Kauli 'tata' zilizomzunguka Nchimbi

..

Chanzo cha picha, VPO

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

"Yuda ni nani?" Hilo lilikuwa moja ya maswali yaliyotawala mjadala wa kisiasa nchini Tanzania katika wiki za mwisho za Julai na mwanzoni mwa Agosti 2026.

Jina hilo lilitamkwa Bungeni na Mbunge wa Tunguu, Zanzibar, Simai Mohammed Said, Juni 2, 2026. Hakumtaja mtu kwa jina, lakini alitumia mfano wa Yuda Iskariote anayekumbukwa katika simulizi za Kikristo kwa kumsaliti Yesu licha ya kuwa mmoja wa watu wake wa karibu.

"Kosa la mama ni wapi? Kwa sababu ya kumuamini mtu? Kumbe ni Yuda," alisema Simai.

Kisha akaongeza: "Yuda huyu amesaliti ndugu zake, hata ile familia ambayo ilimlea kisiasa, hawataki kumuona huyu Yuda. Hata huko nyuma amewahi kutajwa ni mzigo, lakini leo mzigo huu tunao ndani ya Serikali."

Hakumtaja Nchimbi. Lakini kwa sababu ya nafasi yake ndani ya Serikali na CCM, pamoja na historia yake ya kisiasa, kauli hiyo ilianza kutafsiriwa na baadhi ya watu kama ujumbe unaomlenga Makamu wa Rais, Dkt Emmanuel Nchimbi.

Juni 23, Simai alipoulizwa kuhusu kauli hiyo, bado hakutaja jina.

Badala yake akasema: "Nilichokisema Juni mbili. Mimi nafikiri kwanza Watanzania wengi, na nyinyi ni watu wazima, mtakuwa mmenifahamu. Tafsiri ya jambo lile nafikiri Watanzania wamenifahamu na wamenielewa vizuri."

Hapo ndipo "Yuda" ilipoanza kuishi maisha yake kisiasa. Yuda, usaliti na vita vya ndani ya chama

Katika siasa, kutumia jina kama Yuda si jambo dogo.

Ni neno linalobeba maana ya usaliti, mtu kugeuka dhidi ya waliomlea au waliomwamini.

Na Simai hakulitumia katika mazungumzo ya kawaida. Alilitumia ndani ya Bunge, katika kipindi ambacho siasa za CCM zilikuwa tayari zikianza kutazama mbali kuelekea uchaguzi wa mwaka 2030.

Mbunge wa ACT-Wazalendo, Addo Shaibu, naye alichangia kuongeza tafsiri ya kisiasa ya mjadala huo alipowaambia wabunge wa CCM:

"Ninawaomba wabunge wa Chama Cha Mapinduzi, homa yenu ya siasa kuelekea 2030 isiharibu majadiliano ya Bunge hili."

Kauli hiyo ilifanya mjadala usibaki tena kwenye swali la "Yuda ni nani?"

Ukawa mjadala mpana zaidi: Je, tayari mapambano ya urithi wa kisiasa ndani ya CCM yameanza?

Na kama yameanza, nani yuko upande gani?

Ni katika mazingira hayo ambapo historia ya kauli za Nchimbi inaanza kupata uzito mwingine.

Nchimbi na kauli ya "mihula miwili"

.

Chanzo cha picha, VPO

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mwaka 2024, wakati akiwa Katibu Mkuu wa CCM, Nchimbi aliwahi kutoa kauli kuhusu utamaduni wa chama hicho wa Rais kuhudumu kwa mihula miwili.

Kauli hiyo ilizua mjadala miongoni mwa wanaofuatilia siasa za CCM na mchakato wa kuelekea uchaguzi wa 2025 na hatimaye 2030.

Ingawa kauli hiyo haikuwa kuhusu yeye mwenyewe kugombea urais, ilikuwa miongoni mwa kauli zilizowafanya baadhi ya wachambuzi kuanza kumtazama Nchimbi kama mmoja wa wanasiasa ambao nafasi yao ndani ya mfumo wa CCM inaweza kuwa muhimu katika siasa za baada ya uchaguzi wa 2025.

Lakini Nchimbi mwenyewe alikuwa bado ndani ya mfumo.

Na mwaka 2025, alipokuwa Katibu Mkuu wa CCM, sauti yake ilikuwa zaidi ya kulinda nidhamu ya chama.

"CCM haitavumilia…"

Februari 2025, Nchimbi akiwa Katibu Mkuu wa CCM, alionya wanachama waliokuwa wakianza kampeni kabla ya wakati kwa kutumia mbinu mbalimbali, akisema chama hakitasita kuwaengua wanaokiuka Katiba, kanuni na maadili ya CCM.

Alisema baadhi ya wanachama walikuwa wakitumia shughuli za kijamii, mashirika na mbinu nyingine kujijenga kisiasa kabla ya wakati.

"Chama hakitasita kuwaengua wale watakaokiuka Katiba, Kanuni na maadili ya CCM," alisisitiza.

Kauli hiyo ilikuwa muhimu kwa sababu ilimchora Nchimbi kama msimamizi wa nidhamu ya chama katika kipindi ambacho tayari harakati za uchaguzi wa 2025 zilikuwa zikishika kasi.

Miezi michache baadaye, yeye mwenyewe angekuwa sehemu ya timu ya juu ya uchaguzi.

'Watanzania pambaneni mpate Katiba mpya'

Julai 24, 2026, takribani mwaka mmoja baada ya kuingia Ikulu kama Makamu wa Rais, Nchimbi alitoa kauli ambayo ilikuwa tofauti kwa uzito na mazingira yake.

Akiwa mgeni rasmi katika Mkutano Mkuu wa 15 wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania, THRDC, Dar es Salaam, aliwaambia Watanzania jambo moja ambalo angependa walibebe. "Pambaneni mpate Katiba mpya."

Nchimbi alisema Katiba hiyo inapaswa kuwa na makubaliano ya wadau wote na mwafaka wa kitaifa, na iwe Katiba ambayo inaweza kuliongoza taifa kwa miaka 50 ijayo.

Alisema hata akiwa Katibu Mkuu wa CCM alikuwa amewasilisha kwa Mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan, maoni yaliyokusanywa kutoka kwa wananchi, ambapo Katiba mpya ilikuwa miongoni mwa hoja zilizotajwa.

Serikali, alisema, ina dhamira ya kuhakikisha Katiba mpya inapatikana. Hii haikuwa kauli ya mwanasiasa wa upinzani. Ilikuwa kauli ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Na ilikuwa imetolewa katika mkutano uliohusisha watetezi wa haki za binadamu, kundi ambalo kwa muda mrefu limekuwa likisisitiza Katiba mpya, haki za kiraia, maridhiano na utawala bora.

Nchimbi pia alisema haki za binadamu ni pamoja na mwananchi anayetaka kutoa maoni yake bila hofu, kijana anayetaka kusikilizwa na mtuhumiwa anayestahili kutendewa kwa mujibu wa sheria.

Kwa mtazamo wa kawaida, ilikuwa hotuba kuhusu Katiba na haki za binadamu. Lakini kwa mtu anayefuatilia siasa za Tanzania, muda wake ulikuwa muhimu.

Ilikuwa Julai 24. Mjadala wa "Yuda" ulikuwa tayari umeanza.

Na wiki chache baadaye, minong'ono ya kujiuzulu kwa Nchimbi ikaanza kusikika kwa nguvu zaidi.

'Amani na Maridhiano'

.

Chanzo cha picha, VPO

Hata kabla ya kauli ya Katiba, Nchimbi alikuwa amesisitiza mara kadhaa umuhimu wa amani na maridhiano.

Machi 2026, katika futari iliyoandaliwa na Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania, aliwahimiza viongozi wa dini kuendelea kujenga maadili na mshikamano wa kitaifa. Serikali, alisema, inatambua umuhimu wa kazi ya kujenga amani na mahusiano kati ya Watanzania wa dini mbalimbali.

Kauli hizi hazikufanya Nchimbi awe mwanasiasa wa upinzani. Lakini zilijenga taswira ya kiongozi aliyekuwa akizungumza mara kwa mara kuhusu amani, maridhiano, haki na Katiba.

Na baada ya matukio ya uchaguzi wa Oktoba 2025, kila kauli ya aina hiyo ilianza kutazamwa katika mazingira mapana zaidi ya kisiasa.

Matukio ya Oktoba 29

Hapa ndipo kuna sehemu ambayo bado haijapata jibu la wazi.

Baada ya uchaguzi wa Oktoba 29, 2025, kulikuwa na mjadala mkubwa kuhusu matukio ya vurugu, vifo, kukamatwa kwa watu na masuala ya haki za binadamu.

Lakini Nchimbi, licha ya kuwa Makamu wa Rais na kiongozi wa juu wa Serikali, hakuonekana kuwa mmoja wa viongozi waliotoa kauli kubwa za moja kwa moja kuhusu kila kipengele cha mjadala huo.

Ingawa hilo lenyewe halimaanishi kwamba alikuwa akichukua upande fulani, alijaribu kukaa katikati.

Lakini katika siasa, kile kiongozi anachosema na kile anachochagua kutokisema wakati mwingine vyote hupewa tafsiri.

Na hilo ndilo lililofanya kauli zake za baadaye kuhusu haki, maridhiano na Katiba zipate uzito zaidi.

'Yuda'

Jina la "Yuda" lilivuma sana.

Takribani wiki moja baada ya kauli yake kuhusu Katiba mpya, mjadala wa Yuda ukapata nguvu zaidi. Simai alikuwa tayari ametoa kauli yake Juni. Lakini kadri Agosti ilivyokaribia, tafsiri za kisiasa zikazidi kuongezeka.

Gazeti la Mwanahalisi, katika toleo lake la Agosti 6–12, 2026, liliweka suala hilo kwenye ukurasa wake wa mbele kwa kichwa: "Nchimbi agoma kujiuzulu."

Hapo mjadala ukabadilika. Haikuwa tena "Yuda ni nani?" mjadala ukawa

Nchimbi anaondoka? Na kama anaondoka, kwa nini? "Anajiuzulu, hajiuzulu…"

Maneno haya yakasambaa katika mijadala ya kisiasa, mitandao ya kijamii na duru za ndani za siasa. Kisha taarifa kwamba Nchimbi hakuonekana katika kikao au shuguli zinazokihusisha chama chake ikaongeza kasi ya minong'ono.

Hakukuwa na tamko rasmi kutoka kwake wakati huo. Kwa hiyo, uvumi ukaendelea kuwa uvumi, mapaka ilipofika siku ya kujiuluzu.

Asubuhi ya Agosti 25, akaunti rasmi ya Instagram ya Nchimbi ikachapisha taarifa ya kujiuzulu.

Kwa mara ya kwanza, kile kilichokuwa kikizungumzwa kwa wiki kadhaa kikawa jambo rasmi. Na hapo ndipo simulizi ya "Yuda" inapata mashiko.

Nchimbi mwenyewe ndiye anayejua kikamilifu sababu zilizomfanya afikie uamuzi huo. Lakini historia ya siasa zake katika kipindi hiki inaacha nyuma yake kauli kadhaa ambazo sasa zitatazamwa upya.