Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Joseph Kabila: Kutoka urais hadi kuongoza muungano unaojumuisha M23
- Author, Ambia Hirsi
- Nafasi, BBC Swahili
- Akiripoti kutoka, Nairobi
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Aliingia madarakani mwaka 2001 baada ya kuuawa kwa baba yake. Laurent-Désiré Kabila, akaiongoza Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa karibu miaka 18 kabla ya kuondoka madarakani mwaka 2019. Sasa, rais huyo wa zamani ameteuliwa kuwa kiongozi wa muungano mpya wa kisiasa na kijeshi unaojumuisha kundi la waasi la M23.
Kwa zaidi ya miongo miwili, Joseph Kabila Kabange amekuwa mmoja wa watu wenye ushawishi mkubwa katika siasa za DRC.
Kuanzia kuteuliwa kuwa rais akiwa na umri wa miaka 29, hadi kuondoka madarakani mwaka 2019, safari yake ya kisiasa imegubikwa na vita, chaguzi zilizozua mabishano, mivutano ya kisiasa na sasa jukumu jipya katika muungano unaoipinga serikali ya Rais Félix Tshisekedi.
Safari hiyo inaonyesha kwa kiasi kikubwa mabadiliko ya kisiasa yaliyoikumba DR Congo katika kipindi cha zaidi ya miaka 25 iliyopita, huku mgogoro wa mashariki mwa nchi ukiendelea kuwa moja ya changamoto kubwa kwa taifa hilo.
Oktoba 12, 2026, Joseph Kabila alitangazwa kuwa kiongozi wa Front for the Refoundation of the Nation (FRN), muungano mpya wa kisiasa na kijeshi unaojumuisha waasi wa M23 pamoja na makundi mengine yanayoipinga serikali ya Kinshasa.
Tangazo hilo limefungua sura mpya katika safari ya kisiasa ya Kabila huku likizua maswali kuhusu mustakabali wa mgogoro wa mashariki mwa nchi na hatma ya juhudi za kuleta amani.
Lakini Kabila alifikaje katika hatua hii?
Januari 2001: Aingia madarakani akiwa na miaka 29
Mnamo 16 Januari 2001, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Laurent-Désiré Kabila, aliuawa na mmoja wa walinzi wake wa karibu, tukio lililolitumbukiza taifa hilo katika kipindi cha sintofahamu ya kisiasa.
Siku chache baadaye, mwanawe, Joseph Kabila, aliteuliwa kumrithi akiwa na umri wa miaka 29 pekee, na kuwa mmoja wa viongozi vijana zaidi barani Afrika wakati huo.
Kabila alikabidhiwa uongozi wa nchi iliyokuwa katikati ya Vita vya Pili vya Congo, mzozo uliowahusisha majeshi ya serikali, makundi mbalimbali yenye silaha na mataifa ya eneo la Maziwa Makuu ya Afrika.
Changamoto yake ya kwanza ilikuwa kuiongoza nchi iliyogawanywa na vita, huku akitafuta njia ya kurejesha utulivu, kuendeleza juhudi za amani na kuimarisha mamlaka ya serikali katika taifa lililokumbwa na mzozo wa muda mrefu.
Kuteuliwa kwake kulionekana na wengi kama mwanzo wa enzi mpya kwa DRC, huku matumaini yakiongezeka kwamba kiongozi huyo kijana angeweza kusaidia kuiongoza nchi kuelekea amani na maridhiano ya kitaifa.
2003: Serikali ya mpito yaanzishwa
Mwaka 2006, DRC ilifanya uchaguzi wa urais kama sehemu ya juhudi za kurejesha utawala wa kiraia baada ya miaka ya vita. Joseph Kabila alimshinda Jean-Pierre Bemba katika duru ya pili ya kura, na hivyo kupata uhalali wa kisiasa kupitia sanduku la kura.
Hata hivyo, ushindi huo haukumaliza changamoto za usalama na utawala zilizokuwa zikiikabili nchi hiyo.
Makubaliano ya amani yanafungua njia ya kuundwa kwa serikali ya mpito inayowajumuisha wawakilishi wa makundi mbalimbali yaliyokuwa yakipigana.
Kabila aliendelea kuiongoza nchi huku mchakato wa kurejesha utulivu ukiendelea.
2006: Ashinda uchaguzi wa kwanza wa urais
Miaka mitano baadaye, Kabila alikabiliwa na mtihani mwingine mkubwa: uchaguzi.
Mwaka 2006 alishinda uchaguzi wa urais dhidi ya kiongozi wa zamani wa waasi Jean-Pierre Bemba katika uchaguzi uliogubikwa na vurugu.
Ushindi huo ulimpa uhalali wa kisiasa kupitia kura za wananchi na kuibua matumaini kuwa DRC ingeanza kuondoka katika enzi za vita kuelekea utulivu. Hata hivyo, ushindi wa uchaguzi haukumaanisha mwisho wa changamoto za kujenga amani ya kudumu.
2011: Muhula wa pili waanza
Kabila anashinda uchaguzi wa pili wa urais na kuendelea kuongoza nchi kwa muhula mwingine wa miaka mitano.
Hata hivyo, uchaguzi huo unakabiliwa na ukosoaji kutoka kwa sehemu ya upinzani kuhusu namna ulivyoendeshwa.
2016: Mgogoro wa kisiasa wazuka
Kabila alishinda muhula wa pili mwaka 2011. Lakini muhula huo ulipokaribia mwisho wake wa kikatiba mwezi Desemba 2016, mvutano wa kisiasa uliongezeka.
Uchaguzi uliahirishwa mara kadhaa, maandamano yakazuka, huku wapinzani wakimtuhumu Kabila kwa kutaka kuendelea kushikilia madaraka.
Aliendelea kubaki madarakani baada ya muda wake wa kikatiba kumalizika, jambo lililozua mzozo mkubwa wa kisiasa. Mwanasiasa aliyewahi kuonekana kama ishara ya mwanzo mpya baada ya vita sasa alikuwa katikati ya mjadala kuhusu mipaka ya madaraka.
2018-2019: Ang'atuka baada ya miaka 18 madarakani
Baada ya miaka kadhaa ya shinikizo kutoka ndani na nje ya nchi, DRC ilifanya uchaguzi wa urais mwezi Desemba 2018.
Mgombea wa upinzani Félix Tshisekedi alitangazwa mshindi na kuapishwa Januari 2019, katika kile kilichoelezwa kuwa uhamishaji wa kwanza wa madaraka kwa njia ya amani kati ya marais waliochaguliwa nchini humo.
Kabila aliondoka madarakani baada ya karibu miaka 18 ya utawala. Hata hivyo, kuondoka Ikulu hakukumaanisha kuachana kabisa na siasa. Uhusiano kati yake na mrithi wake ulizidi kuwa muhimu katika siasa za DRC.
2025: Kurejea mashariki mwa Congo na kuhukumiwa kifo bila kuwa mahakamani
Mwaka 2025, Joseph Kabila alirejea kwenye ulingo wa siasa za DRC baada ya kuonekana mjini Goma, mashariki mwa nchi, wakati mji huo ukiwa chini ya udhibiti wa waasi wa M23.
Hatua hiyo ilizidisha mjadala kuhusu nafasi yake katika mzozo unaoendelea mashariki mwa DRC. Serikali ya Kinshasa ilimtuhumu kwa kuunga mkono waasi wa M23 na muungano wa Alliance Fleuve Congo (AFC), madai ambayo Kabila aliyakanusha.
Baadaye mwaka huo, mahakama ya kijeshi nchini DRC ilimhukumu kifo akiwa hayupo mahakamani baada ya kumtia hatiani kwa makosa yaliyodaiwa kujumuisha uhaini, uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.
Kabila alipinga hukumu hiyo, akiitaja kuwa ya kisiasa na iliyolenga kumdhoofisha kisiasa.
Kurejea kwake mashariki mwa DRC pamoja na hukumu hiyo kulizidisha uchunguzi kuhusu uhusiano wake unaodaiwa kuwepo na M23, na kumrejesha katikati ya mjadala kuhusu mgogoro unaoendelea nchini humo.
Oktoba 12, 2026: Kabila ateuliwa kuongoza muungano mpya
Mnamo Oktoba 12, 2026, Joseph Kabila alitangazwa kuwa kiongozi wa Front for the Refoundation of the Nation (FRN), muungano mpya wa kisiasa na kijeshi uliozinduliwa mjini Goma, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Muungano huo unajumuisha kundi la waasi la M23 pamoja na viongozi wa makundi ambayo hapo awali yalihusishwa na Alliance Fleuve Congo (AFC). Miongoni mwa viongozi wake ni Corneille Nangaa na Bertrand Bisimwa, huku Jenerali Sultani Makenga akipewa jukumu la kusimamia masuala ya kijeshi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa muungano huo, mshauri wake Claude Ibalanky alisema lengo ni kuunganisha makundi mbalimbali yanayoipinga serikali ya Kinshasa ili kukabiliana na kile walichokitaja kuwa utawala wa mabavu. Pia alieleza kuwa muungano huo haujafunga mlango kwa matumizi ya nguvu katika kufanikisha malengo yake ya kisiasa.
Tangazo hilo linaashiria hatua mpya katika safari ya kisiasa ya Kabila. Mwanasiasa huyo aliyewahi kuiongoza DRC kwa karibu miaka 18 sasa anaongoza muungano unaoipinga serikali ya nchi hiyo na unaojumuisha kundi lenye silaha linalopambana na jeshi la taifa.
Hatua hiyo inaongeza sura mpya katika mzozo wa mashariki mwa DRC, huku ikizua maswali kuhusu athari zake kwa juhudi za amani na uthabiti wa kisiasa nchini humo.
Serikali ya Kinshasa bado haijatoa tamko rasmi baada ya kwa muungano huo kutangazwa.
Nini kinafuata?
Kuibuka kwa muungano huo kumeibua maswali mapya kuhusu mustakabali wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Je, uongozi wa Joseph Kabila utabadilisha mwelekeo wa makundi yenye silaha yanayoendesha operesheni mashariki mwa nchi? Hatua hiyo itaathiri kwa kiwango gani juhudi za amani na mazungumzo ya kisiasa? Na kwa mamilioni ya raia wanaoishi katika maeneo yaliyoathiriwa na mapigano, hali ya usalama itakuwaje katika siku zijazo?
Kwa sasa, hakuna majibu ya wazi kwa maswali hayo.
Kilicho dhahiri ni kwamba Joseph Kabila, aliyeingia madarakani mwaka 2001 wakati DRC ikiwa katikati ya vita, amerejea tena katika kitovu cha mgogoro unaoendelea kuikumba nchi hiyo.
Safari yake kutoka Ikulu ya Kinshasa hadi kuongoza muungano unaojumuisha waasi wa M23 inaonyesha jinsi mwelekeo wa kisiasa wa DRC unavyoendelea kubadilika. Hata hivyo, licha ya mabadiliko hayo, harakati za kutafuta amani ya kudumu bado zinaendelea kuwa mojawapo ya changamoto kubwa zinazoikabili nchi hiyo.