Nchimbi afukuzwa CCM

.

Chanzo cha picha, Mwananchi

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 2

Chama cha Mapinduzi (CCM) kimemfukuza uanachama aliyekuwa Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Emmanuel Nchimbi, siku moja baada ya kujiuzulu wadhifa huo na kutangaza kustaafu siasa pamoja na utumishi wa umma.

Uamuzi huo umetangazwa na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dk Asha-Rose Migiro, baada ya vikao vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya chama vilivyofanyika Dar es Salaam chini ya uenyekiti wa Rais Samia Suluhu Hassan.

Balozi Migiro amesema uamuzi huo umefikiwa baada ya vikao hivyo kupitia taarifa zilizokuwepo kuhusu Nchimbi.

"Baada ya kupitia taarifa zote zilizokuwepo, kwa kauli moja, kutokana na ukiukwaji wa maadili imeazimia afukuzwe uanachama. Na CCM imefikia uamuzi huo, si mwanachama wa CCM tena," amesema Balozi Migiro.

CCM haijaeleza kwa undani katika taarifa hiyo ni ukiukwaji gani wa maadili uliosababisha uamuzi huo.

Hatua hiyo imekuja chini ya saa 24 baada ya Nchimbi kutangaza kujiuzulu nafasi ya Makamu wa Rais na kustaafu siasa na utumishi wa umma.

Dk Nchimbi aliwasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa Rais Samia Suluhu Hassan tarehe 25 Agosti 2026, akisema ameamua kuachia nafasi hiyo kuanzia Septemba 4.

Katika barua yake, alisema uamuzi huo unahusiana na ahadi aliyompa Rais Samia mwaka mmoja uliopita, wakati alipokubali kuwa mgombea mwenza wa rais katika uchaguzi mkuu.

Alisema alimuahidi Rais Samia kuwa atamsaidia kwa uwezo wake wote na kwamba, iwapo siku yoyote rais angeona anahitaji Makamu mwingine wa Rais, angeachia nafasi hiyo.

Dk Nchimbi alisema amejiridhisha kuwa Rais Samia anatamani mabadiliko na hivyo akaamua kutimiza ahadi hiyo.

"Nimejiridhisha pasipo shaka kuwa Mhe. Rais anatamani mabadiliko, hivyo nimeamua kutimiza ahadi yangu."

Rais Samia alilikubali ombi hilo.

Uamuzi huo unafunga sura moja ya safari ya kisiasa ya Dk Nchimbi, lakini pia unaibua maswali kuhusu mustakabali wake baada ya kuondoka katika siasa na utumishi wa umma, hasa kwa namna alivyoondoka.