Muammar Gaddafi: Alitaka kuwa 'mfalme wa wafalme' -ndoto yake iliishia wapi?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, ولید بدران
- Nafasi, بی بی سی عربی
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 9
Muammar Gaddafi, ambaye alikua Waziri Mkuu wa Libya tarehe 16 Januari 1970, hakuwahi kufikiria kwamba utawala wake ungeendelea kwa miaka 42 na kuishia kwa namna ulivyoisha.
Katika kipindi cha uongozi wake, aliwakandamiza kwa ukali wapinzani wote waliompinga. Huenda hii ndiyo sababu hakukuwa na uongozi mbadala uliojitokeza wakati yeye yupo madarakani.
Kisha wimbi la mwamko wa kisiasa katika ulimwengu wa Kiarabu lililoanza Tunisia mwaka 2011 lilifagia utawala wa Kanali Muammar Gaddafi.
Muammar Gaddafi, aliyeuawa na waasi tarehe 20 Oktoba 2011, alikuwa mtoto wa mkulima wa Kibedui. Lakini aliwezaje kuwa mmoja wa viongozi wenye ushawishi mkubwa zaidi katika ulimwengu wa Kiarabu?
Kujiunga na Jeshi na Kupanda Madaraka
Kwa mujibu wa Encyclopedia Britannica, Muammar Gaddafi alizaliwa mwaka 1942 na baba yake alikuwa mkulima wa Kibedui. Baada ya kumaliza masomo yake ya shule, alikwenda Benghazi kusoma katika chuo kikuu.
Alifukuzwa kutoka Chuo Kikuu cha Sabha mwaka 1961 kutokana na shughuli zake za kisiasa na misimamo yake.
Katika kipindi hicho, alipata shahada ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Libya. Pia alipata fursa ya kujiunga na jeshi la Libya, ambalo wakati huo lilitoa elimu bora na lilionekana kuwa njia nzuri ya kuboresha maisha kiuchumi.
Ndiyo sababu huenda alijiunga na jeshi kabla ya kukamilisha elimu yake ya juu.

Chanzo cha picha, Getty Images
Uamuzi huo ndiyo uliomfikisha kwenye kilele cha madaraka baadaye. Katika ujana wake, Gaddafi alikuwa mfuasi wa Rais wa Misri Gamal Abdel Nasser na sera zake.
Alishiriki pia katika maandamano yaliyozuka mwaka 1956 kupinga uvamizi wa Uingereza, Ufaransa na Israel baada ya Misri kutaifisha Mfereji wa Suez.
Baada ya kukamilisha mafunzo yake ya kijeshi, alipelekwa Uingereza mwaka 1965 kwa mafunzo zaidi.
Gaddafi alipandishwa vyeo kwa kasi kubwa ndani ya jeshi la Libya na wakati huo huo akaanza kupanga njama za kuupindua utawala wa kifalme.
Tangu akiwa mafunzoni jeshini alikuwa na wazo la kuuangusha utawala wa mfalme wa Libya. Hatimaye, baada ya kurejea kutoka Uingereza mwaka 1969, aliongoza mapinduzi ya kijeshi kutoka Benghazi na kujitangaza kuwa kiongozi wa Libya.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mapinduzi na Mafuta
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Tarehe 1 Septemba 1969, jeshi lililoongozwa na Kanali Gaddafi lilimng'oa madarakani Mfalme wa Libya.
Gaddafi akawa mkuu wa jeshi, mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na mkuu wa nchi, ingawa aliendelea kushikilia cheo cha kanali.
Baada ya kuingia madarakani, alivunja vituo vya kijeshi vya Marekani na Uingereza nchini Libya na mwaka 1970 akawafukuza Waitaliano na Wayahudi wengi waliokuwa nchini humo.
Mwaka 1973, alitaifisha sekta ya mafuta ya Libya. Pia alipiga marufuku pombe na kamari.
Katika kipindi hicho aliwaambia viongozi wa kampuni za mafuta za kimataifa:
"Watu ambao wameishi kwa miaka elfu tano bila mafuta wanaweza kuendelea kuishi miaka michache zaidi ili kupata haki zao halali."
Msimamo huo ulifanikiwa, na Libya ikawa nchi ya kwanza inayoendelea kupata sehemu kubwa ya mapato kutoka uzalishaji wake wa mafuta. Mataifa mengine ya Kiarabu yalifuata mfano huo, hatua iliyoweka msingi wa mafanikio makubwa ya kiuchumi ya nchi za mafuta katika miaka ya 1970.

Chanzo cha picha, Getty Images
Wakati huo Libya ilikuwa na uzalishaji mkubwa wa mafuta sawa na baadhi ya nchi za Ghuba, lakini ilikuwa na idadi ndogo ya watu, takribani milioni tatu pekee. Hivyo mafuta yaliifanya Libya kuwa tajiri kwa haraka sana.
Gaddafi alikuwa mpinzani mkubwa wa mazungumzo na Israel na alipinga makubaliano ya amani kati ya Misri na Israel. Serikali yake pia ilisaidia jaribio la mapinduzi katika baadhi ya nchi jirani.
Nadharia ya "Kitabu cha Kijani"
Mwanzoni mwa miaka ya 1970, Gaddafi aliwasilisha itikadi yake ya kisiasa kupitia Kitabu cha Kijani (Green Book), ambacho kilitetea ujamaa wa Kiislamu.
Kupitia kitabu hicho, alieleza nia yake ya kutaifisha sekta muhimu za uchumi.
Kwa mujibu wake, suluhisho la matatizo ya jamii halikuwa demokrasia au mfumo wa vyama vya siasa. Alidai kuwa vyama vikubwa huzaa udikteta, na kwamba nchi zinapaswa kuongozwa kupitia kamati za wananchi zinazohusika na nyanja zote za maisha.
Mwaka 1979, Gaddafi aliacha rasmi nafasi ya uongozi wa taifa, lakini kwa vitendo aliendelea kushika mamlaka yote muhimu.
Uingiliaji wake katika masuala ya kimataifa, Milipuko na Vikwazo
Katika ulimwengu wa kimataifa, Gaddafi na utawala wake walijulikana kwa hatua zisizotabirika.
Alifadhili makundi mbalimbali duniani, yakiwemo Black Panthers ya Marekani na Nation of Islam. Pia aliisaidia Irish Republican Army (IRA) nchini Ireland Kaskazini.
Maajenti wa Libya waliendelea kuwalenga wapinzani wa Gaddafi waliokuwa uhamishoni, na serikali yake ilihusishwa na matukio kadhaa ya mauaji.
Mwaka 1986, bomu lililipuka katika klabu moja mjini Berlin iliyokuwa ikitembelewa na wanajeshi wa Marekani. Shambulio hilo lilihusishwa na maajenti wa Libya.
Rais wa Marekani Ronald Reagan akaamuru mashambulizi ya anga dhidi ya Tripoli na Benghazi. Ingawa watu wengi walikufa, akiwemo binti wa Gaddafi, yeye mwenyewe alinusurika.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mwaka 1988, ndege ya Pan Am ilianguka huko Lockerbie, Scotland, na watu 270 waliuawa. Libya ililaumiwa kwa tukio hilo.
Makubaliano ya Lockerbie
Mwanzoni Gaddafi alikataa kuwakabidhi washukiwa wawili wa shambulio la Lockerbie kwa Scotland.
Baada ya miaka ya mazungumzo na vikwazo vya kimataifa, mwaka 1999 aliwakabidhi washukiwa hao. Mmoja alihukumiwa kifungo cha maisha, wakati mwingine aliachiliwa huru.
Mwezi Agosti 2003, Libya ilikubali kuwajibika kwa shambulio hilo katika barua kwa Umoja wa Mataifa na kulipa fidia ya dola bilioni 2.7 kwa waathirika.
Mwezi Septemba 2003, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliondoa vikwazo dhidi ya Libya.
Libya pia iliacha mpango wake wa silaha za maangamizi na kulipa fidia kwa waathirika wa ajali nyingine za ndege pamoja na shambulio la Berlin.

Chanzo cha picha, AFP
Uhusiano Bora na nchi za Magharibi
Makubaliano ya Lockerbie pamoja na kuachwa kwa mpango wa siri wa nyuklia na kemikali yalifungua njia ya kuimarika kwa mahusiano kati ya Libya na mataifa ya Magharibi.
Baada ya kuondolewa kwa vikwazo, viongozi kadhaa wa dunia, akiwemo Waziri Mkuu wa Uingereza Tony Blair, walimtembelea Gaddafi katika hema lake maarufu.
Hema hilo lilikuwa sehemu muhimu ya maisha yake na liliambatana naye katika safari zake nyingi za kimataifa.
Katika kipindi hiki Libya ilisaini mikataba mingi ya biashara na makampuni ya mafuta na watengenezaji wa silaha wa Magharibi.
Gaddafi pia alijulikana kwa mtindo wake wa maisha wa kipekee na kundi la walinzi wanawake waliokuwa wakimzunguka mara nyingi.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mapinduzi ya 2011 na Matumizi ya Nguvu
Mwaka 2011, maandamano yaliyomng'oa Zine El Abidine Ben Ali wa Tunisia na Hosni Mubarak wa Misri yaliwahamasisha Walibya kuandamana dhidi ya Gaddafi.
Serikali yake ilijibu kwa kutumia nguvu, ikiwa ni pamoja na risasi, ndege za kivita na helikopta dhidi ya waandamanaji.
Mashirika ya haki za binadamu na jumuiya ya kimataifa yalilaani hatua hizo.
Tarehe 22 Februari 2011, Gaddafi alikataa kujiuzulu kupitia hotuba ya televisheni, akiwaita waandamanaji "wasaliti."
Aliendelea kudai kuwa wapinzani wake walikuwa wakisaidiwa na al-Qaeda.
Kadri muda ulivyoendelea, waasi walidhibiti maeneo mengi ya Libya na kuizingira Tripoli.
Tarehe 26 Februari, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliweka vikwazo vipya dhidi ya utawala wa Gaddafi na kufungia mali za familia yake.
Baadaye NATO ilianza mashambulizi ya anga yaliyosababisha hasara kubwa kwa jeshi la Libya.
Mwezi Aprili 2011, mwanawe mdogo Saif al-Arab pamoja na wajukuu watatu waliuawa katika mashambulizi ya anga ya NATO.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kifo cha Kanali Gaddafi
Mnamo tarehe 27 Juni, hati za kukamatwa zilitolewa dhidi ya Gaddafi, mwanawe na mkuu wake wa ujasusi. Baadaye, waasi waliingia Tripoli mwezi Agosti na tarehe 23 Agosti waliteka makao makuu ya Gaddafi katika eneo la Bab al-Azizia. Hata hivyo, Gaddafi mwenyewe hakupatikana na kupitia ujumbe kadhaa wa sauti aliwataka wananchi wa Libya waasi dhidi ya wapinzani wake.
Waasi pia walitangaza zawadi ya dola milioni 1.17 za Marekani kwa yeyote ambaye angeweza kutoa taarifa kuhusu alipo Gaddafi. Katika hali hiyo, mji wa Sirte ulikuwa umezingirwa na kwa mujibu wa baadhi ya taarifa, Kanali Gaddafi akiwa na baadhi ya wafuasi wake walijaribu kuvunja mzingiro uliowekwa na wapiganaji wa Baraza la Mpito.
Kanali Gaddafi na wenzake, waliokuwa wakisafiri kwa magari, walikuwa wakijaribu kupenya kupitia safu za wapiganaji wa upande wa pili huku wakipambana. Msafara huo wa magari pia ulimjumuisha mkuu wa jeshi la Gaddafi, Abu Bakr Younis, pamoja na mwana wa Gaddafi, Mutassim. Wakati huo, ndege ya Ufaransa iliyokuwa sehemu ya vikosi vya NATO ilishambulia msafara huo.
Shambulio la NATO liliharibu magari 15 ya kivita. Kanali Gaddafi na baadhi ya watu wake waliokoka shambulio hilo na kujificha katika mabomba mawili makubwa ya kupitishia maji, lakini wapiganaji waliwakaribia haraka.
"Awali tulifyatua risasi za bunduki za kupambana na ndege dhidi ya Kanali Gaddafi na watu wake, lakini haikusaidia. Kisha tuliwaendea kwa miguu. Tulipokaribia mahali ambapo Kanali Gaddafi na watu wake walikuwa wamejificha, ghafla mmoja wa wapiganaji wake alitoka akiwa ameinua bunduki yake juu, na aliponiona alianza kunifyatulia risasi," mpiganaji aliyeitwa Salim Bakir aliambia Reuters baadaye.
"Mpiganaji huyo alipaza sauti akisema, 'Bwana wangu yuko hapa, bwana wangu yuko hapa na amejeruhiwa,'" alisema Salim Bakir. "Tulimlazimisha Kanali Gaddafi kutoka nje," alisema. "Wakati huo aliuliza, 'Nini kinaendelea?'" Hata hivyo, mtu mwingine anayejitambulisha kuwa shahidi wa tukio hilo alisema alimwona Kanali Gaddafi akipigwa risasi tumboni kwa bastola ya milimita 9.

Chanzo cha picha, Getty Images
Inaripotiwa kwamba Kanali Gaddafi alikamatwa akiwa amejeruhiwa vibaya. Video zilizoonyeshwa na televisheni ya Al Jazeera zilimuonyesha akiwa katika hali mbaya kutokana na majeraha na akipigwa na wapinzani wake. Mlolongo kamili wa matukio yaliyofuata hauko wazi, lakini baadaye Waziri Mkuu wa Baraza la Mpito la Taifa, Mahmoud Jibril, aliwaambia waandishi wa habari kwamba ripoti ya uchunguzi wa maiti ya Kanali Gaddafi ilionyesha kuwa alikufa kutokana na majeraha ya risasi.
Kwa mujibu wa Mahmoud Jibril, Kanali Gaddafi alikamatwa akiwa hai na hakutoa upinzani wowote. Hata hivyo, alipokuwa akiingizwa kwenye gari ili kuondolewa eneo hilo, gari hilo lilishambuliwa kwa risasi kutoka kwa wapiganaji wa pande zote mbili, na risasi moja ilimpiga Gaddafi kichwani na kumuua.
Mahmoud Jibril aliongeza kuwa madaktari hawakuweza kubaini kama risasi iliyomuua ilitoka kwa mpiganaji wa Baraza la Mpito la Taifa au kwa mmoja wa wafuasi wa Kanali Gaddafi.
"Mfalme wa Wafalme" na Ndoto ya Ukhalifa
Kanali Gaddafi alikuwa mtawala wa kiimla aliyeiongoza Libya kwa zaidi ya miongo minne. Familia yake ilitajirika kutokana na mapato ya mafuta na mikataba mbalimbali, na inasemekana kuwa sera za Muammar Gaddafi za kusambaza utajiri zililenga kununua uaminifu wa wananchi kwake.
Hata hivyo, Gaddafi alianzisha miradi mingi mikubwa ya maendeleo, mojawapo ikiwa ni mradi wa kusambaza maji katika sehemu za kaskazini mwa nchi. Pia alikuwa maarufu kwa mavazi yake ya kipekee, pamoja na hotuba na kauli zake za kuvutia. Katika moja ya kauli hizo, alisema kwamba Wapalestina na Waisraeli wanapaswa kuunganishwa katika taifa moja kwa sababu eneo hilo si kubwa vya kutosha kuunda mataifa mawili tofauti.
Msimamo huo ulijidhihirisha pia katika mikutano ya Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League), iwe kwa tabia zake za kipekee au kwa kujitangaza kuwa "Mfalme wa Wafalme wa Afrika."
Mnamo Agosti 2008, wafalme na machifu wapatao 200 wa Afrika walimpa Gaddafi cheo hicho huko Benghazi, ambako alitangaza kampeni ya kuanzisha jeshi la Afrika, sarafu ya pamoja ya Afrika na pasipoti ya Afrika.
Mitazamo ya Gaddafi ilibadilika kadiri miaka ilivyopita. Mwanzoni, alisisitiza kaulimbiu ya kuunganisha taifa la Kiarabu na kujitambulisha kama kiongozi wa utaifa wa Kiarabu, akifuata mfano wa Gamal Abdel Nasser.
Lakini alipotambua kuwa ndoto hiyo ilikuwa ngumu kuitekeleza, alielekeza macho yake barani Afrika na kuanza kujionyesha kama kiongozi wa Afrika.
Hata hivyo, baadaye aligeukia ulimwengu wa Kiislamu na kutoa wito wa kuanzishwa kwa Ukhalifa wa pili wa Fatimid, akiamini kwamba hatua hiyo ingeweza kumaliza tofauti zilizokuwepo kati ya Wasunni na Washia katika Afrika Kaskazini.



































