Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, Iran itaishambulia Ulaya?
Iran inaweza kushambulia vituo vya kijeshi vya Marekani barani Ulaya iwapo Donald Trump ataishambulia Iran tena, gazeti la Financial Times linaripoti, likinukuu vyanzo vilivyo karibu na mamlaka za Iran.
Hali hii inaweza kupanua wigo wa vita kwa kiasi kikubwa - na kuvuka mipaka ya Mashariki ya Kati.
Wakati huo huo, Iran inakabiliwa na tatizo jingine: kulingana na CNN, Tehran inapoteza hatua kwa hatua udhibiti wa Mlango-Bahari wa Hormuz - mojawapo ya njia muhimu za usambazaji wa mafuta duniani.
Tishio kwa Ulaya
Kulingana na Financial Times, jeshi la Iran lilikuwa linafikiria kushambulia malengo ya Marekani Kusini-mashariki mwa Ulaya.
Miongoni mwa malengo yanayowezekana, vyanzo vya chapisho hilo vinataja kambi ya anga ya Bezmer ya Bulgaria. Mwezi uliopita, Marekani ilipokea ruhusa ya kuitumia kwa ndege yake ya mafuta.
Lengo lingine linalowezekana linaweza kuwa Cyprus.
Mnamo Machi, kambi ya anga ya Uingereza huko Akrotiri kwenye kisiwa hicho ilishambuliwa na ndege isiyo na rubani. Wakati huo, maafisa wa Magharibi walipendekeza kwamba huenda ilikuwa ya Iran, lakini kwamba huenda ilirushwa na vikosi vilivyounganishwa na Tehran, si Iran yenyewe.
Jeshi la Iran pia linafikiria kushambulia nyaya za intaneti zinazopitia chini ya bahari katika eneo la Mlango wa Hormuz ikiwa mzozo utaongezeka.
Kulingana na vyanzo katika gazeti la Financial Times, msimamo mkali zaidi wa Tehran unatokana na mabadiliko ya mtazamo ndani ya uongozi wa Iran.
Idadi inayoongezeka ya wanachama wa utawala huo inaamini kuwa wimbi jipya la vita ni suala la muda tu.
Wakati huo huo, mazungumzo ya kurejesha uhuru wa usafiri wa majini katika Lango la Hormuz yamekwama.
Siku ya Jumanne, Donald Trump alisema kuwa kwa sasa hakuna mazungumzo wala mawasiliano yaliyopangwa na Tehran.
Wawakilishi wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu na makamanda wengine wa Iran wanaonya kuwa iwapo mzozo mpya mkubwa utazuka, Iran inaweza kubadili mbinu zake za awali.
Hapo awali, Tehran ililenga hasa vituo vya kijeshi vya Marekani, miundombinu ya nishati na maeneo mengine muhimu katika Mashariki ya Kati.
Sasa, maeneo yaliyo nje ya eneo hilo yanaweza kuwa shabaha.
Mmoja wa watu waliozungumza na Financial Times anasema kuwa iwapo kutakuwa na uchokozi wa Marekani, Tehran iko tayari kujibu bila vikwazo: "Marekani ikivuka mipaka, Iran itajilinda kwa gharama yoyote, itatoka nje ya eneo hili na kuishambulia Ulaya."
Iran tayari imeionya Uingereza kuwa vituo vyake vya kijeshi vinaweza kuwa shabaha.
Mwezi uliopita, Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kilisema: "Kituo chochote kitakachotumika kuishambulia Iran kitachukuliwa kuwa shabaha halali."
Je, tishio hilo ni la kweli kiasi gani?
Siddharth Kaushal wa Taasisi ya Uingereza ya Utafiti wa Ulinzi (RUSI) anataja tishio la makombora ya Iran dhidi ya Ulaya kuwa ni "halisi lakini lenye mipaka."
Anasema Iran inaweza kutumia makombora ya balistiki ya masafa ya kati, yakiwemo yale ya familia ya Shahab, dhidi ya shabaha za Marekani Kusini na Kusini-mashariki mwa Ulaya.
Hata hivyo, katika masafa marefu, makombora ya aina hiyo yangekabiliwa na changamoto za usahihi na ufanisi.
Kaushal pia anaamini kuwa ingekuwa na faida zaidi kwa Tehran kutekeleza mashambulizi kupitia makundi ya wapiganaji washirika, vikosi vya Kishia nchini Iraq, Hezbollah nchini Lebanon, au Wahouthi nchini Yemen.
Douglas Barry wa Taasisi ya Kimataifa ya Mafunzo ya Kimkakati (IISS) anabainisha kuwa Iran tayari imeonyesha kuwa ina uwezo wa kushambulia katika masafa marefu.
Kulingana naye, majaribio ya kushambulia kambi ya Marekani ya Diego Garcia katika Bahari ya Hindi yanaonyesha kuwa Tehran ina silaha zenye uwezo wa kufikia umbali wa zaidi ya kilomita 2,000.
Wakati huo huo, Barry anaongeza kuwa haijulikani ni makombora mangapi ya aina hiyo ambayo Iran inayo kwa hakika, na kama Tehran iko tayari kutumia hata idadi ndogo yake kwa shambulio la kuonyesha nguvu.
Lakini tatizo kuu ni usahihi.
"Kadiri masafa yanavyokuwa marefu, ndivyo inavyokuwa vigumu kuhakikisha usahihi wa hali ya juu."
Iran tayari imesjaribu kushambulia shabaha za mbali. Baada ya Marekani na Israel kuanzisha vita dhidi ya Iran mwezi Februari, Washington iliishutumu Tehran kwa kurusha makombora kadhaa kuelekea Diego Garcia. Hakuna hata moja kati ya hayo lililofika kwenye shabaha yake.
Mwezi Machi, Uturuki ilisema kuwa ilizuia makombora kadhaa ya balistiki ya Iran, huku kambi ya jeshi la anga ya Uingereza huko Akrotiri, Cyprus, ikishambuliwa na ndege isiyo na rubani (drone).
Kulingana na mmoja wa watoa taarifa wa gazeti la Financial Times, shambulio la hivi karibuni dhidi ya kambi ya Marekani nchini Jordan, ambalo lilisababisha vifo vya askari watatu wa Marekani, lilikuwa muhimu sana kwa Iran.
Mtoa taarifa huyo alilitaja shambulio hilo kuwa shambulio sahihi zaidi la masafa marefu lililofanywa na Iran. Kwa mujibu wake, shambulio hilo lilipaswa kuwa onyo kwa Ulaya: "Inaweza kulengwa na makombora, na inapaswa kuelewa iko upande gani katika vita hivi."
Kwa mujibu wake, kosa kubwa la Marekani, kama vile shambulio dhidi ya miundombinu ya Iran, linaweza kusababisha vita hivyo kuvuka mipaka ya Mashariki ya Kati.
Tatizo jingine ni Lango la Bahari la Hormuz
Katika muktadha huu, CNN inaandika kuwa Iran inapoteza hatua kwa hatua udhibiti wa Lango la Bahari la Hormuz.
Kulingana na kampuni ya Kpler, katika kipindi cha wiki mbili zilizopita, zaidi ya asilimia 80 ya meli zimetumia njia mbadala kando ya pwani ya Oman, licha ya vitisho kutoka Tehran.
"Inaonekana kuwa Iran imepoteza udhibiti wa lango hilo, angalau kwa kiasi fulani," alisema Homayun Falakshahi, mkuu wa uchambuzi wa soko la mafuta katika kampuni ya Kpler.
Nchi za Ghuba pia zinatafuta njia za kuepuka eneo hilo hatari. Kuwait, Saudi Arabia, na Falme za Kiarabu (UAE) zinatumia meli kubwa za kubeba mafuta kusafirisha mafuta hayo nje ya eneo hilo hatari.
Wakati huo huo, Waziri wa Nishati wa Marekani, Chris Wright, alisema kuwa takriban mapipa milioni 15 ya mafuta kwa siku yanapita sasa kupitia Lango la Bahari la Hormuz na njia mbadala.
Kiasi hiki ni kidogo kuliko takwimu ya kabla ya vita ya mapipa milioni 20, lakini ni kikubwa zaidi kuliko ilivyodhaniwa hapo awali.
Trump anazungumzia "udhibiti kamili," lakini hali ni tata zaidi
Donald Trump amedai kuwa Marekani ina "udhibiti kamili wa mlango-bahari huo." Hata hivyo, CNN inahoji dai hilo: usambazaji wa mafuta uko chini sana ikilinganishwa na viwango vya kabla ya vita na Iran inaendelea kushambulia meli.
Mtaalamu Andy Lipow anashauri tahadhari katika kushughulikia kauli kali kutoka pande zote mbili.
"Ningekuwa mwangalifu kuhusu taarifa na vichwa vya habari hivi vyote."
Wakati huo huo, kwa maoni yake, tunaweza kusema kuwa Iran "imepoteza kwa kiasi fulani udhibiti wa mlango-bahari huo."
Hali hiyo pia inachangiwa na utata wa mazungumzo kati ya Oman na Iran kuhusu kurejesha uhuru wa usafirishaji wa meli kupitia Mlango-bahari wa Hormuz. Marekani haishiriki katika mazungumzo hayo. Kulingana na CNN, jambo hili linamkera sana Trump.
Tehran inazidisha msimamo wake mkali
Haya yote yanatokea huku kukiwa na ongezeko la watu wenye misimamo mikali ndani ya Iran.
Kulingana na gazeti la Financial Times, wengi wao wanaamini kuwa Marekani haiwezi kuaminiwa. Wanataka Tehran iilazimishe Washington kulipa gharama kubwa zaidi ili Marekani iweze kuzingatia makubaliano yatakayofikiwa hapo baadaye.
Uteuzi wa Mohsen Rezaei, kamanda wa zamani wa Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), kuwa katibu wa Baraza Kuu la Usalama wa Taifa la Iran ulikuwa na ujumbe maalum.
Wachambuzi wa Iran waliona hili kama ishara ya kuimarishwa kwa msimamo mkali wa serikali hiyo. Katika mazingira haya, msuluhishi mkuu wa Iran, Mohammad Bagher Ghalibaf, anaonekana kupoteza ushawishi na kusukumwa pembeni, huku matarajio ya kufikia makubaliano ya kudumu na Marekani yakizidi kufifia.
"Iran inatoa ishara: ikiwa hamuwezi kufanya kazi na Ghalibaf, itabidi mfanye kazi na Rezaei," chanzo kimoja kililiambia gazeti la Financial Times.
Aliweka wazi ujumbe huo kwa lugha kali zaidi: "Msituudhi, kwa sababu tutatoa majibu makali zaidi."
NATO: Tuko tayari kukabiliana na tishio lolote
Wakati huo huo, NATO ilisema iko tayari kuwalinda washirika wake wa Ulaya dhidi ya shambulio lolote linaloweza kufanywa na Iran.
"Mapema mwaka huu, vikosi vya NATO vilifanikiwa kuzuia makombora ya balistiki yaliyofyatuliwa na Iran kuelekea Uturuki mara nne. Hii inaonyesha kuwa Muungano huo unaweza kuwalinda washirika wake kwa ufanisi," msemaji wa NATO alisema, kulingana na gazeti la Times of Israel.
Hayo ni makombora manne ya balistiki ya Iran ambayo yalikuwa yakielekea Uturuki mwezi Machi na yakazuiliwa na mifumo ya NATO. Muungano huo unahakikisha kuwa uko tayari kuchukua hatua.
"Tuko tayari kukabiliana na tishio lolote na tutafanya kila linalohitajika ili kuwalinda washirika wote," alisema msemaji wa NATO.