ICC yashinda Tuzo ya Sakharov ya Uhuru wa Mawazo 2026

Mahakama hiyo imechaguliwa kuwa mshindi mbele ya wagombea wengine wawili waliofika hatua ya mwisho: kiongozi wa upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu, na dada wawili wa Iran, Taraneh na Romina Rahimi.

Muhtasari

Ruka Video uendelee
  • xx
  • Wicknell Chivayo
  • Kijanangoma
  • xx
  • Besigye
  • .
  • xx
  • xx
  • xx
  • Lungu
  • xx
  • xx
  • d
  • s
  • a
  • Sonko
  • xx
  • xx
  • xx

Moja kwa moja

Na Beldeen Waliaula & Mariam Mjahid

  1. Mjukuu wa Museveni apandishwa cheo na kuwa luteni wa pili jeshi la Uganda

    h

    Ruhamya Kainerugaba, mjukuu wa Rais wa Uganda Yoweri Museveni, amepandishwa cheo na kuwa luteni wa pili katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Uganda (UPDF).

    Hafla ya kumtawaza ilifanyika katika Chuo cha Kijeshi cha Uganda kilichopo Kabamba, wilayani Mubende.

    Kupitia mtandao wa X, Ruhamya alielezea furaha yake kwa hatua hiyo, akiandika: “Nimekipata cheo hicho kupitia kujitolea na kujitolea mhanga, nakivaa kwa fahari. Safari inaendelea.”

    Ruhamya alikamilisha mafunzo ya maafisa wa kijeshi katika Chuo cha Kijeshi cha Sandhurst nchini Uingereza mwezi Agosti 2026. Mafunzo hayo yalidumu kwa wiki 44, na alitunukiwa rasmi cheo hicho Agosti 7, 2026.

    Baba yake, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ambaye pia ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Uganda, alihitimu katika chuo hicho mwaka 2000.

    Safari ya Ruhamya jeshini ilianza Juni 2025 alipojiunga na UPDF akiwa mwanajeshi wa kawaida. Alihudumu kwa muda mfupi katika kikosi maalumu cha ulinzi kabla ya kwenda Uingereza kwa mafunzo.

    Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Museveni aliwataka maafisa wapya kudumisha nidhamu, kuwa karibu na wananchi na kuitumikia Uganda kwa heshima.

    Alisisitiza pia umuhimu wa maendeleo ya uchumi, mafunzo bora ya kijeshi na uwekezaji katika sayansi na teknolojia kwa ajili ya kuimarisha ulinzi wa taifa.

    Museveni aliwapongeza makamanda wa jeshi kwa juhudi za kupambana na ufisadi, akisema suala hilo linaathiri moja kwa moja ustawi wa wanajeshi.

    Kwa upande wake, Jenerali Muhoozi pia alimpongeza mwanawe Ruhamya kwa kutunukiwa cheo cha luteni wa pili katika UPDF baada ya kukamilisha mafunzo ya kijeshi nchini Uingereza.

    “Ninataka kumpongeza mwanangu mpendwa, Ruhamya Abasheija, kwa kutunukiwa cheo cha afisa katika jeshi la Mungu, UPDF. Mwenyezi Mungu akubariki daima, Luteni wa Pili Ruhamya,” aliandika.

    Kutunukiwa cheo hicho kwa Ruhamya kunaendeleza historia ya utumishi wa kijeshi katika vizazi vitatu vya familia ya karibu ya Rais Museveni, ambaye mwenyewe na mwanawe Muhoozi pia wamehudumu jeshini.

  2. Ufaransa yathibitisha kisa cha kwanza cha virusi vya Shamonda kwa binadamu

    h

    Mamlaka za afya nchini Ufaransa zinasema virusi vya Shamonda, ambavyo kwa kawaida huathiri mifugo, vimegunduliwa kwa binadamu kwa mara ya kwanza. Mgonjwa huyo, aliyekuwa na kinga dhaifu sana ya mwili, alifariki mapema mwezi huu.

    Katika taarifa ya pamoja, wizara za afya na kilimo zimesema hadi sasa hakuna hatari kwa afya ya umma iliyobainika.

    Zimesema maambukizi hayo yanaonekana kuwa ya kipekee, yakihusisha mgonjwa aliyekuwa na kinga dhaifu sana na aliyelazwa hospitalini kutokana na hali mbaya ya kiafya.

    “Tangu awali, virusi vya Shamonda vilidhaniwa kuwa haviwezi kuambukiza binadamu, kwani vilikuwa vimegunduliwa kwa wanyama pekee, licha ya kusambaa Afrika na Asia kwa miongo kadhaa.”

    Virusi hivyo, vilivyokuwepo Afrika na Asia kwa miongo kadhaa bila kugunduliwa kwa binadamu, ni sehemu ya kundi la Orthobunyavirus. Kwa kawaida huenezwa kwa wanyama kupitia kuumwa na wadudu wadogo wanaofyonza damu.

    Kwa mujibu wa mamlaka hizo, uchunguzi wa awali unaashiria kuwa mgonjwa huyo huenda aliambukizwa baada ya kuumwa na mdudu aina ya midge mashariki mwa Ufaransa, ambako virusi hivyo vilikuwa vikizunguka miongoni mwa wanyama katika majira ya kuchipua na kiangazi.

    Mamlaka hizo zimesema matatizo ya mfumo wa fahamu aliyopata mgonjwa kabla ya kifo chake huenda yalihusiana na maambukizi hayo. Hata hivyo, uchunguzi wa kitabibu na wa maabara bado unaendelea.

    Ng'ombe ndio wanyama wakuu wanaoathiriwa na virusi hivyo. Dalili kwa ng'ombe ni pamoja na kuharisha ghafla, homa, uchovu na kupungua kwa uzalishaji wa maziwa.

    Shirika la Afya Duniani (WHO) na Kituo cha Ulaya cha Kuzuia na Kudhibiti Magonjwa vimearifiwa kuhusu kisa hicho.

  3. Iran yaweka sanamu ya Trump ndani ya gereza la mfano kwenye bango la matangazo

    N

    Bango la matangazo lenye umbo la pande tatu limewekwa katika eneo lenye shughuli nyingi la Tajrish Square, kaskazini mwa mji mkuu wa Iran, Tehran.

    Bango hilo linaonyesha mtu aliyevaa barakoa yenye sura inayofanana na Rais wa Marekani Donald Trump, akitembea ndani ya sehemu iliyoundwa kufanana na selo ya gereza. Wapita njia husimama kutazama na kupiga picha.

    Kwa mujibu wa taarifa hiyo, bango hilo lilizinduliwa Jumatano, Oktoba 19, huku baadhi ya watumiaji wa mtandao wa X wakisema ujenzi wake ulikuwa umechukua takriban mwezi mmoja.

    Shirika la habari la Mehr linaripoti kuwa maonyesho hayo yataendelea saa 24 kwa siku. Pembeni yake kuna ujumbe unaosomeka: “Kutokuona tukio hili ni kosa.”

    Bango hilo la kipekee limevutia pia vyombo vya habari vya kimataifa, vikiwemo Reuters, Agence France Presse na gazeti la The Guardian la Uingereza.

    onyesho hilo linajiri wakati Tehran na Washington wakiendelea kuvutana huku mazungumzo ya kusitisha mapigano yakikwama.

    H
  4. UAE yampendekeza mwanadiplomasia mwanamke kuwania ukatibu mkuu wa UN

    d

    Falme za Kiarabu (UAE) zimemteua mwanadiplomasia wake wa zamani katika Umoja wa Mataifa, Lana Nusseibeh, kuwa mgombea wa nafasi ya Katibu Mkuu wa UN, Antonio Guterres, ambaye muhula wake wa pili unatarajiwa kumalizika baada ya chini ya miezi mitatu.

    Nusseibeh, ambaye kwa sasa ni naibu waziri wa mambo ya nje wa UAE, aliwahi kuiwakilisha nchi hiyo katika Umoja wa Mataifa kwa zaidi ya muongo mmoja.

    Amesema, wakati migogoro ya kimataifa ikiendelea kuongezeka, atajitahidi kurejesha nafasi ya Umoja wa Mataifa kama jukwaa la kutatua mizozo kupitia diplomasia.

    Akichaguliwa, Nusseibeh atakuwa mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo.

    Wagombea wengine sita pia wanawania nafasi hiyo. Katika kura za awali za kupima uungwaji mkono wa wagombea, Rebecca Grynspan wa Costa Rica anaongoza kwa tofauti ndogo.

    Mgombea mwingine ni Rafael Grossi, raia wa Argentina ambaye kwa sasa anaongoza Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki (IAEA).

    Soma Pia:

  5. Waandamanaji wavuruga mkutano wa kisiasa wa Trump South Carolina

    x

    Walinzi waliwatoa waandamanaji wasiopungua 10 katika mkutano wa Rais wa Marekani Donald Trump na wafuasi wake katika Chuo Kikuu cha Clemson, jimbo la South Carolina.

    Baadhi ya waandamanaji walimtaja Trump kuwa msaliti na mhalifu wa kivita, huku wakimtaka aachie nyaraka zinazohusiana na Jeffrey Epstein. Mwingine alipinga kushindwa kwake kupata Tuzo ya Amani ya Nobel.

    Trump aliwadhihaki waandamanaji hao, akidai walilipwa kuvuruga mkutano. Pia alimsifu mfuasi aliyempiga mmoja wao.

    Katika hotuba yake, Trump aliwataka wafuasi wake kufikiria jina lake likiwa kwenye karatasi ya kupigia kura. Aliahidi tena kuwapa Wamarekani dola 5,000 iwapo Warepublican wataendelea kudhibiti Bunge la Congress.

    Pia alitabiri kuwa viwango vya riba na bei ya mafuta vitashuka hivi karibuni, huku akitetea ushuru wa bidhaa zinazoagizwa kutoka nje na vita dhidi ya Iran.

    Hata hivyo, shangwe za umati zilipungua alipotetea vituo vikubwa vya kuhifadhi na kuchakata data, ambavyo vimekosolewa kutokana na hofu ya kuongeza gharama za umeme na matumizi ya maji.

  6. DRC: Ubelgiji yapinga kundi la kisiasa na kijeshi la FRN linaloongozwa na Joseph Kabila

    n

    Ubelgiji imepinga kuundwa kwa kundi jipya la kisiasa na kijeshi linalojulikana kama FRN {Front pour la Refondation de la Nation} katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambalo linaongozwa na aliyekuwa rais wa nchi hiyo, Joseph Kabila, ambaye aliwahi kuishi uhamishoni.

    Akizungumza Jumatano mbele ya kamati ya bunge inayoshughulikia masuala ya nje, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ubelgiji, Maxime Prévot, amesema inasikitisha sana kuona kiongozi wa zamani wa nchi ambaye mwenyewe aliwahi kukabiliwa na athari za makundi yenye silaha akiamua kuongoza kundi la kisiasa na kijeshi linalolenga kutwaa madaraka kwa kutumia nguvu za silaha.

    Prévot amesema hatua hiyo inatia wasiwasi, akisisitiza kuwa ni jambo la kusikitisha kwa kiongozi aliyewahi kuongoza nchi kuchagua njia ya kutumia silaha katika jitihada za kurejea au kupata mamlaka.

    Pia Soma:

  7. Macron awashutumu viongozi wa kigeni kutumia maandamano nchini Ufaransa kwa maslahi ya kisiasa

    f

    Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, amewashutumu viongozi wa nchi za kigeni kwa kutumia maandamano yanayoendelea nchini humo kujinufaisha kisiasa na kuongeza uungwaji mkono katika chaguzi za nchi zao.

    Macron, ambaye hakuwataja viongozi hao kwa majina, amesema wanatumia matamshi yao kuhusu ghasia zilizotokana na maandamano dhidi ya kupanda kwa gharama za maisha kama nyenzo za kampeni za uchaguzi, kwa gharama ya Ufaransa.

    Akiwa katika ziara yake Mashariki ya Kati, Macron aliwataja viongozi hao kuwa wanajishughulisha mno na kampeni za uchaguzi, iwe katika eneo hilo au upande mwingine wa Bahari ya Atlantiki.

    Matamshi ya Macron yanaonekana kuelekezwa hasa kwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ambaye anakabiliwa na uchaguzi wa bunge wiki ijayo, na Rais wa Marekani, Donald Trump, ambaye nchi yake inajiandaa kwa uchaguzi wa katikati ya muhula wa Bunge mwezi ujao.

    Tangu ghasia zilipozuka mjini Paris na katika miji mingine ikiwemo Lyon, Marseille na Nice, karibu watu 150 wamehukumiwa, huku zaidi ya watu 800 wakifikishwa mahakamani.

    Soma pia:

  8. Marekani yaamuru wanadiplomasia wake kuondoka Saudi Arabia

    b

    Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imewaamuru wanadiplomasia wake na familia zao kuondoka Saudi Arabia kutokana na tishio la mashambulizi ya waasi wa Houthi nchini humo.

    Maafisa wa Saudi Arabia wanasema wamefanikiwa kuzuia shambulizi la anga la Houthi lililolenga kituo cha mafuta.

    Hata hivyo, watu wawili wamefariki baada ya ndege isiyo na rubani kuanguka, huku mwanaume mwingine akiuawa katika shambulizi lililotokea katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa King Fahad. Watu wengine wanane waliripotiwa kujeruhiwa vibaya katika shambulizi hilo.

    Mapigano kati ya Saudi Arabia na waasi wa Houthi nchini Yemen, wanaoungwa mkono na Iran, yamekuwa yakiongezeka tangu mwezi uliopita.

    Waasi hao wamekuwa wakijibu mashambulizi ya Saudi Arabia kwa kulenga viwanja vya ndege, miundombinu ya nishati na kambi za kijeshi.

    Shambulizi la hivi karibuni katika uwanja wa ndege wa Riyadh limeripotiwa kuwa baya zaidi kuwahi kutokea nchini humo katika miaka ya karibuni.

    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani amesema serikali imewaamuru wafanyakazi wake ambao hawajishughulishi na shughuli za dharura kuondoka nchini Saudi Arabia pamoja na familia zao.

    Ameongeza kuwa mapigano yanayoendelea yanaweza kuongezeka kwa kasi na kuzidisha hali ya hatari.

    Pia Soma:

  9. ICC yashinda Tuzo ya Sakharov ya Uhuru wa Mawazo 2026

    .

    Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) na maafisa wake wameshinda Tuzo ya Sakharov ya Uhuru wa Mawazo ya mwaka 2026, inayotolewa na Bunge la Ulaya.

    Tuzo hiyo inatambua juhudi za kutetea haki za binadamu na uhuru wa msingi. ICC, yenye makao yake makuu mjini The Hague, Uholanzi, inachunguza na kushtaki wahusika wa uhalifu mkubwa wa kimataifa, ukiwemo uhalifu wa kivita, uhalifu dhidi ya binadamu na mauaji ya kimbari.

    Mahakama hiyo imechaguliwa kuwa mshindi mbele ya wagombea wengine wawili waliofika hatua ya mwisho: kiongozi wa upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu, na dada wawili wa Iran, Taraneh na Romina Rahimi.

    Ushindi huo umetangazwa wakati ICC ikikabiliwa na vikwazo vya Marekani dhidi ya taasisi hiyo na baadhi ya maafisa wake. Mahakama hiyo imesema vikwazo hivyo vinatishia uhuru wake wa kimahakama na imezitaka nchi mbalimbali kuunga mkono shughuli zake.

    Tuzo ya Sakharov hutolewa kila mwaka na Bunge la Ulaya kwa watu au taasisi zinazotambuliwa kwa juhudi zao za kutetea haki za binadamu na uhuru wa msingi. Ilianzishwa mwaka 1988 na kupewa jina la mwanasayansi na mwanaharakati wa upinzani wa Kisovieti, Andrei Sakharov.

    Sherehe ya kukabidhi tuzo hiyo inatarajiwa kufanyika mjini Strasbourg, Ufaransa, tarehe 16 Desemba.

    Lissu miongoni mwa waliofika hatua ya mwisho

    Tundu Lissu, mwanasheria na mwenyekiti wa chama cha upinzani cha CHADEMA nchini Tanzania, aliteuliwa kutokana na harakati zake za kutetea demokrasia, mageuzi ya katiba na uchaguzi huru na wa haki.

    Alikamatwa Aprili 2025 na kushtakiwa kwa uhaini, kosa ambalo linaweza kuadhibiwa kwa kifo nchini Tanzania. Lissu amekana mashtaka yanayomkabili.

    Wagombea wengine waliofika hatua ya mwisho walikuwa dada wa Iran, Taraneh na Romina Rahimi, waliotajwa katika uteuzi huo kwa niaba ya watu wanaokabiliwa na mateso chini ya utawala wa Kiislamu nchini Iran.

    Soma Zaidi Hapa:

  10. Netanyahu asema tishio la Iran linaweza kumalizwa tu kwa kuipindua serikali yake

    df

    Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesema kuwa njia pekee ya kuondoa tishio la Iran ni kuipindua serikali ya nchi hiyo.

    Akizungumza katika mkutano wa kampeni za uchaguzi katika mji wa Dimona, kusini mwa Israel, Netanyahu amesema Iran inataka kuiangamiza Israel, lakini nchi yake imetumia nguvu zake zote kuzuia hilo lisitokee.

    Amesema pia kuwa juhudi za Iran kutengeneza silaha za nyuklia zimezuiwa, ingawa amedai kuwa nchi hiyo bado inaendelea na juhudi hizo.

    Netanyahu, ambaye katika siku za hivi karibuni amekuwa akitoa matamshi makali zaidi dhidi ya Iran, amesema: “Kuna njia moja tu ya kumaliza hali hii, nayo ni kuipindua serikali ya Iran.”

    Amesema ametoa maagizo kuhusiana na suala hilo kwa jeshi la Israel, shirika la ujasusi la Mossad pamoja na vyombo vyote vya usalama vya nchi hiyo.

    Hata hivyo, Netanyahu hakufafanua maagizo hayo yatatekelezwa lini au kwa njia gani.

    Iran imekuwa ikikanusha kwa muda mrefu tuhuma kwamba inataka kutengeneza silaha za nyuklia.

    Pia Unaweza Kusoma;

  11. Africa CDC yaonya kuwa hakuna nchi ya Afrika iliyo salama dhidi ya Ebola

    s

    Kituo cha Afrika cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Africa CDC) kimeonya kuwa hakuna nchi barani Afrika iliyo salama dhidi ya Ebola, kufuatia Nigeria kuthibitisha kisa chake cha kwanza cha ugonjwa huo katika kipindi cha zaidi ya muongo mmoja.

    Mkurugenzi Mkuu wa Africa CDC, Jean Kaseya, amesema kisa hicho kinaonyesha umuhimu wa nchi za Afrika kuimarisha maandalizi ya kukabiliana na ugonjwa huo, bila kujali umbali wake kutoka maeneo yenye mlipuko.

    “Tunapaswa kuelewa kuwa hakuna aliye salama kwa sasa. Ndiyo maana tunahitaji kuungana na kufikiria kwa pamoja mipango yetu ya kujiandaa kukabiliana na ugonjwa huu. Na ninamaanisha ninachosema,” amesema Kaseya.

    Ameitolea mfano Nigeria, akisema nchi hiyo ilidhani kuwa iko mbali na mlipuko wa Ebola katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), lakini sasa imeripoti kisa cha ugonjwa huo.

    Kaseya ameonya kuwa hatari hiyo inaweza kufika katika maeneo mengine ya bara la Afrika, yakiwemo Afrika Kaskazini na Kusini, akisisitiza umuhimu wa nchi kushirikiana katika kukabiliana na tishio hilo.

    Nigeria ilithibitisha kisa chake cha kwanza cha Ebola kinachosababishwa na virusi vya Bundibugyo tarehe 20 Oktoba, baada ya mwanamke mmoja kupatikana na ugonjwa huo. Mamlaka za afya zimesema zimewabaini watu 44 waliokutana na mwanamke huyo na zinaendelea kuwafuatilia.

    Kisa hicho kimetokea wakati mlipuko wa Ebola ukiendelea kuenea nje ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, huku visa vya ugonjwa huo vikiripotiwa pia nchini Kenya.

    Africa CDC imetoa wito wa kuimarishwa kwa mifumo ya ufuatiliaji wa magonjwa, ushirikiano kati ya nchi na kasi ya kuchukua hatua za dharura ili kuzuia kuenea zaidi kwa Ebola.

    Taasisi hiyo inatarajiwa kuitisha mkutano wa mawaziri wa afya wa nchi za Afrika tarehe 28 Oktoba, kwa lengo la kuratibu juhudi za kudhibiti mlipuko huo na kuimarisha maandalizi ya kukabiliana na ugonjwa huo katika bara zima.

    Maelezo zaidi:

  12. Trump: Ilhan Omar huenda akakabiliwa na kifungo

    .

    Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema mbunge wa chama cha Democratic kutoka Minnesota, Ilhan Omar, anaweza kukabiliwa na kifungo cha jela na hata kufukuzwa nchini iwapo uchunguzi unaoendelea kuhusu uraia wake utabaini kuwa kulikuwa na ukiukwaji wa sheria za uhamiaji.

    Akizungumza katika Ofisi ya Oval, Trump alisema kuwa licha ya mjadala kuelekezwa zaidi kwenye suala la kufukuzwa nchini, Omar pia anaweza kukabiliwa na mashtaka ya jinai yatakayoweza kusababisha kifungo. Hata hivyo, alieleza kuwa hayo ni maoni yake binafsi.

    Kauli hiyo imekuja wakati maafisa wa shirikisho nchini Marekani wakiendelea na uchunguzi dhidi ya Omar kuhusu madai ya kutolewa kwa taarifa zisizo sahihi katika nyaraka za uhamiaji na uraia. Mapema mwezi huu, maafisa wa Idara ya Usalama wa Taifa walifanya upekuzi katika makazi yake na kutaifisha simu, kompyuta, daftari na pasipoti yake kwa ajili ya uchunguzi.

    Kwa mujibu wa uchunguzi huo, maafisa wanachunguza iwapo Omar au marehemu baba yake walitoa taarifa zisizo sahihi kuhusu umri wake wakati wa mchakato wa kupata uraia wa Marekani mwaka 2000. Hoja kuu inayochunguzwa ni kama alikuwa na umri unaomruhusu kupata uraia kupitia baba yake au alipaswa kuwasilisha ombi lake binafsi

    Omar amekanusha tuhuma hizo, akisema aliwasili Marekani mwaka 1995 akiwa na umri wa miaka 12 na akapata uraia akiwa na miaka 17. Pia ameutaja uchunguzi huo kuwa wenye misukumo ya kisiasa na jaribio la kutumia vyombo vya dola dhidi ya wapinzani wa kisiasa.

    Ilhan Omar, ambaye ni mmoja wa wabunge wa kwanza wa Marekani wenye asili ya Somalia, amekuwa mkosoaji wa muda mrefu wa sera za Donald Trump, hasa katika masuala ya uhamiaji na haki za wakimbizi.

  13. Tanzania yazindua mpango wa Bima ya Afya kwa Wote

    Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa
    Maelezo ya picha, Waziri wa Afya Mohamed Mchengerwa

    Tanzania imeanza utekelezaji wa mpango wa Bima ya Afya kwa Wote unaolenga kuongeza upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi, hususan wenye kipato cha chini.

    Chini ya mpango huo, familia yenye hadi watu sita inaweza kujiunga kwa ada ya Sh150,000 kwa mwaka, huku kaya zitakazotambuliwa kuwa hazina uwezo wa kumudu gharama hizo zikitarajiwa kugharamiwa kupitia utaratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

    Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa, amesema usajili wa wanufaika utafanyika karibu na maeneo wanayoishi na kufanya kazi wananchi, ikiwemo masoko, vituo vya bodaboda na vijiji vya wavuvi, ili kurahisisha upatikanaji wa huduma hiyo.

    Kwa mujibu wa Wizara ya Afya, wanachama wa bima hiyo watapata huduma 372 za afya kwa mwaka, zikiwemo vipimo vya maabara, huduma za uchunguzi kwa mionzi, dawa, vifaa tiba na upasuaji katika ngazi mbalimbali za huduma za afya kuanzia zahanati hadi hospitali za rufaa za taifa.

    Mpango huo unafuatia awamu ya awali iliyoanza Januari 2026 kwa makundi maalumu, yakiwemo wazee, watoto, wajawazito na watu wenye ulemavu.

    Takwimu za serikali zinaonyesha zaidi ya kaya 172,000 zilikuwa zimefikiwa kufikia katikati ya mwaka huu.

    Utekelezaji wa mpango huo unatarajiwa kupanua wigo wa bima ya afya nchini na kuongeza idadi ya wananchi wanaopata huduma za matibabu kupitia mfumo wa bima.

    Soma pia:

  14. Trump: Hakuna mazungumzo yanayoendelea na Iran,lakini tutapata suluhu hivi karibuni

    Picha ya Donald Trump
    Maelezo ya picha, Picha ya Donald Trump

    Katika taarifa yake ya hivi karibuni, Rais wa Marekani Donald Trump amesema kuwa hakuna mazungumzo yanayoendelea na Iran.

    Alipoulizwa na wanahabari iwapo amekata tamaa ya kufanya mazungumzo na Iran, Trump alisema “hatufanyi mazungumzo na Wairani kwa sasa, lakini tutapata suluhisho,hilo litatokea hivi karibuni.”

    Rais huyo aliongezea kuwa “watu wengi wanafikiri kuwa hili litatokea baada ya uchaguzi.”

    Trump alikuwa akirejelea uchaguzi wa katikati ya muhula unaotarajiwa kufanyika nchini Marekani.

    Kauli za Trump kuhusu mazungumzo na Iran zinakuja wakati kiongozi mkuu wa kijeshi wa Pakistan Asim Munir, ambaye amekuwa mpatanishi mkuu katika mzozo wa hivi karibuni kati ya Marekani na Iran, alipozuru Tehran siku ya Jumanne.

    Soma pia:

  15. Serikali na kampuni zaharakisha kulinda tovuti zao baada ya kugunduliwa kwa dosari za kiusalama

    .

    Serikali na baadhi ya kampuni kubwa zaidi duniani, zikiwemo Amazon, zinaharakisha kulinda mifumo yao baada ya kugunduliwa kwa dosari hatari za usalama wa mtandao.

    Dosari hizo zipo katika lugha ya programu iitwayo PHP, inayotumika kuendesha idadi kubwa ya tovuti. Kampuni ya usalama wa mtandao ya Wiz inakadiria kuwa takriban asilimia 70 ya intaneti imeathirika, ingawa BBC haijaweza kuthibitisha kwa njia huru makadirio hayo.

    Nchi kadhaa za Ulaya zimezima baadhi ya huduma za umma zinazopatikana mtandaoni kama tahadhari, huku Wikipedia pia ikiondoa baadhi ya sehemu za tovuti yake kwa muda.

    Hatua hizo zinaendana na ushauri uliotolewa na serikali mbalimbali, zikiwemo za Marekani, wa kuzima tovuti ikiwa dosari hizo haziwezi kurekebishwa mara moja.

    Kampuni ya Wiz, ambayo watafiti wake waligundua dosari hizo, imeitaja kuwa “dosari hatari zaidi kuwahi kugunduliwa na akili unde (AI).”

    Mashirika kadhaa ya usalama wa mtandao yamezitaka taasisi ambazo haziwezi kufanya marekebisho hayo kwa wakati kuzingatia kuzima tovuti zao kwa muda. Hatua hiyo imesababisha taasisi mbalimbali, zikiwemo serikali ya Finland, halmashauri ya Edinburgh na Shirika la Utangazaji la Uingereza BBC, kuziondoa baadhi ya kurasa zao mtandaoni.

    Ikulu ya Marekani imesema mashirika ya serikali yanashirikiana na maabara zinazoongoza katika utafiti wa akili unde ili kuharakisha upatikanaji wa suluhisho la tatizo hilo.

    Soma pia:

  16. Ndege zisizo na rubani zashambulia uwanja wa ndege Saudi Arabia

    .

    Mtu mmoja ameuawa na wengine wanane kujeruhiwa katika shambulio lililotokea hapo jana katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa King Fahd mjini Dammam, mashariki mwa Saudi Arabia, kulingana na Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya nchi hiyo

    Hata hivyo, Saudi Arabia haikutaja chanzo cha ndege isiyo na rubani iliyohusika katika shambulio hilo.

    Katika tukio jingine, Wizara ya Nishati ya Saudi Arabia imesema hapo jana kuwa watu wawili waliuawa na wengine wawili kujeruhiwa baada ya mabaki ya ndege isiyo na rubani kuanguka, kufuatia kunaswa kwa ndege hiyo iliyokuwa ikilenga kituo kimoja katika eneo la uchimbaji mafuta la Shaybah, katika jimbo la Mashariki lenye utajiri wa mafuta.

    Wizara hiyo imesema katika taarifa kuwa watu waliofariki walikuwa raia wa Ufilipino na Nepal, huku waliojeruhiwa wakiwa raia wa Pakistan na India. Hata hivyo, haikutaja chanzo cha ndege hiyo isiyo na rubani.

    Kwa upande wake, Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Marekani imewaagiza wafanyakazi wote wa ubalozi wake mjini Riyadh pamoja na familia zao kuondoka Saudi Arabia, kulingana na taarifa iliyochapishwa na shirika la habari la AFP.

    Chanzo hicho kilisema Washington pia imeamuru wanafamilia wa wafanyakazi wa balozi zake katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Jordan, Qatar na Bahrain kuondoka katika nchi hizo.

    Soma pia:

  17. Tetesi za Soka Ulaya: Arsenal tayari kumuuza Gyokeres?

    Viktor Gyokeres

    Arsenal inataka kurejesha pauni milioni 55 ilizotumia kumsajili mshambuliaji wa Uswidi mwenye miaka 28, Viktor Gyokeres, huku uhamisho wake ukitarajiwa zaidi mwishoni mwa msimu kuliko Januari. (Football Insider)

    Chelsea imejiunga na Galatasaray katika mbio za kumsajili kiungo wa Uswidi mwenye umri wa miaka 23 wa Brighton, Yasin Ayari. (Teamtalk)

    Liverpool haina haraka ya kuanza mazungumzo ya mkataba mpya na kiungo wa Argentina Alexis Mac Allister, 27, licha ya kupanda kwa kiwango chake msimu huu. (Telegraph)

    Manchester United ni miongoni mwa klabu kadhaa za Ulaya zinazomfuatilia beki wa Uholanzi mwenye miaka 18 wa FC Twente, Ruud Nijstad. (The Athletic)

    Barcelona na Real Madrid ni miongoni mwa klabu zinazomfuatilia kiungo wa Uswisi mwenye miaka 21 wa Aston Villa, Johan Manzambi, kufuatia mwanzo mzuri wa maisha yake katika klabu hiyo. (Football Insider)

    Kiungo wa Argentina Alexis Mac Allister
    Maelezo ya picha, Liverpool haina haraka ya kumpa Mac Allister mkataba mpya.

    Sunderland inajiandaa kutoa ofa mpya dirisha la Januari kwa winga wa Msumbiji mwenye miaka 25 wa Sporting, Geny Catamo. (Teamtalk)Everton inamfuatilia Mshambuliaji wa Croatia mwenye miaka 24 wa Dinamo Zagreb, Dion Beljo, kama moja ya chaguo zake za usajili katika dirisha la Januari. (Football Insider)

    Liverpool, pamoja na klabu nyingine kubwa za Ulaya, zinavutiwa na kiungo wa Mexico mwenye miaka 18 wa Tijuana, Gilberto Mora. (Marca)

    Mshambuliaji wa Brazil Vinicius Jr, 26, aliwahi kuvutiwa sana kuhamia Arsenal wakati wa kiangazi, lakini sasa anatamani kuchezea Real Madrid kwa kipindi kilichosalia cha maisha yake ya soka. (Mail)

    Arsenal inaongoza mbio za klabu za Ligi Kuu England kuwania saini ya kiungo wa Uturuki mwenye miaka 20 wa Eintracht Frankfurt, Can Uzun. (The Daily Briefing)

    Pia unaweza kusoama:

  18. Papa Leo hatahitaji matibabu zaidi baada ya kufanyiwa upasuaji - Vatican

    Picha ya Papa Leo
    Maelezo ya picha, Picha ya Papa Leo

    Madaktari wa Papa Leo, wamesema hahitaji matibabu zaidi baada ya kufanyiwa upasuaji siku chache zilizopita, wa kuondoa uvimbe wa saratani kwenye mapafu yake.

    Matokeo ya vipimo vya tishu zilizotolewa wakati wa upasuaji yamethibitisha kuwa alikuwa na saratani ya mapafu aina ya adenocarcinoma, na kwamba ugonjwa huo ulikuwa umejikita katika eneo moja, kulingana na taarifa iliyotolewa na Vatican.

    “Uchunguzi wa baadaye wa saratani umethibitisha kuwa hakuna haja ya matibabu zaidi,” taarifa hiyo ilisema.

    Papa huyo mwenye umri wa miaka 71 aliruhusiwa kutoka hospitali ya Gemelli mjini Rome mwishoni mwa wiki iliyopita, siku nne baada ya kufanyiwa upasuaji.

    Habari hiyo ilitolewa saa chache baada ya Papa Leo kuongoza mkutano wake wa kwanza wa kawaida wa kila wiki katika uwanja wa Mtakatifu Petro tangu kuruhusiwa kutoka hospitalini.

    Papa huyo alifanyiwa upasuaji tarehe 13 mwezi Oktoba, ambapo sehemu ya chini ya pafu lake la kulia iliondolewa. Upasuaji huo ulidumu kwa dakika 90.

    Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki alikuwa ametangaza siku chache kabla, wakati wa sala yake ya Jumapili katika uwanja wa Mtakatifu Petro, kwamba alihitaji kufanyiwa upasuaji baada ya madaktari kugundua uvimbe kwenye pafu lake.

    Soma pia:

  19. Rais Macron awashtumu Trump na Netanyahu kwa kujinufaisha na ghasia zilizozuka Ufaransa

    .

    Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, amewashutumu viongozi wa mataifa ya kigeni kwa kutumia maandamano yaliyozuka nchini humo kisiasa ili kujinufaisha katika uchaguzi unaokaribia katika mataifa yao.

    Bila kuwataja kwa majina, Macron alisema viongozi hao wanajipigia debe katika uchaguzi ujao “kwa gharama ya Ufaransa” kupitia kauli zao kuhusu ghasia hizo, zilizozuka wakati wa maandamano ya kupinga kupanda kwa gharama ya maisha.

    Akizungumza wakati wa ziara yake Mashariki ya Kati, Macron aliwarejelea kama “viongozi ambao wamejikita katika kampeni za uchaguzi, iwe katika eneo hili au upande mwingine wa Bahari ya Atlantiki.”

    Kauli hiyo inaonekana kuelekezwa kwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, anayekabiliwa na uchaguzi wa bunge wiki ijayo, pamoja na Rais wa Marekani, Donald Trump, ambaye nchi yake inatarajiwa kufanya uchaguzi wa katikati ya muhula mwezi ujao.

    Takriban watu 150 wamehukumiwa, huku zaidi ya watu 800 wakifikishwa mahakamani tangu kuzuka kwa ghasia zilizoikumba mji wa Paris na miji mingine, ikiwemo Lyon, Marseille na Nice.

    Soma pia:

  20. Marekani yapunguza 'kimyakimya' wanajeshi wake Mashariki ya Kati

    Jeshi la Marekani

    Shirika la habari la CBS, mshirika wa BBC nchini Marekani, limeripoti kuwa jeshi la Marekani linaendelea kupunguza kwa utaratibu na bila kutangaza wazi idadi ya wanajeshi wake katika baadhi ya kambi za kijeshi za Mashariki ya Kati, kufuatia vitisho vinavyoendelea kutoka kwa waasi wa Houthi na Iran.

    Taarifa hiyo, iliyochapishwa awali na NBC News siku ya Jumatano, ilimnukuu afisa wa serikali ya Marekani na afisa mwandamizi wa jeshi walioeleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya tathmini ya kiusalama inayoendelea katika eneo hilo.

    Akijibu taarifa hizo, msemaji wa Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM), Kapteni Tim Hawkins, alisema jeshi la Marekani hubadilisha mara kwa mara maeneo ya vikosi na vifaa vyake ili kuimarisha utayari wa operesheni zake. Hata hivyo, alikataa kutoa maelezo zaidi kwa sababu za kiusalama, akisisitiza kuwa majeshi ya Marekani bado yako tayari kulinda raia wake na maslahi ya nchi hiyo katika eneo lote.

    Wakati huo huo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani imeagiza wafanyakazi wasio wa lazima katika ubalozi wake nchini Saudi Arabia pamoja na familia zao kuondoka nchini humo kutokana na vitisho vinavyotokana na waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran.

    CBS pia imeripoti kuwa balozi kadhaa za Marekani katika Mashariki ya Kati zimepunguza idadi ya wafanyakazi na kiwango cha huduma chini ya utaratibu wa uendeshaji wenye vikwazo (restricted operations).

    Hatua hiyo ilianzishwa mwezi Agosti wakati mvutano kati ya Marekani na Iran ulipozidi kuongezeka. Utaratibu huo huruhusu balozi kupunguza shughuli na wafanyakazi wake bila kusitisha kabisa huduma za kidiplomasia.

    Soma pia: