Nani anayeongoza Kanisa Katoliki wakati Papa anapougua?

    • Author, Drafting*
    • Nafasi, BBC News Mundo
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Baada ya Papa Leo XIV kugunduliwa kuwa na saratani ya mapafu siku ya Jumanne, swali lililoikumba dunia mwezi Machi mwaka uliotangulia, wakati mtangulizi wake, Papa Fransisko, alipolazwa hospitalini, limeibuka tena: Je, hali hii ina maana gani kwa Kanisa?

Siku ya Jumatano, mwandishi wa habari wa Shirika la Habari la Associated Press (AP), Nicole Winfield, aliuliza swali ambalo Wakatoliki wote wanajiuliza: Ni nani anayechukua usukani wa Kanisa Katoliki wakati Papa amepoteza fahamu, hana uwezo wa kutekeleza majukumu yake, au hawezi kuliongoza Kanisa?

Jibu lake lilikuwa fupi, lenye maneno mawili tu: "Papa mwenyewe."

Jibu hilo fupi la Winfield linafafanua hali tata inayohusu uongozi wa Kanisa.

Tofauti na hali ya kifo au kujiuzulu, ambapo kuna taratibu zilizowekwa wazi za kumrithi kiongozi, hakuna utaratibu maalumu uliofafanuliwa kikamilifu wa kukabidhi uongozi wa Kanisa iwapo Papa hawezi kutekeleza majukumu yake yote kutokana na ugonjwa mahututi.

Papa Leo XIV, mwenye umri wa miaka 71, alifanyiwa upasuaji uliochukua dakika 90 katika Hospitali ya Gemelli jijini Roma, ambapo sehemu ya chini ya pafu lake la kulia iliondolewa.

Vatikani iliripoti kuwa Papa alikuwa katika hali ya utulivu usiku, na kuongeza kuwa taarifa zaidi kuhusu hali yake ya afya zingetolewa kadiri siku ilivyokuwa ikiendelea.

Kabla ya upasuaji huo, mkurugenzi wa Ofisi ya Habari ya Kiti Kitakatifu alikuwa amethibitisha ziara ya Papa Leo XIV nchini Uruguay, Argentina na Peru. Hata hivyo, baada ya utambuzi wa ugonjwa huo siku ya Jumanne, sasa kuna sintofahamu kuhusu iwapo ziara hizo zitaendelea kama ilivyopangwa.

Papa ndiye mwenye mamlaka ya juu zaidi katika Kanisa Katoliki na katika Dola ya Vatikani. Kwa hiyo, uongozi wake ni muhimu katika masuala ya kidini, kiutawala na kidiplomasia.

Papa anaposhindwa kutekeleza majukumu yake binafsi, shughuli za kiutawala za Kanisa husimamiwa na Kuria ya Roma (Roman Curia), chombo kikuu cha utawala wa Kanisa. Katika muundo huo, Katibu wa Nchi wa Vatikani ana nafasi muhimu sana. Kwa sasa, wadhifa huo unashikiliwa na Kardinali Pietro Parolin.

Sheria na taratibu zinasemaje?

Mwezi Machi 2025, Kanisa lilipokabiliwa na hali inayofanana na ile iliyotokana na kuugua kwa Papa Fransisko, Filipe Domingues, mkurugenzi wa Kituo cha Walei jijini Roma na mtaalamu wa masuala ya Vatikani, aliliambia BBC News Mundo kuwa iwapo Papa angepoteza fahamu, shughuli za Kanisa zingeendelea kwa kiasi kikubwa kama kawaida.

"Kila kardinali ana jukumu lake ndani ya Vatikani, na Katibu wa Nchi ana jukumu muhimu sana katika mazingira kama haya," alisema.

Pietro Parolin, ambaye kwa sasa anashikilia wadhifa huo, anasimamia masuala ya kidiplomasia na kiutawala. Kwa namna fulani, nafasi yake inafanana na ile ya waziri mkuu wa Vatikani.

Katika siku za hivi karibuni, waandishi wa habari walipomuuliza iwapo alikuwa na wasiwasi kuhusu afya ya Papa, Parolin alijibu:

"Ndiyo, kwa sababu kwa kweli sikutarajia jambo kama hili."

Hata hivyo, Katibu wa Nchi wa Vatikani aliongeza kuwa alikuwa amezungumza na Papa Jumatatu usiku, na mazungumzo hayo yakampa utulivu wa moyo.

"Ni jambo ambalo, namshukuru Mungu, tuliligundua mara moja. Na kwa kawaida, mambo ya aina hii yanapogunduliwa mapema, yanaweza kutatuliwa."

Hadi sasa, Parolin hajatoa maoni kuhusu utambuzi wa ugonjwa uliotangazwa katika saa za hivi karibuni.

Mamlaka ya Katibu wa Nchi haichukui nafasi ya mamlaka ya Papa. Domingues alisisitiza kuwa, "hawezi kufanya maamuzi ambayo ni haki ya Papa pekee, kama vile kuwateua maaskofu."

Miongoni mwa majukumu mengine yaliyohifadhiwa mahsusi kwa Papa ni kuidhinisha kutangazwa rasmi kwa watu kuwa watakatifu (canonization), pamoja na kutoa jumbe zake kwa waumini siku za Jumatano au Jumapili.

Ingawa Kiti Kitakatifu kina mifumo fulani inayokiwezesha kuendelea na shughuli zake hata kiongozi wake anapokuwa hayupo au hana uwezo wa kutekeleza majukumu yake, kuna mapungufu katika mfumo wa kanuni zake ambayo yanaweza kuleta changamoto iwapo hali ya afya ya Papa itazidi kuwa mbaya kwa kipindi kirefu.

Wataalamu wanaeleza kuwa sheria za kanisa (canon law), ambazo zinafafanua kwa kina taratibu za kumrithi Papa anapofariki au kujiuzulu, hazitoi mwongozo wa kutosha katika hali ambapo Papa bado yuko hai lakini hawezi kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

Kanuni ya 335 inataja uwezekano wa Kiti Kitakatifu kuwa "wazi" (vacant) au "kuzuiwa kabisa" (totally impeded). Hata hivyo, haifafanui maana halisi ya hali ya "kuzuiwa kabisa", wala haielezi hatua zinazopaswa kufuatwa hali hiyo inapotokea.

Kwa mfano, katika ngazi ya maaskofu, Kanisa lina taratibu zilizo wazi. Kwa mujibu wa Kanuni ya 412, dayosisi inaweza kutambuliwa kuwa katika hali ya kuzuiwa (impeded) iwapo askofu wake hawezi kutekeleza mamlaka yake kutokana na ugonjwa, uhamishoni au mazingira mengine yoyote. Katika hali hiyo, mamlaka hukabidhiwa kwa askofu msaidizi au kasisi mkuu wa utawala wa dayosisi (vicar general).

Hata hivyo, kwa kuwa hakuna kifungu sawia kinachohusu Papa, swali la nani anayepaswa kuchukua nafasi yake iwapo atashindwa kutekeleza majukumu yake bado halijapata jibu la kisheria lililo wazi.

Kujiuzulu

Kinadharia, iwapo Papa angekosa uwezo wa kuendelea na wadhifa wake kwa sababu za kiafya, suluhisho pekee lingekuwa kuachia Kiti cha Mtakatifu Petro, yaani kujiuzulu kutoka katika nafasi ya upapa.

Mwaka 1965, Papa Paulo VI aliandika barua kwa Mkuu wa Chuo cha Makardinali, akipendekeza kuwa iwapo angeugua ugonjwa mahututi, Mkuu huyo pamoja na makardinali wengine wakubali kujiuzulu kwake.

Papa Francis, akifahamu uwezekano huo, alithibitisha mwaka 2022 kuwa alikuwa ameandika barua ya kujiuzulu ambayo ingetumika iwapo angepoteza uwezo wa kutekeleza majukumu yake kutokana na hali ya kiafya.

Hata hivyo, swali linabaki kuhusu namna uamuzi huo wa kujiuzulu ungeweza kutekelezwa iwapo Papa asingekuwa tena na uwezo wa kueleza maamuzi yake. Hii ni kwa sababu sheria za kanisa zinaeleza kuwa kujiuzulu kwa Papa lazima kuwe kwa hiari na kutangazwe waziwazi.

Katika kisa cha Papa Benedikto XVI, aliyetawala kuanzia mwaka 2005 hadi 2013, yeye mwenyewe alitangaza hadharani uamuzi wake wa kujiuzulu.

Domingues alieleza: "Iwapo Papa angekuwa na ugonjwa wa Alzeima wa kupoteza kumbukumbu na kufikia wakati ambapo hangeweza tena kufanya uamuzi huo mwenyewe, mtu kutoka Sekretarieti ya Nchi angelipaswa kuitangaza barua hiyo hadharani na kuwasilisha ripoti ya kitabibu."

Mwaka 2021, kundi la wataalamu lilipendekeza kuwa iwapo Papa angepoteza kabisa uwezo wa kutekeleza majukumu yake, Chuo cha Makardinali kingepaswa kuchukua jukumu la kusimamia shughuli za Kanisa na kuteua tume ambayo ingekuwa inatathmini hali yake ya afya mara kwa mara.

Pendekezo hilo lingehusisha kamati ya madaktari inayopaswa kuchunguza hali ya afya ya Papa kila baada ya miezi sita. Iwapo uchunguzi ungeonyesha kuwa hawezi kuendelea na wadhifa wake, Chuo cha Makardinali kingeweza kuanzisha mchakato wa kumchagua mrithi wake.

Hata hivyo, hadi sasa, Vatikani haijatekeleza mapendekezo hayo wala mawazo mengine ya aina hiyo. Hii ina maana kuwa Kanisa Katoliki bado halina utaratibu rasmi uliowekwa wa kushughulikia hali ambapo Papa anapoteza uwezo wa kutekeleza majukumu yake kwa kipindi kirefu.

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Ambia Hirsi