Polisi wanasema sumu ya panya imepatikana kwenye kopo la chakula cha watoto nchini Austria
Polisi nchini Austria wamewataka watu kuwa waangalifu baada ya sampuli ya chakula cha watoto cha HiPP kugundulika kuwa na sumu ya panya.
Polisi katika eneo la mashariki la Burgenland wamesema kopo hilo la chakula cha karoti na viazi liliripotiwa na mteja, na kwa bahati nzuri mtoto hakula chakula hicho.
Polisi wanasema kopo hilo linaonekana kuwa lilichezewa au kufanyiwa uharibifu. Mamlaka zinaamini kuwa kuna kopo jingine lenye sumu bado lipo sokoni, na zimetoa maelekezo ya jinsi ya kutambua makopo yenye dosari.
Hata hivyo, taarifa ya polisi imesema onyo hilo lilitoka kwa wachunguzi wa Ujerumani, na makopo yaliyo na dosari pia yamekamatwa katika Jamhuri ya Czech na Slovakia.
Siku ya Jumamosi, kampuni ya HiPP ilirejesha aina zote za chakula cha watoto cha kwenye makopo kinachouzwa katika maduka ya Spar nchini Austria, ikisema kula chakula hicho kunaweza kuwa hatari kwa maisha.
Kampuni hiyo yenye makao yake Ujerumani imesema kurejeshwa kwa bidhaa hizo si kwa sababu ya tatizo la ubora au uzalishaji, na kwamba makopo yalitoka kiwandani yakiwa katika hali nzuri kabisa.
Imeongeza kuwa tukio hilo linahusiana na kitendo cha uhalifu kinachochunguzwa na mamlaka.