Hatari 5 zinazoitishia dunia 2026

.

Chanzo cha picha, (Photo : BOUREIMA HAMA/AFP via Getty Images)

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Hali ya kutokuwa na uhakika inazidi kuzikumba mataifa meng ikiwemo yaliyoko bara Afrika, hii ni kulingana na ripoti ya hatari za kimataifa ya baraza la uchumi duniani (WEF) ya mwaka 2026.

Ripoti hiyo ya WEF inaonya kuhusu dunia inavyozidi kukumbwa na mizozo, migawanyiko na kupungua kwa ushirikiano wa kimataifa.

Wakati wa utafiti wa ripoti hiyo asilimia 50 ya watu waliohojiwa walisema kuwa wanatarajia mazingira ya kimataifa katika miaka miwili ijayo kuwa "yenye misukosuko" ikilinganishwa na mwaka mmoja uliopita.

Katika enzi hii mpya ya ushindani, ripoti hii ilianisha hatari tano zinazochukuliwa kuwa mbaya zaidi ambazo huenda zikatokea kuanzia mwaka wa 2028. Je madhara ya hatari hizi kwa Afrika itakuwa ipi?

1. Mvutano wa kiuchumi na kijiografia

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Hii ndiyo hatari kubwa zaidi kwa Afrika, mwaka huu wa 2026 ambapo asilimia 18 ya wataalamu waliutaja kuwa na uwezekano mkubwa wa kusababisha mgogoro wa kimataifa, katika kipindi cha miaka miwili ijayo hadi 2028. Hatari hii imeongezeka ikilinganishwa na mwaka uliopita.

Ripoti hiyo inaelezea kuongezeka ushuru wa wa kuagiza bidhaa, udhibiti wa uwekezaji na vikwazo, pamoja na kudhoofika kwa mfumo wa Shirika la Biashara Duniani (WTO) katika kutatua migogoro.

Kwa Afrika, ripoti hii inaibua maeneo mawili ambayo bara hili litakumbana nayo moja kwa moja:

  • Mashindano ya madini muhimu: WEF inatarajia serikali mbalimbali kuanza kujikusanyia akiba ya vyuma na madini yanayohitajika katika hali hii ya mpito kuelekea kuzalisha nishati safi. Hali hiyo inaweza kusababisha shinikizo la kibiashara, kidiplomasia au hata kijeshi kwa nchi zenye rasilimali hizo. Hii inaathiri moja kwa moja uchumi wa Afrika wenye utajiri wa kobalti, lithiamu, shaba na madini adimu ya ardhini.
  • Uhuru wa kifedha na sera ya fedha: Ripoti hiyo inaonya kuwa nchi zenye sarafu dhaifu ziko katika hatari kubwa kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya sarafu za kigeni. Hali hii inaweza kudhoofisha zaidi uwezo wa nchi nyingi za Afrika kudhibiti sera zao za fedha.

2. Taarifa za upotoshaji na taarifa potofu

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Hii ni hatari ya pili kwa ukubwa katika kipindi cha miaka miwili ijayo, na tayari iko katika nafasi ya nne kwa hatari ya kusababisha migogoro mwaka wa 2026.

Ripoti hiyo inaangazia kuongezeka kwa ugumu wa kutofautisha kati ya maudhui halisi na maudhui yaliyotengenezwa kwa kutumia akili mnemba (AI), ikiwemo deepfakes, wakati ambapo imani kwa vyombo vya habari inaendelea kupungua.

Asilimia 73 ya watu waliohojiwa barani Afrika wanasema wana wasiwasi kuhusu uwezo wao wa kutofautisha ukweli na uongo mitandaoni, ikilinganishwa na wastani wa asilimia 58 duniani. Kiwango hicho ni sawa na cha Marekani, ambako pia asilimia 73 ya watu waliohojiwa wana wasiwasi huo.

Afrika ni miongoni mwa maeneo ambayo watu wengi hutumia mitandao ya kijamii kupata habari. Hali hii inaweza kuongeza zaidi uwezekano wa watu kukumbana na taarifa potofu na maudhui bandia.

3. Mgawanyiko wa Kijamii

Taarifa za upotoshaji huchochea mgawanyiko katika jamii, ambao hudhoofisha imani kwa taasisi zilizopo na uwezo wa jamii kukabiliana na migogoro kwa pamoja.

Kwa Afrika, ripoti haitoi takwimu maalum za bara zima kuhusu hatari hii. Hata hivyo, inahusisha moja kwa moja mifumo kama algorithm za mapendekezo zinazoweza kuwaelekeza watumiaji wa mitandao katika maudhui ambayo huenda yakachochea mvutano au kupunguza Imani kwa taasisi tofauti na huenda ikachochea mgawanyiko wa kijamii.

4. Hali mbaya ya hewa

.

Chanzo cha picha, (Photo by HARUNA YAHAYA/AFP via Getty Images)

Hii ni hatari ya nne kwa ukubwa katika kipindi cha miaka miwili ijayo hadi 2028, lakini inaongoza katika orodha ya hatari kwa kipindi cha miaka kumi ijayo hadi 2036.

Hii inaashiria kuwa Baraza la Uchumi Duniani (WEF) linaona mabadiliko ya tabianchi kuwa tishio kubwa zaidi la muda mrefu.

Ripoti hiyo inaangazia kuongezeka kwa uharibifu wa miundombinu muhimu, hasa katika sekta za maji, nishati na usafirishaji, pamoja na kuongezeka kwa muda wa vipindi vya ukame.

Kwa Afrika, athari za hali mbaya ya hewa kwenye miundombinu muhimu zitakuwa kubwa zaidi katika nchi zenye kipato cha chini, ambazo zina uwezo mdogo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Licha ya Afrika kuchangia kwa kiwango kidogo katika mabadiliko ya tabianchi, bado ni miongoni mwa maeneo ambayo hayajajitayarisha vya kutosha kukabiliana na madhara yake ya moja kwa moja.

5. Migogoro na vita kati ya mataifa

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Hii ni hatari ya tano kwa ukubwa katika kipindi cha miaka miwili ijayo hadi 2028.

Hatari hii bado inahusiana kwa karibu na mvutano wa kiuchumi na kijiografia, ambao umeorodheshwa katika nafasi ya kwanza, kwani kuongezeka kwa mvutano katika eneo moja kunaweza kuchochea mvutano katika eneo lingine.

Ripoti hii inaonyesha uhusiano wa moja kwa moja kati ya hatari hii na ushindani wa kimataifa wa kupata rasilimali za asili haswa katika maeneo yenye utajiri wa rasilimali.

Akili Mnemba (AI)

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Aidha, kuna hatari nyingine ambayo haijaorodheshwa miongoni mwa hatari kuu za muda mfupi, lakini inapaswa kupewa umakini mkubwa kutokana na athari zake kwa Afrika: madhara yanayotokana na matumizi ya akili mnemba (AI). Hatari hii imepanda kutoka nafasi ya 30 mwaka 2028 hadi nafasi ya tano mwaka 2036, ikiwa ndiyo iliyopanda kwa kiwango kikubwa zaidi kati ya hatari zote zilizotathminiwa.

Ripoti hiyo inaonyesha pengo kubwa katika matumizi ya teknolojia za akili mnemba.

Kiwango cha matumizi yake Amerika Kaskazini, kinakadiriwa kuwa asilimia 27 ya wafanyakazi, ni mara tatu zaidi ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambako ni asilimia 9. Aidha, ni vituo vichache tu vya kuhifadhi na kuchakata data vilivyotengwa mahsusi kwa ajili ya AI vilivyo katika maeneo yanayoendelea.

Ripoti pia inaonyesha kuwa nchi nyingi za Afrika bado hazina mkakati wa kitaifa wa kompyuta za quantum.

Labda jambo la kutia wasiwasi zaidi ni mvutano kati ya mataifa yenye nguvu, unaweza kusababisha mshtuko wa kiuchumi, huku mzozo ukidhoofisha utulivu wa nchi. Wakati huo huo, mgawanyiko wa kijamii na taarifa za upotoshaji vinaweza kuzidi kudhoofisha taasisi muhimu.

Lakini je, Afrika itakuwa imejiandaa vya kutosha katika dunia ambayo mataifa yenye nguvu yanazidi kupunguza ushirikiano, ambapo rasilimali muhimu na za kimkakati zinageuka kuwa nyenzo za kutumia kujiongezea nguvu, na ambapo majanga yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi yanaongezeka?