Siri Yafichuliwa: Kwa nini Bomu la Nagasaki halikuweza kuzuiwa

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

Mnamo tarehe 9 Agosti 1945, bomu la plutonium lilidondoshwa katika mji wa Nagasaki nchini Japan, na hivyo kuhitimisha Vita vya Pili vya Dunia.

Katika mahojiano na BBC miaka 30 baadaye, mwanafizikia wa Marekani aliyesaidia kuunda bomu hilo alifichua sababu iliyofanya mlipuko huo usiweze kuzuilika, pamoja na mipango ya kutengeneza mabomu mengine zaidi.

"Haikuwa kwa sababu ya kutojali binadamu, bali ilitokana na kujali binadamu. Labda hilo ndilo lililokuwa kosa."

Miaka thelathini baada ya kushiriki katika shambulio la bomu la atomiki dhidi ya Nagasaki mnamo tarehe 9 Agosti 1945, mwanafizikia wa Marekani Philip Morrison alizungumza waziwazi na BBC kuhusu maamuzi yaliyofanywa katika siku na wiki zilizotangulia mlipuko huo mkubwa wa nyuklia ambao haukuwa na mfano wake.

Morrison alikuwa na jukumu muhimu katika Mradi wa Manhattan, mpango wa siri kubwa wa Washirika wa kutengeneza silaha za kwanza za nyuklia, akifanya kazi katika maabara ya Los Alamos. Maabara hiyo iliongozwa na mwalimu wake wa zamani, J. Robert Oppenheimer.

Akiwa amehudhuria jaribio la "Trinity" la bomu la kwanza la atomiki mnamo tarehe 16 Julai 1945, Morrison alibeba kiini cha plutonium cha bomu hilo mapajani mwake ndani ya gari wakati wakielekea New Mexico.

Kisha alisafiri hadi kisiwa kidogo cha Tinian, kusini mwa Saipan, ili kusaidia kuunganisha bomu la plutonium lililopewa jina la "Fat Man" ambalo lilitumika huko Nagasaki, alisimamia upakiaji wa bomu hilo kwenye ndege aina ya B-29 mnamo tarehe 9 Agosti, siku tatu tu baada ya shambulio la bomu huko Hiroshima.

Huko Tinian ndiko majeshi ya Marekani yalipojenga kile Morrison alichokitaja kuwa "uwanja mkubwa zaidi wa ndege duniani".

"Miamba mikubwa ya matumbawe ilisawazishwa kwa kiasi ili kujaza eneo tambarare lenye ardhi mbaya, na kujenga njia sita za kurukia na kutua ndege... kila moja ikiwa na urefu wa karibu maili mbili," alisema katika ushahidi wake mbele ya Kamati ya Seneti mnamo Desemba 1945.

Ukubwa wa uharibifu

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Katika ushahidi wake, Morrison pia alifichua ukubwa wa maandalizi ya mashambulizi ya mabomu ya moto dhidi ya miji ya Japani.

Morrison also revealed the scale of preparations for the fire-bombings of Japanese cities in his testimony.

"Kila siku, meli za kubeba mafuta zilizosheheni maelfu ya tani za petroli ya ndege zilikuwa zimeegeshwa bandarini... Ndege kubwa zilikuwa zikikimbia kwenye njia ndefu za kurukia... Kila baada ya sekunde 15, ndege nyingine aina ya B-29 ilikuwa ikiruka angani. Hali hii iliendelea kwa saa moja na nusu... Ndege elfu moja aina ya B-29, mara kwa mara, zilichoma moto eneo la maili za mraba nyingi za jiji katika shambulio moja."

Kinyume chake, alieleza, "Bomu la atomiki lilikuwa jambo tofauti kabisa."

"Hakukuwa na shehena za meli zilizobeba mabomu ya moto. Badala ya wafanyakazi wengi wa silaha na ghala zao za mabomu, kulikuwa na watu wapatao 25 ​​kutoka Los Alamos, vibanda vichache vya chuma vilivyotengenezwa awali (aina ya Quonset) vilivyobadilishwa kuwa maabara za majaribio, na jengo moja lililozungushiwa vizuizi. Shambulio hilo lilianza baada ya saa sita usiku. Uwanja ulikuwa mtupu... Na ndege moja ilinguruma ikikimbia kwenye njia ya kurukia, ikapaa, na kuelekea kwenye miji ya adui," alisema.

Vita vilikuwa bado vinaendelea. Tulikuwa tukielekea kwenye vita vikubwa katika eneo la Pasifiki... hivyo ilikuwa haiwezekani kusitisha – Philip Morrison

Ingawa makadirio yanatofautiana, inaaminika kuwa watu 40,000 waliuawa na mlipuko wa awali wa bomu huko Nagasaki, huku vifo zaidi ya 100,000 vikihusishwa moja kwa moja na shambulio hilo la bomu katika kipindi cha miaka mitano iliyofuata.

Huko Hiroshima, takriban watu 80,000 walikufa papo hapo, huku jumla ya vifo ikifikia takriban 140,000 kutokana na majeraha mabaya ya kuungua, majeraha mengine, na ugonjwa mkali wa mionzi.

Baadaye, Morrison alikagua uharibifu mkubwa katika miji hiyo miwili ya Japani akiwa sehemu ya timu rasmi ya wanasayansi iliyokuwa ikitathmini uharibifu, na alikumbuka tukio moja mahususi huko Hiroshima.

"Afisa mmoja wa Kijapani alisimama katikati ya vifusi na kutuambia: 'Haya yote yametokana na bomu moja; ni jambo lisilovumilika'," alisema.

"Ndege moja, yenye bomu moja, ilikuwa imeharibu eneo la maili za mraba nyingi za jiji, na iliharibu kwa namna ya kutisha zaidi na bila kuacha nafasi yoyote ya kustahimili au kutoroka, ikilinganishwa na shambulio la ndege elfu moja."

Hata hivyo, alikuwa na matumaini kwamba bomu la atomiki lisingelazimika kutumika vitani; aliongoza kundi la wanafizikia vijana wa Los Alamos waliotaka kuonyeshwa hadharani kwa bomu hilo kabla ya kulitumia nchini Japan.

Morrison ambaye alikuwa na umri wa miaka 30 aliposimamia uunganishaji wa bomu la "Fat Man" huko Tinian alitaka "kutuma ujumbe wa kimataifa kwenda jangwani," kama alivyomwambia Melvyn Bragg wa BBC mwaka wa 1975. "Lakini katika mazingira ya vita, hilo lilikuwa ni wazo lisilowezekana kutimia."

'Kasi isiyozuilika'

Mwanafizikia huyo alielezea kuwepo kwa kasi isiyozuilika, hata wakati ilipobainika wazi kuwa Wanazi wangeshindwa. Hata hivyo, alifafanua: "Vita vilikuwa bado vinaendelea. Tulikuwa tukielekea kwenye vita vikubwa katika eneo la Pasifiki... hivyo ilikuwa haiwezekani kusimamisha mchakato huo."

Kwa maoni ya Morrison, sababu pekee ambayo ingeweza kubadilisha hali hiyo ilikuwa Rais wa Marekani Franklin D. Roosevelt, ambaye alifariki dunia mwezi Aprili 1945.

"Ningesema kuwa fursa pekee ya kubadilisha msimamo wa Marekani kwa kiasi kikubwa ingekuwa ni Roosevelt kuendelea kuishi... [ambaye] alifariki wakati mchakato huo ukiendelea, kabla hatujajua kama bomu hilo lingefanya kazi, na kabla ya kuamuliwa jinsi mabomu hayo yangetumika," alisema Morrison.

"Nadhani yeye ndiye aliyekuwa mtu pekee mwenye hadhi na nguvu za kutosha ndani ya serikali kuzuia mwelekeo huo mbaya," alisema.

Harry S. Truman alipochukua wadhifa wa urais, hakuwa na taarifa yoyote kuhusu mradi huo; alifahamu kuwepo kwake saa chache tu baada ya kuapishwa. Miezi mitatu na ushee baadaye, alitoa amri ya kutumika kwa mabomu hayo.

"Ni kweli yeye ndiye aliyefanya uamuzi huo, lakini nadhani ni sahihi kusema uamuzi huo ndio uliomfanya yeye kuwa jinsi alivyo," alibisha Morrison. "Ingelikuwa hatua ya ujasiri mkubwa kwake kubadilisha mambo hayo baada ya miaka yote ile na kuyasimamisha... fursa hiyo ilipotea kabisa kufuatia kifo cha Roosevelt."

Kulingana na Morrison, nguvu hiyo isiyoweza kuzuilika ilihusika pia katika uamuzi wa kudondosha mabomu mawili mfululizo.

"Haikuchukuliwa kama bomu la kwanza na la pili. Amri zilizotolewa kwa makamanda zilikuwa, 'Dondosheni bomu la kwanza, kisha dondosheni bomu la pili haraka iwezekanavyo.' Ingehitajika mtu mwenye msimamo thabiti huko Washington kuona madhara makubwa ya bomu la kwanza... na kusema, 'Haya, tusubiri kwanza kabla ya bomu la pili.' Ingehitaji tafakari ya kiwango cha juu, na uwezo wa kuelewa uhusiano tata wa mambo na kutoa amri sahihi kwa majenerali husika," alisema.

Hivyo, mashambulizi hayo mawili ya mabomu yalitekelezwa na mengine yalikuwa yamepangwa, Morrison alifichua.

"Uamuzi wa awali ulikuwa kwamba tungeendelea kudondosha mabomu haya kwa mwaka mzima, iwapo ingehitajika... Niliagizwa kuandaa mpango wa kufanya hivyo," alimwambia Bragg. "Nilikuwa na mpango, mkakati, ratiba, mtu wa kuchukua nafasi yangu, na mipango ya safari za kwenda na kurudi."

Haijulikani kama angeweza kuendelea na jambo hilo baada ya yeye na wanasayansi wengine wa Los Alamos kushuhudia matokeo yake.

"Kiakili, tulifahamu vyema athari za muda mfupi na... zile za muda mrefu zilizoogopwa. Lakini uelewa huo ulitokana tu na kusoma vitabu na kuangalia takwimu," alimwambia Bragg.

"Na kuna tofauti kubwa sana kwa kila mtu na kwa dunia nzima kati ya takwimu hizo... na kushuhudia uhalisia wa maisha na uhalisia wa kifo. Hivyo, nadhani tulijua, lakini hatukuhisi uzito wake."

Alikumbuka hali ilivyokuwa katika kambi ya kijeshi kwenye kisiwa cha Pasifiki usiku ule wa shambulio la bomu huko Hiroshima. "Kulikuwa na sherehe kubwa usiku huo, lakini wanasayansi wengi hawakuhudhuria. Watu wa Jeshi la Anga na askari wa kawaida walikunywa pombe. Walijua kuwa vita vilikuwa vinaelekea mwisho. Ilionekana na kuhisiwa kuwa ni ushindi mkubwa sana." Hata hivyo, Morrison alikumbuka kuwa wanasayansi hao "walikaa huku wakiwa na huzuni na kutafakari... kuhusu mwisho wa dunia."

Lakini katika kipindi cha kuelekea mashambulio hayo, Morrison hakuhisi kulazimika kujiondoa kwenye Mradi wa Manhattan. "Licha ya kuwepo kwa upinzani mkali na usioyumba dhidi ya jambo hili, sioni ni kwa namna gani ningeweza kufanya vinginevyo. Sikuwahi hata kufikiria kujiondoa hata wakati mmoja."

Alipoulizwa iwapo Washirika wangeliangusha bomu la atomiki jijini Berlin endapo lingekuwa tayari kabla ya Wanazi kushindwa, alisema: "Lo, bila shaka kabisa, kwa haraka sana... Tulikuwa na hofu kubwa dhidi ya Wajerumani, na walikuwa adui yetu," alisema Morrison.

Baada ya vita, Morrison alikuwa profesa katika Taasisi ya Teknolojia ya Massachusetts (MIT), akipigia debe kampeni dhidi ya kuenea kwa silaha za nyuklia na kuwa mstari wa mbele katika vuguvugu la "kutotaka bomu la tatu."

"Ni dhahiri kwamba, kama ilivyo kwa wanasayansi wengi wa mradi huo, ninaamini kabisa kuwa vita vingine havipaswi kuruhusiwa," alisema katika ushahidi wake mbele ya Seneti mwaka 1945.

Na aliamini kuwa Washirika walipaswa kufanya jambo moja mahususi. "Ninaamini kabisa kuwa onyo mwafaka lilipaswa kutolewa," alisema. "Nikirejea nyuma, hakuna sababu yoyote ya msingi ya kutotoa onyo mwafaka na linalofaa."