Idadi ya watu waliofariki Nepal na Tibet yafikia 469 huku kukiwa na hofu ya mafuriko zaidi

Chanzo cha picha, Reuters
Takriban watu 469 wamefariki dunia nchini Nepal na mamia hawajulikani walipo baada ya mafuriko makubwa ya ghafla yaliyokumba eneo la milimani mpakani mwa Nepal na Tibet Jumatano.
Nchini Tibet, watu watatu wamefariki na zaidi ya 550 hawajulikani walipo. Haijafahamika iwapo baadhi ya watu hao wamehesabiwa pia katika takwimu za Nepal.
Waokoaji wanaendelea kuwasaka manusura, lakini wanakabiliwa na hofu ya kutokea kwa mafuriko mengine katika eneo lililoharibiwa.
Shirika la Msalaba Mwekundu limeiambia BBC kuwa waokoaji wako katika hali ya tahadhari kutokana na ripoti kwamba wimbi jingine la mafuriko linaweza kulikumba eneo hilo.
Ziwa lenye maji yanayoongezeka limejitokeza karibu na mpaka wa China na Nepal, hali inayozua hofu kwamba huenda kingo zake zikapasuka na kusababisha mafuriko mengine.
Maafisa wa eneo hilo wameiambia BBC kuwa kuporomoka kwa barafu ya mlima kulisababisha wimbi kubwa la maji lililosomba nyumba na barabara, pamoja na kuharibu kituo muhimu cha mpakani kinachounganisha Nepal na Tibet.
Eneo hilo hutembelewa na makumi ya maelfu ya watalii kila mwaka.
BBC imezungumza na ndugu za baadhi ya watu ambao bado hawajulikani walipo.
Dada wawili ambao wazazi wao hawajulikani walipo wameeleza matumaini yao ya kuwaona tena, wakisema: "Tunawapenda sana na tunataka warudi nyumbani."
Soma Zaidi hapa:

