Kwa nini mkataba wa Rwanda wa kuandaa mbio za Langalanga-F1 bado unazua utata

Chanzo cha picha, Getty Images
Mashindano ya Formula 1 (F1) yanatarajiwa kurejea barani Afrika kwa mara ya kwanza baada ya takribani kizazi kimoja, kufuatia Rwanda kusaini mkataba wa miaka 10 wa kuandaa mbio hizo, huku shirikisho linalosimamia mchezo huo (FIA) likilenga kuacha "urithi wa kudumu".
Mashindano hayo, yatakayojulikana kama African Grand Prix, yatafanyika katika uwanja mpya wa mashindano utakaokamilika kujengwa mahsusi kwa ajili hiyo, Bugesera, takribani maili 25 kusini mwa mji mkuu Kigali. Toleo la kwanza linatarajiwa kufanyika mwanzoni mwa miaka ya 2030.
Kwa Rais wa Rwanda, Paul Kagame, lengo ni "kufungua njia" kwa nchi nyingine za Afrika kuandaa mashindano ya F1.
Hata hivyo, tangazo hilo limekosolewa na baadhi ya watu kutokana na madai kwamba Rwanda inatumia michezo kuboresha taswira yake ya kimataifa (sportswashing), pamoja na maswali kuhusu rekodi ya nchi hiyo katika kuheshimu haki za binadamu.
Kwa nini hili ni jambo kubwa?
Afrika haijaandaa mashindano ya F1 tangu mwaka 1993, na wito wa kurejesha mchezo huo barani umekuwa ukiongezeka katika miaka ya hivi karibuni. Miongoni mwa wanaoongoza kampeni hiyo ni Lewis Hamilton, bingwa wa dunia mara saba.
Morocco ilikuwa nchi ya kwanza barani Afrika kuandaa mashindano ya Grand Prix mwaka 1958. Baadaye, mashindano 23 yalifanyika Afrika Kusini kati ya mwaka 1962 na 1993.
Rais Kagame alisema ni "heshima na fursa" kwa Rwanda kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa mashindano hayo yatakaporejea barani Afrika.
"Ushirikiano huu umekuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu, lakini ni mafanikio na hatua muhimu kwa bara zima, hasa mashabiki wa Afrika," aliongeza.
Afrika Kusini nayo ilikuwa na nia ya kupata nafasi ya kuandaa mashindano yake ya F1, na Waziri wa Michezo, Gayton McKenzie, bado ana matumaini makubwa kwamba nchi yake itafanikiwa kama Rwanda.
"Wamefanya kazi ya kuwania nafasi hiyo kwa muda mrefu kuliko Afrika Kusini na wanastahili," aliandika kwenye mtandao wa X.
"Hata hivyo, kumbukeni kwamba nchi moja, Italia, imekuwa ikiandaa mashindano mawili ya F1 kwa mwaka, lakini baadhi ya watu wanaitikia kana kwamba bara lenye nchi 54 linaweza kupata mashindano moja tu. Afrika Kusini itaandaa F1, hata kabla ya mwaka 2030."
Ni mambo gani ambayo bado hayajaamuliwa?

Chanzo cha picha, Formula 1
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mwaka kamili ambao African Grand Prix itafanyika kwa mara ya kwanza katika miaka ya 2030, pamoja na nafasi yake katika ratiba ya msimu, bado havijatangazwa.
Inawezekana F1 ikataka kuepuka kuandaa mashindano hayo wakati wa msimu mkuu wa mvua nchini Rwanda, kati ya Machi na Mei. Pia kuna msimu mfupi wa mvua kati ya Oktoba na Novemba ambao hauna athari kubwa kama ule mkuu.
F1 imeahidi kutoruhusu msimu wake kuwa na mashindano zaidi ya 24.
Dereva wa zamani wa F1, Alex Wurz, atahusika katika usanifu wa uwanja huo. Inatarajiwa kutumia mandhari ya Rwanda yenye vilima na miteremko ili kutengeneza njia ya mbio yenye mtiririko wa asili na mabadiliko ya mwinuko yanayokaribia mita 200, jambo litakalowapa madereva changamoto.
Je, mashindano hayo yanaweza kuongeza ushiriki wa Waafrika?
Jody Scheckter bado ndiye Mwafrika pekee aliyewahi kushinda ubingwa wa dunia wa madereva wa F1. Alitwaa taji hilo mwaka 1979 akiendesha gari la Ferrari.
"Ni gharama kubwa sana kuingia katika mchezo huu," raia huyo wa Afrika Kusini aliambia kipindi cha Newsday cha BBC World Service alipoulizwa kama mashindano ya Rwanda yanaweza kufungua njia kwa madereva wengi zaidi kutoka barani Afrika.
"Mwanzoni nilikuwa nikitengeneza magari yangu mwenyewe. Siku hizi huwezi tena kufanya hivyo."
Kwa mujibu wa dereva mwingine, Axcil Jefferies, ambaye amewahi kushiriki mashindano ya Formula 2, Waafrika wanaotaka kujenga taaluma katika mchezo wa magari wamekuwa wakilazimika kwenda nje ya bara hilo kutimiza ndoto zao.
Hata hivyo, raia huyo wa Zimbabwe anaamini hali hiyo inaweza kubadilika.
"Kufika kwa F1 barani Afrika kutawaonyesha watu wote ukubwa wa sekta ya mchezo wa magari," alisema.
"Vipengele vyote vya mchezo huu vitawatia moyo vijana, iwe ni kuwa wahandisi, mafundi, madereva au waratibu wa timu."
Mtangazaji wa Afrika Kusini, Kriya Gangiah, anayeendesha kipindi cha F1 Extra Africa Trackside cha SuperSport, pia ana matumaini kwamba mashindano hayo yataongeza idadi ya mashabiki wanawake na madereva wanawake barani Afrika.
"Kadiri unavyozidi kuona kitu na kadiri kinavyokuwa sehemu ya maisha yako, ndivyo unavyozidi kukipenda na kuvutiwa nacho," alisema.
"Unapokuwa katika maeneo ya timu za mashindano Afrika Kusini, unaona idadi ya wanawake wanaoingia katika mchezo huu na kufanya vizuri sana. Wanawake wengi wanawapa wanaume ushindani mkubwa kweli."
Kwa nini mkataba huo unazua utata?

Chanzo cha picha, Getty Images
Rwanda imekuwa ikikabiliwa kwa muda mrefu na madai ya kutumia michezo kuboresha taswira yake ya kimataifa, jambo linalojulikana kama sportswashing.
Kupata mashindano ya F1 ni sehemu ya mkakati mpana wa nchi hiyo wa kuongeza utalii, uwekezaji wa kimataifa, huduma na burudani.
Rwanda imekuwa mwenyeji wa fainali za Basketball Africa League katika miaka yote isipokuwa mmoja tangu 2021. Pia iliandaa Mashindano ya Dunia ya Baiskeli Barabarani mwaka jana, ikiwa ni mara ya kwanza kwa tukio hilo kufanyika barani Afrika.
Chapa ya utalii ya Visit Rwanda imekuwa mdhamini au mshirika wa klabu za Arsenal, Bayern Munich na Paris Saint-Germain (PSG). Hata hivyo, udhamini wake wa kuweka nembo kwenye mikono ya jezi za Arsenal ulimalizika mwaka huu baada ya kukosolewa na baadhi ya makundi ya mashabiki.
Baadaye, Visit Rwanda ikawa mdhamini mkuu wa mbele ya jezi za Aston Villa, klabu nyingine inayoshiriki Ligi Kuu ya England.
Wakati huohuo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambayo ni jirani ya Rwanda upande wa magharibi, imefungua kesi dhidi ya nchi hiyo katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ). DRC inaishutumu Rwanda kwa kukiuka mikataba kadhaa ya kimataifa inayohusu kuzuia mauaji ya kimbari, ubaguzi wa rangi, haki za wanawake na mateso.
Shirika la Human Rights Watch liliwahi kusema kuwa nafasi ya uhuru wa kujieleza na uhuru wa kisiasa nchini Rwanda inazidi kupungua.
"Rwanda inawekeza katika michezo mikubwa zaidi duniani ili kung'arisha taswira yake na kugeuza macho ya watu kutoka kwenye rekodi yake mbaya ya haki za binadamu," alisema Felix Jakens, mkuu wa kampeni wa Amnesty International nchini Uingereza.
"Kuandaa mashindano ya Grand Prix kwa miaka 10 chini ya jina la 'Presented by Visit Rwanda' ni tuzo ya sportswashing kwa mamlaka za Rwanda."
Serikali ya Rwanda imepuuzilia mbali tuhuma hizo. Afisa Mkuu wa Utalii nchini humo, Irene Murerwa, aliwahi kuziita "kero inayokengeusha watu" kutoka kwenye "mafanikio makubwa na ya kipekee ambayo nchi imeyapata", alipohojiwa na BBC Sport Africa kuhusu suala hilo.
"Faida zake zinawafikia Warwanda wote," alisema Desemba 2024. "Kuandaa F1 kutakuwa hatua nyingine katika safari yetu ya kuwa kituo cha kiwango cha kimataifa."
F1 imesema nini?
F1 inafahamu suala la sportswashing, kwani baadhi ya nchi zinazoandaa mashindano hayo zimeshutumiwa kutumia michezo kuboresha taswira zao za kimataifa, ikiwemo Saudi Arabia.
Mkataba wa F1 wenyewe unaahidi kuheshimu haki za binadamu zinazotambuliwa kimataifa katika shughuli zake duniani kote. Pia unasisitiza umuhimu wa kuelewa na kufuatilia athari zinazoweza kujitokeza kwa haki za binadamu, pamoja na kushirikiana na wadau mbalimbali.
Katika taarifa iliyotolewa baada ya kutangazwa kwa makubaliano na Rwanda, F1 ilisema: "Tuna fursa ya kuhamasisha na kuleta shauku ya F1 kwa watu milioni 100 barani Afrika, na michezo inaweza kuwa nguvu chanya inayoleta manufaa."
Hata hivyo, tangazo hilo bado limekosolewa na mashirika ya haki za binadamu. Jakens wa Amnesty International anaamini kuwa kauli za F1 kuhusu suala hilo "hazina uzito wala uaminifu".
"Inapaswa kutumia ushawishi wake kwa mamlaka za Rwanda kushinikiza mabadiliko, badala ya kuipa chapa yake nafasi ya kutumika katika kampeni ya kujitangaza," alisema.
Alipoulizwa kuhusu tuhuma za sportswashing dhidi ya Rwanda wakati nchi hiyo ikiwania kuandaa mashindano ya F1, Rais wa FIA, Mohammed Ben Sulayem, aliiambia BBC Sport Africa:
"Watu wanapokosa kupata wanachotaka, daima huitaja sportswashing."
"Kwa kweli, sijali wanachosema."



































