Miji ya Ufaransa yawa tulivu usiku kucha baada ya amri za kutotoka nje
Waziri Mkuu wa Ufaransa, Sébastien Lecornu, amesema kuwa utekelezaji wa amri maalum za kutotoka nje katika maeneo mbalimbali umechangia kuwepo kwa utulivu usiku uliopita, kufuatia wikendi iliyoshuhudia ghasia na uporaji katika sehemu kadhaa za nchi.
Amri hizo zilianzishwa katika maeneo ya katikati ya jiji la Paris, ikiwemo Place de la République, ambako waandamanaji walikuwa wamekusanyika mwishoni mwa wiki, pamoja na eneo la biashara la Les Halles.
Hatua nyingine za kuzuia mikusanyiko na kudhibiti harakati za vijana pia ziliwekwa katika miji ya Marseille, Bordeaux, Nice na Lyon kusini mwa Ufaransa, pamoja na Lille na miji mingine ya kaskazini.
Lecornu aliwashukuru maafisa wa polisi na askari wa Gendarmerie kwa kusimamia na kutekeleza hatua hizo za usalama, akisema zimechangia kurejesha utulivu katika maeneo yaliyoathirika.
Aidha, amesema uamuzi kuhusu kuendelea au kutekelezwa kwa amri nyingine za kutotoka nje usiku wa Jumanne utafanywa kulingana na hali ya usalama katika kila eneo.
Katika ujumbe aliouchapisha kwenye mtandao wa X, Lecornu alisema maamuzi hayo yatafanywa "moja kwa moja katika maeneo husika" na mamlaka za mikoa pamoja na mameya wa serikali za mitaa kulingana na mahitaji ya kila eneo.