Viboko wa kokeni: Kwa nini Colombia inataka kuwaua viboko wa Pablo Escobar?

    • Author, Fernando Duarte
    • Nafasi, BBC News World Service
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Pablo Escobar ni jina ambalo Colombia imekuwa ikijaribu kulisahau kwa zaidi ya miaka 30.

Ni mmoja wa wahalifu mashuhuri, alikuwa mwanzilishi wa genge maarufu la dawa za kulevya la Medellin miaka ya 1980 na aliwahi kuwa mmoja wa watu matajiri duniani.

Mfalme huyo wa zamani wa kokeini pia alihusika kuingiza kundi la viboko kwenye bustani yake ya wanyama katika miaka ya 1980, na sasa wameongezeka na kuenea katika moja ya mito mikubwa ya nchi - Mto Magdalena.

Utafiti wa mwaka 2022 unaonyesha kuwa sasa kuna "viboko wa kokeini" kama 250, na baada ya miongo kadhaa ya majadiliano, serikali ya Colombia imetangaza mipango ya kuwaua hadi 80 kati yao.

"Tusipofanya hivi, hatutaweza kudhibiti idadi yao," Waziri wa Mazingira Irene Vélez alisema. "Tunapaswa kuchukua hatua hii ili kuhifadhi mifumo yetu ya ikolojia."

Hata hivyo, mashirika ya haki za wanyama yamekosoa uamuzi huo, huku seneta Andrea Padilla akiuita "ni ukatili."

"Siwezi kuunga mkono mauaji ya viumbe wenye afya njema," aliandika kwenye X, "viboko hao ni waathiriwa uzembe, kutojali na ufisadi wa serikali."

Wanyama vamizi

Wanasayansi nchini Colombia wametetea kwa muda mrefu kwamba kuwauwa ndiyo njia pekee ya kupunguza athari zao za kimazingira. Tatizo kuu hapa ni kwamba viboko si wanyama wenye asilia ya nchi za Amerika Kusini - au mahali popote nje ya Afrika.

Hiyo ina maana kwamba hakuna wanyama wanaowawinda viboko hao kama vile simba na mamba na hivyo wanaweza kuzaliana kwa kiwango kikubwa.

"Ni dhahiri kwamba tunawahurumia wanyama hawa, lakini kama wanasayansi tunahitaji kuwa wakweli,” Mwanabiolojia wa Colombia Nataly Castelblanco, mmoja wa wataalamu wa viboko hao, ameiambia BBC.

"Viboko ni spishi vamizi nchini Colombia na tusipowapunguza kwa kuwauwa, tunaweza kukosa udhibiti nao katika miaka 10 au 20 tu."

Barani Afrika, kuna misimu mikali ya kiangazi ambayo pia husaidia kudhibiti idadi yao. Hilo ni tofauti na mvua inayonyesha mara kwa mara katika bonde la Mto Magdalena.

Mazingira ya makazi yao ya Amerika Kusini ni bora sana kiasi cha kuonekana wanakuwa mapema - huanza kuzaa watoto wakiwa na umri mdogo.

Viboko walifikaje Colombia?

Kuibuka kwa kile kinachoitwa "viboko wa kokaini" kunahusiana moja kwa moja na mauaji ya Pablo Escobar, yaliyofanywa na vikosi vya usalama vya Colombia mwaka 1993.

Baada ya kifo chake katika jumba lake la kifahari huko Hacienda Napoles, lililoko kilomita 250 kaskazini magharibi mwa mji mkuu wa Colombia, Bogota, eneo lake lilitekwa na serikali.

Walibomoa bustani yake ya wanyama - lakini kwa sasa imekuwa ni sehemu maarufu ya bustani ya kuvutia.

Wanyama hao mwanzoni walisambazwa katika mbuga za wanyama kote nchini. Lakini si viboko.

"Ilikuwa vigumu kuwahamisha, kwa hivyo mamlaka iliwaacha tu pale, labda ikifikiri wangekufa," Castelblanco anasema.

Badala yake, waliongezeka.

"Ni kundi kubwa zaidi la viboko nje ya Afrika, kwani Afrika ndio eneo lao la asili," daktari wa mifugo na mhifadhi Carlos Valderrama anaeleza kwa BBC.

Na idadi inakadiriwa kuongezeka. Castelblanco na wenzake wanasema idadi yao itafikia 1,400 mapema mwaka 2034 ikiwa hawatopunguzwa - wote walitokana na kundi la awali la dume na jike watatu.

Katika utafiti wa 2021, walipendekeza wanyama 30 wanahitaji kuchinjwa au kuhasiwa kila mwaka ili idadi hiyo isifike.

Viboko hawa ni tatizo?

Wanasayansi wanaosoma athari za kimazingira za viboko wanaamini uwepo wao unaweza kuathiri mfumo ikolojia wa eneo hilo kwa njia kadhaa: kukimbia kwa spishi asilia ambazo tayari ziko hatarini kutoweka, kama vile nguva, na kubadilisha muundo wa kemikali wa njia za maji, mabadiliko yanayoweza kuhatarisha uvuvi.

"Viboko wameenea katika bonde kubwa la mto huo, ambapo maelfu ya watu hujipatia riziki," Castelblanco anasema. "Wanaonekana hadi umbali wa kilomita 370 kutoka Hacienda Napoles."

Pia ni hatari kwa watu: ingawa hakujawa na mashambulizi yoyote mabaya nchini Colombia hadi sasa, viboko ni wanyama wanaokadiriwa kuwaua takriban watu 500 kwa mwaka barani Afrika – idadi kubwa zaidi kuliko watu wanaouwawa na simba, mamba au tembo.

Kuna njia nyingine?

Pia ni muhimu kutambua kwamba kuna wataalamu wanaopinga wazo la kuwapunguza kwa kuwauwa.

Enrique Ordoñez, mwanabiolojia katika Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Colombia, anasema "viboko wa kokeni" wanaleta matumaini ya kuhifadhi idadi ya viboko duniani - wanachukuliwa kuwa spishi zilizo hatarini na mashirika yasiyo ya kiserikali kama vile Umoja wa Kimataifa wa Uhifadhi wa Mazingira (IUCN).

Yeye ni mmoja wa wataalamu wanaotetea njia ya kuwafunga vizazi ili kudhibiti idadi yao.

Lakini njia hiyo si rahisi.

Carlos Valderrama anasema mwaka 2009, alifanya uhasishaji wa wa kuondoa kizazi cha "kiboko wa kokaini" dume kama sehemu ya jaribio la kusoma chaguzi za kudhibiti idadi ya viboko.

"Tunazungumzia mnyama ambaye anaweza kuwa na uzito wa tani tano na ni mkali sana," anasema Valderrama.

"Ingawa tulikuwa tumemtuliza mnyama huyo kwa usingizi, lakini alikaribia kuipindua kreni tuliyotumia kumbemba katika upasuaji. Ilikuwa kama kubeba dinosaur."

Daktari huyo wa mifugo anasema somo kuu katika jaribio hilo lilikuwa kwamba kuhasiwa pekee sio chaguo - hasa ukizingatia gharama ya dola $50,000.

Takwimu rasmi za serikali zinasema ni wanyama wanne pekee waliofanyiwa upasuaji wa kufunga kizazi kati ya 2011 na 2019.

"Wengi wa viboko hawa wanaishi porini. Haiwezekani kuwafikia wote kwa urahisi."

"Wakati huo huo, wataendelea kuzaliana. Na viboko huwa na wake wengi, kumaanisha dume mmoja anaweza kuwapa mimba majike wengi," anasema Valderrama.

Serikali ya Colombia hapo awali ilipendekeza mbinu nyingine - kuwakamata viboko hao na kuwapeleka kwenye bustani za wanyama kote ulimwenguni - lakini juhudi za kuwahamisha zilishindwa, haswa kwa sababu ya gharama za usafirishaji.

Na kuwapeleka Afrika, asili yao, haikuwa chaguo sawa. Wakiwa wamezaliwa na kukulia Colombia – wanaweza kusababisha hatari ya magonjwa na hatari za kijenetiki.

Kwa nini hawajauawa?

Kipi kiliizuia serikali kuchukua hatua kali zaidi? Jibu fupi: maoni ya umma.

Watu wana huruma sana na "viboko wa kokeini," anasema Nataly Castelblanco.

Baada ya vyombo vya habari vya Colombia kuripoti kuhusu utafiti wake, mwanabiolojia huyo alianza kupokea jumbe za matusi na vitisho vya kuuawa kwenye mitandao ya kijamii.

"Niliitwa 'muuaji' miongoni mwa mambo mengine. Baadhi ya watu nchini Colombia wanaweza kukasirika sana wanapozungumzia kuhusu viboko," anasema.

Pia kuna jamii za bonde la Mto Magdalena. Bustani ya wanyama huko Hacienda Napoles ina viboko wachache waliokamatwa tena na huvutia maelfu ya watalii kwa mwaka - cha kushangaza, wakati Escobar alipokuwa hai, alikuwa akiruhusu ziara za watu na Nataly Castelblanco anakumbuka kwenda huko na familia yake akiwa mtoto.

2009 wakati wanajeshi wa Colombia walipompiga risasi kiboko Pepe, aliyeaminika kuwa tishio kwa jamii zilizo karibu na eneo hilo, ukosoaji mkubwa ulitokea – hasira zaidi zilitokana na watu hao wenye silaha kupiga picha za selfie na mwili wa kiboko huyo na hilo lilisababisha ulinzi wa kisheria kwa viboko hao.

Lakini sasa hali imekuwa mbaya, mwanabiolojia David Echeverri, wa shirika la mazingira la Colombia Cornare, anaiambia BBC News World Service. "Kupunguzwa idadi ndio suluhisho pekee na la muhimu."

Zaidi ya miaka 30 baada ya kifo cha Pablo Escobar, "viboko wa kokaini" wanawakilisha ushahidi wa historia ya mlanguzi wa dawa za kulevya nchini Colombia.