Nchimbi ni nani? Safari ya mwanasiasa mwenye misimamo

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 3

Emmanuel John Nchimbi, ambaye ametangaza kujiuzulu nafasi ya Makamu wa Rais wa Tanzania na kustaafu siasa na utumishi wa umma, amekuwa katika siasa na uongozi wa Serikali kwa zaidi ya miongo miwili.

Safari yake imepitia uongozi wa vijana wa CCM, ubunge, uwaziri, diplomasia na uongozi wa juu wa chama tawala.

Nchimbi alizaliwa Desemba 24, 1971, mkoani Mbeya. Kwa mujibu wa wasifu rasmi wa Serikali uliowekwa na Ubalozi wa Tanzania, alianza elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi Oysterbay, Dar es Salaam, mwaka 1980 na kumaliza mwaka 1986.

Aliendelea na elimu ya sekondari katika Shule ya Uru kuanzia 1987 hadi 1989, kabla ya kuhamia Shule ya Sekondari Sangu, ambako alimaliza kidato cha nne mwaka 1990. Kwa kidato cha tano na sita alisoma Forest Hill mkoani Morogoro, kuanzia 1991 hadi 1993.

Mwaka 1994 alijiunga na IDM Mzumbe, ambako alihitimu Stashahada ya Juu ya Utawala mwaka 1997. Baadaye aliendelea na masomo ya juu katika Chuo Kikuu cha Mzumbe, akipata shahada ya uzamili katika usimamizi wa biashara, akijikita katika benki na fedha, na baadaye shahada ya uzamivu.

Safari yake ya uongozi

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Mwaka 1998, Nchimbi alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), baada ya kujenga uzoefu katika uongozi wa chama. Wakati huo pia alifanya kazi katika Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC).

Kutoka katika uongozi wa vijana, safari yake ilimfikisha katika siasa za kitaifa na Bunge. Nchimbi aliingia Bungeni kupitia Jimbo la Songea Mjini, na baadaye akashika nyadhifa mbalimbali serikalini.

Aliwahi kuwa Naibu Waziri katika wizara mbalimbali, kabla ya kuwa Waziri. Miongoni mwa nafasi kubwa ukiacha nafasi ya makamu ya Rais alizowahi kushika ilikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi katika Serikali ya Rais Jakaya Kikwete.

Baada ya safari yake katika Serikali, Nchimbi alihamia kwenye diplomasia. Mwaka 2016 aliteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Brazil, kabla ya mwaka 2022 kuhamia Misri kama Balozi wa Tanzania. Alihudumu nchini Misri hadi mwaka 2023.

Baada ya kurejea nchini, Nchimbi alirudi katika uongozi wa juu wa CCM. Mwaka 2024, alishika nafasi ya Katibu Mkuu wa CCM, akiwa mtendaji mkuu wa chama hicho.

Baadaye akawa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Safari yake imepitia karibu kila ngazi muhimu ya uongozi wa chama na Serikali, UVCCM, Bunge, uwaziri, diplomasia, uongozi wa CCM na hatimaye Makamu wa Rais.

Mwanasiasa anayejulikana kwa misimamo

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Lakini katika safari hiyo, kuna jambo jingine ambalo limekuwa sehemu ya utambulisho wake wa kisiasa, kuwa na msimamo.

Mfano maarufu ulijitokeza mwaka 2015, wakati wa mchakato wa ndani wa CCM wa kumpata mgombea urais.

Nchimbi, akiwa mjumbe wa Kamati Kuu pamoja na Sophia Simba na Adam Kimbisa, alijitokeza hadharani kupinga uamuzi wa chombo hicho kuhusu mchakato wa uteuzi wa mgombea. Watatu hao walieleza kwamba hawakuwa pamoja na uamuzi huo.

Hatua hiyo ilikuwa muhimu kwa sababu ilionyesha utayari wake wa kuweka hadharani tofauti za kisiasa ndani ya chama, badala ya kuzificha kabisa.

Miaka kadhaa baadaye, akiwa Katibu Mkuu wa CCM, Nchimbi mwenyewe alizungumzia sifa hiyo alipowajibu waliodai kuwa tatizo lake ni kuwa na "vimisimamo".

"Kuna watu wanasema Nchimbi tatizo lake ni ana vimisimamo. Kwenye mambo ya msingi mimi nina msimamo. Kama mnataka kunitimua kwa misimamo, nitimueni leo leo."

Kauli hiyo ilitoa picha ya namna alivyotaka kujitambulisha kisiasa kama mwanasiasa anayesema yuko tayari kusimamia anachoamini hata kama msimamo huo unaweza kumweka katika mazingira ya kutofautiana na wengine.

Lakini kutofautiana huko hakukumtoa katika mfumo wa CCM. Badala yake, aliendelea kupanda katika safu za chama hadi kuwa Katibu Mkuu, na baadaye akawa chaguo la Rais Samia kuwa mgombea mwenza katika uchaguzi wa 2025.

Hatimaye, akafikia nafasi ya Makamu wa Rais, nafasi ya pili kwa ukubwa katika uongozi wa Jamhuri ya Muungano. Kwa zaidi ya miaka 20, safari ya Nchimbi imekuwa ya kutoka kiongozi wa vijana wa CCM hadi mbunge, waziri, balozi, Katibu Mkuu na hatimaye Makamu wa Rais.

Ni safari iliyomjengea uzoefu mpana ndani ya chama na Serikali, lakini pia taswira ya mwanasiasa ambaye, kwa maneno yake mwenyewe, anapendelea kuwa na msimamo kuliko kuuficha.

Nchimbi ametangaza kujiuzulu nafasi ya Makamu wa Rais, japo taarifa ya kujiuzulu kwake inasema amestaafu siasa. Ni kweli atakuwa amestaafu siasa?