Kukaa uchi mbele ya watu wengine kunaweza kukusaidia kuuthamini zaidi mwili wako

Chanzo cha picha, BBC/ Prashanti Aswani
Tafiti zinaonyesha kuwa kukaa uchi mbele ya watu wengine, kukaa bila nguo pamoja na watu wengine bila uhusiano wowote wa kingono, jambo linalojulikana kama ukaaji uchi au naturism, kunaweza kuwasaidia watu kuwa na mtazamo chanya zaidi kuhusu miili yao.
Watu wanaopenda kukaa uchi kwa pamoja na wataalamu wanaeleza BBC jinsi hali hiyo inavyoweza kumsaidia mtu.
Helen Berriman anasema huenda angeweza 'kuuelewa mwili wake vizuri zaidi' tangu akiwa mdogo kama angejua suala la ukaaji uchi mapema.
Katika msimu wa joto wa mwaka 2020, Helen alinunua bikini ili kukabiliana na joto kali. Hakuwa amewahi kuvaa bikini katika miaka 20 iliyotangulia, kwa sababu alikuwa na hana Imani na anavyokaa hali inayomfanya ajikite kupita kiasi katika kasoro anazoziona kwenye mwili na mwonekano wake. Wakati mmoja, mume wake alimweleza kuhusu ukaaji uchi.
"Kukaa uchi ni kuvua nguo na kuwa uchi pamoja na watu wengine, bila matarajio yoyote maalum na bila kuhusisha masuala ya ngono," anaeleza Kerem Soylemez, mhadhiri wa sayansi ya tabia katika Chuo Kikuu cha Regent's jijini London.
Utafiti unaonyesha kuwa kukaa uchi pamoja na watu wengine kunaweza kuwasaidia watu kuwa na mtazamo mzuri zaidi kuhusu miili yao na kuithamini zaidi
Ukaaji uchi na mtazamo kuhusu mwili
Martha Vickery anasema kabla ya kuanza kujihusisha na kukaa uchi, "alichukia kila sehemu ya mwili wake."
Kutokuwa na furaha na mwili wako ni tatizo linalowakabili watu wengi duniani. Hali hii huhusisha mtu kujishughulisha kupita kiasi na mwili wake na kutoridhika nao, hasa kuhusu mwonekano, umbo, sehemu fulani za mwili au uzito.
Nchini Marekani, takriban 51% ya watu wazima hawaridhishwi na mwonekano wa miili yao. Nchini Uingereza, karibu mtu mmoja kati ya wanane amewahi kuwa na mawazo ya kujiua kutokana na changamoto zinazohusiana na mtazamo wake kuhusu mwili.
Kutoridhika na mwili wako kunaweza kuathiri tabia ya mtu kutokana na wasiwasi huo. Kwa mfano, kutoweza kufikia mwonekano wa mwili unaoutamani kunaweza kumfanya mtu akwepe shughuli au maeneo ya kijamii, kufanya mazoezi kupita kiasi, au hata kufanyiwa upasuaji ili kubadilisha umbo au mwonekano wa mwili wake.
"Si suala la kukubalika na wengine tu, bali pia ni kujifunza kujikubali wewe mwenyewe" – Kerem Soylemez

Chanzo cha picha, BBC/ Prashanti Aswani
Kuna faida nyingi za kukuza mtazamo chanya kuhusu mwili wako. Miongoni mwa faida hizo ni kujiamini, kuwa na matumaini kuhusu siku zijazo, kufanya ngono salama na kuwa na afya bora kwa ujumla.
Hata hivyo, namna mtu anavyouona mwili wake ni jambo tata, na madhara yake yanaweza kutofautiana kutoka mtu mmoja hadi mwingine. Kwa mfano, watu wa jamii ya LGBTQ+ wanaweza kuwa na wasiwasi mkubwa zaidi kuhusu miili yao kutokana na ubaguzi wanaokabiliwa nao au hisia zao kuhusu jinsia yao.
Muhtasari wa historia ya kuwa uchi mbele ya watu wengine
Katika nchi za Magharibi, mashindano ya mbio za kukimbia wakati mwingine wanaoshiriki walikimbia wakiwa uchi, kama ilivyokuwa katika mashindano ya michezo ya Ugiriki ya kale.
Mwishoni mwa karne ya 19, mashirika ya kisasa ya kukaa uchi yalianza kujitokeza nchini India iliyokuwa chini ya utawala wa Uingereza.
Nchini Marekani, kukaa uchi kulianza kupata umaarufu mwaka wa 1929, wakati Wajerumani watatu waliokuwa wakiishi New York walipokutana katika mkahawa wa Micholob Café kujadili kuanzisha shirika moja.
Mwaka wa 1974, gazeti la New York Times liliripoti kuwa desturi ya kuwa uchi hadharani na mbele ya watu wengine ilikuwa inaanza kupata umaarufu zaidi nchini Marekani.
Kukaa uchi pia kulipata umaarufu nchini Uingereza katika miaka ya 1920 na 1930.
Tabia ya kujilinganisha na wengine
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Soylemez, ambaye hukaa uchi mwenyewe lakini amekuwa akichunguza kwa miaka mingi ubaguzi dhidi ya watu wanaofuata ukaaji uchi pamoja na jinsi jamii kwa ujumla inavyoiona kukaa uchi anasema watu wanaweza kupinga namna vyombo vya habari vimepotosha taswira ya mwili wa binadamu kwa "kuwa karibu na miili halisi na watu halisi."
Anaongeza: "Si suala la kukubalika na wengine tu, bali pia ni kujifunza kujikubali wewe mwenyewe."
Marina Rachitskiy, mhadhiri wa saikolojia katika Chuo Kikuu cha Roehampton jijini London, ana mtazamo unaofanana. Anaeleza kuwa mara nyingi familia, jamii au mitandao ya kijamii ndiyo huamua au kuweka viwango vya kile kinachopaswa kuchukuliwa kuwa "cha kawaida" au "kinachokubalika", lakini kwa maoni yake, viwango hivyo si lazima viwe kipimo sahihi cha kufuata.
Tafiti nyingi zinaonyesha kuwa mitandao ya kijamii imesababisha baadhi ya watu kuwa na mtazamo hasi zaidi kuhusu miili yao, kwa kuwa mitandao hiyo ina mchango katika kuunda au kuimarisha dhana kuhusu kile kinachochukuliwa kuwa kizuri au cha kuvutia.
Teknolojia za kidijitali, akili mnemba (AI) na zana za kuboresha au kuhariri mwonekano zinazopatikana kwenye simu zinaweza kuwafanya watu kujilinganisha zaidi na wengine, au hata kuufahamu mwili wao kwa mtazamo usio sahihi.
Utafiti mmoja ulibaini kuwa vijana walipopunguza matumizi yao ya mitandao ya kijamii kwa kipindi cha wiki tatu, mtazamo wao kuhusu mwonekano na miili yao, pamoja na jinsi walivyoutazama uzito wao, uliimarika.















