Taliban inavyotawala Afghanistan: Uchunguzi wa BBC

Chanzo cha picha, Getty Images
Gavana Abdullah Sarhadi anatoa msaada wa fedha kwa ajili ya matibabu ya mkono uliovunjika wa mvulana na baadaye kutoa fedha kwa msikiti wa eneo hilo. Kisha, katika ofisi yake kaskazini mwa Afghanistan, kunatokea mazungumzo ya kushangaza.
Mwanamke kijana anamweleza kamanda wa zamani wa Taliban mwenye ndevu za mvi kwamba anataka talaka kutoka kwa mumewe, ambaye anamtuhumu kwa kumnyanyasa na kumpiga kwa miezi kadhaa.
Hakubali kutoskizwa.
Katika nchi ambayo wasichana hawaruhusiwi kupata elimu ya sekondari, mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 18 anatetea hoja yake kwa utulivu na kujiamini, huku uso wake ukiwa umefunikwa kabisa na vazi la sitara na miwani ya jua.
"Kama kungekuwa na hata chembe ya uwezekano wa kuishi pamoja, nisingekuwa hapa... Nimeshafanya uamuzi wangu," alisema.
Baada ya kujaribu kumshawishi asidai talaka, gavana huyo anatangaza kuwa wanawake "hawana akili timamu" na "wana uwezo mdogo wa kufikiri," kauli inayoibua vicheko kutoka kwa maafisa, walinzi, na wazee waliomzunguka.
Tukio hili linatoa taswira adimu ya hali halisi ya maisha ya kila siku chini ya utawala wa Taliban, miaka mitano baada ya kundi hilo kuipindua serikali iliyoungwa mkono na Marekani mwaka 2021.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Katika kipindi hiki, wanawake wametengwa kutofanya kazi, wamezuiwa kujiunga na vyuo vikuu, na wamekatazwa kusafiri peke yao au kuzuru bustani na vituo vya burudani.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Katika mfululizo wa mikutano iliyodumu kwa miaka miwili, BBC ilipata fursa ya kipekee ya kukutana na watu wenye ushawishi katika vuguvugu la Kiislamu lenye msimamo mkali, na kushirikiana na wanaume ambao hapo awali walipanga mashambulizi ya kujitoa mhanga au kuishi kwa miaka mingi mafichoni, lakini sasa ni viongozi na wapiganaji.
Taliban waliingia madarakani wakidai kuwa wamebadilika, lakini sera zao nyingi zinafanana na tafsiri kali ya Sharia, sheria ya dini ya Kiislamu,ambayo waliitekeleza katika miaka ya 1990.
Wanaume tuliokutana nao walionekana kutaka kujionyesha kama watu wenye busara, lakini hawakuwa tayari kabisa kujadili vitendo vyao vya vurugu vya siku zilizopita. Pia tuliona hali ya kutoelewana au wasiwasi kati ya viongozi na wale wanaowaongoza.
Gavana Sarhadi anaamini kuwa Tuba, jina lisilo la kweli, anapaswa kubaki katika ndoa yake.
"Jiulize: 'Ni nani angependa kunioa baada ya talaka?'" Sarhadi alimwambia. "Utalazimika kufanya makubaliano mengi na kulegeza msimamo, vinginevyo utapoteza heshima na hadhi yako."
"Bwana Gavana, heshima na hadhi yangu tayari zimevunjwa," alijibu.
Mumewe anasikiliza, akisubiri zamu yake ya kuzungumza.
Chini ya sheria ya Sharia, mwanamke anayemuomba mumewe talaka anaweza kulazimishwa kurudisha pesa yote au sehemu yake aliyopewa wakati wa ndoa. Mara nyingi makubaliano ya kifedha hufikiwa. Hata hivyo, mume wa mwanamke huyu anadai kiasi mara nne ya pesa hiyo, jambo ambalo familia yake inakataa kulilipa.
Gavana anaamini kuwa mwanamke huyo anapaswa kuwa na chumba chake mwenyewe. Anaongeza kuwa mamlaka zitampa mume onyo la kutompiga mkewe, "vinginevyo atafungwa jela."
Baba yake Tuba, akiwa hajaridhishwa na hali hiyo, baadaye aliambia BBC kuwa familia hiyo itawasilisha ombi la talaka mahakamani, ingawa katika mfumo wa kisheria wa Taliban, ni vigumu sana kwa mwanamke kupata talaka bila ridhaa ya mumewe.

Chanzo cha picha, EPA/REX/Shutterstock
Sarhadi alikuwa kamanda wa kijeshi wakati wa kipindi cha kwanza cha utawala wa Taliban katika miaka ya 1990.
Alikuwa miongoni mwa maelfu ya wapiganaji waliojisalimisha mwishoni mwa mwaka 2001, wakati muungano ulioongozwa na Marekani ulipoiangusha serikali ya kundi hilo.
Aliwekwa kizuizini kwa miaka kadhaa katika kituo cha kizuizini cha Marekani huko Guantanamo Bay, kabla ya hatimaye kuachiliwa huru.
Wakati Taliban waliporejea madarakani, aliteuliwa kuwa gavana,kwanza katika jimbo la Bamiyan, na baadaye, tulipokutana naye mwishoni mwa mwezi Juni, katika mji wa Sheberghan katika jimbo la Jawzjan.
Hivi karibuni aliteuliwa kuwa naibu kamanda wa kikosi cha jeshi katika jimbo la kaskazini la Kunduz.
Akiwa anabonyeza simu ya zamani yenye skrini ndogo, anaeleza kuwa marufuku ya hivi karibuni ya matumizi ya simu, kwa watumishi wa umma imepunguza kasi ya utendaji kazi.
"Awali, ungeweza kutuma ujumbe wa haraka... kutuma ujumbe na kupata majibu ya haraka." Akizungumzia zaidi kuhusu marufuku hiyo, anaongeza kuwa "italeta matatizo."
Lakini kwa mambo mengine mengi, mtazamo wake unaonekana kutobadilika sana ukilinganishwa na msimamo wa Taliban wa miaka 25 iliyopita.
Wakati huo, alikuwa kamanda wa kijeshi huko Bamiyan, ambapo Taliban walilipua sanamu kubwa za kale za Buddha, jambo lililozua hasira na kulaaniwa vikali na jumuiya ya kimataifa.
Awali anajaribu kukwepa maswali yetu kuhusu eneo hilo la kihistoria, lakini hatimaye anakiri: "Niliziharibu kwa mikono yangu mwenyewe.
"Kila kitu tulichofanya na kila kitu tunachofanya kinaendana na kanuni na sheria za Mungu... Tunaharibu sanamu badala ya kuziuza. Kwa nini nijute? Ilikuwa ni mapenzi ya Mungu."
Huko Kabul, mji mkuu, tunakutana na kiongozi mwingine wa Taliban ambaye ameachana na maisha yake ya zamani yaliyojaa vurugu na sasa anashikilia wadhifa katika serikali ya sasa.
Habibullah Badr anatuendeshea gari la deraya katika mitaa ya jiji.
Anaeleza kuwa hapo awali alikuwa "akisimamia operesheni za washambuliaji wa kujitoa mhanga" jijini Kabul.
"Nazijua barabara na mitaa yote vizuri sana... tulikuwa na taarifa zote muhimu kuhusu Kabul na vichochoro vyake," anaeleza. "Kulikuwa na maeneo yaliyohitaji maandalizi ya kina."
Mashambulizi ya kujitoa mhanga ya Taliban yamesababisha vifo na majeraha kwa maelfu ya watu nchini Afghanistan, wakiwemo raia wengi.
Hata hivyo, Badr anasita kuzungumzia maisha yake ya zamani, akiogopa kuwa "yatawaudhi watu" na "kufungua upya vidonda vya zamani".
Alipoulizwa kuhusu madhara kwa raia, alisema kuwa Taliban walikuwa wakilenga misafara ya Marekani na kwamba raia walikuwa wakihimizwa kukaa mbali na kambi za kigeni.
Kila ninapojaribu kumuuliza kuhusu mashambulizi mahususi yaliyotokea katika maeneo ya raia, hukwepa swali hilo.

Chanzo cha picha, shutterstock
Kwa sasa ameachana na majukumu yake rasmi ili kupata matibabu, lakini hapo awali alikuwa naibu mkurugenzi wa magereza nchi nzima, na aliwahi kusimamia gereza lilelile ambamo aliwahi kufungwa na kusubiri hukumu ya kifo chini ya serikali iliyopita.
Badr anatualika kuongozana naye kwenye mkutano wa kikabila, ambapo rais wa taasisi ya hisani anatarajiwa kumkabidhi medali kwa heshima yake. Hata hivyo, mambo yanachukua mkondo usiotarajiwa.
"Bw. Badr ni fahari kwa Afghanistan na ni mpiganaji shupavu," anasema Sultan Mohammad Talaee. "Lakini nina hoja ya kukosoa pia. Kama shule na elimu zingekuwa wazi kwa wote, ingekuwa hatua kubwa ya maendeleo kwa Afghanistan. Natumai hilo halitakukwaza."
Ukimya wa wasiwasi ulitawala, huku waliohudhuria mkutano huo wakikosa kujua jinsi ya kuitikia. Kipaza sauti cha Talaee kiliondolewa haraka.
Baadaye, aliiambia BBC: "Nimeitisha kufunguliwa tena kwa shule za wasichana... Kutafuta elimu ni wajibu kwa wanaume na wanawake katika Uislamu."
Aliongeza: "Kuna mambo mengine nilitaka kuyasema, lakini hawakuniruhusu kuendelea kuzungumza."
Mara nyingi, wale wanaothubutu kusema waziwazi hukumbwa na madhara makubwa zaidi.
Wanawake walituelezea hisia zao za kukata tamaa sana baada ya ndoto zao kuvunjwa na vikwazo vya elimu, na kutuambia kuhusu marafiki wao waliofungwa jela kwa sababu ya kuandamana.
Waandishi wengi wa habari tuliozungumza nao walisema waliwahi kuitwa au kuhojiwa na idara ya ujasusi ya Taliban, inayojulikana kama Estikhbaraat.
BBC iliwasilisha baadhi ya hoja hizi kwa msemaji wa serikali ya Taliban, Zabihullah Mujahid.

Chanzo cha picha, Shutterstock
Amekuwa mmoja wa viongozi wakuu katika serikali ya Taliban tangu mwaka 2021. Bado anatumia jina bandia alilolitumia kwa miaka mingi wakati wa uasi, lakini alituambia kuwa jina lake halisi ni Tahir Shah Seddiqi, na hivyo kulibainisha hadharani kwa mara ya kwanza.
Tukiwa katika kituo cha habari cha kifahari kilichojengwa kwa ufadhili wa Marekani kwa ajili ya serikali iliyopita, tunamuuliza kuhusu mkutano wa kwanza na waandishi wa habari alioufanya hapo, siku mbili baada ya Taliban kuingia madarakani.
Wakati huo alitangaza kwa dunia nzima kwamba serikali ya Taliban ingewaruhusu wanawake kufanya kazi na kusoma "ndani ya mfumo wa kanuni zetu" na kwamba wangekuwa "hai sana" katika jamii. Kwa nini hawakutimiza ahadi hiyo?
"Tumejitolea kulinda haki za wanawake, uhuru wa kujieleza, na kanuni nyingine ndani ya mfumo wa sheria ya Sharia," alijibu. "Lazima tuzingatie kila jambo kwa mtazamo wa Sharia."
Anasema kuwa kuruhusu wanawake kufanya kazi katika ofisi kama yake "kungesababisha maovu" na "heshima yao ingedhoofishwa."
Anaeleza kuwa suala la elimu kwa wanawake "linafanyiwa kazi... tunahitaji suluhisho linalozingatia Sharia ili kulishughulikia."
Alipoulizwa kuhusu hatua za Taliban za kukandamiza uhuru wa vyombo vya habari, alijibu: "Katika jamii kama ya Afghanistan, tuna vikwazo vyetu. Hatuwezi kuruhusu vyombo vya habari kueneza propaganda zozote wanazotaka... hawawezi kurusha maudhui yanayokwenda kinyume na sheria na taratibu za Kiislamu."

Chanzo cha picha, EPA
Serikali ya Taliban ina makao yake makuu mjini Kabul, lakini Mujahid hutumia muda mwingi Kandahar, mji ulioko kusini mwa nchi hiyo na ngome ya Taliban, ambao baadhi ya watu sasa wanauchukulia kuwa ndio mji mkuu halisi.
Tuliomba kukutana na kiongozi mkuu wa Taliban, Hibatullah Akhundzada, ambaye ana makazi yake huko. Yeye huonekana hadharani mara chache sana na hajawahi kutoa mahojiano kwa vyombo vya habari, tuliambiwa kuwa jambo hilo halingewezekana kwa wakati huo.
Masharti yamekazwa zaidi mjini Kandahar tangu ziara yangu ya mwisho miaka miwili iliyopita. Sasa, wanaume wanapaswa kufuga ndevu. Vituo vya redio haviruhusiwi kurusha muziki au sauti za wanawake, na hatukuruhusiwa kurekodi picha za video jijini humo.
Katika eneo lililo umbali wa safari ya saa mbili kupitia barabara zenye vumbi, baadhi ya wapiganaji wa zamani waliojitolea zaidi katika kundi hilo walionyesha BBC mtandao wa zamani wa siri wa mapango yaliyotumiwa na waasi.
Abid Lalai, mpiganaji wa zamani ambaye sasa anasimamia kituo cha ukaguzi katika kikosi cha usalama chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani, anatuonyesha matundu aliyokuwa akitumia kufyatulia risasi pamoja na maeneo aliyokuwa akiweka nakala yake ya Quran na kutundika bunduki zake aina ya AK-47.

Chanzo cha picha, EPA
Mkuu wake, Abdul Samad, anatuonyesha makaburi yasiyo na misalaba, akieleza kuwa baba yake amezikwa hapo baada ya kuuawa akipigana bega kwa bega na Taliban.
Eneo hili ni mojawapo ya maeneo yenye hali duni zaidi katika nchi ambayo, kulingana na Umoja wa Mataifa, watu watatu kati ya wanne hawawezi kukidhi mahitaji yao ya msingi. Samad anaeleza kuwa wakazi wa eneo hilo wanahitaji sana maji, barabara, na vituo vya afya.
"Maafisa wa Utawala wa Taliban hawatusahau," anasisitiza Samad. Anaongeza kuwa huenda viongozi hao wana mambo mengine ya kipaumbele yanayowashughulisha. "Bado tuna matumaini kwamba siku moja watatujali."
Miaka mitano tangu Taliban warejee madarakani, umaskini, ukosefu wa ajira, na kuyumba kwa uchumi bado ni changamoto kubwa.
Maafisa wa Taliban tuliozungumza nao walisema wanajitahidi kushughulikia hali hiyo, lakini tulikutana na watu wengine wanaoamini kuwa kundi hilo lenyewe ndilo tatizo kuu la nchi.
"Nakosa la kusema ninapowaza jinsi kundi lisiloelewa maisha lilivyojikuta ghafla likiwa madarakani," anasema Hoda, jina bandia, mwanamke aliyeandamana mitaani wakati Taliban walipochukua madaraka.
"Wanawake hawawezi kukubali hali hii," aliambia BBC. "Wanaweza kuongeza vikwazo kadiri wanavyotaka, lakini hali hiyo haitadumu milele."
"Nadhani Taliban wanawaogopa wanawake walioelimika," anaongeza. "Ndiyo maana wanawawekea vikwazo wanawake. Wanataka wanawake wasioelimika ili wasiweze kulea wanaume wenye busara. Kwa sababu kufanya hivyo kungeashiria mwisho wa Taliban."
Ripoti ya ziada na Hafizullah Maroof















