Ndejembi kumrithi Nchimbi, ni mwanasiasa wa aina gani?

Chanzo cha picha, URT
Chama cha Mapinduzi (CCM) kimempendekeza Deogratius John Ndejembi kuwa Makamu mpya wa Rais wa Tanzania, baada ya aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo, Dk. Emmanuel Nchimbi, kujiuzulu.
Uamuzi huo umefikiwa na Halmashauri Kuu ya CCM chini ya Mwenyekiti wake, Rais Samia Suluhu Hassan.
Iwapo atathibitishwa kwa mujibu wa taratibu za kikatiba, Ndejembi mwenye umri wa miaka 43 atachukua nafasi iliyoachwa na Nchimbi, ambaye alijiuzulu baada ya kuitumikia kwa takriban miezi 10.
Na akithibitishwa pia Ndejembi atakuwa Makamu wa rais wa 13 tangu Tanzania ipate uhuru, akiwa miongoni mwa Makamu wa raisi vijana zaidi kuwahi kushika nafasi hiyo.
Lakini Ndejembi ni mwanasiasa wa aina gani, na amekujaje hadi kufikia nafasi hii?
Amepikwa sekta binafsi, ameiva serikalini
Ndejembi, ambaye amekuwa Waziri wa Nishati tangu mwaka 2025, anaingia katika kinyang'anyiro hicho akiwa na uzoefu wa zaidi ya muongo mmoja katika siasa na utumishi wa umma, lakini safari yake haikuanza serikalini.
Kabla ya kuingia kwenye uongozi wa serikali, Ndejembi alifanya kazi katika sekta binafsi. Mwaka 2012 alikuwa meneja wa kampuni ya A1 Outdoor, kabla ya kuwa Mkuu wa Mauzo katika kampuni ya Smile Communication kati ya mwaka 2012 na 2014.
Mwaka 2014 alijiunga na Tigo kama Meneja wa Kanda, nafasi aliyoshikilia hadi mwaka 2015, na mwaka 2016 alikuwa Mkuu wa Masoko wa GSM Group.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Wakati huo huo, alikuwa akijenga nafasi yake ndani ya CCM. Rekodi ya Bunge inaonyesha alianza kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya chama hicho tangu akiwa kijana, ikiwemo kuwa mwanachama wa Baraza la Taifa la Umoja wa Vijana wa CCM kuanzia mwaka 2008 hadi 2017.
Alikuwa pia mwanachama wa Baraza Kuu la CCM na baadaye Kamati ya Siasa ya chama hicho katika ngazi mbalimbali.
Mwaka 2016, Ndejembi aliingia katika utumishi wa serikali baada ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Dodoma, nafasi aliyoshikilia hadi mwaka 2020.
Hii ilikuwa hatua muhimu katika safari yake ya kisiasa, ikimpa uzoefu wa uongozi wa serikali za mitaa kabla ya kuingia Bungeni.
Mwaka 2020 alichaguliwa kuwa Mbunge wa Chamwino, Dodoma, na baadaye akaingia katika serikali kuu kama Naibu Waziri.
Kuanzia mwaka 2021 hadi 2023 alikuwa Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kabla ya kuhamia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa.
Mwaka 2023 hadi 2024 alikuwa Naibu Waziri katika Ofisi hiyo, akisimamia masuala yanayohusu tawala za mikoa na serikali za mitaa.
Mwaka 2024 alipandishwa kuwa Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu.
Baadaye mwaka huo alihamishiwa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ambako alihudumu kama Waziri hadi mwaka 2025.
Baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, Rais Samia alimteua kuwa Waziri wa Nishati, akipewa jukumu la kusimamia sekta yenye umuhimu mkubwa katika uchumi wa Tanzania.
Katika nafasi hiyo, Ndejembi amekuwa akisimamia masuala ya uzalishaji na usambazaji wa umeme pamoja na sekta za mafuta na gesi.
Ameshiriki pia katika mazungumzo ya ushirikiano wa nishati na nchi nyingine, ikiwemo Zambia, katika masuala ya mafuta na gesi.
Kwa upande wa miradi mikubwa ya nishati, amekuwa akieleza mipango ya serikali ya kuongeza upatikanaji wa umeme na kuimarisha miundombinu ya nishati nchini.
Hivyo, tofauti na mwanasiasa ambaye safari yake imejikita zaidi katika siasa za chama, Ndejembi ana historia inayochanganya sekta binafsi, uongozi wa serikali za mitaa, Bunge na uwaziri.
Rekodi yake inaonyesha pia kuwa amekuwa akipanda hatua kwa hatua ndani ya mfumo wa serikali. Kutoka Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, akawa mbunge, Naibu Waziri na baadaye Waziri wa wizara kadhaa.
Mwanasiasa-mtendaji

Chanzo cha picha, RS-Ruvuma
Katika elimu, Ndejembi alianza shule ya msingi katika Shule ya Msingi Cannon Andrea Mwaka, alikosoma kati ya mwaka 1988 na 1995. Aliendelea na Shule ya Sekondari Kigurunyembe kuanzia mwaka 1996 hadi 1998, kabla ya kwenda Merton College kati ya mwaka 2002 na 2004.
Kati ya mwaka 2006 na 2009, alisoma Shahada ya Uhusiano wa Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Lincoln nchini Uingereza. Baadaye, kati ya mwaka 2009 na 2012, alisoma Stashahada ya Juu katika Taasisi ya Usimamizi wa Utawala.
Historia hiyo ya elimu ya uhusiano wa kimataifa, pamoja na uzoefu wake katika sekta binafsi na serikali, inaweza kuwa muhimu katika nafasi ya Makamu wa Rais, ambayo inahusisha pia masuala ya Muungano na majukumu mapana ya kitaifa.
Hata hivyo, Ndejembi hajaijenga historia yake kwa kuwa mmoja wa sura zinazojulikana zaidi katika siasa za kitaifa za CCM. Umaarufu wake umeongezeka zaidi kupitia nafasi alizoshika serikalini, hasa katika miaka ya hivi karibuni.
Kwa maana hiyo, anaweza kuelezewa zaidi kama mwanasiasa-mtendaji, ambaye amejenga uzoefu wake kupitia utekelezaji wa majukumu ya serikali na uongozi wa taasisi, huku akiwa na mizizi ndani ya CCM.
Sasa, endapo uteuzi wake utakamilika kwa mujibu wa Katiba, Ndejembi atatoka katika uongozi wa wizara moja na kuingia katika nafasi yenye majukumu mapana zaidi ya kitaifa.
Hii itakuwa hatua kubwa zaidi katika safari yake ya kisiasa, miaka 10 tu baada ya kuanza kazi kama Mkuu wa Wilaya ya Kongwa.
Ametyoka sekta binafsi, uongozi wa wilaya, Bunge, unaibu waziri na uwaziri, Ndejembi sasa amependekezwa kushika nafasi ya nafasi ya pili kwa ukubwa katika uongozi wa Tanzania.
Swali kubwa litakuwa namna mwanasiasa huyu, aliyejenga uzoefu wake zaidi kupitia utendaji wa serikali, atakavyobadilika kutoka kusimamia wizara moja hadi kushughulikia masuala mapana ya taifa na Muungano.












