kushughulikia maandamano na mikusanyiko ya kisiasa. Hali hiyo imeibua mjadala kuhusu uhuru wa kisiasa, haki ya kukusanyika na namna ya kudumisha amani huku ushindani wa kisiasa ukizidi kupamba moto.

Kwa jumla, mazingira ya kisiasa yaliyojitokeza baada ya kifo cha Raila yameongeza ushindani wa kisiasa nchini, huku masuala ya usalama, mipasuko ya kisiasa na harakati za kujaza pengo la uongozi aliloliacha yakichukua nafasi kubwa katika mjadala wa kitaifa. Wachambuzi wanaonya kuwa namna vyama vya kisiasa, serikali na taasisi za usalama zitakavyosimamia kipindi hiki cha mpito itakuwa muhimu katika kudumisha utulivu wa nchi kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027.

Kuimarika kwa utamaduni wa kumuenzi Raila

Kifo cha Raila Amolo Odinga mnamo hakikuashiria tu mwisho wa safari ya mmoja wa wanasiasa mashuhuri zaidi barani Afrika, bali pia mwanzo wa mchakato wa kitaifa wa kutafakari na kuhifadhi urithi wake wa kisiasa.

Akiwa kiongozi aliyekuwa mstari wa mbele katika harakati za demokrasia, mageuzi ya kisiasa na utetezi wa haki za kiraia nchini Kenya kwa miongo kadhaa, Raila ameendelea kuwa kiungo muhimu katika historia ya kisasa ya taifa la Kenya hata baada ya kifo chake.

''Raila Odinga, alikuwa mzalendo sana...alikua mkombozi kwa sababu alikuwa anataka mageuzi kila mara. Alikua anashughulikia huduma za wananchi nyumbani Afrka na ulimwengu kwa ujumla. Bila shaka kumpata mtu kama yeye ambaye alikua amejitoa kuhakikisha tunapata suluhu ya matatizo yaliyotukabili kama nchi itakua vigumu..alisema Gavana James Orengo katika mahojiano na BBC.

Matokeo yake, kumeshuhudiwa kuimarika kwa utamaduni wa kumuenzi kupitia shughuli za kisiasa, hafla za kitaifa na matukio ya kijamii yanayolenga kuhifadhi kumbukumbu na mchango wake kwa vizazi vya sasa na vijavyo.