Kesi 5 za wanasiasa Afrika zilizochukua miaka mingi kuamuliwa

n

Chanzo cha picha, EATV

    • Author, Mariam Mjahid
    • Nafasi, BBC Swahili
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 8

Tangu mwaka 1945, viongozi na watu mashuhuri wa kisiasa wamefikishwa mbele ya mahakama na mahakama maalumu za ndani na za kimataifa katika nchi mbalimbali duniani.

Baadhi yao wamehukumiwa, huku wengine wakifariki kabla kesi zao hazijakamilika. Wengine, kama Augusto Pinochet wa Chile na Charles Taylor wa Liberia, walikabiliwa na mchakato mrefu kabla ya hatimaye kufikishwa mahakamani.

Nchini Tanzania, kesi inayomkabili Tundu Lissu, kiongozi wa chama cha upinzani cha CHADEMA, imeibua mjadala kuhusu muda ambao kesi zenye mwelekeo wa kisiasa huchukua kufikia mwisho wake.

Mahakama Kuu ya Tanzania imetoa uamuzi kuhusu Lissu kwamba ana kesi ya kujibu katika shtaka la uhaini. Huo si uamuzi wa mwisho kuhusu hatia au kutokuwa na hatia, bali ni hatua muhimu katika mchakato wa kesi ambao umefuatiliwa kwa karibu ndani na nje ya Tanzania. Kesi hiyo imeingia katika hatua ya utetezi, ambapo Lissu ameanza kuwasilisha ushahidi na mashahidi wake.

Barani Afrika, historia inaonyesha kuwa kesi zinazowahusisha wanasiasa, viongozi wa upinzani au masuala yenye uzito mkubwa wa kisiasa zinaweza kuchukua miaka kadhaa, wakati mwingine hata miongo, kabla ya hukumu kutolewa au mchakato wa kisheria kukamilika.

Makala haya yanaangazia baadhi ya kesi maarufu zilizochukua muda mrefu kuamuliwa barani Afrika na moja ya wanasiasa wa Afrika waliopelekwa mahakama ya kimataifa. Zipo kesi nyingi zilizochukua muda zaidi, lakini hizi ziligusa wanasiasa wakubwa na zilivuta hisia za wengi.

Kenya na kesi za ICC zilizodumu miaka kadhaa

s

Chanzo cha picha, AFP

Kenya nayo ina historia ya kesi zilizohusishwa na siasa ambazo zilivuta muda mrefu bila kufikia hukumu ya hatia. Hikuendeshwa Afrika lakini ilihusisha wanasiasa wa Afrika.

Baada ya ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 na 2008, Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, ilifungua mchakato wa kuwawajibisha baadhi ya viongozi na watu mashuhuri waliotajwa kuhusika na ghasia hizo. Miongoni mwa waliokabiliwa na mashtaka walikuwa aliyekuwa Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta, na William Ruto, ambaye sasa ni Rais wa Kenya.

Kesi dhidi ya Kenyatta ilikuwa miongoni mwa zilizovuta kwa miaka kadhaa. Mashtaka dhidi yake yalithibitishwa na ICC Januari 2012, lakini upande wa mashtaka uliwasilisha ombi la kuyaondoa Desemba 2014. Hatimaye, tarehe 13 Machi 2015, mahakama ilikomesha rasmi mwenendo wa kesi hiyo. ICC ilisema ushahidi uliokuwepo haukutosha kuendelea na mashtaka.

Kwa kuanzia hatua ya ICC ya mwaka 2010 hadi kesi ya Kenyatta kufungwa mwaka 2015, mchakato huo ulichukua takribani miaka mitano.

ICC ilisema hakukuwa na ushahidi wa kutosha dhidi ya Joshua arap Sang (kushoto) na William Ruto (wa pili kutoka kulia), walioonekana hapa muda mfupi baada ya mahakama kutoa uamuzi wake.

Chanzo cha picha, AFP

Maelezo ya picha, ICC ilisema hakukuwa na ushahidi wa kutosha dhidi ya Joshua arap Sang (kushoto) na William Ruto (wa pili kutoka kulia), walioonekana hapa muda mfupi baada ya mahakama kutoa uamuzi wake.
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kesi dhidi ya William Ruto na mtangazaji wa redio Joshua Sang nayo ilichukua muda mrefu zaidi. Mashtaka yao yalithibitishwa Januari 2012 na kesi ikaanza kusikilizwa Septemba 2013. Hata hivyo, tarehe 5 Aprili 2016, ICC ilikomesha kesi hiyo bila kuzuia uwezekano wa mashtaka kufufuliwa baadaye.

Kwa kuhesabu kutoka mwaka 2010 hadi mwaka 2016, mchakato wa kesi ya Ruto na Sang ulichukua takribani miaka sita.

Changamoto kubwa katika kesi hizi zilihusisha upatikanaji wa ushahidi, ushirikiano na mashahidi pamoja na madai ya kuingiliwa kwa mashahidi. Katika kesi ya Ruto na Sang, mahakama ilibaini ushahidi kuhusu kuingiliwa kwa mashahidi kadhaa, jambo ambalo liliathiri kwa kiasi kikubwa uwezo wa upande wa mashtaka kuendelea na kesi yake.

Kesi hizi zinaonyesha changamoto inayoweza kujitokeza katika mashauri yenye uzito mkubwa wa kisiasa na jinai za kimataifa.

Mchakato wa kisheria unaweza kuchukua miaka kadhaa, lakini si kila kesi inayodumu kwa muda mrefu huishia katika hukumu ya hatia.

Baadhi ya kesi hukoma kwa sababu ushahidi hautoshi, mashahidi hawawezi kutoa ushahidi unaohitajika au kuna vikwazo vingine vinavyoathiri uwezo wa upande wa mashtaka kuthibitisha kesi yake.

Kesi ya uhalifu ya aliyekuwa Rais wa Chad Hissène Habré

Hissène Habré alikataa kutambua uhalali wa mahakama iliyosikiliza kesi dhidi yake.

Chanzo cha picha, AP

Maelezo ya picha, Hissène Habré alikataa kutambua uhalali wa mahakama iliyosikiliza kesi dhidi yake.

Kwingineko barani Afrika, safari ya Hissène Habré kuelekea mahakamani ilikuwa ndefu zaidi.

Juhudi za kumfikisha aliyekuwa rais wa Chad mbele ya haki zilianza mwaka 2000. Baada ya miaka ya mabishano ya kisheria na mapambano kuhusu mamlaka ya mahakama, Habré alifikishwa mahakamani nchini Senegal.

Mwaka 2016, alihukumiwa kwa uhalifu dhidi ya ubinadamu, uhalifu wa kivita na mateso.

Hukumu hiyo ilikuwa kilele cha mapambano ya miaka 17 ya waathiriwa wa utawala wake, waliopigania kumfikisha mbele ya haki.

Tume ya Uchunguzi iliyoundwa nchini Chad baada ya Habré kuondolewa madarakani mwaka 1990 ilisema serikali yake ilihusika katika mauaji ya kisiasa ya takribani watu 40,000 na visa 200,000 vya mateso katika kipindi cha miaka minane aliyokuwa madarakani.

Kikosi chake cha polisi wa kisiasa, Directorate of Documentation and Security, DDS, kilihusishwa na baadhi ya ukiukaji mbaya zaidi wa haki za binadamu.

Habré, aliyekuwa na umri wa miaka 73, alikanusha kufahamu kuhusu mauaji, mateso na ubakaji ambao hatimaye alitiwa hatiani kwa kuhusika nao.

Alitwaa madaraka mwaka 1982 baada ya kumuondoa Goukouni Oueddei, aliyekuwa mwenzake katika harakati za uasi na ambaye alikuwa ameshinda uchaguzi.

Wakati huo, kulikuwa na imani kubwa kwamba Habré aliungwa mkono na Shirika la Ujasusi la Marekani, CIA, kama ngome dhidi ya utawala wa Kanali Muammar Gaddafi wa Libya.

Kesi ya uhaini ya Nelson Mandela - Afrika Kusini

Msimamo wa Nelson Mandela ulijulikana na kufafanuliwa vyema katika kesi iliyohujumiwa mwaka 1964. Alisema, 'Nimepigana dhidi ya ubaguzi wa rangi na pia nimepigana dhidi ya utawala wa waaafrika weusi usiofaa.''

Chanzo cha picha, Socials

Maelezo ya picha, Msimamo wa Nelson Mandela ulijulikana na kufafanuliwa vyema katika kesi iliyohujumiwa mwaka 1964. Alisema, 'Nimepigana dhidi ya ubaguzi wa rangi na pia nimepigana dhidi ya utawala wa waaafrika weusi usiofaa.''

Miaka ya hamsini na mapema miaka ya tisini, wakati maandamano yao yalipotibuliwa kwa nguvu, chama cha ANC kikaanza vita haslisi dhidi ya utawala wa wazungu.

Mwaka 1956, watu 156, akiwemo Nelson Mandela, walikamatwa na kushtakiwa kwa uhaini katika kile kilichokuja kujulikana kama Kesi ya Uhaini. Kesi hiyo iliendelea kwa takriban miaka minne na nusu kabla ya washtakiwa wote kuachiliwa huru mwaka 1961.

Kesi ya uhaini ya Delmas - Afrika Kusini

Kesi ya Delmas ilianza mwaka 1985 na kumalizika Desemba 1989, ikiwa miongoni mwa kesi zilizodumu kwa muda mrefu zaidi katika historia ya mahakama za Afrika Kusini.

Kesi hiyo iliwahusisha viongozi na wanaharakati wa harakati za kupinga ubaguzi wa rangi wa apartheid, wakiwemo Frank Chikane, Mosiuoa Lekota na Popo Molefe, waliotajwa kwa pamoja kama mabingwa watatu 'Big Three'.

Walifikishwa mahakamani chini ya sheria za usalama za utawala wa apartheid na kushtakiwa kwa uhaini dhidi ya dola.

Kesi hiyo ilichukua siku 431 za vikao vya mahakama katika kipindi cha karibu miaka minne. Mwaka 1988, baadhi ya washtakiwa walihukumiwa vifungo vikali, lakini hukumu hizo zilikatiwa rufaa na baadaye kubatilishwa na Mahakama ya Rufaa mwishoni mwa mwaka 1989.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo walikuwa Mabuya Baleka, Oupa Hlomoka, Tebogo Moselane, Mohapi More, Gcinumuzi Malindi, Morake Mokoena, Tsietsi Mphuti, Naphtali Nkopane, Tebello Ramakgula, Bavumile Vilakazi, Sekwati Mokoena, Simon Nkoli, Pelamotse Thlopane, Serame Hlanyane, Thomas Manthata, Hlabeng Matlole, Maxala Vilakazi na Thabiso Ratsomo.

Kesi ya mauaji ya Hosni Mubarak- Misri

f

Chanzo cha picha, Reuters

Nchini Misri, kuanguka kwa Hosni Mubarak mwaka 2011 kulifuatiwa na kesi iliyochukua miaka sita.

Rais huyo wa zamani alikabiliwa na mashtaka yaliyohusisha mauaji ya waandamanaji na ufisadi. Kulikuwa na hukumu, rufaa na kesi za marudio kabla ya mahakama ya juu mwaka 2017 kumwondolea lawama kuhusu vifo vya waandamanaji.

Hosni Mubarak alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 91, Februari 2020, alipokuwa akipokea matibabu katika hospitali ya kijeshi mjini Cairo.

Kesi ya uhaini ya Besigye - Uganda

Besigye sasa anahukumiwa mjini Kampala na wala sio Nairobi kwa sababu uhalifu uliopangwa ulikuwa "dhidi ya Uganda na sio Kenya", msemaji wa jeshi la Uganda Brigedia Jenerali Felix Kulayigye aliambia podcast ya BBC Africa Daily.

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Besigye sasa anahukumiwa mjini Kampala na wala sio Nairobi kwa sababu uhalifu uliopangwa ulikuwa "dhidi ya Uganda na sio Kenya", msemaji wa jeshi la Uganda Brigedia Jenerali Felix Kulayigye aliambia podcast ya BBC Africa Daily.

Nchini Uganda, mwanasiasa Kizza Besigye amekuwa akikabiliwa na msururu wa kesi, kukamatwa na mashtaka katika vipindi tofauti tangu alipojitokeza kuwa mmoja wa wapinzani wakuu wa Rais Yoweri Museveni.

Mwaka 2005, alikabiliwa na mashtaka ya uhaini wakati wa kampeni za uchaguzi. Baadhi ya kesi hizo ziliendelea kwa miaka kabla ya kuondolewa au kufikia hitimisho.

Mnamo Novemba 16 mwaka 2024, Besigye alikabiliwa tena na mashtaka makubwa baada ya kukamatwa nchini Kenya na kupelekwa Uganda kushtakiwa, ambako awali alifikishwa katika mahakama ya kijeshi.

Hatua hiyo ilizua mjadala mkubwa kuhusu haki ya raia kushtakiwa katika mahakama za kijeshi. Baadaye, Mahakama ya Juu ya Uganda iliamua kwamba raia hawapaswi kushtakiwa katika mahakama hizo kwa makosa ya jinai.

Winnie Byanyima, ambaye ni mkurugenzi mtendaji wa UNAIDS, ameshtumu vikali kuendelea kwa kesi hiyo wakati Besigye hawezi kufika mahakamani kutokana na hali yake ya kiafya.

"Hii si kesi, ni utani, kwa sababu Kizza Besigye hajakataa kufika mahakamani amelazwa kitandani, ni mgonjwa sana, hawezi kuzungumza," Byanyima aliiambia shirika la habari la AFP.

Kizza Besigye amekuwa kizuizini kwa zaidi ya mwaka mmoja na miezi tisa, huku kesi yake ikipitia mabadiliko kadhaa ya kisheria katika mazingira ambayo imeelezwa afya yake imezorota.

Kesi hizi zote ni tofauti

Baadhi ya kesi zilimalizika kwa kuachiliwa kwa washtakiwa. Nyingine zilianguka kutokana na changamoto za ushahidi. Nyingine zilifikia hukumu baada ya miaka mingi ya mapambano ya kisheria.

Serikali zinaweza kubadilika. Mashahidi wanaweza kupotea. Ushahidi unaweza kuwa mgumu kupatikana. Washtakiwa wanaweza kukata rufaa. Na katika kesi zenye maslahi makubwa ya kisiasa, mahakama yenyewe inaweza kugeuka kuwa sehemu ya mjadala mpana kuhusu demokrasia na utawala wa sheria.

Wachambuzi wa siasa za Afrika Mashariki wameeleza kuwa kwa mazingira ya sasa kesi ya Lissu inapaswa kutazamwa si tu kama shauri linalomhusu mwanasiasa mmoja. Ni sehemu ya mjadala mpana zaidi kuhusu namna taasisi za haki zinavyoshughulikia kesi zenye uzito wa kisiasa, namna haki inavyosimamiwa na muda gani ni muda unaokubalika kwa mtu kusubiri hatima ya kesi yake.

Lakini zinaibua swali moja linalojirudia katika mifumo ya haki duniani.

Hata hivyo, wachambuzi wamehoji kuwa haki inaweza kusubiriwa kwa muda gani kabla ya kuchelewa kwake kuwa sehemu ya kesi yenyewe?

Kwa waathiriwa, washtakiwa na familia zao, miaka si takwimu tu.

Ni maisha!

Aidha, kile kinachobaki katika historia si muda uliotumika mahakamani pekee, bali namna haki ilivyotafutwa, ushahidi ulivyoshughulikiwa na kama taasisi zilifanikiwa kuaminisha umma kwamba mwisho wa safari ulikuwa wa haki.