Dawa za kifafa, kilevi kipya cha vijana?

Ili kufurahia kuwa nje usiku na marafiki, awali ilimbidi Matt anywe pombe hadi kuzidiwa na kuwa na maumivu.
Kama asingefanya hivyo, kijana huyo mwenye umri wa miaka 22 kutoka kaskazini mwa Uingereza angekaa kimya usiku kucha, akiwa na hofu ya kusema jambo lisilofaa.
Kisha, miaka miwili iliyopita, aliacha kunywa pombe na kuanza kutumia dawa alizozigundua kupitia mitandao ya kijamii.
Anapojiandaa kwenda kujivinjari siku ya Ijumaa, Matt ambaye jina lake limebadilishwa, sasa hutumia dawa anazonunua kinyume cha sheria mtandaoni ambazo kwa kawaida hutibu kifafa na maumivu ya neva, pamoja na dawa ya aina ya 'beta-blocker' iliyoundwa kupunguza kasi ya mapigo ya moyo na kutuliza misuli inayotetemeka.
Anasema dawa hizo humpa hisia sawa na zile za kunywa pombe lakini bila madhara ya uchovu na maumivu ya kichwa yanayofuata baada ya kunywa pombe.
"Kiasi cha pombe unachopaswa kunywa ili kupata matokeo sawa na ya dawa hizi ni hatari sana kwa afya na haileti hisia nzuri," anasema.
Matt anasema dawa anazotumia humfanya ajihisi mwenye furaha tele, hutuliza mawazo yake ya wasiwasi na kurahisisha kutangamana na watu wengine.
Kwa Matt, ambaye anasema tayari amejaribu tiba ya kuangazia hali ya wasiwasi, jambo lililoanza kama njia ya kumsaidia wakati wa kutoka usiku sasa limeenea hadi kwenye nafasi amnbapo vijana wanakutana na wachumba wao na mikutano ya familia. Bila dawa hizo, Matt anasema, kuna hali nyingi ambazo "asingethubutu kujaribu".
Matt anakanusha kuwa sasa anategemea sana dawa hizo.
Duniani kote, ushahidi unaonyesha kuwa vijana wanageukia dawa na kemikali mbalimbali kama njia mbadala ya pombe.
Baadhi yake zinapatikana katika mfumo wa vidonge na nyingine hudungwa mwilini aina inayozidi kupata umaarufu mtandaoni.
'Kizazi kisichotumia pombe'
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Harakati za kutafuta njia mbadala "zenye afya zaidi" badala ya kunywa pombe zimesaidia kuunda soko jipya la dawa za aina hiyo zinazotangazwa kwenye mitandao ya kijamii kama dawa zisizo na madhara yakuhisi kisunzi, (ulegevu au maumivu ya kichwa baada ya kunywa pombe).
Zinachukuliwa kama "njia mbadala safi na salama zaidi," anasema Liam Knowles, mtafiti wa masuala ya uraibu katika Chuo Kikuu cha Teesside. "Watumiaji hawahisi vibaya sana siku inayofuata kwa hivyo, watu hufikiri ni salama zaidi."
Ni vigumu kujua idadi kamili ya vijana wanaotumia dawa za hospitali zisizodhibitiwa kwa nia tofauti, kwani wengi huzipata bila cheti cha daktari.
Dawa hizi zimesambaa sana kwenye maelfu ya video katika mitandao ya kijamii, huku watumiaji wakihimizwa kutengeneza mchanganyiko wa dawa.
Kuongezeka kwa hamu ya kutumia dawa hizi kunajiri wakati ambapo vijana wanazidi kuacha pombe, jambo linalofanya Kizazi cha Z kupata jina la utani la 'kizazi kisichotumia pombe'.
Wale wale wenye ushawishi mkubwa mtandaoni wanaotangaza faida za michanganyiko hii ya dawa pia wanashauri watu kuepuka pombe.

Chanzo cha picha, Getty Images
Utafiti uliofanywa mwaka jana na shirika la hisani la Drinkaware ulibaini kuwa asilimia 26 ya vijana wenye umri wa miaka 18 hadi 24 nchini Uingereza hawanywi pombe, ikilinganishwa na asilimia 7 mwaka wa 2012.
Kwa vijana wanaotaka kujaribu vitu vipya wamevutiwa sana na dawa hizi.
Utafiti uliochapishwa katika jarida la *Nature Communications* ulikadiria kuwa matumizi ya dawa hiyo duniani yaliongezeka zaidi ya mara nne kati ya mwaka wa 2008 na 2018.

Chanzo cha picha, Getty Images
Nchini Uingereza, dawa ya pregabalin iliwekwa upya katika kundi la dawa zinazodhibitiwa la kiwango cha C, mnamo mwaka wa 2019, wale wanaoinunua bila cheti cha daktari wanaweza kuhukumiwa kifungo cha miaka miwili jela (ingawa kwa uhalisia, ni watu wachache sana wanaofungwa).
Bado inaagizwa sana na madaktari kwa ajili ya kutibu kifafa, maumivu ya neva, na wasiwasi. Washauri huru wa serikali ya Uingereza kuhusu masuala ya dawa pia wameanzisha uchunguzi wa kina kuhusu matumizi mabaya ya dawa hiyo.
Nchini Jordan, Ukraine, na India, watafiti pia wamebaini ongezeko la matumizi mabaya ya dawa ya pregabalin.
Nchini China, serikali iliimarisha udhibiti wa dawa hiyo mapema mwaka huu kwa kupiga marufuku mauzo mengi ya mtandaoni na kuweka mipaka ya kiasi cha dawa hiyo kinachoweza kuzalishwa katika kila jimbo.
Matumizi ya mchanganyiko wa dawa
Matt alipata habari kuhusu dawa anazotumia akiwa na umri wa miaka 20 kupitia kwa Braden Peters, anayefahamika zaidi kama 'Clavicular', mtu maarufu kwenye mitandao ya kijamii anayezua utata, ambaye amezungumza waziwazi katika matangazo ya moja kwa moja kuhusu kutumia dawa hizo kama sehemu ya mchanganyiko wa dawa, ili kupunguza wasiwasi wake katika mazingira ya kijamii.
Na dawa hizo zimeanza kujadiliwa sana katika mazungumzo ya kawaida ya umma. Waigizaji Rachel Sennott na Kristen Bell ni miongoni mwa watu mashuhuri waliozungumza hadharani kuhusu kutumia dawa za aina ya 'beta blockers', pamoja na mtu maarufu wa mitandao ya kijamii Khloé Kardashian.
Pregabalin, hasa inapotumiwa kwa viwango vinavyozidi vile vilivyoelekezwa na daktari, inaweza kuwafanya watumiaji kuhisi utulivu na furaha, hali inayofanana na ile ya kulewa pombe.
Kwa Mei, mwanafunzi wa chuo kikuu mwenye umri wa miaka 20 nchini China (ambaye jina lake halisi limebadilishwa), haya ndiyo madhara aliyokumbana nayo.
Anasema dawa hizo hupunguza dalili za wasiwasi alionao na zinaweza kumfanya ahisi furaha iliyopitiliza. Alianza kuzitumia wakati wa sherehe. "Ilikuwa kana kwamba naweza kuwa mtu wa kuvutia zaidi chumbani," anasema.
'Hakuna kitu cha bure'
Dawa hizi pia zinaweza kuwa bei nafuu zaidi kuliko pombe.
Matt anasema hutumia kiasi kidogo cha senti 18 (pauni 0.18) kwa dawa hizo anapotoka usiku mmoja, akielezea kuwa ni gharama ya chini.
Knowles, mtafiti wa masuala ya uraibu, anasema vijana wengi aliokutana nao wakitumia dawa hizi kwa ajili ya starehe nchini Uingereza wanajali sana afya zao.
"Watu katika pia jamii hii wanaamini kuwa pregabalin haina madhara ya kiafya ikilinganishwa na pombe," Matt anasema.
Pombe imehusishwa na angalau aina saba za saratani, na Shirika la Afya Duniani lilionya miaka michache iliyopita kuwa unywaji wa pombe kwa kiwango chochote huleta hatari.

Chanzo cha picha, Getty Images
"Propranolol na pregabalin bila shaka ni salama zaidi kuliko pombe, lakini si salama kabisa," anasema.
Lakini anasema hali hubadilika wakati pregabalin inapotumiwa kwa dozi kubwa ili kulewa kama vile Matt anavyosema anavyofanya.
"Ikiwa wanaitumia kama aina ya kileo ili kulewa, basi wako katika hatari ya kuwa waraibu," anasema. "Hakuna kitu cha bure katika hali hiyo."
Propranolol pia ina hatari zake. Ingawa kwa ujumla inachukuliwa kuwa salama inapotumiwa kama ilivyoelekezwa, matumizi yasiyofaa au ya dozi kubwa yanaweza kusababisha kizunguzungu, kuzirai, na mapigo ya moyo kwenda polepole kupita kiasi.
Hatari zinaweza kuwa kubwa zaidi wakati dawa zinapotoka katika vyanzo visivyodhibitiwa.
"Daima kuna hatari ya kupata dawa ambazo hazijatengenezwa kwa kuzingatia viwango vya kimatibabu," anasema Nutt.
Hatari za uraibu
Jones, mwanasaikolojia kutoka King's College, anasema kuwa kulinganisha madhara ya kimwili ya dawa hizi na yale ya pombe kunaweza kufanya tukose kuona swali la msingi zaidi, ni nini hutokea wakati watu wanaanza kuamini kuwa wanaweza tu kushiriki katika shughuli za kijamii kwa msaada wa kunywa dawa?
"Pombe kwa kiasi kikubwa ni hatari, lakini pia ni hatari kutumia dawa mara kwa mara bila usimamizi wa daktari," anasema.
Sofia, mfanyakazi wa huduma kwa wateja kutoka Ukraine, alifuata mkondo kama huo, mwanzoni alitumia dawa ya *pregabalin* kabla ya sherehe na hafla za kijamii, lakini punde alianza kuitumia kazini. "Ilinisaidia," anasema. "Ninafanya kazi na watu. Ilifanya iwe rahisi kuwasiliana na kutatua matatizo."
Aliposhindwa kupata dawa hiyo kwa wiki mbili, anasema alipatwa na vipindi vya huzuni kali na mawazo ya kutaka kujiua. "Sikuelewa kilichonipata. Nilikuwa na wasiwasi, sikuweza kula, wala kuonana na marafiki."
Knowles anasema watumiaji vijana mara nyingi hawatambui uraibu wao wa dawa ikiwa bado wanaendelea na maisha yao ya kawaida (kama vile kudumisha kazi au uhusiano). Badala yake, wanahusisha uraibu na watu ambao maisha yao yameharibika.
Dawa za soko haramu
Wakati China, India na nchi nyingine zikichukua hatua za kudhibiti dawa hizi, baadhi ya watu wanahoji kuwa kuweka vikwazo zaidi kunaweza kuleta hatari nyingine.
Mykyta Lapin, mtaalamu wa magonjwa ya mlipuko na mkuu wa shirika la Ukraine la kupunguza madhara liitwalo *Mind Games*, anasema kupiga marufuku dawa hizo hakuzuii watu kuzitumia.
"Kupiga marufuku dawa fulani husababisha watu kugeukia soko haramu na kununua dawa zenye ubora usioaminika," anasema, jambo linaloleta hatari ya kuzitumia kwa kiasi kikubwa kupita kiasi (*overdose*).
Knowles anasema *pregabalin* inayopatikana kinyume cha sheria ina hatari ya ziada kwa sababu watumiaji huenda wasijue hasa wanachotumia.
Imetafsiriwa na Sarafina Robi na kuhaririwa na Asha Juma












