Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Wahouthi waua 53 katika shambulizi dhidi ya kambi ya kijeshi
Video zilizothibitishwa na shirika la habari la Reuters zinaonyesha watu waliojeruhiwa na miili yenye damu ikiwa imetapakaa ardhini katika eneo hilo la mkoa wa Shabwa.
Muhtasari
- Ufaransa yaidhinisha amri ya kutotoka nje kukabiliana na ghasia
- Urusi yasema haitasitisha ushirikiano wa kimkakati na Iran
- Marekani yatoa tahadhari ya kiusalama kwa raia wake wanaoishi Mashariki ya Kati
- Watu 53 wauawa katika shambulizi la Wahouthi dhidi ya kambi ya mafunzo ya kijeshi Yemen
- Iran: Marekani ikitushambulia kwa mabomu yenye nguvu, wanajeshi wake wataangamizwa
- Amnesty yaitaka Kenya kushughulikia malalamiko yanayochochea maandamano
- Mkulima wa Eritrea atambuliwa miongoni mwa wanawake 100 mashujaa wa mwaka 2026
- Marekani yaonya kuhusu uwezekano wa vita kati ya Ethiopia na Eritrea
- Mashabiki wa muziki wa Reggae wamkumbuka Lucky Dube
- Macky Sall ajiondoa katika kinyang'anyiro cha ukatibu mkuu wa Umoja wa Mataifa
- UN kupunguza msaada wa chakula kwa wakazi wa Gaza
- Mzozo wa Iran: IRGC yatoa vitisho dhidi ya Trump na Netanyahu
- Saudi Arabia yawanyonga Wabangladesh wawili kwa tuhuma za vitendo visivyo vya maadili msikitini Makka
- Rais Macron apinga kujiuzulu kwa waziri wa usalama wa ndani baada ya ghasia
- Human Rights Watch yaishtumu jeshi la Mali na Urusi kwa mauaji ya raia
- DRC yamshutumu Kabila kwa kuunga mkono kundi la waasi
- Rais Macron atoa wito wa utulivu Ufaransa, baada ya maandamano kugeuka ghasia
- Tetesi za Soka Ulaya: Beki huyu wa Hispania kutua Getafe?
- Misri kutoa msaada wa kijeshi kwa Saudi Arabia kudhibiti Wahouthi
- Ndege ya Austrian Airlines yatua kwa dharura Bulgaria baada ya tishio la bomu
- Mchungaji Paul Mackenzie kusomewa hukumu katika mauaji ya Shakahola
- Visa vya Ebola vyaongezeka Kenya na kufikia nane
Moja kwa moja
Na Beldeen Waliaula & Mariam Mjahid
Ufaransa yaidhinisha amri ya kutotoka nje kukabiliana na ghasia
Waziri wa Ulinzi wa Ufaransa, Sébastien Lecornu, amesema waziri mkuu amewapa viongozi wa maeneo mamlaka ya kuweka amri ya kutotoka nje kwa muda katika baadhi ya maeneo ya nchi hiyo, kwa lengo la kulinda maisha ya watu na mali zao.
Amesema Waziri wa Sheria atatoa taarifa baadaye kuhusu hatua zinazochukuliwa na serikali kuzuia ghasia zaidi.
Lecornu amesema uchunguzi mkubwa utaanza leo mjini Paris, ambapo wachunguzi 200 watachunguza video za ghasia zilizotokea mwishoni mwa wiki.
Amesema uchunguzi huo unatarajiwa kusaidia kuwabaini waliohusika na ghasia hizo na kuchukua hatua za kisheria dhidi yao.
Soma Pia:
Urusi yasema haitasitisha ushirikiano wa kimkakati na Iran
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov, amesema nchi yake haitaachana na ushirikiano wake na Iran, akibainisha kuwa uhusiano wa kimkakati kati ya mataifa hayo mawili unaendelea kuimarika.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Tehran Jumatatu, akiwa pamoja na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, Lavrov amesema Moscow imejizatiti kikamilifu kutekeleza makubaliano ya kimkakati kati ya nchi hizo na haitaachana na ushirikiano huo.
Lavrov amesema Urusi imejitolea kuipatia Iran msaada wa chakula na vifaa vya matibabu. Pia amesema Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, atahudhuria mkutano kuhusu gesi mjini Moscow.
Kwa upande wake, Araqchi amesema nchi hizo mbili zinakubaliana kuwa hakuna suluhisho la kijeshi kwa changamoto za Mashariki ya Kati.
Ameihusisha hali ya ukosefu wa usalama katika eneo hilo na Marekani, vita dhidi ya Iran na vizuizi vya usafiri wa baharini.
Araqchi amesema pia amejadili hali katika Mlango-Bahari wa Hormuz na Ghuba ya Uajemi na Lavrov.
Soma pia:
Marekani yatoa tahadhari ya kiusalama kwa raia wake wanaoishi Mashariki ya Kati
Balozi za Marekani katika maeneo mbalimbali ya Mashariki ya Kati zimewataka raia wa nchi hiyo kuwa waangalifu zaidi kutokana na hali tata ya usalama na usumbufu katika usafiri.
Tahadhari iliyotolewa na balozi za Marekani katika nchi za Ghuba ya Uajemi, Israel, Iraq, Lebanon na Jordan inasema raia wa Marekani waliopo Mashariki ya Kati wanapaswa kuongeza umakini kutokana na hali ya usalama katika eneo hilo.
Tahadhari hiyo pia inawaonya kuhusu uwezekano wa safari za ndege kufutwa, anga kufungwa na huduma za usafiri kuvurugika.
Balozi hizo zimeonya kuwa vita vinaweza kusambaa kwa haraka na kuathiri maeneo mengine.
Raia wa Marekani wametakiwa kufuatilia taarifa kuhusu safari za ndege na kuwa na mipango mbadala iwapo dharura itatokea.
Tahadhari hiyo pia imetaja mashambulizi ya waasi wa Kihouthi wa Yemen dhidi ya Saudi Arabia. Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Riyadh unaendelea kufungwa baada ya watu 18 kuuawa katika mashambulizi hayo.
Rais wa Marekani, Donald Trump, na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, walitishia jana kukamilisha makubaliano hayo hivi karibuni. Kauli hiyo ilijibiwa vikali na Iran, ambayo nayo ilitoa vitisho vya kulipiza kisasi.
Pia Unaweza Kusoma:
Watu 53 wauawa katika shambulizi la Wahouthi dhidi ya kambi ya mafunzo ya kijeshi Yemen
Takriban watu 53 wameuawa, wengine 200 kujeruhiwa vibaya hii leo katika shambulizi la Wahouthi dhidi ya kambi ya mafunzo ya kijeshi ya vikosi vya serikali ya Yemen katika mkoa wa Shabwa, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, likinukuu vyanzo vinne kutoka serikalini na sekta ya afya.
Video zilizothibitishwa na shirika la habari la Reuters zinaonyesha watu waliojeruhiwa pamoja na miili yenye damu ikiwa imetapakaa ardhini katika eneo hilo la mkoa wa Shabwa.
Maafisa wa eneo hilo wameiambia Reuters, kwa sharti la kutotajwa majina yao, kuwa Wahouthi walirusha makombora matatu ya balistiki dhidi ya vikosi vya usalama wakati mafunzo ya kijeshi yakiendelea katika kambi hiyo.
Wahouthi wamekubali kuhusika na shambulizi hilo
Wahouthi wamekuwa wakishambulia mara kwa mara vituo vinavyohusishwa na serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa, pamoja na vikosi vinavyoungwa mkono na muungano unaoongozwa na Saudi Arabia.
Awali, Wahouthi walirusha makombora matano ya balistiki kuelekea Jumba la Al Maashiq, ambalo walisema ni kituo cha operesheni cha muungano huo.
Taarifa za hivi karibuni zinaeleza kuwa watu watano waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa katika shambulizi hilo.
Jumba la Al Maashiq ni miongoni mwa makao makuu ya serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa.
Pia unaweza kusoma:
Michael Carrick ashinikizwa kufuatia matokeo duni ya Man utd
Kocha wa Manchester United, Michael Carrick, anakabiliwa na shinikizo zaidi baada ya timu yake kutoka sare ya bao 1 kwa 1 dhidi ya Leeds United katika mchezo wa Ligi Kuu England uliochezwa jana katika uwanja wa Elland Road.
Matokeo hayo yameendeleza kipindi kigumu kwa United, ambayo imeshinda mechi moja pekee kati ya saba za ligi msimu huu na kukusanya pointi saba, hali inayoendelea kuzua maswali kuhusu kiwango cha timu hiyo na uwezo wake wa kurejea katika ushindani.
Manchester United ilitangulia kupata bao kupitia Bryan Mbeumo dakika ya 35, lakini Leeds ilisawazisha kupitia Dominic Calvert Lewin dakika ya 51 na kufanya timu hizo kugawana pointi.
Akijibu maswali kuhusu mwanzo huo usioridhisha wa msimu, Carrick amekiri kuwa hali ya timu hiyo si nzuri, lakini amesema ana imani kuwa kikosi chake kina uwezo wa kubadilisha matokeo.
“Hatusemi kwamba kila kitu kiko sawa. Wakati mwingine unapitia kipindi kigumu na inabidi utafute namna ya kukivuka. Sina shaka kwamba tunaweza kupata mfululizo mzuri wa matokeo,” amesema Carrick.
Kocha huyo ameongeza kuwa timu inahitaji kuwa thabiti na kuendelea kufanya mambo sahihi ili kuvuka kipindi hicho, akisisitiza kuwa anaamini wachezaji wake wana uwezo wa kushinda mechi.
Hata hivyo, sare hiyo haijaondoa wasiwasi kuhusu mwenendo wa United, ambayo sasa inahitaji matokeo mazuri ili kurejesha imani ya mashabiki na kuboresha nafasi yake katika msimamo wa ligi.
United kwa sasa inashika nafasi ya 13 ikiwa na pointi saba baada ya mechi saba, huku Carrick akitarajiwa kutafuta suluhisho la matatizo yanayoendelea kuikabili timu yake.
Obama amtetea Ilhan Omar, aonya dhidi ya matumizi ya vyombo vya dola kwa shinikizo la kisiasa
Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama, amemtetea mbunge Ilhan Omar baada ya maafisa wa serikali ya shirikisho kufanya upekuzi katika makazi yake mjini Washington, akionya kuwa matumizi ya vyombo vya sheria kuwalenga watu kwa misimamo yao ya kisiasa yanaweza kuhatarisha demokrasia ya nchi hiyo.
Ilhan Omar, ambaye ni mbunge wa Baraza la Wawakilishi la Marekani kutoka jimbo la Minnesota, amekanusha vikali kufanya kosa lolote. Amesema uchunguzi dhidi yake una chocheo la kisiasa na unalenga kuwatisha wakosoaji wa utawala wa Rais Donald Trump.
Katika taarifa yake, Obama amesema mojawapo ya misingi muhimu ya demokrasia ya Marekani ni kwamba serikali haipaswi kumlenga mtu kwa sababu ya maoni yake au kauli zake za kisiasa, isipokuwa pale zinapohusisha uchochezi wa ghasia au mzozo.
“Hili ndilo hasa utawala wa Trump unalofanya dhidi ya Mwakilishi Ilhan Omar wa Minnesota,” amesema Obama.
Obama pia ameeleza historia ya Omar, akisema alifika Marekani akiwa na umri wa miaka 12, akisafiri pamoja na baba yake, ambaye alipata uraia wa Marekani miaka mitano baadaye. Amesema Omar naye alipata uraia wa Marekani moja kwa moja, kwa kuwa wakati huo alikuwa na umri wa miaka 17.
Ameongeza kuwa Omar alihitimu masomo ya chuo kikuu na kufanya kazi katika shughuli za kuhamasisha na kuandaa jamii kabla ya kuwa mwanasiasa wa kwanza mwenye asili ya Somalia kuchaguliwa kushika wadhifa katika chombo cha kutunga sheria nchini Marekani. Baadaye alichaguliwa kuwa mjumbe wa Baraza la Wawakilishi.
Obama amesema Omar ni miongoni mwa wakosoaji wakubwa wa utawala wa Trump, akidai kuwa hali hiyo ndiyo inayochangia rais huyo kuwalenga wabunge fulani moja kwa moja.
Ameongeza kuwa utawala wa Trump sasa unajaribu kumfukuza Omar nchini Marekani, akisema hatua hiyo inaonekana kutegemea tuhuma zisizothibitishwa kuhusu umri wake wakati baba yake alipopata uraia wa Marekani.
Unaweza pia kusoma:
Iran: Marekani ikitushambulia kwa mabomu yenye nguvu, wanajeshi wake wataangamizwa
Wakati Bunge la Iran likipiga kura kuidhinisha mawaziri wapya, Mehrdad Akhlaqi amewaambia waandishi wa habari kuwa nchi yake imejiandaa kukabiliana na uwezekano wa Marekani kutumia bomu lenye nguvu kubwa linalojulikana kama ''Mama wa mabomu yote''.
Amesema: “Tumefanya maamuzi yanayohitajika kuhusu suala hili na tuko watulivu. Tunaendelea na kazi yetu bila hofu, tukiwa na imani katika uwezo wetu.”
Baada ya kuthibitishwa kuwa waziri mpya wa ulinzi, Akhlaqi amesema Rais wa Marekani anapaswa kufikiria namna ya kuwaondoa wanajeshi wake katika eneo hilo kwa usalama.
“Akidondosha bomu hilo, ataona ni wanajeshi wangapi atalazimika kuwaondoa katika eneo hili wakiwa wamekufa,” alisema.
Kwa mujibu wa waziri huyo, ndiyo sababu Marekani haijafikia hatua ya kutekeleza vitisho vyake hadi sasa. Hata hivyo, alionya kuwa iwapo Marekani itabadilisha vitisho vyake kutoka maneno na kuvigeuza vitendo, itakabiliana na matokeo yake.
Pia Unaweza Kusoma:
Amnesty yaitaka Kenya kushughulikia malalamiko yanayochochea maandamano
Shirika la kutetea haki za binadamu la Amnesty International limeitaka serikali ya Kenya kushughulikia malalamiko ya kiuchumi yanayochochea maandamano yanayoongozwa na vijana, na kukomesha kile ilichokitaja kuwa ukandamizaji unaozidi kuongezeka dhidi ya wakosoaji wa serikali, ukiwemo ukamataji wa kiholela, utekaji nyara, mateso na ufuatiliaji wa watu.
Katika ripoti iliyotolewa Jumatatu, Oktoba 19, 2026, shirika hilo limeeleza madai ya ukiukaji wa haki dhidi ya waandamanaji, wanaharakati na waandishi wa habari wakati wa maandamano yaliyofanyika kati ya mwaka 2023 na 2025.
Ripoti hiyo, yenye kichwa Haki za Binadamu Ziko Hatarini: Kuchunguza Mbinu za Kiimla Katika Kipindi cha Shinikizo la Kiuchumi na Maandamano Yanayoongozwa na Vijana nchini Kenya, inahusisha maandamano hayo na kupanda kwa gharama za chakula na usafiri, kuongezeka kwa kodi na tozo, deni la umma, ufisadi, umaskini, ukosefu wa usawa na ahadi za uchaguzi ambazo hazijatekelezwa.
“Matokeo ya ripoti hii yanatia wasiwasi na yanaonyesha wazi namna serikali ya Kenya inavyojibu kwa ukandamizaji malalamiko halisi yanayoathiri maisha ya kila siku ya wananchi wa kawaida,” amesema Mkurugenzi Mtendaji wa Amnesty International nchini Kenya, George Morara.
Aidha, amewataka viongozi kushughulikia changamoto za kiuchumi zinazosababisha malalamiko hayo, kukomesha ukandamizaji dhidi ya wakosoaji wa serikali na kuhakikisha wanaohusika na ukiukaji wa haki za binadamu wakati wa maandamano wanawajibishwa.
Kati ya Aprili na Julai 2026, watafiti wa Amnesty International waliwahoji watu 102, wakiwemo waandamanaji, mawakili, waandishi wa habari, maafisa wa serikali, wahudumu wa afya na wanaharakati wa mashirika ya kiraia.
Pia walichunguza kumbukumbu za Bunge, bajeti na sera za kodi za kipindi cha mwaka 2023 hadi 2025.
Ripoti hiyo imekusanya ushuhuda wa watu 36 kutoka kaunti tano, ambao walisema walikamatwa na polisi au kutekwa nyara na watu wanaoshukiwa kuwa maafisa wa usalama, wakati wa maandamano au baada yake.
Baadhi yao walisema walizuiliwa kwa siku kadhaa, kupigwa, kuteswa au kuhojiwa bila uwakilishi wa kisheria. Wengine walisema walizuiwa kuwasiliana na familia zao.
Benjamin*, ambaye alituhumiwa kuandaa maandamano mjini Kisumu kupinga gharama ya maisha na miswada tata ya fedha, aliwaeleza watafiti jinsi alivyochukuliwa na kupelekwa eneo asilolifahamu.
“Nilichukuliwa na kupelekwa mahali nisipopajua na kufungiwa huko usiku kucha. Siku iliyofuata, majira ya saa tano asubuhi, walinivua nguo na kunitupa katika chumba kilichokuwa katikati ya shamba la miwa la Chemelil,” aliwaambia watafiti.
Shirika hilo pia limeandika madai ya ufuatiliaji usio halali uliolenga simu za waandamanaji, makundi ya WhatsApp, mijadala kwenye mitandao ya kijamii na makazi ya familia zao.
Vile vile, Waandamanaji 54 waliohojiwa na Amnesty walisema ufisadi ni miongoni mwa sababu kuu zilizowafanya kuandamana, wakipinga kuendelea kufujwa kwa fedha za umma zilizotengwa kwa ajili ya huduma za kijamii na ulinzi wa wananchi, wakati gharama za chakula na mafuta zikiendelea kupanda.
“Mantiki ya kuongeza kodi haieleweki. Serikali inapaswa kushughulikia ufisadi na kuwawajibisha wanaohusika,” alisema mmoja wa waandamanaji.
Soma Pia:
Mkulima wa Eritrea atambuliwa miongoni mwa wanawake 100 mashujaa wa mwaka 2026
Mkulima kutoka Eritrea ametambuliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) kuwa miongoni mwa “Wanawake 100 Mashujaa wa mwaka 2026”, kwa mchango wake katika sekta ya kilimo na mifumo ya chakula.
Kwa mujibu wa Wizara ya Kilimo ya Eritrea, Rosina Mebrahtom alipokea tuzo hiyo Oktoba 16, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani yaliyofanyika mjini Roma, Italia.
Rosina alichaguliwa miongoni mwa wanawake 100 baada ya kuungwa mkono kupitia mapendekezo zaidi ya 600 kutoka nchi 131. Wanawake hao walitambuliwa na FAO kwa mchango wao katika kuendeleza kilimo na mifumo ya uzalishaji na usambazaji wa chakula.
Wizara ya Kilimo imesema Rosina alitambuliwa kwa juhudi zake za kurejesha ardhi iliyoharibika katika uzalishaji, kuhifadhi rasilimali za asili na kuendeleza kilimo hai.
Kupitia kazi yake, amefanikiwa kubadilisha ardhi iliyokuwa kame na yenye chumvi nyingi, ambayo hapo awali haikufaa kwa kilimo, na kuifanya kuwa yenye rutuba na inayoweza kuzalisha mazao.
Kwa mujibu wa wizara hiyo, FAO pia ilizingatia dhamira yake ya kulinda mazingira, kuimarisha usalama wa chakula na kuboresha maisha ya jamii za vijijini.
Rosina ni mkulima anayejishughulisha na shughuli mbalimbali za kilimo na ufugaji. Anaishi katika kijiji cha Mesalih, utawala wa Tekonda, eneo la Adikeih, kusini mwa Eritrea. Analima mazao na mboga, pamoja na kufuga mifugo.
Wizara ya Kilimo ya Eritrea imekuwa ikihimiza mfumo wa kilimo jumuishi cha familia, unaolenga kuwawezesha wakulima kuzalisha aina mbalimbali za vyakula vyenye virutubisho.
Mfumo huo unajumuisha ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na kondoo, kilimo cha mazao, mboga na matunda, ufugaji wa kuku, ufugaji wa nyuki na uzalishaji wa asali, upandaji miti, utengenezaji wa mboji na uhifadhi wa malisho ya mifugo.
Lengo ni kuongeza uzalishaji wa chakula, kuboresha lishe ya kaya na kuimarisha maisha ya wakulima.
Soma Pia:
Marekani yaonya kuhusu uwezekano wa vita kati ya Ethiopia na Eritrea
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, amewataka viongozi wa Ethiopia na Eritrea kujizuia na kuepuka hatua zinazoweza kuongeza mvutano wa kijeshi mpakani mwa nchi hizo, akionya kuwa hali hiyo inaweza kusababisha vita.
Rubio amesema ana wasiwasi mkubwa kuhusu taarifa za kuongezeka kwa harakati za wanajeshi katika mpaka wa Ethiopia na Eritrea. Ameonya kuwa kuendelea kupeleka na kukusanya wanajeshi mpakani kunaongeza hatari ya kuzuka kwa vita.
Wakati wa vita vya mwaka 2020 hadi 2022 kati ya jeshi la serikali ya Ethiopia na vikosi vya Tigray, jeshi la Eritrea liliunga mkono jeshi la serikali ya shirikisho na kushiriki katika mapigano dhidi ya vikosi vya Tigray.
Hata hivyo, baada ya vita hivyo kumalizika kupitia Mkataba wa Pretoria, tofauti zilianza kujitokeza kati ya serikali za Ethiopia na Eritrea.
Maafisa kadhaa waandamizi wa Ethiopia, akiwemo Waziri Mkuu Abiy Ahmed, wamekuwa wakisema wazi kuwa nchi hiyo inahitaji bandari. Abiy amesisitiza kuwa Ethiopia, yenye wakazi takribani milioni 130 na uchumi unaokua, haiwezi kuendelea kukosa njia ya moja kwa moja ya kufikia bahari.
Kwa upande wa Ethiopia, Eritrea inatuhumiwa kushirikiana na chama cha TPLF na makundi mengine yenye silaha nchini humo kwa lengo la kuigawa Ethiopia.
Nchi hizo mbili zimekuwa katika mvutano wa kidiplomasia huku hali ya kijeshi mpakani ikiendelea kuibua wasiwasi.
Baada ya vikosi vya Tigray vilivyokuwa vimeelekea kusini mwa eneo hilo kurejea upande wa mpaka wa Eritrea, kumekuwa na ongezeko la wanajeshi wa Eritrea na wa serikali ya shirikisho la Ethiopia katika maeneo ya mpakani.
Akizungumza na waandishi wa habari, Rubio alisema:
“Unaona wanajeshi wakielekea mpakani kutoka pande zote mbili. Katika hali kama hii, unapowaona wanajeshi wa pande zote mbili wakikusanyika mpakani, huwa na wasiwasi kwamba hali hiyo inaweza kugeuka na kuwa mzozo mkubwa zaidi.”
Aliongeza kuwa dunia haihitaji vita nyingine kwa sasa.
Soma pia:
Mashabiki wa muziki wa Reggae wamkumbuka Lucky Dube
Mashabiki wa mwanamuziki Lucky Dube wameingia mtandaoni na kucheza baadhi ya nyimbo zake huku wakieleza kuwa atazidi kuishi mioyoni mwao.
Haya yanajiri wakati zikitimia miaka 19 tangu kuuawa kwa Lucky Philip Dube, mwanamuziki mashuhuri wa reggae kutoka Afrika Kusini, aliyepigwa risasi na kufariki dunia Oktoba 18, 2007.
Dube aliuawa Oktoba 18, 2007, mjini Johannesburg, akiwa na umri wa miaka 43.
Wakati huo, alikuwa miongoni mwa wanamuziki wa reggae waliofanikiwa zaidi nchini Afrika Kusini, akiwa ameuza idadi kubwa ya albamu. Alipata umaarufu mkubwa nchini humo na kimataifa kupitia nyimbo zilizoangazia ukandamizaji na dhuluma walizokumbana nazo Waafrika Kusini wakati wa utawala wa ubaguzi wa rangi, uliokuwa ukijulikana kama apartheid.
Albamu yake ya kwanza iliitwa Rasta Never Die. Hata hivyo, kutokana na sera za utawala wa wazungu wakati huo, albamu hiyo ilipigwa marufuku katika vituo mbalimbali vya redio nchini Afrika Kusini.
Kwa wengi, urithi wa Lucky Dube unaenda mbali zaidi ya muziki na uimbaji. Anakumbukwa kama mmoja wa wanamuziki wakubwa wa reggae barani Afrika, aliyetumia nyimbo zake kuwasilisha ujumbe kuhusu uhuru, usawa mbele ya sheria, ubaguzi wa rangi, ukosefu wa haki na utu wa binadamu.
Macky Sall ajiondoa katika kinyang’anyiro cha ukatibu mkuu wa Umoja wa Mataifa
Aliyekuwa rais wa Senegal, Macky Sall, amejiondoa katika kinyang’anyiro cha kuwania nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
Katika taarifa iliyotolewa Jumamosi mjini Marrakesh, Morocco, Sall alisema amefikia uamuzi huo kufuatia kura ya maoni isiyo rasmi iliyofanyika katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa tarehe 16 Oktoba, pamoja na mazungumzo aliyofanya na marais wawili waliounga mkono azma yake: Évariste Ndayishimiye wa Burundi na Bassirou Diomaye Faye wa Senegal.
Rais wa Burundi, Évariste Ndayishimiye, ambaye kwa sasa anaongoza Umoja wa Afrika (AU), ndiye aliyependekeza jina la Sall kwa nafasi hiyo.
Sall alisema ameamua kujiondoa kwa kuzingatia misingi ya haki na usawa, ili kusaidia kuhakikisha kuwa mgombea atakayechaguliwa anapata uungwaji mkono mpana kutoka kwa pande mbalimbali.
Alisema kura ya majaribio iliyofanyika kwa siri katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ilionyesha kuwa nchi nyingi zinaunga mkono nafasi hiyo kupewa mgombea kutoka Amerika ya Kusini na Karibiani.
“Matokeo ya kura mbalimbali za majaribio yanaonyesha kuwa kuna uungwaji mkono kwa mgombea kutoka eneo la Amerika ya Kusini na Karibiani, ambaye pia anaweza kuwa mwanamke,” alisema Sall.
Alisisitiza kuwa ataendelea kuunga mkono juhudi za kuimarisha amani, usalama, maendeleo na mazungumzo baina ya nchi.
Pia alitoa wito wa kufanyika kwa mageuzi makubwa ndani ya Umoja wa Mataifa ili kuipa Afrika nafasi kubwa zaidi katika kufanya maamuzi yanayohusu masuala ya kimataifa.
“Afrika, ambayo inakabiliwa na changamoto za amani, usalama na maendeleo, lazima iendelee kutoa sauti yake na kufanya kila linalowezekana ili kupata nafasi inayostahili katika maamuzi ya kimataifa,” alisema.
UN kupunguza msaada wa chakula kwa wakazi wa Gaza
Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) linasema litalazimika kupunguza msaada wa chakula kwa wakazi wa Gaza kutokana na ukosefu wa fedha.
Hatua hiyo inatarajiwa kupunguza idadi ya watu wanaonufaika na mpango huo katika maeneo ya Palestina kwa takriban watu 500,000.
Kupunguzwa kwa msaada huo kunakuja wakati majira ya baridi yakikaribia, huku familia nyingi zinazoishi katika mahema ya muda zikiendelea kukabiliwa na uhaba wa chakula licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano kufikiwa.
Soma Pia;
Mzozo wa Iran: IRGC yatoa vitisho dhidi ya Trump na Netanyahu
Vikosi vya Ulinzi wa Mapinduzi ya Kiislam nchini Iran (IRGC) vimeonya kuwa vitatekeleza hatua kali za kulipiza kisasi iwapo miundombinu ya nishati ya nchi hiyo itashambuliwa, kufuatia kauli za Rais wa Marekani Donald Trump na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuhusu ushirikiano wao dhidi ya Tehran.
Msemaji wa Walinzi hao, Hossein Mohebi, alitoa onyo hilo Jumapili, akisema shambulio lolote dhidi ya miundombinu ya nishati ya Iran lingekuwa na madhara makubwa kwa Israel.
“Shambulio lolote dhidi ya miundombinu ya nishati ya Iran, hata kama wanasayansi wetu vijana watairekebisha haraka, litageuza milele ardhi inayokaliwa kwa mabavu kuwa jangwa lililoteketezwa na kuwalazimisha wakazi wake kukimbilia jangwa la Sinai. Dunia itaona kitakachotokea,” alisema.
Kauli hiyo ilitolewa takriban saa moja baada ya Netanyahu kuchapisha ujumbe kwenye mitandao ya kijamii, akisema Israel na Marekani zitakamilisha kazi yao kwa pamoja katika miaka ijayo.
Awali, Trump alikuwa ameeleza tena uungaji mkono wake kwa Netanyahu kupitia mtandao wake wa Truth Social, akisema Iran imekuwa ikitoa kauli mbiu za “Kifo kwa Israel, Kifo kwa Marekani” kwa miaka 51.
“Tutawaangamiza mashetani wakubwa na wadogo,” Trump aliandika.
Rais huyo wa Marekani aliongeza kuwa ni suala la muda tu kabla Iran haijageuza matamshi yake makali kuwa vitendo.
Pia alidai kuwa uwezo wa Iran kijeshi na kiuchumi umeharibiwa kwa kiasi kikubwa, na kuonya kuwa Marekani itachukua hatua za kumaliza suala hilo hivi karibuni ikiwa Tehran haitabadilisha mwenendo wake.
Pia unaweza Kusoma:
Saudi Arabia yawanyonga Wabangladesh wawili kwa tuhuma za vitendo visivyo vya maadili msikitini Makka
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Saudi Arabia imesema imetekeleza hukumu ya kifo dhidi ya raia wawili wa Bangladesh, mwanamume na mwanamke, waliokamatwa kwa tuhuma za kufanya vitendo visivyo vya maadili ndani ya mmoja wa misikiti katika mji mtakatifu wa Makka.
Shirika la habari la serikali ya Saudi Arabia, SPA, limeripoti kuwa mwanamume huyo, Nazarul Islam Abdul Basir, na mwanamke, Siti Akter, walituhumiwa kutenda kile kilichoelezwa na mamlaka kuwa ni kitendo kisicho cha maadili ndani ya msikiti.
Kwa mujibu wa mamlaka za Saudi Arabia, vikosi vya usalama viliwakamata wawili hao na kuwafikisha katika mahakama husika kwa ajili ya kusikilizwa kwa kesi yao.
Wizara hiyo imesema mahakama iliwatia hatiani wawili hao, ikizingatia uzito wa kosa, kukiukwa kwa utakatifu wa msikiti na mazingira ambayo tukio hilo lilidaiwa kutokea. Mahakama iliwaadhibu kwa hukumu ya kifo.
Mamlaka zimesema hukumu hiyo ilithibitishwa na mahakama ya juu baada ya kukata rufaa. Baadaye, amri ya kifalme ilitolewa kuidhinisha utekelezaji wa hukumu hiyo, ambao ulifanyika Jumatano, Oktoba 14.
Hata hivyo, mamlaka za Saudi Arabia hazijaeleza kwa kina aina ya vitendo walivyotuhumiwa kufanya, tarehe ya tukio, lini hukumu ya kifo ilitolewa au lini rufaa yao ilikataliwa.
Vyombo vya habari vya ndani nchini Saudi Arabia pia havijatoa maelezo zaidi kuhusu kesi hiyo, na vimeripoti tu taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Ndani.
Upande wa serikali ya Bangladesh umeeleza haukufahamishwa kuhusu hukumu hiyo na kudokeza itafuatilia kiundani.
Rais Macron apinga kujiuzulu kwa waziri wa usalama wa ndani baada ya ghasia
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amekataa ombi la kujiuzulu kwa Waziri wa Usalama wa Ndani, kufuatia ghasia zilizozuka nchini humo.
Macron amesema waziri Laurent Nunez, anapaswa kuendelea kuhudumu katika wadhfa wake na kutafuta suluhisho za kukabiliana na waandamanaji waliohusika na ghasia haraka iwezekanavyo.
Macron ameilaumu idara ya usalama kwa kushindwa kukusanya taarifa za kijasusi mapema, hali iliyochangia kuzuka kwa vurugu hizo.
Ghasia hizo zilitokea baada ya maandamano makubwa kufanyika, kupinga kupanda kwa gharama za maisha na kudorora kwa huduma za umma.
Mkutano wa dharura wa serikali unatarajiwa kufanyika hii leo kujadili yaliyotokea.
Macron ameonya kuwa wote waliohusika na ghasia hizo watawajibishwa kwa mujibu wa sheria.
Soma pia:
Human Rights Watch yaishtumu jeshi la Mali na Urusi kwa mauaji ya raia
Jeshi la Mali na washirika wake wa Urusi walitumia mashambulizi ya ndege zisizo na rubani Pamoja na mashambulizi mengine yenye mateso kuwashambulia waasi, hatua iliyosababisha vifo vya raia. Hii ni kulingana na ripoti iliyochapishwa na shirika la kutetea haki za kibanadamu la Human Rights Watch (HRW)
Ripoti hiyo imesema vifo vya raia kutokana na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani viliongezeka zaidi ya mara mbili kati ya mwezi Aprili na Agosti, ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Ripoti hiyo ilinukuu takwimu za ACLED, shirika linalofuatilia migogoro, baada ya mashambulizi ya kitaifa yaliyotekelezwa na kundi la JNIM, lenye uhusiano na Al-Qaeda, pamoja na waasi wa Tuaureg.
Mashambulizi hayo ya waasi yaliyoanza tarehe 25 mwezi Aprili, yalisababisha kifo cha waziri wa ulinzi wa Mali na pia yalilenga miji na maeneo kadhaa, pamoja na uwanja mkuu wa ndege mjini Bamako.
Viongozi wa kijeshi wa Mali, waliochukua mamlaka kupitia mapinduzi ya kijeshi mwaka 2020 na 2021, wamegeukia Urusi kupata msaada katika mapambano ya kudhibiti waasi.
Wanajeshi wa Urusi wa kikosi cha Africa Corps, walihusika pia katika kukabiliana na mashambulizi ya mwezi Aprili.
Takwimu za ACLED yenye makao yake nchini Marekani zinaonyesha kuwa vikosi vya Mali na Africa Corps vilifanya mashambulizi 47 kwa kutumia ndege zisizo na rubani kati ya mwezi Aprili na Agosti, na kusababisha vifo vya raia 94. Hii ni ongezeko kutoka mashambulizi 22 yaliyosababisha vifo vya raia 44 katika kipindi kama hicho mwaka uliopita.
Soma pia:
DRC yamshutumu Kabila kwa kuunga mkono kundi la waasi
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imemtuhumu rais wa zamani wa taifa hilo, Joseph Kabila,kwa kujaribu kuipindua serikali ya sasa ili kurejea madarakani.
Waziri wa Habari wa DRC, Patrick Muyaya, ambaye pia ni msemaji wa serikali, amesema uamuzi wa Kabila kutumia nguvu na silaha unaashiria nia yake ya kutaka kuwaangamiza raia wa DRC na kukiuka katiba.
Katika taarifa yake kuhusu vuguvugu jipya la waasi linalohusishwa na Kabila, Muyaya amesema kuwa “ingawa kundi hilo linajaribu kubadilisha sura yake, nia yake, mipango yake na mbinu zake zinafahamika.”
Waziri huyo amedai kuwa kundi hilo ni muungano wa waasi wanaoshirikiana na Rwanda, tuhuma ambazo hazijathibitishwa.
Muyaya amesema serikali ya DRC bado imejitolea kutafuta suluhu ya mzozo wa usalama unaoikumba taifa hilo,kupitia michakato ya kidiplomasia ya Washington na Doha.
Soma pia:
Rais Macron atoa wito wa utulivu Ufaransa, baada ya maandamano kugeuka ghasia
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ametoa wito wa utulivu na amani kudumishwa, siku moja tu baada ya nchi hiyo kushuhudia mojawapo ya siku mbaya zaidi za ghasia katika miaka ya hivi karibuni, huku maelfu ya watu wakikamatwa na maduka kuporwa, kufuatia maandamano kuhusu kupanda kwa gharama za maisha na kudorora kwa huduma za umma.
Mapigano mapya yalizuka mjini Paris na Marseille, ambapo polisi wa kutuliza ghasia waliingilia kati kuzuia majaribio ya kuvamia na kupora sehemu za biashara.
“Tunapotazama picha hizi, sote tumejiuliza: Ni nini kilikuwa kikipita akilini mwao? Inawezekanaje Wafaransa kuifanyia hivi kwa Ufaransa?” Macron alisema katika hotuba yake kwa taifa.
Kwanini watu wanaandamana Ufaransa?
Vurugu hizo zimetokana na mambo matatu: vuguvugu la wanafunzi wanaotaka kuboreshwa kwa mazingira ya shule, vuguvugu linalochipuka linalopinga gharama kubwa za maisha, na wahalifu waliotumia maandamano hayo kama kisingizio cha kupora mali.
Ghasia zilizoshuhudiwa siku ya Jumamosi zimefichua uwepo wa hasira na kutoridhishwa na utawala wa Macron, ambaye anatarajiwa kuondoka madarakani mwaka 2027 baada ya kuwa madarakani kwa Zaidi ya muongo mmoja.
Maandamano hayo yamezidisha hali ya wasiwasi kuhusu mgogoro wa kifedha na kijamii nchini Ufaransa, ambayo ni nchi ya pili kwa ukubwa wa uchumi katika Umoja wa Ulaya.
Soma pia: