'Sasa niko vizuri': Simulizi ya wanaume waliopandikizwa uume Tanzania

.

Chanzo cha picha, BMKH

    • Author, Yusuph Mazimu
    • Akiripoti kutoka, BBC Dar es Salaam
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Kwa baadhi ya wanaume, tatizo la nguvu za kiume linaweza kuathiri zaidi ya maisha ya tendo la ndoa. Linaweza kugusa kujiamini, mahusiano na maisha ya ndoa.

"Yani sasa hivi niko vizuri, inawezekana ni zaidi ya hata vile nilivyokuwa awali. Nina uhakika siwezi kufeli." Hayo ni maneno ya Titi, mmoja wa wanaume wa kwanza Tanzania kufanyiwa upasuaji wa kupandikiza uume katika hospitali ya umma.

Miaka mitatu iliyopita, Titi na Didi( sio majina yao halisi) walifika Hospitali ya Benjamin Mkapa mjini Dodoma kwa matumaini ya kupata suluhisho la tatizo la nguvu za kiume ambalo lilikuwa limeanza kuathiri maisha yao.

Kwao, uamuzi wa kufanyiwa upasuaji huo haukuwa rahisi. Ulikuja baada ya kujaribu njia nyingine za matibabu na kuishi na tatizo ambalo wanaume wengi husita kulizungumzia wazi.

"Hakuda dawa ambayo hatukuwahi kuchemsha,alishafanyiwa upasuaji mara nyingi tu bila mafanikio", anasema mke wa Didi.

Kwa upande wa Titi, ambaye alipata tatizo la nguvu za kiume kufuatia ajali aliyoipata, yeye anasema alijaribu dawa zote mpaka nje ya nchi alikwenda lakini tatizo halikupata ufumbuzi.

Sasa, miaka mitatu baada ya upasuaji, wamekubali kueleza yaliyowapata. Tumeficha utambulisho wao kwa sababu ya unyeti wa suala hili.

'Baba alikuwa amelala kabisa'

,
Maelezo ya picha, Titi na Didi

Kwa upande wa Titi, tatizo la nguvu za kiume halikuwa tu kuhusu uwezo wa kufanya tendo la ndoa. Anasema hisia zilikuwepo, lakini mwili haukuweza kuitikia.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

"Kwa upande wa hisia, hisia ziko vile vile. Hata wakati ule hisia zilikuwepo, sema baba ndo amelala kabisa."

Baada ya kufanyiwa upasuaji, anasema hali imebadilika kwa kiasi kikubwa. Anaweza kufanya tendo la ndoa na anahisi kujiamini zaidi kuliko alivyokuwa kabla ya matibabu.

Titi alikuwa miongoni mwa wanaume wa kwanza kufanyiwa upasuaji huo katika Hospitali ya Benjamin Mkapa.

Didi alikuwa katika kundi hilo pia. Anakumbuka wakati wao wanaanza matibabu hayo, ulikuwa utaratibu mpya katika hospitali ya umma nchini.

"Kipindi sisi tunaanza hili jaribio ilikuwa mara ya kwanza. Waliamini madaktari wa Benjamin Mkapa, upasuaji ulienda vizuri. Wanaweka vitu bora na halisi, tofauti ni kubwa," anasema.

Didi anacheka anapomweleza mwandishi kwamba angependekeza hata yeye afanyiwe upasuaji huo.

"Ningekushauri hata wewe ukafanye… maana mama anafurahi."

Lakini kwa mke wa Didi, uamuzi huo haukuja bila hofu. Anasema walikuwa wamewahi kutafuta matibabu katika hospitali mbalimbali na kufanyiwa matibabu kadhaa, hivyo alihofia kama upasuaji huo ungeleta matokeo yaliyotarajiwa.

"Kwanza mimi niliogopa kwa sababu tumetumia madawa mengi, tumekwenda hospitali nyingi, amefanya upasuaji mara nyingi. Hakuna mafanikio...

Anaendelea "Halaf ilikuwa mara ya kwanza, hatujawahi kusikia mgonjwa amepona, ilitutia hofu (kuhusu kupandikizwa uume) Lakini alivyorudi…" Anamalizia kwa kicheko.....akimaanisha sasa mambo ya tendo la sasa yako safi

Upandikizaji wa uume unafanyikaje?

.
Maelezo ya picha, Dkt. Remigius Rugakingira

Kusikia neno kupandikiza uume kunaweza kumfanya mtu afikirie kuwa uume mwingine unapandikizwa ama kuwekwa kwa mwanaume mwingine.

Lakini sivyo inavyofanyika. Dkt. Remigius Rugakingira, bingwa wa mfumo wa mkojo na uzazi kwa wanaume katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, anasema madaktari huweka vipandikizi maalum ndani ya uume uliopo.

"Tunachofanya tunaweka vipandikizi viwili kwenye uume baada ya kufanya upasuaji, ambavyo vina vipimo tofauti na mgonjwa anakaa navyo maisha yake yote", anasema Dkt. Rugakingira

Kwa aina ya upandikizaji, vipandikizi hivyo husaidia uume kusimama wakati mwanaume anapohitaji kufanya tendo la ndoa. Kuna aina zinazoweza kuwekewa hali ya kusimama kwa kutumia mfumo wa pampu, huku nyingine zikiwa na vijiti vinavyobaki katika hali ya kukakamaa lakini vinaweza kupindishwa.

Upasuaji huo kwa kawaida hufanywa kwa wanaume ambao tatizo lao ni kubwa na ambao matibabu mengine, kama dawa au njia nyingine za kusaidia kusimamisha uume, hayajasaidia au hayafai kwao.

"Vipandikizi vinavyowekwa hava madhara, havimpi maumivu, vinauwezo wa kumfanya kudumu kwenye tendo la kwa muda wowote anaotaka na kukubaliana na mwenza wake', anasema Dkt. Rugakingira

Baada ya upasuaji, mgonjwa huhitaji muda wa kupona kabla ya kurejea katika shughuli za kawaida. Madaktari katika Hospitali ya Benjamin Mkapa wanasema wagonjwa wanaweza kuanza tena kushiriki tendo la ndoa baada ya takribani wiki sita.

Muhimu zaidi kwa wanaume wengi wanaohofia matokeo ya upasuaji huu ni suala la hisia. Dkt. Rugakingira anasema upasuaji huo unalenga kusaidia uwezo wa kusimamisha uume, lakini hauondoi hisia za tendo la ndoa. Kwa maneno mengine, kifaa hicho si dawa ya kuongeza hamu ya tendo la ndoa; kinasaidia tatizo la kusimamisha uume.

Anathibitisha Titi kwa kauli yake: "Kwa upande wa hisia, hisia ziko vile vile. Hata wakati ule hisia zilikuwepo, sema baba ndo amelala kabisa."

Madaktari wanaeleza kuwa mwanaume wanaofanyiwa upasuaji huu wa kupandikizwa uume wanaweza kupata watoto na kupanga uzazi, kutegemea hali yake ya jumla ya kiafya.

Tatizo la nguvu za kiume ni kubwa

Tatizo la nguvu za kiume ni kubwa kuliko linavyoonekana. Makadirio ya kimataifa yanaonyesha kuwa tatizo hilo linaweza kuathiri sehemu kubwa ya wanaume watu wazima, huku uwezekano wa kupata tatizo ukiongezeka kadri umri unavyoongezeka. Pia linaweza kuhusishwa na matatizo mbalimbali ya kiafya, yakiwemo kisukari, magonjwa ya moyo na shinikizo la damu.

Shirika la Afya Duniani limewahi kuonyesha ukubwa wa tatizo hili duniani, huku makadirio ya kimataifa yakionyesha kuwa asilimia 20%-50% ya wanaume wanakutana na tatizo hili. Hata hivyo, viwango hutofautiana kulingana na umri wa wanaume na namna tatizo linavyopimwa. Wanaume wenye umri wa zaidi miaka 40 na kuendelea ni waathirika zaidi.

Pamoja na kuenea kwake, bado ni tatizo ambalo wanaume wengi hawazungumzii. Aibu, hofu na mtazamo kwamba nguvu za kiume ni sehemu ya uanaume zinaweza kuwafanya baadhi ya wanaume kuchelewa kutafuta msaada wa kitabibu.

Kwa wanaume ambao dawa au matibabu mengine hayajawasaidia, upasuaji wa uopandikizaji wa uume unaweza kuwa moja ya chaguo muhimu na la mwisho la matibabu. Lakini si kila mwanaume mwenye tatizo la nguvu za kiume anahitaji au anafaa kufanyiwa upasuaji huu.

Je, huduma hii inaweza kuwafikia wanaume wengi zaidi?

.
Maelezo ya picha, Hospitali ya Benjamin Mkapa, Dodoma

Hospitali ya Benjamin Mkapa inasema wanaume 14 wamefanyiwa upasuaji huu tangu huduma hiyo ianze miaka mitatu iliyopita.

Lakini gharama bado ni changamoto.

Kwa sasa, upasuaji huo unagharimu kati ya shilingi milioni sita na 10, sawa na takribani dola 2,300 hadi 3,800 za Marekani.

Kwa wanaume wengi, hiyo ni gharama kubwa ya matibabu.

Ndiyo maana madaktari na mamlaka za afya wanaangalia namna ya kupunguza gharama na kufanya huduma hiyo ipatikane kwa wanaume wengi zaidi wanaohitaji.

Kuhusu gharama Dkt. Rugakingira anasema; " Mtu mwenye tatizo la nguvu za kiume wakati mwingine unakuta anakuwa na shida zingine kama msongo wa mawazo, kisukari, presha, kwa hiyo yule mtu anapimwa kila kitu, anatibiwa hayo matatizo pia, usipotibu inaweza kuathiri zoezi letu zima".

Kwa upande wa Didi na Titi, hata hivyo, miaka mitatu imepita tangu walipoingia katika kile kilichokuwa kipindi kipya na cha hofu katika maisha yao.

Leo, wanazungumza kuhusu tofauti wanayoiona. Kwa hospitali ya Benjamini Mkapa na Tanzania kwa ujumla, mafanikio ya matibabu haya hayapaswi kupimwa kwa uwezo wa mwili pekee, yanapimwa kwa hatua katika afya ya akina baba.

"Kauli mbiu kubwa katika afya ya kinababa, tunataka mwanaume awe na furaha pamoja na mwenza wake."

Madaktari na wataalam wengine wa afya kwao huo ndio ushuhuda mkubwa zaidi.