Kwa nini Marekani inafikiria kutumia 'Mama wa Mabomu Yote' dhidi ya Iran?

.
Maelezo ya picha, Bomu kubwa la mlipuko wa angani katika kambi ya Jeshi la Anga la Marekani ya Eglin, Florida, Machi 11, 2003.
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

CNN imeripoti kuwa Marekani inafikiria kuishambulia Iran kwa kutumia bomu lake lisilo la nyuklia lenye nguvu kubwa zaidi, iwapo Rais wa Marekani Donald Trump ataamua kuanzisha tena mashambulizi baada ya vita vilivyoanza Februari mwaka huu kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran kufikia hatua ya kukwama.

Mtandao huo umenukuu vyanzo vyenye taarifa kuhusu mipango hiyo vikisema kuwa jeshi la Marekani linafikiria uwezekano wa kutumia bomu la GBU-43/B, linalojulikana kama "Mama wa Mabomu Yote", kulenga miundombinu ya nishati na maeneo ya nyuklia ya Iran.

Hata hivyo, vyanzo hivyo vilieleza mashaka kuhusu uwezo wa bomu hilo kuharibu maeneo ya nyuklia ya Iran yaliyojengwa chini ya ardhi, vikisema kuwa matumizi yake yanaweza kuwa na athari kubwa zaidi kisaikolojia.

Trump alisema kuwa watu wanaovujisha taarifa kuhusu operesheni za kijeshi za nchi hiyo kwa vyombo vya habari "wanapaswa kupigwa risasi".

Akizungumza katika mkutano wa kampeni mjini Bullhead City, Arizona, Jumatano, Trump alisema: "Nadhani watoa taarifa za siri wanapaswa kupigwa risasi. Hapo awali, tulikuwa tukiwapiga risasi watu waliovujisha taarifa, kwa mfano, kuhusu nchi iliyokuwa inakaribia kushambuliwa."

Akizungumzia shambulizi la Marekani dhidi ya maeneo ya nyuklia ya Iran mwezi Juni 2025, alidai kuwa mtu fulani alikuwa amefichua muda wa kuondoka na kuwasili kwa ndege za kijeshi za Marekani zilizohusika katika operesheni hiyo.

Trump alikosoa uchapishaji wa taarifa hizo katika vyombo vya habari, vikiwemo The New York Times na CNN, akisema kuwa waliozivujisha wanapaswa kukabiliwa na adhabu kali. Aliwataja kuwa "watu waliopotoka zaidi duniani".

Wiki iliyopita, rais huyo wa Marekani aliondoa uwezekano wa kuishambulia Iran kabla ya uchaguzi wa katikati ya muhula uliopangwa kufanyika Novemba 3, na akazungumzia kuwepo kwa "mazungumzo yenye tija" na Tehran.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hayo yanajiri wakati vita dhidi ya Iran na athari zake kwa bei za bidhaa na mafuta zikichangia kupungua kwa umaarufu wa Trump katika kura za maoni, muda mfupi kabla ya uchaguzi huo.

Marekani na Israel zilisema kuwa lengo la mashambulizi hayo lilikuwa kuizuia Iran kupata silaha ya nyuklia. Tehran inakanusha kuwa inajitahidi kutengeneza silaha hizo, huku ikisisitiza haki yake ya kuendesha mpango wa nyuklia kwa madhumuni ya amani.

Washington na Tehran zilitia saini hati ya maelewano mwezi Juni 2016, kwa upatanishi wa Pakistan, kabla ya makubaliano hayo kuvunjika mwezi Julai kufuatia kuanza tena kwa mashambulizi ya Iran dhidi ya meli katika Mlango-Bahari wa Hormuz na mashambulizi ya kijeshi ya kulipiza kisasi yaliyofanywa na Marekani dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Tangu wakati huo, mazungumzo yamekwama.

Hata hivyo, ripoti kadhaa za vyombo vya habari zinaeleza kuwa Ikulu ya White House ilikuwa imeiomba Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon, kuandaa mipango mbalimbali ya kushambulia maeneo nchini Iran kabla ya uchaguzi.

CNN ilinukuu chanzo kimoja kikisema kuwa Trump alitoa maelekezo kwamba mipango hiyo ijumuisha kulenga "miundombinu ya nishati kwa kiwango kikubwa", pamoja na uwezekano wa kutumia bomu la "Mama wa Mabomu Yote".

Hata hivyo, baadhi ya maafisa wanatilia shaka ufanisi wa bomu hilo, hasa uwezo wake wa kuharibu maeneo ya nyuklia ya Iran yaliyo chini ya ardhi.

Chanzo kimoja kinachofahamu mipango hiyo kiliiambia CNN kuwa bomu hilo "linafaa kuharibu maeneo makubwa, lakini haliwezi kufanya mengi zaidi ya hapo", kikibainisha kuwa halijatengenezwa kama kichwa cha kombora kinachoweza kupenya ngome imara.

Matumizi ya mabomu hayo pia yanaweza kusababisha vifo vya raia.

Katika muhula wake wa kwanza wa urais, jeshi la Marekani lilitumia kwa mara ya kwanza bomu la "Mama wa Mabomu Yote" mwaka 2017, kulenga maficho na vichuguu vya kundi la Islamic State nchini Afghanistan. Shambulizi hilo liliwaua wapiganaji zaidi ya 90.

Bomu 'Mama la Mabomu Yote' ni nini?

.
Maelezo ya picha, Utengenezaji wa bomu hilo kubwa ulianza mwaka 2003, lakini halikutumika katika mapigano halisi hadi mwaka 2017.

Ni bomu aina ya GBU-43/B Massive Ordnance Air Blast (MOAB), lenye uzito wa takriban tani 10. Linachukuliwa kuwa silaha kubwa zaidi isiyo ya nyuklia katika ghala la silaha za Marekani.

Bomu hilo lina urefu wa takriban mita tisa na kipenyo cha mita moja, na linaongozwa kwa kutumia mfumo wa satelaiti.

Ni silaha kubwa yenye urefu wa futi 30 (mita tisa) na uzito wa pauni 21,600 (takriban kilogramu 9,800). Linaongozwa kwa mfumo wa GPS na hudondoshwa kutoka kwenye ndege ya usafirishaji ya kijeshi aina ya MC-130, kisha hulipuka muda mfupi kabla ya kugonga ardhi.

Bomu hilo hudondoshwa kutoka kwenye ndege likiwa limefungwa kwenye jukwaa maalumu la kubebea mizigo. Jukwaa hilo huvutwa kuelekea pembeni kwa kutumia parachuti, hatua inayoliruhusu bomu kuelekea ardhini huku likitulia na kuelekezwa na mapezi manne yenye umbo la wavu.

Athari yake kuu ni wimbi kubwa la mlipuko ambalo, kwa mujibu wa taarifa, linaweza kuenea kwa umbali wa maili moja katika kila upande. Nguvu hiyo hutokana na mlipuko unaolingana na tani 8.2 za TNT.

Ganda jembamba la alumini la bomu hilo lilibuniwa mahsusi ili kuongeza eneo linaloweza kuathiriwa na mlipuko.

Aina hii ya silaha imeundwa kusababisha uharibifu mkubwa katika maeneo ya chini ya ardhi na vichuguu.

Bomu hilo lilitengenezwa kwa ajili ya matumizi katika Vita vya Iraq, na kila moja liliripotiwa kugharimu dola milioni 16. Lilifanyiwa jaribio lake la kwanza mwaka 2003, lakini halikutumika katika mapigano hadi mwaka 2017.

Hata hivyo, bomu hilo kubwa si bomu zito zaidi lisilo la nyuklia katika ghala la silaha za jeshi la Marekani.

Jina hilo linatokana na bomu la MOB, ambalo ni bomu la kuharibu ngome za chini ya ardhi na lina uzito mkubwa wa pauni 30,000.

Urusi pia imetengeneza bomu lake kubwa la kawaida, linalojulikana kama "Baba wa Mabomu Yote" au FOAB. Ni bomu linalotumia mchanganyiko wa mafuta na hewa kulipuka, ambalo kitaalamu hujulikana kama silaha ya kithermobaric inayozalisha shinikizo kubwa.

Kwa kawaida, mabomu ya kithermobaric hulipuka kwa hatua mbili. Kwanza, mlipuko mdogo hutengeneza wingu la dutu inayoweza kuwaka. Kisha wingu hilo huwashwa na kutoa wimbi la shinikizo lenye nguvu kubwa ya uharibifu.

Inaelezwa kuwa sehemu muhimu ya athari za silaha kama vile "Mama wa Mabomu Yote" ni ya kisaikolojia, kwa kuwa lengo lake pia ni kueneza hofu kupitia nguvu kubwa ya mlipuko wake.

Utengenezaji wa bomu hilo ulifanyika baada ya matumizi ya silaha nyingine zinazofanana, zikiwemo bomu la BLU-82 lenye uzito wa pauni 15,000. Bomu hilo lilibuniwa kusawazisha eneo la msitu ili kutengeneza sehemu ya kutua kwa helikopta.

Bomu la "Mama wa Mabomu Yote" lilitengenezwa na kampuni ya Denitex, inayojishughulisha na masuala ya anga na iliyoko Alabama, Marekani.

Bomu hilo, ambalo pia hujulikana kwa jina hilo katika istilahi za kijeshi, lilitumika kwa mara ya kwanza nchini Afghanistan.

Jeshi la Marekani lilitumia silaha hii, ambayo ni bomu kubwa zaidi la kawaida lisilo la nyuklia kuwahi kutumika katika mapigano, kwa mara ya kwanza katika operesheni halisi ya kijeshi mwaka 2017, katika jimbo la Nangarhar mashariki mwa Afghanistan.

Wakati huo, ilielezwa kuwa shabaha ilikuwa mtandao wa vichuguu uliokuwa ukitumiwa na kundi linalojulikana kama Islamic State katika eneo la Achin.

Kwa kuwa ni silaha isiyo ya nyuklia, matumizi ya bomu hili hayahitaji lazima idhini ya rais wa Marekani.

Imetafsiriwa na Faidha Ngaga na kuhaririwa na Dinah Gahamanyi