Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, Mashariki ya Kati ipo katika hatari ya kuingia katika vita vingine?
Kuongezeka kwa mashambulizi dhidi ya meli za kibiashara katika Mlango Bahari wa Hormuz, kupanda kwa bei ya mafuta na kuongezeka kwa mvutano wakati Marekani inaelekea katika uchaguzi wa katikati ya muhula, kumeibua wasiwasi kuhusu uwezekano wa vita kuzuka tena kati ya Iran, Marekani na Israel.
Baadhi ya wachambuzi wanaonya kuwa mfululizo wa matukio ya hivi karibuni yanaweza kuisukuma eneo hilo katika mgogoro mkubwa wa kikanda.
Shirika la habari la Reuters limeripoti kuhusu mabadiliko katika mbinu za kivita ya Iran, ambapo wamekuwa wakilenga meli za kibiashara zinazopita katika Mlango bahari wa Hormuz.
Kulingana na Reuters, Iran imekuwa ikijaribu kuongeza gharama kwa Marekani na washirika wake kwa kuongeza shinikizo katika njia ya usafiri baharini, na hivyo kuchochea kupanda kwa bei ya mafuta.
Marekani inatarajiwa kufanya uchaguzi wa nusu wa muhula wiki tatu zijazo.
Reuters pia imeripoti kuwa baada ya sehemu za mtandao wa rada wa Iran kuharibiwa, vikosi vya kijeshi vya nchi hiyo vimekuwa vikitumia boti ndogo na pamoja na wanajeshi ili kufuatilia meli zinazopita katika Mlango Bahari wa Hormuz.
Kando na hayo, shirika la habari la Associated Press, likinukuu tangazo la Jeshi la Mapinduzi ya Kiislamu la Iran, limeripoti kuwa meli ya mizigo ilizama baada ya kugonga bomu la baharini katika Mlango Bahari wa Hormuz. Shirika hilo limesema hatari zinazozikabili meli za kibiashara katika njia hiyo ya majini zimeongezeka.
Kulingana na AP, meli za kibiashara sasa zinakabiliwa si tu na vitisho vya maneno na vikwazo vya kupita, bali pia na hatari ya moja kwa moja ya kushambuliwa.
Kuendelea kuongezeka kwa mashambulizi ya meli kunaweza kuilazimisha Washington kuchagua kati ya kukubali vikwazo vya usafiri wa majini katika njia hiyo au kuongeza juhudi za kuifungua tena ili kuhakikisha meli zinapita bila vikwazo.
Shirika la habari la Associated Press pia limeangazia matamshi ya Mohammad Baqer Qalibaf, aliyesema kuwa Iran lazima iendelee kuwa tayari kwa vita licha ya mazungumzo na Washington kuendelea. Shirika hilo limechambua kuwa kauli hizo zinaashiria kuwa juhudi za kidiplomasia na makabiliano ya kijeshi yanaendelea kwa wakati mmoja.
Bei ya mafuta kama kigezo cha kupima hali ilivyo
Mafuta sasa inauzwa kwa takriban dola 100 kwa pipa, bei hiyo ikichochewa na mbinu mpya za Iran za kijeshi baharini na mashambulizi ya Wahouthi dhidi ya miundombinu ya nishati ya Saudi Arabia.
Kupanda kwa bei ya mafuta na nishati nchini Marekani, pamoja na athari zake katika mfumuko wa bei za bidhaa, imekuwa suala muhimu katika kampeni za uchaguzi nchini Marekani.
Takwimu zilizotolewa mapema wiki hii, zilionyesha kuwa kiwango cha mfumuko wa bei nchini Marekani imefikia asilimia 3.7, ikiwa kiwango cha juu kuliko matarajio ya wengi.
Hofu ya vita vya tatu vya dunia
Baadhi ya wachambuzi wanatafsiri maendeleo haya kama ishara ya kuongezeka kwa hatari ya kuzuka tena kwa makabiliano ya kijeshi.
Kwa maoni yao, kuongezeka kwa mashambulizi ya Iran katika Mlango-Bahari wa Hormuz, kuimarika kwa uwepo wa vikosi vya Marekani katika kanda hiyo, pamoja na kuongezeka kwa shughuli za Jeshi la Anga la Israel karibu na Iran, kunaweza kuandaa mazingira ya kuzuka kwa mgogoro mpya katika wiki zijazo.
Wachambuzi hao wanaamini kuwa hatari ya vita huongezeka pale upande mmoja unapoamini kuwa umepata fursa ya kipekee ya kubadilisha uwiano wa nguvu kwa manufaa yake na kwamba haupaswi kuipoteza.
Baadhi ya wachambuzi nchini Marekani wanaamini kuwa Ikulu ya White House na Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, huenda bado wanatathmini iwapo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa dhaifu kutokana na shinikizo la kiuchumi, uharibifu uliotokea na changamoto zinazoendelea nchini humo.
Huenda Marekani na Israel wamehitimisha kuwa kuishambulia Iran tena kijeshi, kunaweza kuisukuma serikali ya taifa hilo kuporomoka au hata kuweka mazingira ya kuondolewa kwake madarakani.
Katika hali hiyo, Marekani na Israel zinaweza kuanzisha operesheni kubwa ya kijeshi inayolenga miundombinu muhimu ya Iran, taasisi za serikali, vituo vya kijeshi na kulemaza uwezo wa Jeshi la IRGC kujenga upya uwezo wake wa kijeshi.
Kwa upande mwingine, huenda maafisa wa Iran wakahitimisha kuwa Donald Trump hana nia ya kuanzisha vita vingine vikubwa Mashariki ya Kati, na kwamba operesheni ya kijeshi ya Iran inaweza kuilazimisha Washington kutathmini upya mkakati wake wa kuikandamiza Iran.
Kwa mtazamo huu, shambulizi la Iran huenda lisichukuliwe kama mwaliko wa kuanzisha vita vya moja kwa moja vinavyohusisha pande zote, bali kama njia ya kuongeza gharama za kuendelea kwa shinikizo la Marekani na kuilazimisha serikali ya Trump kubadili msimamo wake.
Katika hali hiyo Tehran pia inaweza kufikiria kuwa Donald Trump anaweza kubadili mawazo yake katika kuivamia kijeshi tena Iran, ila kusuburia hadi kushambuliwa kunaweza kuwa kosa la kimkakati kwa Iran.
Tathmini hii ni muhimu hasa kwa sababu Tehran imelipia gharama ya kupoteza katika hatua ya kwanza katika migogoro iliyopita. Kwa hiyo, huenda ikapendelea kuchukua hatua ya kwanza wakati huu badala ya kusubiria kushambuliwa bila kutarajia.
Baadhi ya wachambuzi wa Marekani wanaonya kuhusu uwezekano wa mvutano kuingia katika hatua mpya na hatari zaidi katika wiki zijazo.
Pande zote mbili zinaamini kuwa hatua nyingine ya kijeshi inaweza kuchochea uwiano na kufikia suluhisho kwa haraka.
Hata hivyo, matokeo yanaweza kuwa kinyume kabisa; kuongezeka kwa mgogoro, kupanda kwa gharama ya Maisha, na kuzidi kuongezeka kwa mzozo, bila upande wowote kuwa tayari kufikia suluhisho la kudumu, huenda ukawa na madhara makubwa.