Tundu Lissu: Kuwa na kesi ya kujibu maana yake nini?

Chanzo cha picha, Getty Images
Mahakama Kuu ya Tanzania imetoa uamuzi kuhusu Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini humo, Tundu Lissu, kwamba ana kesi ya kujibu katika shtaka la uhaini linalomkabili. Hatua hii ina maanisha nini?
Kwa lugha rahisi kwa mujibu wa wanasheria, hii ni hatua katika kesi ya jinai ambapo Mahakama huangalia ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka na kuamua kama kuna msingi wa kumtaka mshtakiwa aendelee na hatua ya kujitetea.
Hii ndiyo hatua ambayo kesi ya Lissu imefikia baada ya upande wa mashtaka kuwasilisha ushahidi wake.
Mwanasheria Jebra Kambole amezungumza na BBC kwa ajili ya kufananua hatua hii na anaeleza kuwa Mahakama haiamui moja kwa moja kwamba mshtakiwa ana hatia kwa kusema ana kesi ya kujibu.
"Mahakama imeona kuna viashiria ambavyo inafikiria ni muhimu kupata maelezo ya upande wa pili."
Hii ndiyo tofauti muhimu ya kuelewa kuhusu uamuzi wa aina hii. Kuwa na kesi ya kujibu si sawa na kupatikana na hatia, anasema Jebra Kambole.
Kwa mujibu wake, Mahakama inaposema mshtakiwa ana kesi ya kujibu, haimaanishi kwamba tayari imeamua kuwa ametenda kosa analoshtakiwa nalo.
Badala yake, inamaanisha kwamba ushahidi uliowasilishwa katika hatua hiyo umeonekana kuwa na msingi wa kutosha kisheria wa kumtaka mshtakiwa apewe nafasi ya kujibu.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kambole anasema:
"Sio moja kwa moja kwamba hakuna shaka, hapana. Mahakama imeona kuna viashiria ambavyo inafikiria ni muhimu kupata maelezo ya upande wa pili."
Kwa hiyo, uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania ni kwamba Lissu ana kesi ya kujibu, hatua inayofuata itakuwa utetezi.
Na katika hatua hii Lissu anaweza kutoa ushahidi yeye mwenyewe, kuwasilisha ushahidi mwingine au kuwaita mashahidi ambao yeye na mawakili wake wanaamini wanaweza kusaidia kujibu mashitaka dhidi yake.
Hii ni sehemu muhimu ya haki ya mshtakiwa katika kesi ya jinai.
Kambole anaeleza kuwa Lissu ana haki ya kuomba Mahakama iwaite mashahidi anaowaona ni muhimu kwa utetezi wake.
Lissu alishaomba tangu Mahakama ya ukabidhi Kisutu, kuitwa kwa mashahidi kadhaa anaoamini ni muhimu, akiwemo Rais Samia Suluhu. Hata hivyo upande wa mashtaka, umepinga hilo.
"Mshtakiwa ana haki yake ya kikatiba na kisheria kuiomba Mahakama iwaite mashahidi ambao anadhani watamtetea na ni muhimu kwenye kesi."
Baada ya hatua ya utetezi kukamilika, Mahakama itatathmini ushahidi wa pande zote kabla ya kutoa hukumu ya mwisho.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Lakini kingetokea nini kama Mahakama ingesema hana kesi ya kujibu?
Kwa mujibu wa Jebra, hii ingemaanisha kwamba, baada ya kuangalia ushahidi uliowasilishwa na upande wa mashtaka, Mahakama haijaona msingi wa kutosha wa kumtaka mshtakiwa aanze kujitetea.
Katika mazingira hayo, kesi inaweza kumalizika katika hatua hiyo, kwa mujibu wa utaratibu wa sheria.
Kwa Lissu, ikiwa Mahakama imesema ana kesi ya kujibu, maana yake ni kwamba sasa anapata nafasi ya kujibu ushahidi uliowasilishwa dhidi yake.
Lissu alikamatwa 9 Aprili 2025, muda mfupi baada ya kuhutubia mkutano wa chama chake, CHADEMA, mjini Mbinga, kusini mwa Tanzania.
Siku iliyofuata, 10 Aprili 2025, alifikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam.
Alishtakiwa kwa kosa la uhaini, pamoja na shtaka jingine la kuchapisha taarifa zinazodaiwa kuwa za uongo. Shtaka la uhaini ni miongoni mwa makosa mazito zaidi katika sheria za Tanzania.
Upande wa mashtaka uliwasilisha mashahidi na ushahidi wake kuunga mkono mashitaka dhidi ya Lissu. Baada ya upande wa mashtaka kumaliza kuwasilisha ushahidi wake, Mahakama ikatoa uamuzi kwamba ushahidi huo unatosha kumtaka Lissu ajitetee. Hapo ndipo linapokuja swali la "kesi ya kujibu".
Kwa hiyo, uamuzi wa leo una umuhimu mkubwa kwa sababu unaamua hatua inayofuata ya kesi hiyo: Kwa ufupi, kwa mujibu wa mwanasheria Jebra Kambole, hatua ya leo, si hukumu kwamba Lissu ana hatia. Ni uamuzi kwamba, kwa hatua hiyo ya kesi, kuna msingi wa kumtaka mshtakiwa apewe nafasi ya kujibu.












